MHE. JUMA DUNI HAJI - IN ONE OF HIS PRESS CONFERENCES IN ZANZIBAR LAMBASTING THE RULING PARTY.
MIAKA TISA YA DR. SHEIN AKIWA MADARAKANI ZANZIBAR
Ndugu Waandishi wa Habari.
Naomba kutoa shukurani zangu za dhati kwa kukubali kwenu kuja kunisikiliza. Leo nimekusudia kutoa tathmini fupi juu ya miaka tisa ya Dr. Shein akiwa madarakani Zanzibar.
Tarehe 28.10.2019 Dr. Shein katimiza miaka tisa akiwa madarakani Zanzibar. Wiki mbili zilizopita nimemsikia kwenye taarifa ya TVZ na kwenye mitandao ya kijamii akijinasibu kwamba amefanya mengi katika kuiletea maendeleo Zanzibar na kwamba hajamdhulumu au kumuonea mtu. Mwanadam kujitambulisha kwa wema mbele ya jamii yake ni uungwana, na kujisifu kwa mazuri aliyofanya ni wajibu wake hususan kwa nafasi ya juu ya madaraka aliyoishikilia.
Watawala wa Zanzibar.
Zanzibar imeshawahi kutawaliwa na viongozi wengi wakiwemo, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, Marehemu Mzee Aboud Jumbe, Marehemu Mzee Abdul Wakil, Mzee Ali Hassan Mwinyi Dr. Salmin Amour na Amani Abeid Aman Karume.
Kila mmoja kati ya hawa ameacha kumbukumbu njema na mbaya juu ya utawala wake. Wananchi wa Zanzibar yamewakuta mema na madhilla ya tawala hizo. Madhilla ya utawala wa Dr. Shein yametia fora. Maelezo mafupi yafuatayo yatupe nafasi kuona kwa lipi tutalomkumbuka pale anapoondoka madarakani hapo 2020.
Kila mmoja kati ya hawa ameacha kumbukumbu njema na mbaya juu ya utawala wake. Wananchi wa Zanzibar yamewakuta mema na madhilla ya tawala hizo. Madhilla ya utawala wa Dr. Shein yametia fora. Maelezo mafupi yafuatayo yatupe nafasi kuona kwa lipi tutalomkumbuka pale anapoondoka madarakani hapo 2020.
Bahati ya Dr. Shein.
Dr. Shein alipata bahati sana maana hapo 2010, Dr. Amani Karume alimkabidhi nchi yenye amani na utulivu na iliyojaa matumaini ya kujenga umoja wa kitaifa na kumaliza kabisa uhasama wa siasa za makundi ambao umedumu zaidi ya karne moja . Kipindi hiki cha miaka mitano ya awali ya utawala wake ndipo tulikua na serikali ya umoja wa kitaifa iliyofanya kazi kwa mshikamano mkubwa wa kitaifa. Jamii ilianza kuzoea maisha ya furaha na ushirikiano bila siasa za uhasama au chuki za vyama na au za kubaguana.
Ni wakati huu ambapo miradi ya maendeleo ikitekelezwa kitaifa kwa faida ya taifa. Huduma za kijamii kama elimu na afya ziliimarika. Dawa za hospitali zikipatikana. Wafanya biashara na wakulima hasa wa karafuu walifurahia bei ya mazao yao. Wafanya biashara wakubwa walishirikiana na serikali kuleta na kuuza bidhaa zao nchini na huko Tanganyika bila vikwazo na hivyo serikali ikikusanya kodi bila kuwaongezea kodi zisizokua za lazima.
Ni kipindi ambacho tulikua na baraza la wawakilishi lenye nguvu na liloisimamia serikali bila kuogopa wala kujali kwamba anaehoji serikali ni wa chama cha upinzani au CCM. Lilikua ni baraza linalowakilisha watu hasa. Ni wakati huu ambapo wazanzibari tulisimama katika baraza la wawakilishi na hata katika Baraza la Mapinduzi kujadili masuala ya kupokonywa mafuta yetu na uhalali wa kisiwa chetu cha Fungu Mbaraka. Kwa ufupi nchi yetu ilianza kutoka kwenye historia za malumbano na kuhasimiana na kila mmoja wetu alijiona ni sehemu ya jamii ya Zanzibar. Hali hiyo ya matumaini imebadilika vibaya katika kipindi chake cha pili chenye utata wa madara yake.
Uchaguzi wa 2015 na utawala wenye utata.
Baada ya kushindwa vibaya na Maalim Seif Sharif hapo 2015, Dr Shein aliibua mgogoro usio wa lazima wa hesabu za uchaguzi wa Rais wa 2015. Maalim alimfuata Dr. shein kwa kutaka maelewano na kuepuka uhasama mpya. Bila aibu Dr. Shein aliyabeza mazungumzo hayo ya pamoja na Maalim Seif Sharif na kuyatumia mazungumzo yale kuandaa uchaguzi bandia wa March 2016. Wananchi waliususia uchaguzi huu na hivyo matokeo yake yalikua mabaya sana, maana waliokwenda kupiga kura walikua chini ya 60,000. Bila kujali kauli ya wengi Dr. Shein akaiiba serikali na kwa mshangao mkubwa Dr. Shein alianza siasa za uhasama na kuharibu matumaini mema ya umoja wa kitaifa.
Mapema mwaka 2016 Dr. Shein alianzisha kikosi maalum cha askari waliotoka kwenye vikosi maalum vya serikali, na kukipa kazi maalum ya kutesa raia wasio na hatia na kuuwa. Askari hawa awali wakiitwa Janjawiid (mazombi) walikua na kawaida ya kupita katika makazi na mabaraza ya kijamii na kupiga watu ovyo na wengine kuwateka na kuwatesa na wakisha huwatupa porini. Huu ni utawala wa ajabu sana.
Kwa kweli vijana hawa ndio walipaswa kuitwa magaidi wa kidola (state terrorist). Hivyo basi Dr. Shein anaondoka madarakani huku nae mikono yake imejaa damu ya wazanzibari wasio na hatia. Mfano hai ni ule wa Mr. Ali Juma wa kijiji cha Mtoni aliekwenda kuchukuliwa nyumbani kwake wakamtesa na kumuuwa.Hadi leo hakuna kesi yeyote kama kwamba kauliwa kuku wa sikukuu. Yale yaliyowakuta ndugu zetu wapemba sina haja yakuyaeleza, sote tunayaelewa.
Kinyume na katiba yetu ambayo aliapa kuitetea, na hata baada ya ushauri wa kisheria aliopewa na wataalam wetu wa sheria, Dr. Shein ameiingiza jamii kwenye uhasama wa kidini kwa kuwachukua masheikh wa uamsho na Maulamaa wa kiislam wengine wa Zanzibar, na kuwapeleka Tanzania Bara ambako walifunguliwa kesi ya miujiza ya ugaidi, hadi leo hawakurejeshwa wala kuhukumiwa. Wabunge wetu na watetezi wengine wa haki za binaadam wamelitolea kauli kila mwaka , lakini hadi leo miaka 7 sasa eti ushahidi haujakamilika. Hii ni moja kati ya uonevu usitakaosahaulika kwa miaka mingi ijayo. Leo Dar es salaam inaitwa gwamtanamo ya wafungwa wa Zanzibar.
Hali ya maisha ya wananchi.
Wakati akiendelea kutisha wananchi kwa kuwatumia mazombi, Dr. Shein alibaki kuwa muumin mkubwa wa kuuwa sekta za kiuchumi na za kijamii na kutuongezea umasikini na kuwafanya wazanzibari kuishi maisha ya ufukara. Wananchi wamekosa ajira isipokua Kila unapokaribia uchaguzi vijana wa maskani wanaochaguliwa maalum kupitia kwa masheha ,hupelekwa katika vikosi vya SMZ kwa ajili ya maandilizi ya kuja kupiga kura kwa CCM.
Bila huruma Dr. Shein ameiua sekta isiyorasmi kwa kuwanyanyasa wananchi wa kawaida wanaojishughulisha na maisha yao kwa kujituma wenyewe. Kila mara Serikali haramu ya Dr. Shein imeanzisha utaratibu mgumu wa kufanyika shughuli hizo kwa kuweka masharti magumu ya vibali vya leseni za biashara ndogo ndogo zikiwemo kodi za ajabu. Wenye maduka ya reja reja, wauza maandazi, wenye daladala, wauza samaki, mafundi na vijana wajua kali wote hawa wametoweka kutokana na vikwazo, aidha vya kuhamishwa kwenye maeneo yao au kuwekewa masharti magumu ya kufanya shughuli hizo.
Dr Shein ameiuwa kwa maksudi sekta ya ujenzi ambayo wengi ya wananchi ndiyo wakiitegemea kwa maisha yao ya kila siku. Kwa kisingizio cha kuharibu mazingira sekta hizi ziliporomoka baada ya bei za gari la mchanga na mawe kupanda sana, Bei ya lori tani saba lilipanda toka 250,000 mpaka 800,000 . Hivyo sekta ya ujenzi imeporomoka na hivyo kuathiri mwenendo mzima wa sekta ya ujenzi na uchimbaji mawe na kila aina ya biashara inayohusiana na ujenzi, wauza saruji, wauza kokoto, wauza vifaa vya ujenzi vibarua na mafundi aina mbali mbali, wauza milango ya mbao na vyuma (magirili).
Ndiyo maana baadhi yetu hushangaa pale serikali inaposema pato la mwananchi limeongezeka. Maelezo ya aina hii huaonekana ni fikra za kinadharia maana hazilingani na hali ilivyo mitaani. Kwa kweli serikali imedumaa, maana baada ya kuzuia na kubadili bei za mchanga na mawe, (chini ya kivuli cha magendo na rushwa kubwa) inayofanywa na maafisa wa serikali, sasa Zanzibar mchanga hauna tafauti na dhahabu.
Watu wa mikoa ya kusini unguja na wa Micheweni Pemba wameathirika sana na maamuzi haya na sasa wanaishi maisha ya kifukara kwa sababu bidhaa hizi ndivyo vilikuwa vitega uchumi kwao. Serikali haikuwatayarishia mbadala wa kujikimu kwa maisha yao ya kila siku.
Kwa hivyo Dr. Shein ameshindwa kabisa kuwa na mipango madhubuti ya kuitafutia maendeleo Zanzibar kiuchumi. Ameshindwa kudai na kusimamia haki zetu zilizoko kwenye serikali ya muungano. Malalamiko ya kuzuiliwa bidhaa zetu kuingia Tanganyika limemshinda. Upatikanaji wa dhamana za amana kwa mikopo ya Zanzibar limemshinda. Hata masuala ya michezo yanalazimishwa kufanyika kimuungano, na Dr. Shein anashindwa kulitetea hili. Tangu 1964 Zanzibar imekua na utaratibu wa kusajili meli za kigeni na kutupatia fedha chache za kigeni, hata hili nalo tumezuiliwa na Dr. Shein amenyamaza kimya.
Ujenzi wa Bandari na uwanja wa ndege imekuwa ni ndoto ya mchana, na kuna kila dalili mpaka ataondoka bado tutabaki hakuna bandari wala uwanja wa ndege ambao unahitajika. Kwa jumla milango ya kiuchumi bado imefungwa na hali ya kiuchumi ya Zanzibar ni mbaya na inazidi kuwa mbaya wakati yeye anaziba masikio hasikilizi ya muazini wala ya mkosha choo msikitini.
Si hilo tu ila pia Dr. Shein anaendelea kuwadanganya wa Zanzibari kwa kuwahadaa juu ya Sheria ya mafuta iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi akiwaaminisha wa Zanzibari kwamba suala la mafuta sio suala la Muungano jambo ambalo sio kweli. Alifanya pupa na mbwembwe binafsi na serikali yake kuwapa maeneo yote kampuni ya Sharja (RAK GAS) ya utafiti wa mafuta. Juhudi hiyo ambayo havionyeshi tu dalili za wazi za mazalio ya rushwa lakini pia limeiweka taifa kwenye pingu za mkataba mibovu ambayo italitesa Taifa hilo siku za baadae
Ubaguzi na Mazingira ya uchaguzi wa 2020.
Kati ya mengine maovu ya utawala wake ni pale Dr. Shein anaposhabikia Ubaguzi wa wazi kwa wananchi kunyimwa vitambulisho vya Zanzibari na vile vya kupigia kura. Masheha wameagizwa kutowapa ruhusa wapinzani na yeyote anaeoneka si CCM kupewa vitambulisho hivyo
Ni kitendo kilichowazi kwamba hivi sasa huwezi kuajiriwa kama huna kadi ya uzanzibari. Vivohivyo huwezi kupata huduma yeyote kama huna kitambulisho cha mzanzibari. Kilicho aibu zaidi ni kwamba wageni wanavipata bila taabu na kuajiriwa bila taabu. Kitengo maalum (GSO) kimewekwa kuwachunguza wote wale wanaomba kazi serikalini. Bila aibu wala kificho uamuzi huu alishautetea hadharani na hivyo ameendeleza sumu mbaya sana ya kuligawa taifa mapande mawili, kwa alie CCM ana haki ya kuajiriwa na wengine hawana.
Uchaguzi 2020.
Dr. Shein ametuandalia mazingira magumu ya uchaguzi ujao kwa kujali zaidi maslahi ya chama chake na ya wale walomuweka madarakani yaani Tanganyika Dr. Shein amevunja mfumo mzima wa sheria ya uchaguzi na Tume ya uchaguzi uliokuwa uwe na wajumbe kutoka vyama vya upianzani na hivyo kuvunja dhamira ya kulinda umoja wa taifa. Dr. Shein ameteuwa Tume yenye wajumbe takriban wote wastaafu wakereketwa wa CCM wenye kumbukumbu mbaya za kiutendaji dhidi ya upinzani walipokua serikalini
Bila kujali maafa yatakayotokea uamuzi wa kutoa kitambulisho kipya cha mzanzibari mkaazi, na kujinasibu kwamba sasa wazanzibari si wazaliwa wa Zanzibar bali ni wakaazi tu kama vile ambavyo mtu wa Burundi au Kenya alokwisha ingia Zanzibar, ni dhambi kubwa inayoweza kuleta vita vya wahamiaji na wazaliwa. Maamuzi ya kubadilisha kitambulisho itaingiza Zanzibar kwenye mgogoro wa kiuraia na vita vya kugombania ardhi kama ilivyotokea visiswa vya Fiji huko bahari ya Pacific.
Visiwa vya Fiji vilikumbwa na mgogogro wa uraia na umiliki wa ardhi pale jamii ya kihindi kutoka India ilipoongezeka maradufu kwa ajili ya kufanya kazi kwenye mashamba ya miwa. Baada ya miaka kupita jamii ya kihindi ikawa kubwa kuliko wenyeji na hivyo chaguzi za kuchagua viongozi wa nchi hiyo ikamilikiwa na jamii ya kihindi walio wageni
Tatizo hilo la Fiji la mgogoro wa kijamii lilibua mapinduzi ya mara kwa mara pale mvutano mkubwa wa wageni na wenyeji ulipozuka katika kumiliki madaraka ya Serikali. Mapinduzi ya mwanzo yaliongozwa na mzaliwa anaitwa Sitiveni Rabuka hapo 14 May 1987. Mapinduzi haya yalizaa uhasama mkubwa kati ya makundi ya kijamii na kusababisha katiba mara kwa mara kubadilishwa, hali ya kutokubaliana kwa mfumo wa kikatiba kukaendelea kuzaa mapinduzi mengine. Huko ndiko anakotusukuma Dr. Shein.
Tulitegemea Dr. Shein angejuta kwa maovu aliyokwisha kuyafanya na kutumia nafasi ya kuendesha serikali bila kuwepo wapinzani, kujijengea mazingira rafiki ya kujenga mahusiano mema ya kijamii. Badala yake Dr. Shein ameivuruga jamii na kuzalisha uhasama wa makundi kwa kutumia siasa. Amesahau kwamba kuna maisha baada ya siasa.
Sisi wengine tunapata mashaka, juu ya dhamira hizi mbovu za Dr. Shein, labda inaonekana dhamiri ya Dr. Shein ni kutuwekea mgogoro wa kudumu kwa mambo mawili. a) Kila uchaguzi utapofanyika chama chake kishinde kwa kutumia hadaa za kulivuruga daftari la wapiga kura na (b) pale litakapochimbuka upya suala la katiba mpya ya muungano, wakaazi wa Zanzibar wawe wachache na wageni wawe wengi na hivyo kuwapiku wazaliwa ili kufikiwa lengo la muda mrefu la kuundwa kwa serikali moja.
KHITIMISHO.
Naomba kuwaeleza wazanzibari kwamba idhilali tulizopata kutokana na tawala za Zanzibar zilizopita hazijawahi kutukatisha tamaa juu ya lengo letu la kudai haki zetu za kuzaliwa na zile zilizoporwa na Serikali ya muungano kwa hadaa. Tumeelewa kwamba Vitimbakwiri na manokoya wa nchi yetu ndio wamekua wakitugombanisha kwa maslahi yao. Hivyo hakuna ujanja wowote utakaofanywa dhidi yetu utakaofanikiwa. Wazanzibari tumevuka madhila yote ya tawala zilizopita kwa sababu ya umoja wetu na kujitambua kwetu kwamba sisi ni wazanzibari na tutabaki kuwa wazanzibari dumu daima kama vile wengine wanavyojitambua kwa nchi zao. Zanzibar itabaki Zanzibar
Historia ya nchi hii inatueleza kwamba wazanzibari hatujawahipo kupata maisha ya utulivu na amani kwa vipindi verefu sana. Walikufa wazanzibari vita vya ngombe, wakafa wazanzibari vita vya June 1961, wamekufa wazanzibari wakati wa Mapinduzi 1964, wamekufa wazanzibari Januari 2001, na bado wazanzibari wanaendelea kuteswa na kuuliwa kidogo kidogo bila hatia. Sisi tunaamini na tuliamini kwamba maafa hayo iwe imetosha. Na ndiyo maana tumebaki kutetea njia ya kikatiba na kidimokrasia ya wengi wape wachache washirikishwe. Dr. Shein anaukataa mfumo huo.
Mipango ya Dr. Shein kuuvuruga uchaguzi wa 2020 tunaijua. Chini ya uongozi wenye kujiamini na wenye kujua unachokifanya, wa chama chetu cha ACT - Wazalendo upo tayari kushinda uchaguzi huo na kuchukua serikali. Utamaduni wa kwamba kundi moja la wazanzibari kuwekewa utamadumi wa kukosa haki na heshima ya kiutu, na kundi dogo jingine liwe ndilo linalotumiliki haukubaliki.
Hivyo mfumo wa kubadilishana madaraka bila fujo na kwa utaratibu unaoeleweka umo kwenye katiba yetu ya Zanzibar. ACT-Wazalendo inasisitiza kwamba mfumo huu lazima uheshimiwe kwa hiari au kwa nguvu. Shime wananchi tuusimamie mfumo huo maana CCM imeshakataliwa Zanzibar na ndiyo maana Dr. Shein anataka kutulazimisha kuingia kwenye vurugu. ACT-Wazalendo tumejiandaa. Hilo halitatokea tena, Tusilaumiane.
JUMA DUNI HAJI
NAIBU KIONGOZI ACT-WAZALENDO
TAREHE: 17/11/2019
VUGA - ZANZIBAR
No comments :
Post a Comment