"Waheshimiwa Wabunge wetu. Nimemsikiliza Spika Ndugai akiweka msimamo wake kuhusu hatua yenu ya kuondoka Bungeni kwa muda.
Spika Ndugai anastahili kujibiwa rasmi na hadharani, na napendekeza yafuatayo kuwa sehemu ya majibu yenu.
1. Je, Wabunge wa CHADEMA ni watoro?
Kwa kadri ninavyofuatilia mijadala ya Bunge, ni Wabunge wa CHADEMA peke yenu ambao tangu mwanzo mmedai Wabunge wote wapimwe ili kuona kama kuna yeyote mwenye maambukizi ya coronavirus. Nimemsikia KUB akisema hivyo mara kadhaa. Nimemsikia Mh. Goddie Lema akisisitiza umuhimu wa Wabunge kupimwa, n.k.
Maombi na madai yenu ya kupimwa yamepuuzwa na uongozi wa Bunge na wa Serikali na hadi sasa hakuna Mbunge hata mmoja aliyepimwa. Ushahidi wa hili ni kauli yake mwenyewe Spika Ndugai leo kwamba mkapimwe kwanza ndio mruhusiwe kurudi Bungeni. Maana yake ni kwamba anajua hamjapimwa.
Tayari kuna Wabunge watatu wameshakufa kwa coronavirus. Gertrude Lwakatare, Richard Ndassa na Dr. Augustine Mahiga ni wahanga wa coronavirus. Kama Serikali ya Magufuli na Spika Ndugai wanabisha basi waseme kwa nini wamewazika Waheshimiwa hawa kwa taratibu za mazishi ya coronavirus.
Baada ya vifo vya Wabunge watatu na Bunge kukataa kuchukua hatua za kuwapima Wabunge kama inavyotakiwa na miongozo ya kupambana na coronavirus ya WHO, n.k., Wabunge wa CHADEMA wamechukua hatua za kujilinda wao na wale walio karibu nao. Na wametangaza hivyo hadharani. Utoro wao unaanzia wapi???
2. Kati ya Wabunge wa CHADEMA na Rais Magufuli mtoro ni nani???
Kama, kwa kauli ya Spika Ndugai, Wabunge wa CHADEMA ni watoro, basi mtoro wa kwanza ni Rais John Pombe Magufuli. Na kama Wabunge wa CHADEMA ni wezi kwa kuchukua posho za vikao na kuondoka Bungeni, basi mwizi wa kwanza ni Rais John Pombe Magufuli.
Tangu janga la coronavirus lilipoanza kuwa kubwa hapa nchini, Rais Magufuli ametoroka Ikulu na kujificha nyumbani kwake Chato. Sheria ya Presidential Affairs Act ya mwaka 1962 inamlazimu Rais wa Tanzania kufanyia shughuli rasmi za Rais Ikulu au katika makazi rasmi ya Rais nje ya Ikulu. Kila Mkoa na kila Wilaya ina makazi rasmi ya Rais. Chato sio makazi rasmi ya Rais Magufuli, kama ambavyo Msoga haikuwa makazi rasmi ya Rais Kikwete; au Masasi au Lushoto haikuwa makazi rasmi ya Rais Mkapa na Butiama au Msasani haikuwa makazi rasmi ya Mwalimu Nyerere.
Chato na Msoga na Masasi/Lushoto na Butiama ni makazi binafsi ya Rais na shughuli rasmi za Serikali hazipaswi kufanyiwa kwenye makazi hayo. Kwa hiyo kama Wabunge wa CHADEMA ni watoro na wezi, Rais Magufuli naye ni mtoro na mwizi. Hakuwezi kukawa na ubaguzi kwenye jambo hili.
Na kama suala ni kurudisha pesa kwa sababu ya kutokuwepo Bungeni kwa sababu halali kama hii ya kujikinga na coronavirus, basi na Rais Magufuli naye arudishe pesa zote alizopokea au kupewa kwa kipindi chote ambacho ametorokea Chato. Nasisitiza hakuwezi kukawa na kauli mbili tofauti juu ya suala hili.
3. Je, Wabunge wa CHADEMA ni wezi kweli?
Mwizi ni yule anayechukua mali ya mwingine bila ridhaa yake na bila haki ya kufanya hivyo. Hii ndio tafsiri rahisi ya wizi kwa mujibu wa sheria zetu.
Je, Wabunge wa CHADEMA walichukua pesa bila ridhaa ya Bunge na hawakuwa na haki nazo???
Posho na mishahara ya Wabunge huingizwa kwenye akaunti zao na Bunge lenyewe bila hata Wabunge wenyewe kuziomba au kujua. Hawa wa CHADEMA wanakuwaje wezi kwa kuingiziwa posho kwenye akaunti zao na uongozi wa Bunge???
Na je, sio halali kupewa posho za kujikimu??? Kuna posho za aina mbili zinazotolewa kwa Wabunge. Posho za kujikimu (per diem) na posho za vikao (sitting allowance).
Kila Mbunge aliyeko Dodoma analipwa posho za kujikimu, hata kama haingii Bungeni. Kama Spika Ndugai anabishia hili aseme wazi wazi na hadharani.
Posho za vikao zinalipwa kwa kuhudhuria Bungeni, na hulipwa baada, sio kabla, ya mahudhurio ya vikao. Kama Spika Ndugai anabishia hili aseme wazi wazi na hadharani pia.
Wabunge wa CHADEMA wamelipwa per diem kwa sababu wako Dodoma kwa ajili ya vikao vya Bunge. Wangekuwa wamelazwa hospitalini bado wangelipwa per diem. Wako in isolation kujikinga na coronavirus na kwa hiyo wanastahili kulipwa per diem.
Sijamsikia Spika Ndugai akizungumzia malipo ya sitting allowance. Kama Wabunge wa CHADEMA wamelipwa sitting allowance na hawajahudhuria vikao vya Bunge basi aseme ili tuulize wamelipwaje kabla ya mahudhurio ya vikao??? Hii ni kwa sababu hawapaswi kulipwa sitting allowance kama hawajahudhuria vikao vya Bunge.
4. Tabia ya Spika Ndugai kutaja taja hadharani malipo ya Wabunge wa upinzani wenye ugomvi naye au na Serikali ya Magufuli.
Hii sio mara ya kwanza kwa Spika Ndugai kutaja mamilioni waliyolipwa Wabunge wa CHADEMA wenye ugomvi naye au na Serikali ya Magufuli. Hatujawahi kuona tabia hii ya hovyo kwa miaka yote ya kabla Rais Magufuli kuingia madarakani.
Spika Ndugai hajawahi hata mara moja kutaja pesa anazolipwa yeye mwenyewe au Wabunge wa CCM. Je, ina maana ni Wabunge wa CHADEMA peke yao ndio hulipwa mamilioni haya???
Spika Ndugai mwenyewe amelipwa mabilioni mangapi kwa sababu hii au ile??? Mbona hajawahi kuzungumzia mabilioni aliyolipwa kwa ajili ya matibabu yake India ambayo hata CAG aliyahoji kwenye taarifa yake ya mwaka jana??? Hivi mwizi ni nani hasa kati ya Wabunge wa CHADEMA na Spika Ndugai???
Spika Ndugai anataka watu wasiojua waamini kwamba Wabunge wa CHADEMA wamelipwa pesa hizo bila halali yoyote. Kama hiyo ni kweli, je, kwa nini Bunge linawalipa pesa hizo haramu???
5. Spika Ndugai ametishia kuwachukulia hatua nyingine ambazo hajazitaja lakini amesema hiki ni kipindi cha mwisho cha Bunge. Kama hamjaelewa, hapa anamaanisha kwamba watazuia malipo ya kiinua mgongo cha Wabunge wa CHADEMA.
Hii ni blackmail ya moja kwa moja. Kiinua mgongo ni haki ya kisheria ya kila Mbunge aliyetumikia kipindi fulani cha Ubunge. Kiinua mgongo sio fadhila ya Spika Ndugai au ya Kuhani Mkuu kwa Wabunge wenye tabia njema kwao. Ni haki ya Wabunge wote. Asiwatishe!!!
6. Ushauri wangu kwenu ni huu:
a. Msirudi Bungeni hadi muda wa kujitenga kwa hiari wa siku 14 utakapoisha. Baada ya muda huo kwisha rudini Bungeni wakawazuie kuingia ili dunia nzima ifahamu jinsi walivyo watu wa hovyo.
b. Msirudishe posho za kujikimu mlizolipwa kwa sababu mko kwenye eneo la kibunge Dodoma na mko nje ya Bunge kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya coronavirus. Hivi ndivyo inavyoshauriwa na wataalamu wa afya na WHO. Posho hizo ni haki yenu.
Aidha, kulipa madeni ya Bunge sio, na haijawahi kuwa, sharti la Mbunge kuruhusiwa kuingia bungeni. Kama wanafikiri wanawadai basi wawakate kwenye mishahara, lakini sio kuwazuia kuingia Bungeni.
c. Kuhusu kutishiwa kuripotiwa polisi, hii haitakuwa ajabu kwa nchi yetu katika zama hizi za Tanzania ya Magufuli.
Kumbukeni tu kwamba hamjafanya kosa lolote lile la jinai kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. Kama Jeshi la Polisi litawakamata, haitakuwa ni kwa sababu ya kufanya kosa lolote lile bali ni kwa sababu hili limekuwa jeshi linalofanya kazi zake kwa 'maelekezo kutoka juu.'
d. Kuhusu kupimwa coronavirus. Muulizeni Spika Ndugai au Waziri wa Afya awaelekeze mahali palipotengwa kwa ajili ya kupimia coronavirus.
Na sisitizeni hadharani kwamba kila Mbunge na mtumishi wa Bunge akapimwe kama utaratibu wa WHO unavyosema.
Sio Wabunge wa CHADEMA peke yao wanaopaswa kupimwa; ni Wabunge wote. Marehemu Lwakatare, Ndassa na Dr. Mahiga hawakuwa Wabunge wa CHADEMA, walikuwa ni wa CCM. Kwa hiyo kupimwa kunawahusu Wabunge wote.
e. Kurudi Bungeni kwa sababu ya vitisho hivi haramu ni kupoteza credibility yote mliyo nayo. Ni kuonyesha Watanzania kwamba mnachohofia sio afya wala maisha yenu au ya Watanzania bali ni pesa zenu tu.
Simameni imara. Msikubali vitisho hivi vya kijinga!!!"
No comments :
Post a Comment