Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, May 26, 2020

Nani ni nani Zanzibar: Mfahamu Othman Masoud Othman (Ochu)!

Othman Masoud Othman (Ochu).
Othman Masoud Othman (Ochu) ni mmojawapo ya Wazanzibari mahiri na wa kutajika katika masuala ya sheria na mikakati. Ochu kazaliwa kijiji cha Pandani Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, mwanzoni mwa miaka ya sitini. Babake mzazi Ochu Sheikh Masoud Bin Othman alikuwa moja ya walimu mahiri wa dini misikitini, madrasa na hususan katika Skuli ya Pandani ambako alifundisha Quran.

Picha imepigwa na waandishi wa Zanzibar Daily wakiwa safarini kuelekea Pandani kukamilisha utafiti wa makala hii
Picha imepigwa na waandishi wa Zanzibar Daily wakiwa safarini kuelekea Pandani kukamilisha utafiti wa makala hii.

Ochu alianza masomo yake ya msingi katika Skuli ya Pandani ambapo alionyesha umahiri mkubwa darasani, akishika nafasi ya kwanza katika miaka yake yote na kuwaacha wanafunzi wenzake kwa mbali sana kiwastani. Kama ilivyokuwa matarajio ya wengi na Ochu mwenyewe, alipasi vizuri mitihani yake ya michepuo na kupata nafasi ya kuendelea na masomo katika Skuli ya Fidel Castro, Chake Chake, Kusini Pemba.

Ochu akaendeleza ukipanga na kufaulu kwa daraja la kwanza (Division One) na kufanikiwa kuchaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa Shahada ya Kwanza katika Sheria (LL.B). Akiwa UDSM Ochu alikuwa mwanafunzi mahiri kwenye Kitivo cha Sheria akiwa na uwezo mzuri darasani na kujenga hoja kwenye mijadala. Alihitimu masomo yake chuoni hapo kwa kupata digrii ya kwanza ya Sheria yenye heshima (Cum Laude/With Honors).
Baada ya mahafali UDSM Ochu alirejea Zanzibar na kuajiriwa na SMZ katika Wizara ya Katiba na Sheria kama Wakili wa Serikali. 

Alifanya kazi vizuri serikalini na baadaye SMZ ikampa ufadhili kwenda Chuo Kikuu cha London kuongeza ujuzi kwa kuchukua Shahada ya Pili ya Sheria (LL.M). Alipohitimu akarejea tena Zanzibar na baada ya muda mfupi akateuliwa kuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Utawala Bora na Sheria katika kipindi uongozi wa Awamu ya Tano chini ya Dk Salmin Amour. Ochu alikuwa msomi aliyejiamini kazini na kutimiza majukumu yake bila ajizi hivyo aliaminiwa sana na mfumo wa uongozi wa nchi. 

Rais wa Awamu ya Tano Dk Salmin Amour Juma alimteua Ochu kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Utawala Bora na Sheria
Rais wa Awamu ya Tano Dk Salmin Amour Juma alimteua Ochu kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Utawala Bora na Sheria.

Rais Amani Abeid Karume alipoingia madarakani alimteua kuwa Mkurugenzi wa kwanza wa Mashtaka Zanzibar kazi ambayo nyaraka zinaonyesha aliifanya vizuri japo yalikuwepo malalamiko kuwa alitumia nafasi yake kulazimisha kuajiriwa watu wa asili ya Pemba zaidi katika ofisi hiyo.

Novemba 2010 Dk Ali Mohamed Shein alichaguliwa kuwa Rais wa 7 wa Zanzibar na katika moja ya teuzi alizofanya kwenye kuunda serikali yake ilikuwa kumteua Ochu kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Moja ya kazi kubwa ya Ochu katika cheo hicho kipya ilikuwa mapitio ya sheria mbalimbali za Zanzibar na Muungano. Katika mchakato wa majadiliano ya mabadiliko ya katiba ya Tanzania Ochu alikuwa nyota iliyotoa mwanga hasa kwenye mijadala migumu na tata ilohusu mambo mbalimbali.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein akimwapisha Othman Masoud Othman kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein akimwapisha Othman Masoud Othman kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar

Wakati wa mchakato huo wa mabadiliko ya Katiba, mabalaa yakaanza kumuandama Ochu hasa kutokana na misimamo yake kwenye utetezi wa mambo yahusuyo Zanzibar, uumini wa Serikali tatu na kupunguzwa mambo ya muungano. 

Moja ya nadharia yake mashuhuri ni ile ya kusema kila jambo moja la muungano ni kama liko katika kontena na ndani ya kontena hilo yako makontena mengine elfu. Katika sekeseke hilo la Katiba na misimamo yake Ochu alitimuliwa kwa aibu katika Bunge la Katiba chini ya ulinzi wa vyombo ya usalama na kisha kurejeshwa Zanzibar ambako alivuliwa nafasi yake kama Mwanasheria Mkuu wa SMZ.

Ochu akiondolewa katika ukumbi wa Bunge baada ya kuvutana katika Bunge la Katiba
Ochu akiondolewa katika ukumbi wa Bunge baada ya kuvutana katika Bunge la Katiba

Baada ya mitihani hiyo Ochu akaamua kuingia kwenye siasa, akiamini ni njia nyengine ya kusimamia yale anayoyaamini. Akajiunga na Chama cha Wananchi (CUF) na kuteuliwa kuwa Mshauri Mkuu wa Chama na Mshauri Maalum wa aliyekuwa Katibu Mkuu CUF Maalim Seif Shariff Hamad.

Mbali na misukosuko aliyokuwa akiipata, Ochu mbongo bado ilikuwa inachemka na aliamua kurudi tena darasani, safari hii akajiunga na Chuo Kikuu cha Turin nchini Italia kusoma Shahada namba mbili ya Uzamili (Master) katika Sheria (LL.M) na kuhitimu vizuri.

Hivi sasa akiwa nje ya SMZ na ndani ya siasa za upinzani, popote anapokwenda ndani na nje ya Zanzibar bado anatoa na kusimamia mawazo yake yale yale kuhusu haki za Zanzibar akiamini kwenye serikali tatu na mamlaka kamili. Dhoruba ilipoipiga CUF na wababe kuamua kugawana mbao huku Maalim na kundi lake wakitimkia ACT Wazalendo, Ochu naye akajiunga na naye. 

Ochu akizungumza katika moja ya makongamano
Ochu akizungumza katika moja ya makongamano

Mbali na siasa, Ochu anamiliki kampuni yake binafsi ya masuala ya sheria iliyopo eneo la Mombasa mjini Zanzibar kwenye jengo la Bopar Enterprise. Wateja wake ni watu binafsi na makampuni lakini pia hutoa huduma kama mshauri mwelekezi katika mashirika mbali mbali ya kimataifa nje ya nchi.

Ochu ni msomi, mtumishi mahiri wa umma na kaiweka Zanzibar moyoni lakini mbali na hayo kama alivyo mja yeyote yule anayo mapungufu yake ambayo mara nyingi huibuka na kutikisa ama kufuta ndoto za yeye kuchaguliwa katika nafasi kubwa za uongozi Zanzibar hasa ile ya Urais wa Zanzibar ambaye amekuwa akitajwatajwa.

Ochu anatajwa katika kashfa nyingi za kudhalilisha wanawake hata wake zake mwenyewe hasa ile ya kuoa na kuacha karibu kila miaka mitatu. Tukio moja la kuhuzunisha ni lile la kuwaita wake zake wawili na kuwataliki kwa wakati mmoja. Watetezi wengi wa haki za wanawake hasa Zanzibar wamekuwa wakinyooshea kidole mambo haya mara nyingi. Mmoja kati ya walokuwa wake zake ambaye sasa keshamtaliki ni aliyekuwa Balozi wa Tanzani nchini Kenya na Japan Bi Batilda Salha Burian. Wawili hawa walikutana Uingereza wakisoma pamoja katika Chuo Kikuu Cha London (School of Law).

Bi Batilda Salha Burian
Bi Batilda Salha Burian

Ochu bado anachunguzwa na mamlaka za Zanzibar kuhusu tuhuma za rushwa ya ngono na maafisa wake wa kike wakati akiwa Mwanasheria Mkuu SMZ.  Mmoja katika maafisa wake wa zamani anasema alipokuwa Mkurugenzi Idara ya Mashtaka, wanawake wote wanasheria katika ofisi hiyo akiwemo yeye walikuwa na uhusiano nae kimapenzi. 

Nafasi yake katika siasa za Zanzibar 
Ochu ni mtu anayetegemewa sana na chama chake cha ACT Wazalendo katika siasa za Zanzibar kutokana uelewa wake wa eneo hili. Yuko karibu sana na viongozi wakuu wa chama hicho hasa Seif Shariff Hamad, Jussa na Mazrui. 

Maalim Seif Sharif Hamad
Maalim Seif Sharif Hamad

Ochu pia ndiye mpanga mikakati mkuu wa ACT Wazalendo Zanzibar anayetoa mwongozo wa vipi chama hicho kinaweza kushinda katika uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu. 

Tayari mvutano umeanza ndani ya ACT Wazalendo kuhusu nani atasimama kama Mgombea Urais Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho iwapo Maalim Seif atatundika daluga. Lipo kundi linalopendekeza nafasi hiyo apewe Ochu. Ana nafasi kubwa ya kushinda ndani ya ACT kwani Wapemba wana nguvu zaidi ACT Zanzibar na mara nyingi wao hupiga kura kwa kuangalia kwanza kama mgombea ni Mpemba au la. 

Changamoto ni kwamba hata kama Ochu atateuliwa kuwa mgombea wa Urais Zanzibar kwa tiketi ya ACT, atapoteza uchaguzi huo kirahisi mbele ya CCM kutokana na kwanza msimamo wake wa serikali tatu ambao una maadui chungu mzima, pili kukosa msingi mzuri Unguja, tatu kutokuwa na mizizi ndani ya serikali ili kuwa na mbinu za kushinda, na nne kuonekana kama kibaraka (stooge) tu wa Maalim. 

Mansoor Yussuf Himid
Mansoor Yussuf Himid

Wanaompinga Ochu wanamuunga mkono Mansoor Yussuf Himid kuchukua nafasi ya Mgombea Urais Zanzibar kwa tiketi ya ACT iwapo Maalim atajiondoa. Moja, Mansoor anaonekana kuwa na nguvu kubwa Unguja na kiasi (moderate) Pemba hivyo kuwa mtu muhimu kuwaleta Wapemba na Waunguja pamoja. 

Pili, anatajwa kuwa na uzoefu mkubwa zaidi serikalini kuliko Ochu na mahusiano ya kidamu na mfumo (Shemeji yake Amani Abeid Karume) ambayo anaweza kuyatumia kwa faida yake. Wachambuzi wa siasa za Zanzibar wanaeleza kuwa iwapo Maalim Seif hatagombea, ACT ina nafasi nzuri zaidi Zanzibar iwapo itamteua Mansoor kuchukua nafasi hiyo kuliko Ochu. Iwapo hilo litatokea au la, ni suala la kusubiri. 

https://zanzibardaily.com/f/nani-ni-nani-zanzibar-mfahamu-othman-masoud-othman-ochu



No comments :

Post a Comment