Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, June 13, 2020

Hotuba Ya Waziri Mpango Akiwasilisha Bungeni Bajeti Ya Mwaka 2020/21!

  1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kukubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2020/21. Bajeti hii ni ya tano ya Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bajeti hii inawasilishwa kwa mujibu wa matakwa ya Ibara ya 137 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na Kifungu cha 26 cha Sheria ya Bajeti, Sura 439.
  1. Mheshimiwa Spika, hotuba hii inaambatana na vitabu vinne vya bajeti. Kitabu cha Kwanza ni Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, na Wakala wa Serikali; Kitabu cha Tatu ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni Makadirio ya Matumizi ya Maendeleo kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2020 pamoja na Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Serikali wa mwaka 2020 ambavyo ni sehemu ya bajeti hii.

  1. TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2019/20
Mwenendo wa Mapato
  1. Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2019/20, Serikali ilitarajia kukusanya jumla ya shilingi trilioni 33.11 kutoka katika vyanzo vyote vya ndani na nje ambapo hadi Aprili 2020 kiasi cha shilingi trilioni 26.13 kimekusanywa sawa na asilimia 93.2 ya lengo la mwaka. Mchanganuo wa mapato yaliyopatikana hadi Aprili 2020 ikilinganishwa na lengo la kipindi hicho ni kama ifuatavyo:
    • Mapato yaliyokusanywa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yalikuwa ni shilingi trilioni 14.64, sawa na asilimia 93.5 ya lengo;
    • Mapato yasiyo ya kodi yalifikia shilingi trilioni 2.25, sawa na asilimia 87.2 ya lengo;
    • Mapato ya Halmashauri yalifikia shilingi bilioni 561.49, sawa na asilimia 88.1 ya lengo;
    • Misaada na mikopo iliyopokelewa ilikuwa shilingi trilioni 2.41 sawa na asilimia 94.5 ya lengo;
    • Mikopo ya ndani ikijumuisha mikopo ya kulipia dhamana za Serikali zilizoiva ilifikia shilingi trilioni 4.45, sawa na asilimia 103.8 ya lengo; na
    • Mikopo ya masharti ya kibiashara ya nje ilifikia shilingi trilioni 1.82 sawa na asilimia 78.7 ya lengo.
  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020, mapato yaliyokusanywa na TRA yamekua kwa asilimia 13.6 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2018/19. Ukuaji huo umetokana na: kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi na matumizi sahihi ya mashine za kutolea risiti za kielektroniki ili kudhibiti upotevu wa mapato; utoaji wa elimu na maboresho ya huduma kwa mlipa kodi; na kuimarika kwa udhibiti wa madini. Aidha, wananchi wamehamasika kulipa kodi kutokana na kuimarika kwa utoaji wa huduma za kiuchumi na kijamii ikijumuisha maji, elimu, afya, miundombinu wezeshi ya barabara na umeme; na kufutwa kwa ada na tozo za kero ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuwekeza hapa nchini.
  1. Mheshimiwa Spika, mwenendo wa upatikanaji wa fedha kutoka soko la ndani umeimarika kutokana na: Kuongezeka kwa ukwasi kwenye benki za kibiashara; Serikali kuendelea kuorodhesha Hatifungani za Serikali katika Soko la Hisa la Dar es Salaam; na kutoa elimu kwa umma ili kuhamasisha ushiriki wao katika kuwekeza kwenye Hatifungani na Dhamana za Serikali.
  1. Mheshimiwa Spika, mwenendo mzuri wa misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo umetokana na juhudi za Serikali katika kutekeleza misingi ya ushirikiano kama ilivyoainishwa katika Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo (Development Cooperation Framework – DCF). Mwongozo huo unatoa fursa mbalimbali za majadiliano yanayowezesha kufikia makubaliano ya utoaji fedha za maendeleo kwa wakati ili kutekeleza miradi ya maendeleo.
Mwenendo wa Matumizi
  1. Mheshimiwa Spika, makadirio ya matumizi kwa mwaka wa fedha 2019/20 yalikuwa shilingi trilioni 33.11 ambapo shilingi trilioni 20.86 ni matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 12.25 ni matumizi ya maendeleo. Katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Aprili 2020, jumla ya shilingi trilioni 24.85 zimetolewa sawa na asilimia 88.6 ya lengo. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 17.22 zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambazo zinajumuisha shilingi trilioni 5.83 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa umma, shilingi trilioni 2.91 kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi trilioni 8.48 kwa ajili ya kugharamia deni la Serikali na mahitaji mengine ya Mfuko Mkuu.
  1. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2020, jumla ya shilingi trilioni 7.63 sawa na asilimia 65.9 ya lengo zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo shilingi trilioni 6.65 ni fedha za ndani sawa na asilimia 87.2 na shilingi bilioni 976.9 ni fedha za nje sawa na asilimia 12.8. Aidha, kiasi cha shilingi trilioni 1.28 zilielekezwa moja kwa moja na Washirika wa Maendeleo kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali bila kupitia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
  1. Mheshimiwa Spika, naomba nieleze baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa bajeti kwa kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020 kama ifuatavyo:
  • Jumla ya shilingi trilioni 2.44 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya barabara, reli na viwanja vya ndege;
  • Serikali ilifanikiwa kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, uimarishaji wa vyuo vya VETA na kukuza ujuzi kwa vijana ambapo shilingi bilioni 467.89 zimetolewa;
  • Serikali imegharamia utekelezaji wa miradi ya maji mijini na vijijini ambapo jumla ya shilingi bilioni 346.01 zimetolewa;
  • Serikali imelipa jumla ya shilingi bilioni 315.20 kwa ajili ya kukamilisha malipo ya awali ya ununuzi wa ndege mpya 3 (shilingi bilioni 85.6), uimarishaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (shilingi bilioni 14.67) na malipo ya mwisho ya ndege mbili aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na Havilland Dash 8-400 (shilingi bilioni 214.93);
  • Serikali imeendelea kutekeleza mradi wa kufua umeme unaotokana na nguvu za maji katika Mto Rufiji ambapo shilingi bilioni 356.72 zimetolewa;
  • Serikali imeendelea kutekeleza Awamu ya Tatu ya Mradi wa Kupeleka Umeme Vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambapo jumla ya shilingi bilioni 280.95 zimetolewa;
  • Serikali imeendelea kugharamia elimumsingi bila ada ambapo zimetolewa shilingi bilioni 211.28;
  • Serikali imeendeleza ujenzi na ukarabati wa meli katika maziwa makuu ambapo zimetolewa shilingi bilioni 53.49;
  • Serikali imegharamia ujenzi na ukarabati wa hospitali za mikoa, vituo vya kutolea huduma za afya katika ngazi ya Halmashauri ambapo jumla ya shilingi bilioni 35.73 zimetolewa. Aidha, Serikali imetoa shilingi bilioni 9.10 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma ya nyumba 364 za walimu wa shule za msingi hasa kwenye maeneo yenye mazingira magumu; na
  • Serikali imegharamia shughuli za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo (Constituency Development Catalyst Fund – CDCF) ambapo shilingi bilioni 11.0 zimetolewa.
Ulipaji wa Malimbikizo ya Madai  
  1. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2020, Serikali imehakiki na kulipa madai ya wazabuni, wakandarasi na watumishi yenye jumla ya shilingi bilioni 734.99, sawa na asilimia 122.5 ya bajeti iliyotengwa. Kati ya kiasi hicho, wakandarasi wamelipwa shilingi bilioni 327.62, wazabuni shilingi bilioni 148.95, watumishi shilingi bilioni 103.69 na shilingi bilioni 154.73 kwa ajili ya watoa huduma na madeni mengineyo. Ulipaji huu wa madai umesaidia kuongeza ukwasi na hivyo kuongeza mzunguko wa fedha kwenye uchumi.
Tathmini ya Uhimilivu wa Deni la Taifa
  1. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia deni la Taifa kwa mujibu wa Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada Sura ya 134 kwa lengo la kuhakikisha linakuwa himilivu muda wote. Tathmini ya uhimilivu wa deni la Taifa iliyofanyika Desemba, 2019 ilibainisha kuwa deni ni himilivu kwa muda mfupi, wa kati na mrefu. Katika tathmini hiyo, viashiria vinavyopima uwezo wa nchi kukopa vinaonesha kuwa: Katika mwaka 2019/20, uwiano wa thamani ya sasa ya deni lote kwa Pato la Taifa ni asilimia 27.1 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 70; uwiano wa thamani ya sasa ya deni la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 16.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55; na uwiano wa thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 103.9 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 240.
  1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa viashiria vinavyopima uwezo wa nchi kulipa deni, matokeo yalibainisha kuwa, uwiano wa ulipaji wa deni la nje kwa mapato ya ndani ni asilimia 11.9 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 23 na uwiano wa ulipaji wa deni la nje kwa mapato yatokanayo na mauzo ya nje ni asilimia 11.9 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 21.
Mwenendo wa Sekta ya Fedha
  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka unaoishia Aprili 2020, viwango vya riba za mikopo ya benki kwa ujumla vilipungua hadi asilimia 16.91 kutoka wastani wa asilimia 17.25 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Aidha, riba za mikopo za kipindi cha mwaka mmoja zimepungua na kufikia wastani wa asilimia 16.37 kutoka asilimia 16.94. Pamoja na mafanikio hayo, bado viwango vya riba za mikopo vimeendelea kuwa juu kinyume na matarajio ya Serikali. Hivyo, Serikali imedhamiria kuweka msukumo zaidi katika usimamizi ili kuongeza kasi ya kushuka kwa viwango vya riba.
  1. Mheshimiwa Spika, ukwasi umeendelea kuwa juu ya kiwango cha kisheria cha asilimia 20 ya amana zinazoweza kubadilishwa kwa muda mfupi kuwa fedha taslimu (Demand liabilities) na kufikia asilimia 32.7 mwezi Aprili 2020. Aidha, ubora wa rasilimali za sekta ya benki umebaki kama ulivyokuwa mwaka 2019. Uwiano wa mikopo chechefu na mikopo yote umepungua kwa kiasi kidogo kutoka asilimia 11.10 ya mikopo yote mwezi Aprili 2019 hadi asilimia 11.04 Aprili 2020. Vile vile, mikopo kwa sekta binafsi imekua kwa asilimia 5.8 Aprili 2020 na kufikia shilingi trilioni 19.7 kutoka shilingi trilioni 18.6 Aprili 2019. Ukuaji huo unaenda sambamba na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kuongeza ukwasi kwenye uchumi, na utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuboresha mazingira ya biashara nchini.

  1. MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO
  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka minne na miezi saba ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, yapo mafanikio mengi yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa Ilani ya CCM Kwa Ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 pamoja na ahadi alizotoa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mafanikio makubwa ya kujivunia yamepatikana katika nyanja mbalimbali hususan uchumi, miundombinu, huduma za kijamii, madini na udhibiti wa rasilimali za Taifa, ardhi na mazingira na utawala bora.
Uchumi
  1. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika hotuba yangu kuhusu hali ya uchumi leo asubuhi, Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani mwaka 2015, ukuaji wa Pato la Taifa ulikuwa asilimia 6.2. Katika kipindi cha utawala wa Rais Magufuli, ukuaji wa Pato la Taifa uliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 6.9. Ukuaji huu umetokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ya kiuchumi (ujenzi, uchukuzi na nishati) na ugharamiaji wa huduma za jamii (afya, elimu na maji). Mwenendo mzuri wa ukuaji wa Pato la Taifa umeiwezesha nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi kumi (10) za bara la Afrika zenye uchumi mkubwa zaidi (10 largest economies in Africa) na hii ni kwa mujibu wa taarifa ya IMF (2019). Aidha, ukuaji wa uchumi wa Taifa umewezesha kuongezeka kwa mapato ya Serikali na uwezo wa Serikali kugharamia miradi ya maendeleo, kuboresha huduma za kijamii na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.
  1. Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei uliendelea kuwa tulivu na kubakia katika wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia 4.4 kwa kipindi chote cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano ambapo mwaka 2019, mfumuko wa bei ulifikia asilimia 3.4. Kiwango hiki ni cha chini kabisa kuwahi kutokea kwa kipindi cha nusu karne tangu mwaka 1970 tulipokuwa na mfumuko wa bei wa asilimia 2.4. Kudhibitiwa kwa mfumuko wa bei kumetokana na usimamizi madhubuti wa sera za fedha na bajeti, kuimarika kwa bei za mafuta pamoja na upatikanaji wa chakula katika masoko ya ndani na nchi jirani. Aidha, mwenendo huu mzuri wa mfumuko wa bei umesaidia kupunguza kasi ya kupanda kwa gharama za maisha kwa wananchi na ni kiashiria kizuri cha kuvutia uwekezaji nchini.
  1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20 akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha na kukidhi mahitaji ya kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi. Hadi Aprili 2020, akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 5.3. Kiasi hiki kinatosheleza mahitaji ya fedha za kigeni za kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 6.1 ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 4.4 kilichotosheleza mahitaji ya fedha za kigeni za kuagiza bidhaa na huduma kwa kipindi cha miezi 4.3 kwa kipindi kama hicho mwaka 2015. Ongezeko hili lilitokana na kuongezeka kwa uwekezaji wa kigeni na mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi. Aidha, kiwango cha akiba ya fedha za kigeni kilichofikiwa ni zaidi ya lengo la kuwa na akiba ya kutosha kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa muda wa miezi 4.0 na pia ni juu ya lengo la miezi 4.5 lililowekwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na lengo la miezi isiyopungua 6.0 kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika – SADC.
Mapato
  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, mapato ya ndani yameongezeka kufikia shilingi trilioni 18.5 mwaka 2018/19 kutoka shilingi trilioni 11.0 mwaka 2014/15, sawa na ongezeko la asilimia 69.1. Wastani wa mapato ya kodi kwa mwezi umeongezeka kutoka shilingi bilioni 825 mwaka 2014/15 hadi wastani wa shilingi trilioni 1.3 mwaka 2018/19 na kuongezeka zaidi hadi wastani wa shilingi trilioni 1.5 kwa mwezi katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020. Aidha, mapato ya kodi yameongezeka kutoka shilingi trilioni 9.9 mwaka 2014/15 hadi shilingi trilioni 15.5 mwaka 2018/19, sawa na ongezeko la asilimia 56.5. Vile vile, mapato yasiyo ya kodi yameongezeka kutoka shilingi bilioni 688.7 mwaka 2014/15 hadi shilingi trilioni 2.4 mwaka 2018/19 na shilingi trilioni 2.25 katika kipindi cha miezi kumi ya kwanza ya mwaka 2019/20. Kama nilivyoeleza awali, ongezeko la mapato limetokana na juhudi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kudhibiti upotevu wa mapato kwa kuimarisha usimamizi wa Sheria za kodi na matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika ukusanyaji wa mapato.
Mifumo ya kielektroniki
  1. Mheshimiwa Spika, Sera za Mapato na Matumizi za Serikali ya Awamu ya tano zinalenga kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma. Katika kutekeleza sera hizo, Serikali imejenga na kuimarisha mifumo mbalimbali ikiwemo mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato (Government e-Payment Gateway System-GePGs), Mfumo wa Usimamizi wa Utoaji wa Risiti za Kielektroniki za Kodi (Electronic Fiscal Device Management System-EFDMS), Mfumo Jumuishi wa Forodha (Tanzania Customs Intergrated System-TANCIS), Mfumo wa Ulipaji Serikalini (MUSE), Mfumo wa Usimamizi wa Mali za Serikali (Government Assets Management Information System-GAMIS), Mfumo wa Serikali wa Malipo ya Mishahara (Government Salary Payment Platform-GSPP), Mfumo wa Ununuzi Serikalini (Tanzanian National e-Procurement System-TANePS) na Mfumo wa Akaunti Jumuifu ya Hazina (Treasury Single Account-TSA).
  1. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla mifumo hii imeleta manufaa yafuatayo:
  • Kudhibiti upotevu wa mapato na kurahisisha upatikanaji wa taarifa za makusanyo kwa wakati pamoja na kuwarahisishia wananchi kulipia huduma mbalimbali za Serikali;
  • Kurahisisha uandaaji wa Hesabu za Serikali;
  • Kuongeza ufanisi katika usimamizi na udhibiti wa mali za Serikali;
  • Kuimarisha usimamizi na ulipaji wa mishahara kwa watumishi wanaostahili na kwa wakati;
  • Kuongeza uwazi katika taratibu za ununuzi na kuiwezesha Serikali kupata thamani halisi ya fedha zinazotumika katika ununuzi wa bidhaa, huduma na kazi za ujenzi; na
  • Kuimarisha ukwasi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, hivyo kurahisisha utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Serikali.
  1. Mheshimiwa Spika, jambo la kujivunia ni kuwa, mifumo yote hii imejengwa na inasimamiwa na wataalamu wa ndani wa Serikali na hivyo kuokoa fedha zilizokuwa zinatumika awali kulipia gharama za ujenzi na uendeshaji wa mifumo ya kielektroniki.
Ulipaji wa Madai
  1. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kulipa madai ya wakandarasi, wazabuni, watoa huduma na watumishi. Tangu Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli iingie madarakani hadi Aprili, 2020 Serikali imelipa madai mbalimbali yenye jumla ya shilingi trilioni 3.2. Vile vile, Serikali imelipa madai ya kimshahara ya watumishi wa Umma ya jumla ya shilingi bilioni 114.5. Azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuendelea kuhakiki na kulipa madai yote ya watoa huduma, wazabuni, wakandarasi na watumishi kwa lengo la kuchochea shughuli za kiuchumi na kudhibiti madai hewa bila kuathiri mitaji na utendaji kazi katika sekta binafsi.
Huduma za Jamii
  1. Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu, Serikali imechukua hatua madhubuti katika kuboresha upatikanaji wa huduma za jamii kwa wananchi zikiwemo afya, elimu na maji katika maeneo ya mijini na vijijini.
  1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa uboreshaji wa huduma za afya mafanikio yaliyopatikana katika awamu hii ya uongozi hadi Aprili 2020 ni pamoja na: kuboresha miundombinu ya afya kwa kujenga zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za Halmashauri za Wilaya 71, hospitali za rufaa za Mikoa 10 na hospitali za rufaa za kanda tatu (3); kuongezeka kwa bajeti ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015 hadi bilioni 269 mwaka 2019; na kuimarika kwa upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kufikia asilimia 94.4 mwaka 2019/20 kutoka asilimia 36 mwaka 2014/15. Aidha, kuimarika kwa huduma za afya nchini kumesaidia kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa za matibabu kwenda nje ya nchi kwa asilimia 95 na kuokoa takribani shilingi bilioni 20 ambazo zingetumika kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi.
  1. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua katika kuboresha upatikanaji wa huduma za maji safi na salama mijini na vijijini ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Mfuko wa Maji ambapo katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, kiwango cha upatikanaji wa maji vijijini kimeongezeka kufikia asilimia 70.1 na mijini asilimia 84. Aidha, Serikali imejenga na kukarabati miundombinu ya maji 1,423 ambapo miradi 1,268 ni ya vijijini na 155 ni ya mijini. Utekelezaji wa miradi ya maji imegharimu jumla ya shilingi trilioni 1.55 kati ya mwaka 2015/16 hadi Aprili 2020. Kuongozeka kwa kiwango cha upatikanaji maji nchini kumeokoa muda ambao wananchi hususan wanawake walikuwa wakiutumia kutafuta maji na kwa sasa wanautumia katika shughuli za uzalishaji mali ikijumuisha kilimo na biashara. Vile vile, upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijjini umepunguza kiwango cha maradhi kwa wananchi, hivyo kuokoa gharama za matibabu na kuimarisha nguvu kazi kuwa yenye afya bora na tija.
  1. Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana katika eneo la elimu ni pamoja na: Kugharamia elimumsingi bila ada ambapo jumla ya shilingi trilioni 1.03 zilitumika kati ya mwaka 2015/16 hadi 2019/20; kugharamia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ikiwemo madarasa, maabara, maktaba na mabweni; kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi na wahitimu wa kidato cha nne kutoka asilimia 67.8 na asilimia 67.9 mwaka 2015 hadi asilimia 81.5 na asilimia 80.6 mwaka 2019 mtawalia; uimarishaji wa vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi; na kuimarisha upatikanaji wa elimu ya juu kwa kutoa ruzuku kwa vyuo vya elimu ya juu na mikopo kwa wanafunzi. Mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu iliongezeka kutoka shilingi bilioni 348.7 mwaka 2014/15 hadi shilingi bilioni 450 mwaka 2019/20. Jumla ya shilingi trilioni 2.20 zimetumika kugharamia mikopo katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020, hivyo kuwezesha wanafunzi wengi zaidi kutoka familia zenye kipato cha chini kupata elimu ya juu. Jitihada hizi za Serikali zimesaidia kupunguza mzigo kwa wananchi kugharamia huduma za elimu, kuongezeka kwa uandikishaji, udahili na ufaulu wa wanafunzi katika ngazi zote za elimu.
Miundombinu ya Ujenzi, Uchukuzi na Nishati
Ujenzi
  1. Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana katika eneo la ujenzi ni: Kuendelea na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zikiwemo barabara kuu, barabara za mikoa na za wilaya ambapo kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi Aprili 2020, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa km 2,624.27 umekamilika; ujenzi wa daraja la juu la Mfugale (Dar es Salaam), daraja la Furahisha (Mwanza) na daraja la Magufuli (mto Kilombero) umekamilika; ujenzi wa barabara kuu kwa kiwango cha lami zenye urefu wa km 1,298.44 unaendelea; ujenzi wa barabara ya pete (Ubungo interchange) umefikia asilimia 77; ujenzi wa barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha (km 19.2) umefikia asilimia 80; Aidha, ujenzi unaendelea kwa daraja la New Selander (Dar es Salaam) lenye urefu wa km 1.03 pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa km 5.2 na umefikia asilimia 38.2, daraja la Kigongo hadi Busisi (Mwanza) lenye urefu wa km 3.2, daraja jipya mto Wami katika barabara ya Chalinze hadi Segera litakalokuwa na urefu wa m 513.5 pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa km 4.3 umefikia asilimia 39 na daraja la Ruhuhu (Ruvuma) umefikia asilimia 86. Miradi ya ujenzi wa barabara, madaraja na vivuko imegharimu jumla ya shilingi trilioni 7.63 kati ya mwaka 2015/16 hadi Aprili 2020. Kati ya kiasi hicho, ujenzi wa barabara umegharimu shilingi trilioni 6.4 fedha za ndani na shilingi trilioni 1.02 fedha za nje, ujenzi wa madaraja shilingi bilioni 205.0 na ujenzi wa vivuko shilingi bilioni 20.1. Utekelezaji wa miradi hii umechochea shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuwawezesha wananchi kupata huduma za jamii kama vile shule na zahanati na kutoa fursa mbalimbali za ajira. Aidha, miradi iliyokamilika imepunguza muda uliokuwa unatumiwa na wananchi kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
  1. Mheshimiwa Spika, hatua iliyofikiwa katika uboreshaji wa huduma za Bandari ni pamoja na: kukamilika kwa uboreshaji wa gati namba moja hadi nne na gati la kupakia na kupakua magari (Ro-Ro) na uwekaji wa Mfumo Jumuishi wa Ulinzi wa Bandari (Intergrated Port Security) na ufungaji wa mashine za kukagua mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam ambao umegharimu jumla ya dola za Marekani milioni 113.9; ujenzi wa gati lenye urefu wa m 300 katika bandari ya Mtwara; ukarabati wa maghala na gati namba moja na mbili katika Bandari ya Tanga; kukamilika kwa uongezaji wa kina cha bandari ya Tanga; na ujenzi na ukarabati wa magati ya Lushamba, Ntama, Nyamirembe, Magarine na gati la majahazi Mwigobero katika mwambao wa Ziwa Viktoria; magati ya Kagunga, Sibwesa, Kabwe, Lagosa na Kibirizi katika mwambao wa Ziwa Tanganyika na gati la Ndumbi kule Ziwa Nyasa. Ukarabati huu umewezesha meli kubwa kuingia na kutoka katika bandari zetu kwa ajili ya kushusha na kupakia mizigo. Aidha, umeongeza ukusanyaji wa mapato kwa kupunguza ukwepaji wa kodi.
  1. Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine yaliyopatikana ni: Kuendelea na ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria na ujenzi wa chelezo; ukarabati wa meli ya MV Victoria na MV Butiama ambapo katika kipindi cha mwaka 2015/16 hadi Aprili, 2020 jumla ya shilingi bilioni 111.7 zimetumika. Vile vile, Serikali imekamilisha ujenzi wa meli moja mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo katika Ziwa Nyasa; ujenzi wa vivuko vya MV Kigamboni, MV Utete, kivuko cha Kigongo – Busisi, kivuko cha MV Sengerema, kivuko cha Nyamisati kwenda Mafia; na ukarabati wa meli ya mafuta ya MT Sangara katika Ziwa Tanganyika.
Uchukuzi
  1. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha miundombinu ya uchukuzi, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: Kuanza ujenzi wa mradi wa kihistoria wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway) kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro (km 300) na kipande cha Morogoro hadi Makutupora (km 422) ambapo jumla ya shilingi bilioni 170 na dola za Marekani bilioni 1.5 zimetumika hadi sasa. Utekelezaji wa mradi huu umewezesha kupatikana kwa ajira 13,177 kwa wananchi na ushiriki wa wakandarasi wa ndani 640. Mafanikio mengine yaliyopatikana katika eneo la reli ni: kurejesha huduma ya kusafirisha shehena za mizigo kwa njia ya reli kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda Uganda; Kukamilisha ukarabati wa reli ya Dar es Salaam hadi Moshi (km 558.8) na kuanza kutumika; kukamilisha ukarabati wa reli ya Tanga hadi Korogwe (km 84); ukarabati wa reli ya Moshi hadi Arusha (Km 86) ili kuipandisha uwezo kutoka ratili 45 hadi ratili 60 umefikia km 42 sawa na asilimia 48.8; na ukarabati wa reli ya Dar es Salaam hadi Kilosa (Km 283) na Kilosa hadi Isaka (Km 687) unaendelea.
  1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa usafiri wa anga, mafanikio yaliyopatikana ni: Kuimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kununua ndege mpya 11 ambapo hadi Aprili, 2020 ndege nane (8) mpya zenye thamani ya shilingi trilioni 1.27 zimepokelewa na kuanza kutoa huduma katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi; kukamilisha malipo ya awali ya shilingi bilioni 85.7 kwa ajili ya ununuzi wa ndege nyingine mpya tatu (3); na kukamilika na kuanza kutumika kwa Jengo la Tatu la Abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) ambalo liligharimu takribani shilingi bilioni 722.1. Jengo hilo lina uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka. Aidha, ufungaji wa rada tatu za kuongozea ndege za kiraia katika viwanja vya ndege vya JNIA, KIA, na Mwanza umekamilika; ukarabati wa viwanja vya ndege vya Kilimanjaro na Dodoma umekamilika na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya baadhi ya mikoa upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ambavyo vyote kwa pamoja vimegharimu kiasi cha shilingi bilioni 445.9.
Nishati
  1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya nishati, baadhi ya mafanikio ni: Kuanza ujenzi wa mradi wa kihistoria wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2,115) katika mto Rufiji ambao hadi sasa umegharimu kiasi cha shilingi trilioni 1.42; kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kufua umeme ya Kinyerezi I – Extension (MW 185) na Kinyerezi II (MW 240) ambayo kwa pamoja imegharimu shilingi trilioni 1.22; kuendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya usafirishaji umeme ya North – West Grid Extension kV 400 (Mbeya – Sumbawanga- Mpanda – Kigoma – Nyakanazi), kV 220 (Makambako – Songea), kV 400 (Singida – Arusha – Namanga), kV 400 (Rufiji – Chalinze – Kinyerezi na Chalinze – Dodoma), kV 220 (Rusumo – Nyakanazi), kV 220 (Geita – Nyakanazi) na kV 220 (Bulyanhulu – Geita).
  1. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme vijijini, Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambapo hadi Aprili 2020 jumla ya vijiji 9,112 kati ya 12,268 vya Tanzania Bara vimeunganishwa na umeme kutoka vijiji 2,118 mwaka 2015. Gharama zilizotumika katika utekelezaji wa mradi huu kuanzia mwaka 2015/16 hadi Aprili 2020 ni shilingi trilioni 2.27. Utekelezaji wa miradi hii umenufaisha wananchi vijijini na pia taasisi 11,128 zikiwemo za elimu, afya, maji na dini, pamoja na huduma za biashara.
  1. Mheshimiwa Spika, napenda nisisitize kuwa miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu wezeshi katika sekta za ujenzi, uchukuzi na nishati niliyoeleza italiwezesha Taifa letu kuwa na uchumi imara wenye kuhimili ushindani. Aidha, miradi hii imekuwa chanzo cha ajira kwa Watanzania na kuwasaidia kujiongezea kipato. Vile vile, miradi hii itaongeza ufanisi wa upatikanaji wa huduma na kuchochea ukuaji wa miji na sekta nyingine kama vile kilimo, viwanda, utalii na biashara na kupanua wigo wa mapato ya Serikali.
Madini
  1. Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya madini ni pamoja na: Kuongezeka kwa maduhuli yatokanayo na madini kutoka shilingi bilioni 196.0 kwa mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 470.0 kwa kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili, 2020; marekebisho ya sheria na mikataba ya uwekezaji na hivyo kuanzishwa kwa Kampuni mpya ya Twiga Minerals Corporation Limited inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali (hisa asilimia 16) na Kampuni ya Barrick (hisa asilimia 84); na malipo ya fidia ya dola za kimarekani milioni 100 sawa na shilingi bilioni 250 kutoka Kampuni ya Barrick ikiwa ni sehemu ya kwanza ya kiasi cha makubaliano ya awali ya kulipa fidia ya dola milioni 300 sawa na shilingi bilioni 750. Aidha, marekebisho ya sheria yamewezesha kuanza majadiliano baina ya Serikali na makampuni yote makubwa ya madini kwa lengo la kupata asilimia 16 ya hisa kwa Serikali. Vile vile, Serikali imefanikiwa kuanzisha masoko 28 na vituo 25 vya ununuzi wa madini nchini; imekamilisha ujenzi wa vituo vinne (4) vya umahiri kule Bukoba, Handeni, Bariadi, na Musoma; kukamilika kwa ujenzi wa viwanda 2 vya mfano vya kuchenjua dhahabu vya Lwamgasa na Katente; na kukamilika kwa ujenzi wa one stop center Mirerani, kuimarika kwa udhibiti wa madini na kupungua kwa utoroshaji madini hasa kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa ukuta wenye mzingo wa kilomita 24.5 kuzunguka mgodi wa madini ya Tanzanite, Mirerani.
Mazingira ya Biashara na Uwekezaji
  1. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini (The Government Roadmap for Improvement of Business and Investment Climate) na Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara (Blue Print for regulatory Reform to Improve Business Environment) kwa lengo la kuhakikisha vikwazo na kero mbalimbali za biashara na uwekezaji zinaondolewa ili kuvutia uwekezaji zaidi nchini. Utekelezaji wa programu hizo umewezesha: Kufutwa kwa takribani tozo 114 katika Sekta za Kilimo, mifugo na uvuvi kwa mwaka 2017/2018, kufutwa kwa tozo tano (5) zilizokuwa zinatozwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi, na tozo 54 katika sekta mbalimbali mwaka 2018/19; kuanzishwa kwa vituo vya utoaji huduma kwa pamoja mpakani (One Stop Border Posts-OSBPs) katika mipaka ya Tanzania na nchi jirani ambavyo vimeimarisha biashara baina ya Tanzania na nchi hizo; kuanzishwa kwa One stop Service Centres ambazo zimewezesha utoaji wa huduma kwa wateja kwa uharaka zaidi; na kuhuishwa kwa majukumu ya Shirika la Viwango (TBS) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (zamani ikiitwa Mamlaka ya Chakula na Dawa) ambazo zilikuwa na majukumu yanayoingiliana. Utekelezaji wa hatua hizo umewezesha mazingira ya biashara nchini kuimarika. Na hii imedhihirishwa na Taarifa ya Benki ya Dunia ya Wepesi wa Kufanya Biashara (Ease of Doing Business Report) ya mwaka 2020 inayoonesha Tanzania imepanda kwa nafasi 3 kufikia nafasi ya 141 kutoka nafasi ya 144 mwaka 2019.
Viwanda
  1. Mheshimiwa Spika, sekta ya viwanda imeendelea kukua kwa kipindi chote cha awamu ya kwanza ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano ambapo hadi Aprili 2020 jumla ya viwanda vipya 8,477 vimeanzishwa katika maeneo mbalimbali nchini na hivyo kuwezesha ongezeko la ajira 482,601 viwandani. Ongezeko hilo la viwanda ambalo pia lilienda sambamba na ongezeko la uwezo wa uzalishaji, limeongeza utoshelevu wa bidhaa nchini. Mathalani, uwezo wa uzalishaji wa saruji umeongezeka kutoka tani milioni 4.7 mwaka 2015 hadi tani milioni 9.1 mwaka 2019. Aidha, uzalishaji halisi wa saruji umeongezeka kufikia tani milioni 6.5 mwaka 2019 ikilinganishwa na tani milioni 3.3 mwaka 2015. Mahitaji halisi ya saruji nchini yalikuwa tani milioni 4.8 mwaka 2019 na hivyo kuiwezesha nchi kukidhi mahitaji ya ndani na kuuza ziada nje ya nchi. Viwanda 16 vya nondo kati ya 25 vilivyoko nchini vina uwezo wa kuzalisha nondo tani milioni 1.083 kwa mwaka ikilinganishwa na mahitaji ya tani 295,000 kwa mwaka. Vile vile, ongezeko la viwanda limewezesha upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ambayo yanatumika kama malighafi viwandani na upatikanaji wa bidhaa muhimu kwa mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
Kilimo, Mifugo na Uvuvi
  1. Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Kilimo ni pamoja na: Kuongezeka kwa eneo la umwagiliaji kutoka hekta 461,326 mwaka 2015 hadi hekta 694,715 mwaka 2020; kuongezeka kwa uwezo wa kuhifadhi mazao ya chakula kwa Taasisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania (CPB) umeongezeka kutoka tani 371,000 mwaka 2015 hadi tani 621,000 mwaka 2020; kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao makuu ya biashara kutoka tani 796,502 mwaka 2015/2016 hadi tani 1,144,631 mwaka 2018/2019; kuongezeka kwa thamani ya mauzo ya mazao ya bustani yakiwemo mbogamboga na maua nje ya nchi kutoka Dola za Marekani milioni 412 mwaka 2015 hadi Dola za Marekani milioni 779 mwaka 2018/2019; na kuanzishwa kwa Bima ya Mazao yenye lengo la kumsadia mkulima kujikinga na athari za majanga ya asili na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kupata dhamana ya mikopo.
  1. Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya mifugo ni pamoja na: Kuongezeka kwa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho kufikia hekta milioni 2.82 Aprili 2020 kutoka hekta milioni4 mwaka 2015. Ongezeko hili limewezesha kupungua kwa migogoro ya ardhi baina ya wafugaji na wakulima nchini. Aidha, sekta ya mifugo ilifanikiwa kupata mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 22 kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo hakukuwa na mkopo kutoka TADB. Vile vile, ujenzi wa viwanda vya nyama vya Tan Choice Limited, Elia Foods Overseas Ltd, Binjiang Company Ltd na kiwanda cha kusindika maziwa cha Galaxy chenye uwezo wa kusindika lita 75,000 kwa siku umekamilika.
  1. Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya uvuvi ni pamoja na: Kuongezeka kwa mauzo ya samaki nje ya nchi kufikia wastani wa shilingi bilioni 692 kwa mwaka kutoka wastani wa shilingi bilioni 379; kuimarika kwa usimamizi na udhibiti wa rasilimali za uvuvi nchini; kuongezeka kwa samaki waliovuliwa kutoka tani 387,543 na kufikia tani 448,467; kuongezeka kwa wingi wa samaki aina ya Sangara kutoka tani 417,936 mwaka 2015 hadi kufikia tani 816,964 mwaka 2020; kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO); na kudhibiti uvuvi haramu kwa asilimia zaidi ya 80 katika maji baridi na asilimia 100 kwa uvuvi wa kutumia mabomu kwa ukanda wa pwani ya bahari. Aidha, Serikali imeendelea kuhamasisha uwekezaji katika tasnia ya ufugaji samaki na kufanikiwa kuongeza idadi ya wafugaji samaki kutoka 18,843 hadi 26,474 mwaka 2020.
Ardhi
  1. Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya ardhi ni pamoja na: Kupungua kwa migogoro ya ardhi; kuongezeka kwa kasi ya upimaji wa mashamba na viwanja; kujenga kituo cha Taifa cha Taarifa za Ardhi na kusimika mfumo unganishi wa kielektroniki wa kuhifadhi kumbukumbu za ardhi ambapo jumla ya kumbukumbu za majalada yenye taarifa 728,370 za usajili wa hati, upimaji na umilikishaji wa ardhi yamebadilishwa kutoka mfumo wa analojia na kuwa wa kidijitali zilizowezesha kuanza kutolewa kwa hati za kielektroniki; na kuimarishwa kwa huduma za ardhi kwa wananchi kwa kuanzisha Ofisi za Ardhi za Mikoa yote na kuimarisha ofisi za ardhi za halmashauri 185. Hatua hizi zimeimarisha usalama wa milki na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali ambapo mapato yanayotokana na ardhi yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 54.55 mwaka 2014/15 hadi kufikia wastani wa shilingi bilioni 100 mwaka 2019/20.
Utalii, Maliasili na Mazingira
  1. Mheshimiwa Spika, baadhi ya mafanikio katika maeneo hayo ni pamoja na kuanzishwa na kupandishwa hadhi maeneo ya hifadhi ya wanyamapori, misitu na nyuki ili kuimarisha uhifadhi na kuendeleza utalii kutoka hifadhi 15 mwaka 2015 hadi 22 mwaka 2020. Aidha, Serikali imeendelea kutoa elimu na miongozo mbalimbali kwa umma juu ya umuhimu wa hifadhi ya mazingira nchini kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Utawala bora, Ulinzi na Usalama
  1. Mheshimiwa Spika, juhudi zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na vitendo vya rushwa na biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini ikiwa ni pamoja na kuendelea kuimarisha TAKUKURU, kuanzishwa kwa mahakama ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi katika Mahakama Kuu na kuanzisha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya, zimeleta mafanikio makubwa kwa kuokoa fedha za umma, kuzuia uingizaji wa heroin na kemikali bashirifu (zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya), kuanzisha vituo vya kuhudumia walioathirika na dawa za kulevya, kuongeza nidhamu, uadilifu na uwajibikaji katika nyanja mbalimbali zikiwemo za utumishi wa umma, biashara, na kuongeza tija katika ukusanyaji mapato na matumizi ya fedha za umma. Taarifa ya utafiti wa taasisi ya kimataifa ya Transparency International ya mwaka 2019 imeonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 96 kati ya nchi 180 duniani ikilinganishwa na nafasi ya 119 ya mwaka 2015. Aidha, chini ya Serikali ya Awamu ya Tano, umoja, amani na usalama nchini vimeendelea kutamalaki na hivyo kutoa fursa kwa wananchi kuendelea kufanya kazi zao kwa utulivu. Aidha, Serikali imeendelea kuboresha makazi ya askari na maafisa wa vyombo vya ulinzi na usalama. Vile vile, chini ya Serikali ya Awamu ya Tano, muungano umeendelea kudumishwa na kuimarishwa na vyombo vya utoaji haki ikiwemo mahakama vimeendelea kuboreshwa ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya Waheshimiwa Majaji na watumishi wa sekta ya mahakama pamoja miundombinu ya mahakama.
Bunge
  1. Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua majukumu muhimu ya Bunge na hivyo ilihakikisha kwamba inaliwezesha ili liweze kutekeleza majukumu yake. Serikali imekuwa ikitoa kwa Bunge lako Tukufu taarifa zote muhimu zilizohitajika na kwa wakati na vile vile kuhakikisha kuwa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Bunge zinatolewa kwa wakati.
Hali ya Umaskini
  1. Mheshimiwa Spika, hali ya umaskini wa kipato na usio wa kipato iliendelea kupungua ambapo kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi (basic needs poverty) kimepungua kutoka asilima 28.2 mwaka 2011/12 hadi asilimia 26.4 mwaka 2017/18. Kiwango cha umaskini kimepungua katika maeneo yote ya mijini na vijijini ambapo katika maeneo ya mijini, umaskini ulipungua kutoka asilimia 21.7 hadi asilimia 15.8 na maeneo ya vijijini ulipungua kutoka asilimia 33.3 hadi asilimia 31.3. Aidha, kina cha umaskini (poverty depth) kilipungua kutoka asilimia 6.7 mwaka 2011/12 hadi asilimia 6.2 mwaka 2017/18 na ukali wa umaskini (poverty severity) ulipungua kutoka asilimia 2.3 hadi asilimia 2.1. Wastani wa matumizi ya kaya kwa mwezi yameongezeka kutoka shilingi 258,751 hadi shilingi 416,927.
  1. Mheshimiwa Spika, kupungua kwa umaskini kumetokana na juhudi kubwa zilizofanywa na Wananchi na Serikali yao kupambana na umaskini wa kipato na usio wa kipato. Juhudi za Serikali zinahusisha: uwekezaji katika miundombinu wezeshi kwa shughuli za uzalishaji mali na biashara ili kukuza uchumi na hatimaye kuongeza pato la wastani kwa kila Mtanzania; kusimamia na kuboresha sekta ya fedha; kuongeza upatikanaji wa huduma za msingi kama vile afya, elimu, maji na umeme hususan maeneo ya vijijini; na kuendelea kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya jamii (TASAF) ili kuongeza kipato chao na kuwawezesha kupata mahitaji ya msingi. Hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa TASAF III ni pamoja na: kutambuliwa na kuandikishwa kwa kaya takribani 1,084,018 zenye wanakaya 5,217,985 katika vijiji na mitaa 9,785 kwenye Halmashauri 159 Tanzania Bara na kaya 34,490 zenye wanakaya 196,301 katika shehia 204 za Zanzibar. Aidha, ruzuku ya fedha shilingi bilioni 968.73 imehawilishwa katika kaya hizo. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 935.94 ni kwa Tanzania Bara na shilingi bilioni 32.79 ni kwa Zanzibar. Kazi nyingine zilizofanyika ni pamoja na kutekeleza miradi 8,384 ambayo imezalisha ajira za muda kwa kaya 230,738 Tanzania Bara na kaya 14,555 katika miradi 251 kwa Zanzibar. Aidha, miradi 47 ya kuendeleza miundombinu katika sekta za elimu, afya na maji Tanzania Bara na miradi 8 katika sekta za elimu na afya kwa Zanzibar imekamilika.
  1. Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali, natoa pongezi kwa Watanzania wote (wafanyabiashara, wenye viwanda, wafanyakazi na wakulima) waliotikia wito wa Rais wetu wa kulipa kodi stahiki, jambo ambalo limepelekea kupatikana kwa mafanikio haya ya kishindo.

  • ATHARI ZA COVID–19 KIUCHUMI NA KIJAMII
  1. Mheshimiwa Spika, ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) ulianzia nchini China mwishoni mwa mwaka 2019 na kusambaa kwa kasi katika nchi mbalimbali duniani. COVID-19 sio janga la kiafya pekee kwa maana ya kusababisha vifo vya watu wengi na kuongeza mara dufu mahitaji ya sekta ya afya, bali ni janga la kiuchumi pia kwani limeambatana na kuvurugika kwa mfumo wa uzalishaji na uhitaji (disruption in supply and demand chain) duniani. Mataifa mengi yalikumbana na changamoto zifuatazo: kasi kubwa ya maambukizi kwa raia; vifo vya watu wengi; sekta ya afya kukabiliwa na jukumu la ziada la kuhudumia waathirika; na upungufu wa vifaa, dawa na watoa huduma za afya. Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limetabiri kuwa ukuaji wa uchumi wa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara (SSA) utaanguka kutoka makadirio ya awali ya asilimia 3.6 mwaka 2020 hadi asilimia hasi 1.6. Aidha, uchambuzi huo wa IMF unabashiri kuwa takribani asilimia 60 ya nchi za SSA zitakuwa na ukuaji hasi katika mwaka 2020 kutokana na athari za mlipuko wa COVID-19. Vile vile, nchi ambazo Uchumi wao unategemea zaidi utalii na zile zinazozalisha mafuta ndizo zinatabiriwa kuwa zitaathirika zaidi.
  1. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na janga hili, nchi mbalimbali duniani zimechukua hatua kadhaa zikiwemo kulazimisha wananchi wao kubaki majumbani (lockdown); kuzuia safari za ndege kuingia na kutoka; kuzuia mikusanyiko kama michezo na hata ibada; kufunga mipaka ya nchi; na kuweka udhibiti katika usafiri wa ndani. Hatua za kiuchumi zilizochukuliwa na Mataifa hayo ni pamoja na kupunguza kodi na gharama za ukopaji ili kusaidia biashara; kuahirisha malipo ya kodi hususan kodi ya mapato na kodi ya ongezeko la thamani; kutoa msaada wa kifedha kwa kaya maskini; na kusaidia kampuni na mashirika yaliyoathirika zaidi kupata mikopo, ruzuku na unafuu wa urejeshaji wa mikopo. Kwa upande wa sekta binafsi, baadhi ya makampuni yalifunga shughuli za uzalishaji/biashara na kupunguza wafanyakazi au mishahara.
  1. Mheshimiwa Spika, mataifa 20 tajiri duniani (G20) yalipendekeza kwa wakopeshaji (bilateral official creditors) kutoa unafuu wa madeni kwa mataifa maskini duniani ikiwemo Tanzania. Mpango huo unahusisha kuahirisha malipo ya madeni yanayoiva kwa kipindi kinachoanzia Mei hadi Desemba 2020 ili ahueni hiyo itumike kukabiliana na COVID-19 na kunusuru uchumi. Serikali imeshaanza mazungumzo na wakopeshaji ili kunufaika na hatua hiyo. Aidha, Serikali iko katika mazungumzo na taasisi mbalimbali za fedha za kimataifa ili kupata fedha za kukabiliana na COVID-19 na kutegemeza uchumi. Katika mazungumzo hayo, Serikali imepata msamaha wa madeni kupitia dirisha la Catastrophe Containment Relief Trust (CCRT) kiasi cha dola za Marekani milioni 14.3 ambao uliridhiwa na Bodi ya IMF jana tarehe 10 Juni, 2020. Kiasi hicho kinaweza kuongezeka hadi kufikia dola za Marekani milioni 25.7. Kwa niaba ya Serikali, napenda kutoa salamu zangu za shukrani kwao kwa hatua hii muhimu kwetu katika kukabiliana na athari za COVID-19. Taasisi nyingine ambazo Serikali inaendelea na mazungumzo nazo ni pamoja na: Benki ya Dunia kupitia Dirisha la Pandemic Emergency Financing Facility (PEF) kiasi cha dola za kimarekani milioni 3.98; Mfuko wa Ushirikiano na Maendeleo ya Uchumi (Economic Development Cooperation Fund – ECDF) kupitia Exim Bank ya Korea dola za Marekani 501,169; BADEA dola za Marekani milioni 1.7; msaada wa kibajeti kutoka Umoja wa Nchi za Ulaya kupitia dirisha la EU COVID-19 Response Package Euro milioni 27; na IMF ili kupata mkopo chini ya mpango wa Rapid Credit Facility (RCFambapo Serikali inaweza kukopa hadi Special Drawing Rights (SDR) milioni 198.9 sawa na takribani dola za Marekani milioni 272 kwa ajili ya kuimarisha urari wa malipo. Vile vile, Benki ya Maendeleo ya Afrika imeahidi kutoa mkopo wa kibajeti wenye masharti nafuu (concessional loan) wa dola za Marekani milioni 50 ambapo Serikali itapanga matumizi ya fedha hizo kwa mujibu wa vipaumbele vyake.
  1. Mheshimiwa Spika, tathmini ya kiuchumi iliyofanyika kwa kipindi cha Januari hadi Aprili 2020 inaonesha kuwa tofauti na nchi nyingi ambazo uchumi wao umeporomoka, kwa upande wa Tanzania athari za COVID-19 kwenye uchumi ni ndogo. Mwenendo huo umetokana kwa kiasi kikubwa na maono na ujasiri wa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alielekeza wananchi wake kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kujenga uchumi na kujipatia kipato lakini wakati huo huo wakiendelea kuzingatia maelekezo ya wataalam wa afya kujikinga na COVID-19, kushinda hofu ya ugonjwa huu na pia kumuomba mwenyezi Mungu. Kwa muhtasari, tathmini inaonesha kuwa kuna maeneo ambayo athari za COVID-19 ni kidogo au hazijajitokeza waziwazi katika kipindi cha marejeo. Maeneo ambayo hayakuathirika ni pamoja na:
  • Mapato ya ndani kwa ujumla yaliongezeka kwa asilimia 8.2 kwa kipindi cha Januari hadi Aprili 2020 kufikia shilingi trilioni 6.8 ikilinganishwa na makusanyo ya shilingi trilioni 6.3 kwa kipindi kama hicho mwaka 2019;
  • Uzalishaji wa mazao ya chakula umeendelea kuwa mzuri ambapo utoshelevu wa chakula nchini kwa mwaka 2019/20 umefikia asilimia 118;
  • Thamani ya mauzo ya dhahabu nje ya nchi iliongezeka mara mbili kufikia dola za Marekani milioni 631.0 Aprili 2020 kutoka dola milioni 323.4 Aprili 2019, kutokana na kuongezeka kwa mauzo na kupanda kwa bei kwenye soko la dunia;
  • Sekta ya benki imeendelea kuwa imara kwa viashiria muhimu vya mtaji, ubora wa mali, ukwasi na faida kwa kipindi kilichoishia Aprili, 2020. Kwa ujumla ukwasi wa benki umeendelea kuwa juu ya kiwango cha kisheria cha asilimia 20 ya amana zinazoweza kubadilishwa kwa muda mfupi kuwa fedha taslimu na kufikia asilimia 32.7 mwezi Aprili 2020.
  • Mikopo chechefu imepungua japo kwa kasi ndogo kutoka asilimia 11.10 Aprili, 2019 hadi asilimia 11.04 Aprili, 2020.
  • Akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 5.3 Aprili 2020, ambayo ilikuwa inatosha kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 6.1, ikilinganishwa na kiasi cha dola za Marekani bilioni 4.4 kilichokuwa kinatosha kuagiza bidhaa na huduma kwa miezi 4.3 mwaka 2019;
  • Mauzo katika Soko la Hisa la Dar es Salaam yameanza kuongezeka baada ya kuyumba katika kipindi cha mwezi Machi 2020 kutokana na kupungua kwa ushiriki wa wawekezaji wa kigeni kutokana na janga la COVID-19; na
  • Hali ya upatikanaji wa mafuta nchini kwa sasa ni nzuri. Nchi ina kiasi cha mafuta cha kutosha, yaani wastani wa siku 40 kwa aina zote za mafuta.
  1. Mheshimiwa Spika, mbali na athari za kiafya zinazojumuisha vifo, ugonjwa, ongezeko la mahitaji ya madaktari na watumishi wa afya, vituo vya kuhudumia wagonjwa na gharama za vifaa, vifaa tiba, dawa na vitendanishi, yapo maeneo mengine ambayo yamebainika kuwa yameathirika japo siyo athari zote zimetokana na COVID-19 Baadhi ya maeneo hayo ni yafuatayo:
  • Uchumi jumla: Tathmini ya awali ya Serikali inaonesha kuwa ukuaji wa uchumi wa Taifa utapungua kutoka makadirio ya awali ya asilimia 6.9 mwaka 2020 hadi asilimia 5.5 kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na athari za COVID-19 na mvua nyingi zilizopelekea mafuriko na uharibifu wa miundombinu ya usafirishaji na kuchelewa kwa utekelezaji wa baadhi ya miradi;
  • Usafiri wa anga na utalii: Jumla ya mashirika ya Kimataifa 21 ya ndege yalifuta safari 632 zilizopangwa kufanyika kuja hapa nchini kuanzia tarehe 20 Machi 2020. Hatua hii imesababisha kudorora kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi hususan biashara ya utalii na huduma husika kama usafirishaji wa watalii, malazi, chakula, vinywaji na burudani. Aidha, baadhi ya hoteli zilifungwa au kupunguza watumishi. Vile vile, nchi yetu ilifunga anga yake na kuzuia ndege kutua/kuruka. Mathalani, taasisi za sekta ya utalii ambazo ni Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Mamlaka ya Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania zimeathiriwa sana na ukosefu wa mapato kufuatia kuporomoka kwa utalii baada ya kusambaa kwa COVID-19 katika nchi zinazoleta watalii wengi nchini;
  • Uchukuzi na usafirishaji: Usafirishaji wa mizigo kwenda na kutoka nchi jirani (transit goods) ulipungua kufuatia baadhi ya nchi hizo kufunga mipaka na kudhibiti biashara mipakani;
  • Bei za bidhaa za mazao (pamba, korosho, kahawa na chai) katika soko la dunia imepungua kutokana na kupungua kwa mahitaji;
  • Michezo, sanaa na burudani: Serikali ilisitisha shughuli za michezo, sanaa na burudani kama sehemu ya hatua za kudhibiti misongamano ya watu kuepuka CORONA kusambaa kwa kasi;
  • Biashara: Biashara za jumla na rejareja zilipungua hususan zile zilizohusu bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi kama China, India na baadhi ya nchi za Ulaya;
  • Mapato ya Serikali: Mapato ya kodi na maduhuli kutoka katika sekta zilizoathirika zaidi na COVID-19 yalipungua hususan mapato ya sekta ya utalii, tozo/ada za Visa, kodi zinazolipwa na hoteli, ada za viingilio kwenye viwanja vya michezo na maeneo ya sanaa na burudani; na
  • Mikopo kwa sekta binafsi: Kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi imepungua kutoka asilimia 10.6 kwa mwaka ulioishia Aprili 2019 hadi asilimia 5.8 mwaka ulioishia Aprili 2020.
  1. Mheshimiwa Spika, hatua zilizochukuliwa awali na Serikali kukabiliana na COVID-19 ilikuwa ni pamoja na: kusitisha masomo katika ngazi zote za elimu ili kudhibiti kasi ya maambukizi. Hata hivyo, walimu katika shule za Serikali na vyuo waliendelea kulipwa mishahara kama kawaida; kudhibiti safari zisizo za lazima; kusambaza vifaa na vifaa tiba katika maeneo mbalimbali nchini vikiwemo vipima joto, magari ya kubeba wagonjwa na mavazi maalum ya kujikinga yanayotumiwa na madaktari na wahudumu wa afya; Kutoa elimu kwa jamii juu ya dalili na namna ya kujikinga na COVID-19; kujenga na kuimarisha maeneo maalum ya kutenga na kutibu wagonjwa; na kuahirisha baadhi ya matumizi yaliyopangwa katika bajeti ya 2019/20 hususan gharama za safari na mafunzo ya nje ya nchi na maadhimisho ya sherehe za kitaifa na kuelekeza fedha hizo kwenye mapambano dhidi ya COVID-19.
  1. Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa jumla ya shilingi bilioni 19.5 hadi mwezi Mei 2020 kwa ajili ya kukabiliana na COVID-19. Kati ya hizo, shilingi milioni 500 zilizokuwa zitumike katika sherehe za Muungano zilielekezwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na shilingi bilioni 14.3 ni fedha zilizotokana na Global Fund ambazo awali zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya mradi wa Malaria, Kifua Kikuu na UKIMWI. Aidha, Wadau mbalimbali wameendelea kushiriki mapambano dhidi ya COVID-19 kwa kutoa michango ya fedha na vifaa. Hadi mwezi Mei 2020, wadau mbalimbali walichangia kupitia Mfuko wa Maafa jumla ya shilingi bilioni 3.4 na pia Serikali ilipokea vifaa na vifaa tiba kwa ajili ya kujilinda na kujikinga na maambukizi ya COVID-19 vyenye thamani ya shilingi bilioni 3.3. Serikali inawashukuru kwa dhati wadau wote wa ndani na nje waliochangia fedha na vifaa hivyo kusaidia katika mapambano dhidi ya COVID-19.
  1. Mheshimiwa Spika, katika mapambano hayo, kipaumbele cha kwanza cha Serikali kilikuwa ni kukinga watoa huduma za afya pamoja na wananchi kwa ujumla wasiathirike na janga la COVID-19. Hivyo, mikakati ya Serikali ya kukabiliana na athari za ugonjwa huu kwa upande wa sekta ya afya ni pamoja na: kugharamia upatikanaji wa mahitaji ya msingi kwa watoa huduma za afya; kuongeza idadi ya madaktari na watoa huduma wa afya; kuhamasisha matumizi ya tiba asili badala ya kutegemea tiba za kisasa pekee pamoja na kuimarisha taasisi za uchunguzi na utafiti wa tiba/dawa asili. Aidha, Serikali imefungua maabara mpya yenye mashine tano (5) zenye uwezo wa kupima sampuli 1,800 kwa siku na kutoa ajira za watumishi wa sekta ya afya elfu moja (1,000).
Mikakati ya Kutegemeza Uchumi
  1. Mheshimiwa Spika, kufuatia tathmini iliyofanyika ya athari zinazotokana na COVID-19 na kufuatilia mwenendo wa maambukizi nchini, Serikali imechukua hatua zifuatazo kwa lengo la kutegemeza uchumi na kusaidia sekta zilizopata athari zaidi:
  • Kutoa unafuu wa kodi kama nitakavyoeleza hivi punde katika sehemu ya maboresho ya kodi ya hotuba hii. Lengo ni kuwezesha upatikanaji vifaa, vifaa tiba, dawa na vitendanishi kwa gharama nafuu na kuhamasisha uzalishaji wa vifaa hivyo na bidhaa nyingine hapa nchini;
  • Kuingia makubaliano maalum na baadhi ya mashirika ya ndege ili kukodi ndege kwa ajili ya kusafirisha maua, mbogamboga na minofu ya samaki nje ya nchi moja kwa moja kutoka Tanzania (Uwanja wa ndege wa Mwanza na KIA);
  • Kugharamia mahitaji ya Taasisi za sekta ya utalii za Shirika la Hifadhi ya Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ambazo ziliathiriwa na COVID-19 pamoja na uharibifu wa miundombinu ya uhifadhi na utalii kutokana na mvua. Taasisi hizo zitapatiwa fedha za uendeshaji kupitia bajeti ya Serikali kwa ajili ya kulipa mishahara ya watumishi, matumizi mengineyo na matumizi ya maendeleo;
  • Kufungua rasmi anga ya Tanzania na kuruhusu ndege zote za kibiashara, misaada, diplomasia na za dharura kuweza kutua na kuruka kama ilivyokuwa hapo awali;
  • Kufungua na kutangaza sekta ya utalii na kutoa mwongozo wa utalii ambapo tayari watalii wameanza kuingia nchini kwa ndege binafsi na kwa kupitia baadhi ya kampuni za ndege;
  • Kuongeza kasi ya kulipa madeni na malimbikizo ya madai ya makandarasi, watumishi, wazabuni na watoa huduma ambapo kiasi cha shilingi trilioni 1.145 kililipwa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020. Kati ya kiasi hiki, shilingi bilioni 916.4 zililipwa mwezi Machi 2020. Vile vile, malipo ya marejesho ya kodi ya ongezeko la thamani yaliyolipwa hadi Aprili 2020 yalifikia shilingi bilioni 173.7 sawa na asilimia 148 ya lengo la kulipa shilingi bilioni 117.4 kwa kipindi hicho. Lengo la hatua hizi ni kuongeza mzunguko wa fedha katika uchumi ili kuwawezesha wakandarasi, wafanyabiashara na watoa huduma kuendelea kufanya biashara au kutoa huduma katika kipindi cha janga la COVID-19;
  • Kushusha kiwango cha riba kinachotozwa kwa benki kukopa Benki Kuu (discount rate) kutoka asilimia 7 hadi asilimia 5. Hatua hii inalenga kuongeza wigo wa benki kukopa kutoka Benki Kuu kwa riba nafuu kwa kutarajia benki nazo zitapunguza riba ya mikopo kwa wateja;
  • Kushusha kiwango cha chini cha kisheria cha sehemu ya amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu ya Tanzania (Statutory Minimum Reserve Requirement) kutoka asilimia 7 hadi asilimia 6. Hatua hii inatarajiwa kuongeza ukwasi katika sekta ya benki na hivyo kuwezesha benki kutoa mikopo kwa sekta binafsi;
  • Kuyataka makampuni yanayotoa huduma za fedha kwa njia ya mtandao kupunguza gharama za kufanya miamala kwa wateja ili kuongeza kiwango cha miamala kwa siku kwa mteja kutoka shilingi milioni 3.0 hadi shilingi milioni 5.0 na kiwango cha akiba kwa siku kwa mteja kutoka shilingi milioni 5.0 hadi shilingi milioni 10.0. Hatua hii inalenga kuhamasisha matumizi ya huduma za kifedha za kidigitali katika kufanya miamala mbalimbali na hivyo kupunguza ulazima wa wateja kwenda benki;
  • Serikali imeagiza benki na taasisi za fedha kutathmini kwa kina athari zinazotokana na mlipuko wa COVID-19 kwenye urejeshaji wa mikopo, kujadiliana (re-negotiation) na kukubaliana na wakopaji namna ya kurejesha mikopo na kutoa unafuu wa urejeshaji wa mikopo (loan rescheduling). Serikali kupitia Benki Kuu itatoa unafuu kwa benki na taasisi za fedha zitakazotoa unafuu katika urejeshwaji wa mikopo hiyo kwa kuzingatia uwazi na bila upendeleo. Katika hili, napenda kuzipongeza baadhi ya benki kama Exim ambazo tayari zimetangaza kuongeza muda wa urejeshaji wa mikopo ili kusaidia wateja wao katika sekta ambazo biashara zao zimeathiriwa na COVID-19 na naziomba benki nyingine zifuate mfano huo;
  • Taasisi za umma na binafsi zimesisitizwa kutumia mifumo ya kielektroniki katika kufanya shughuli mbalimbali kama vile mikutano kwa njia ya mtandao; ukusanyaji wa takwimu; mafunzo; miamala ya fedha; na mifumo ya huduma za afya;
  • Serikali itaimarisha zaidi Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na kuongeza wigo wa upatikanaji wa mikopo ya gharama nafuu kwa wajasiriamali wadogo na wa kati (SME financing) pamoja na kuhakikisha halmashauri zinatenga fedha asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kama Sheria inavyotaka;
  • Kufuatia kupungua kwa maambukizi ya COVID-19 nchini, Serikali imeruhusu vyuo na shule za sekondari (kwa wanafunzi wa kidato cha sita) zifunguliwe kuanzia tarehe 1 Juni 2020; na
  • Serikali imeruhusu shughuli zote za michezo kuanza tena kama ilivyokuwa awali.
Fursa Zilizojitokeza Kutokana na COVID-19
  1. Mheshimiwa Spika, pamoja na athari zilizojitokeza, zipo pia fursa kadhaa zilizoambatana na janga hili zikijumuisha: kuongezeka kwa matumizi ya njia za mtandao katika shughuli mbalimbali ikiwemo mikutano (pamoja na ya Bunge); miamala ya fedha kwa njia za kielektroniki; matumizi ya tiba asili; fursa za kuongeza uzalishaji viwandani na kuuza mazao ya chakula katika masoko ya kikanda; na kupungua kwa gharama za usafirishaji na uzalishaji viwandani kutokana na kuendelea kushuka kwa bei za mafuta. Aidha, janga hili limetupa fundisho la umuhimu wa kutumia mikakati inayoendana na mazingira yetu katika kukabiliana na majanga badala ya kuiga mikakati ya nchi nyingine. Vile vile, COVID-19 imetukumbusha umuhimu wa kuhakikisha kuwa tunajitosheleza kwa uzalishaji wa mahitaji ya bidhaa muhimu hapa nchini.
  1. Mheshimiwa Spika, licha ya athari za COVID-19 ambazo zimeonekana kwenye uchumi wa Taifa hadi sasa na hatua ambazo zimechukuliwa, napenda pamoja na mwenendo mzuri wa kupungua kwa COVID-19 nchini, nami niwaombe Watanzania kuendelea kuzingatia ushauri wa wataalam wetu wa afya kuhusu kujikinga na COVID-19. Aidha, niwahakikishie watanzania kwamba fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo kwa mwaka ujao wa fedha 2020/21 hazitapunguzwa kwa sababu ya COVID-19.

  1. SERA ZA BAJETI KWA MWAKA 2020/21
Shabaha za Uchumi Jumla
  1. Mheshimiwa Spika, huu ni mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP II) 2016/17-2020/21 wenye dhima ya “kujenga uchumi wa viwanda utakaochochea ajira na ustawi endelevu wa jamii”. Hivyo, bajeti hii imeandaliwa kwa kuzingatia lengo hilo kuu ambalo linaitaka Serikali iendelee kuimarisha mazingira wezeshi ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini. Hii ni pamoja na kuhakikisha miundombinu ya kiuchumi inaboreshwa, panakuwepo na sera rafiki za kikodi na fedha, mfumo rekebu mzuri, upatikanaji mzuri wa ardhi, vibali vya kazi na nguvu kazi yenye ujuzi pamoja na kuendelea kutilia mkazo nafasi muhimu ya kilimo katika ujenzi wa uchumi wa viwanda. Aidha, bajeti hii imeandaliwa kwa kuzingatia kwamba ni muhimu kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuwezesha ujenzi na ukarabati wa miundombinu, kuendelea kugharamia mahitaji mengine ya msingi na uendeshaji wa Serikali. Aidha, kama ilivyo kwa nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, dhima ya bajeti ya 2020/21 ni kuchochea ukuaji wa uchumi ili kulinda na kuboresha maisha ya wananchi, ajira na biashara pamoja na kufufua viwanda.
  1. Mheshimiwa Spika, maandalizi ya bajeti hii yamezingatia pia mazingira tuliyonayo hivi sasa ikiwemo athari za ugonjwa wa homa kali ya mapafu katika sekta mbalimbali na mvua nyingi ambazo zimeharibu miundombinu ya usafiri na usafirishaji mijini na vijijini na hata mazao kama vile zabibu. Licha ya athari hizo, bajeti hii imezingatia fursa zilizoibuka ikiwemo kushuka kwa bei za mafuta, kuongezeka kwa bei za dhahabu na mwanya wa kuzalisha vifaa na vifaa tiba katika viwanda vya ndani ili kukabiliana na COVID-19. Janga la COVID-19 pia limeilazimu bajeti hii kuweka msukumo zaidi kwenye utafiti upande wa dawa, virusi na maendeleo ya viwanda.
  1. Mheshimiwa Spika, ni wazi pia kwamba maandalizi ya bajeti hii yamezingatia kuwa mwaka huu 2020 ni mwaka wa uchaguzi mkuu. Hivyo, bajeti hii imetilia maanani umuhimu wa kuwezesha zoezi hili muhimu kibajeti kwa lengo la kuimarisha demokrasia na utawala bora nchini. Aidha, bajeti hii itaimarisha na kuendeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana upande wa huduma za jamii na miundombinu ya kiuchumi, hususan kuhakikisha kwamba miradi ya kitaifa ya kimkakati inaendelea kutekelezwa kama ilivyopangwa.
  1. Mheshimiwa Spika, kutokana na mambo ya msingi yaliyozingatiwa katika kuandaa bajeti hii kama nilivyoeleza hapo awali, shabaha za uchumi jumla katika kipindi cha mwaka 2020/21 ni kama ifuatavyo: –
  • Ukuaji wa Pato Halisi la Taifa unatarajiwa kupungua kutoka maoteo ya awali ya asilimia 6.9 na kufikia asilimia 5.5 mwaka 2020 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2019. Hii ni kutokana na mvua nyingi ambazo zimeharibu miundombinu ya usafirishaji nchini na athari za ugonjwa wa COVID–19 ulioenea katika nchi nyingi ambazo ni washirika wetu wakubwa wa kibiashara;
  • Mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja kati ya wastani wa asilimia 3 hadi 5 kwa mwaka 2020/21;
  • Mapato ya ndani yanakadiriwa kuwa asilimia 14.7 ya Pato la Taifa mwaka 2020/21 kutoka matarajio ya asilimia 14.0 mwaka 2019/20;
  • Mapato ya kodi yanatarajiwa kufikia asilimia 12.9 ya Pato la Taifa mwaka 2020/21 kutoka matarajio ya asilimia 12.1 mwaka 2019/20;
  • Matumizi ya Serikali yanatarajiwa kuwa asilimia 22.1 ya Pato la Taifa mwaka 2020/21;
  • Nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) inakadiriwa kuwa asilimia 2.6 ya Pato la Taifa mwaka 2020/21 ikiwa ni chini ya asilimia 3.0 iliyokubaliwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; na
  • Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne (4).
Sera na Mikakati ya Kuongeza Mapato
  1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21, Serikali itaendelea kuweka kipaumbele katika ukusanyaji wa mapato ya ndani. Masuala muhimu yatakayozingatiwa ni pamoja na kuimarisha zaidi usimamizi wa ukusanyaji wa mapato kwa kutekeleza hatua zifuatazo:
  • Kuendelea na utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuwianisha na kupunguza viwango vya kodi, tozo na ada mbalimbali;
  • Mamlaka ya Mapato Tanzania kuchukua hatua za kupanua wigo wa kodi na kujenga mahusiano na mazingira rafiki kwa mlipakodi;
  • Kuimarisha Ofisi ya Msajili wa Hazina na kuiwezesha kukusanya gawio na michango ya Mashirika kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali;
  • Kuwezesha na kuimarisha Baraza la Rufaa za Kodi (TRAT) na Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) kushughulikia pingamizi na rufaa za kodi kwa haraka;
  • Kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato; na
  • Kuhimiza matumizi ya mifumo ya TEHAMA ili kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.
  1. Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua hizo za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma ili kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kuwekeza kwenye Hatifungani na Dhamana za Serikali na kuorodhesha Hatifungani za Serikali katika Soko la Hisa la Dar es Salaam. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo (Development Cooperation Framework – DCF) ili kuwezesha upatikanaji wa misaada na mikopo ya masharti nafuu na kukopa kwa utaratibu wa udhamini kutoka taasisi za udhamini wa mikopo (Export Credit Agencies -ECA), ambayo masharti yake yana unafuu.
Sera za Matumizi
  1. Mheshimiwa Spika, Sera za Matumizi katika mwaka 2020/21 zitajumuisha yafuatayo:
  • Kuendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima;
  • Kuhakikisha kuwa nakisi ya bajeti haizidi asilimia 3.0 ya Pato la Taifa kuendana na vigezo vya Jumuiya ya Afrika Mashariki;
  • Kuelekeza fedha kwenye maeneo ya kipaumbele yatakayochochea ukuaji wa uchumi;
  • Kuhakikisha kuwa miradi inayoendelea inapewa kipaumbele kabla ya miradi mipya;
  • Kudhibiti ulimbikizaji wa madai; na
  • Kuongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA katika miamala na shughuli za Serikali.
Maeneo ya Vipaumbele kwa Mwaka 2020/21
  1. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2020/21 ni ya tano na ya mwisho katika utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21. Hivyo, utekelezaji wa bajeti hii utajikita zaidi katika maeneo mbalimbali ya vipaumbele yenye kuchochea mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu.
Kukarabati Miundombinu Iliyoharibiwa na Mvua Nyingi/Mafuriko na Kupambana na Homa Kali ya Mapafu (COVID-19)
  1. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tunamaliza mwaka 2019/20 katika hali isiyo ya kawaida kutokana na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya usafirishaji nchi nzima uliosababishwa na mvua nyingi/mafuriko pamoja na athari za ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababiswa na virusi vya CORONA, Serikali italazimika kuelekeza rasilimali zaidi kukarabati barabara, madaraja, reli na miundombinu mingine iliyoharibiwa na mafuriko pamoja na kuendelea kupambana na athari za janga la COVID-19 ikiwa ni pamoja na kusaidia sekta zilizoathirika zaidi.
Miradi ya Kielelezo
  1. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kugharamia utekelezaji wa miradi ya Kitaifa ya kimkakati ikiwemo: Ujenzi wa Reli ya Kati ya Standard Gauge; Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere – MW 2,115; Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania; kuwezesha Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga; na Kuendelea na ujenzi na ukarabati wa reli, barabara, madaraja, viwanja vya ndege, bandari, meli katika maziwa makuu na vivuko; kuimarisha miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme na gesi; Uendelezaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi; na Kusomesha kwa wingi Wataalamu kwenye Fani na Ujuzi Adimu/Maalum.
Huduma za Jamii
  1. Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la huduma za jamii miradi itakayotekelezwa inalenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, elimu na ujuzi na huduma za maji safi na majitaka. Kwa upande wa elimu, shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na kuendelea kugharamia utoaji wa elimumsingi bila ada, kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi, sekondari, vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi na vyuo vya elimu ya juu ikijumuisha mifumo ya TEHAMA, kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kuboresha huduma ya maji, elimu ya afya na usafi wa mazingira shuleni.
  1. Mheshimiwa Spika, katika uboreshaji wa huduma za afya, shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na ununuzi na usambazaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi, ujenzi wa hospitali za rufaa za mikoa na kanda, hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati, kuimarisha huduma za afya kwa watu wote kupitia bima ya afya na kuajiri wataalam mbalimbali katika sekta ya afya.
  1. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha huduma za maji safi na salama mijini na vijijini. Shughuli zitakazotekelezwa ni kuimarisha Mfuko wa Maji Vijijini, kuendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya usambazaji maji, kuendeleza rasilimali za maji, kuimarisha huduma za ubora wa maabara za maji, kuimarisha huduma za majitaka na kuimarisha usimamizi wa mazingira ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi;
Kilimo na Viwanda
  1. Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, miradi itakayotiliwa mkazo ni ujenzi wa viwanda vinavyotumia kwa wingi malighafi zinazopatikana hapa nchini zikiwemo za kilimo, madini na gesi asilia ili kukuza mnyororo wa thamani. Miradi hiyo ni pamoja na Ujenzi wa Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia; Uanzishwaji na Uendelezaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi na Kongane za Viwanda; viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi; kuongeza thamani ya madini; kuimarisha masoko ya madini na usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu. Katika eneo hili, Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) ikijumuisha kuboresha miundombinu ya umwagiliaji na masoko na upatikanaji wa pembejeo za kilimo na huduma za ugani, kuimarisha Ushindani katika Soko kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Ushindani Sawa na kusimamia Sheria ya Mapitio na Majadiliano Kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Utajiri na Maliasili za Nchi ya mwaka 2017.
  1. Mheshimiwa Spika, mikakati mingine katika sekta ya kilimo ni pamoja na: kuhimiza matumizi ya TEHAMA kwa ajili ya huduma za kilimo zikiwemo masoko, pembejeo na ugani; kuimarisha mfumo wa usimamizi wa ushirika ikiwa ni pamoja na kuboresha mifumo ya ushirika katika malipo ya fedha za wakulima; na kuanzisha mfumo wa kulinda wazalishaji wa ndani wa mazao ya kilimo, dhidi ya mazao na bidhaa zinazoagizwa nje ya nchi kama ngano, shayiri na mchuzi wa zabibu ili kuwahakikishia wakulima soko na kuwa na uzalishaji endelevu na wenye tija.
Maeneo Mengine Muhimu
  1. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha maisha ya wananchi wanyonge kwa kuendelea na utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ambapo katika Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu (2020-2023) jumla ya shilingi trilioni 2.03 zitatumika. Katika awamu hii, utekelezaji utafanyika katika Halmashauri zote 185 za Tanzania Bara na Wilaya zote 11 za Zanzibar. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 1.22, sawa na asilimia 60 zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye vijiji na mitaa 16,596 Tanzania bara na shehia 388 Zanzibar. Kipaumbele kitatolewa kwa watu wenye nguvu wanaotoka kwenye kaya maskini ambapo ajira milioni 1.2 zitazalishwa na kuwapatia walengwa ujuzi pamoja na stadi za kazi.
  1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji, Serikali itaendelea kutenga na kuendeleza maeneo ya uwekezaji kwa kujenga miundombinu wezeshi. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji kwa kuendelea kupunguza tozo na kodi kero na kuondoa mwingiliano wa majukumu miongoni mwa taasisi za Serikali zinazohusika na masuala ya biashara na uwekezaji.
  1. Mheshimiwa Spika, ukiacha utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III), ipo pia miradi mingine itakayotekelezwa kwa pamoja kati ya Tanzania bara na Zanzibar ikiwemo Mradi wa Kikanda wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish), programu ya mabadiliko ya tabianchi ambayo inalenga kulinda mazingira ya fukwe katika ukanda wa bahari kuu na mradi wa Kupitia Mifumo ya Ikolojia kwa lengo la kuongeza uwezo wa jamii kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika ngazi ya vijiji kwa kuimarisha mifumo ikolojia katika Wilaya za Mvomero (Morogoro), Simanjiro (Manyara), Kishapu (Shinyanga), Mpwapwa (Dodoma) na Kaskazini A, (Kaskazini Unguja). Shehia zitakazonufaika na mradi kutoka Kaskazini A ni pamoja na Shehia ya Matemwe Kijijini, Matemwe Jugakuu na Matemwe Mbuyutende.
  1. Mheshimiwa Spika, Mpango wa maendeleo wa Taifa wa mwaka 2020/21 niliouwasilisha leo asubuhi, umeainisha kwa kina maeneo ya kipaumbele ambayo Serikali itayatekeleza katika bajeti ya mwaka 2020/21.

  1. MABORESHO YA MFUMO WA KODI, ADA NA TOZO MBALIMBALI
  1. Mheshimiwa Spikanapenda sasa kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu mapendekezo ya kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi, ikiwemo baadhi ya viwango vya kodi, tozo na ada zinazotozwa chini ya Sheria mbalimbali na kurekebisha taratibu za ukusanyaji na usimamiaji wa mapato ya Serikali. Marekebisho haya yamezingatia dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwa na mfumo wa kodi ambao ni tulivu na wa kutabirika. Aidha, marekebisho yanalenga kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi hususan katika sekta ya kilimo na viwanda, kuongeza kipato kwa waajiriwa na kuongeza mapato ya Serikali. Vile vile, maboresho haya yamezingatia uhitaji wa kuwekeza nguvu katika kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba na dawa. Serikali pia inaendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara (BluePrint) ulioidhinishwa mwaka 2017/18 kwa kupitia mfumo wa tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na Wizara na Mamlaka za Udhibiti kwa lengo la kupunguza au kuzifuta baadhi ya tozo na ada hizi. Hadi sasa, jumla ya tozo na ada 114 zimefutwa. Marekebisho yanayopendekezwa yanahusu maeneo 16 yafuatayo:
  • Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148
  1. Mheshimiwa Spikanapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148 kama ifuatavyo:
  • Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye bima ya kilimo cha mazao. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama na kutoa unafuu katika bima za kilimo ili kuwawezesha wakulima kuziwekea bima shughuli za kilimo na kuvutia wananchi kutumia huduma za bima kwa ajili ya kujikinga na majanga mbalimbali yanayoathiri shughuli zao za kilimo mfano ukame, mafuriko n.k; na
  • Kufanya marekebisho ya kuwawezesha wauzaji wa bidhaa ghafi nje ya nchi kuendelea kujirudishia Kodi ya Ongezeko la Thamani iliyolipwa kwenye gharama za huduma au bidhaa katika shughuli hizo ili bidhaa hizo ziweze kushindana katika masoko ya nje. Hatua hii pia inalenga kuendana na msingi wa utozaji VAT kwa kuzingatia mahali bidhaa inapotumika (destination principle).
Hatua zote za Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa ujumla wake zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 46.
  • Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332
  1. Mheshimiwa Spikanapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 kama ifuatavyo:
  • Kupandisha kiwango cha mapato ya waajiriwa ili kuongeza kiwango cha mapato yasiyotozwa kodi (threshold) kutoka shilingi 170,000 kwa mwezi hadi shilingi 270,000 kwa mwezi (sawa na kutoka shilingi 2,040,000/= kwa mwaka hadi shilingi 3,240,000/= kwa mwaka) na kubadilisha makundi mengine kwa viwango kama vilivyobainishwa katika Jedwali Na. 1b. Lengo la mabadiliko haya ni kutoa unafuu wa Kodi ya Mapato kwa wafanyakazi. Hatua hii pekee inatarajiwa kupunguza mapato kwa shilingi milioni 517.2
  • Kuongeza kiwango cha Mapato ghafi ya Vyama vya Ushirika vya Msingi yasiyotakiwa kutozwa Kodi ya Mapato kutoka shilingi milioni hamsini (50,000,000/=) hadi shilingi milioni mia moja (100,000,000/=) kwa mwaka. Lengo la hatua hii ni kutoa nafuu ya kulipa Kodi ya Mapato kwa Vyama vya Ushirika vya Msingi zikiwemo SACCOS kutokana na kuwa na mitaji midogo ili kuwanufaisha wanachama wake kwa njia ya gawio na mikopo;
  • Kufuta msamaha wa Kodi ya Mapato kwa wazalishaji walio ndani ya maeneo maalum ya kiuchumi (Special Economic Zones) wanaozalisha bidhaa na kuuza ndani ya nchi kwa asilimia 100. Hatua hii inalenga kuweka usawa katika utozaji wa kodi ya mapato baina ya wazalishaji wa bidhaa walio nje na walio ndani ya maeneo maalum ya Kiuchumi;
  • Kuruhusu michango ya wadau kwenye Mfuko wa Ukimwi isitozwe kodi ya Mapato (allowable deduction). Aidha, napendekeza pia michango iliyotolewa na wananchi kwa Serikali na itakayoendelea kutolewa katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID 19) isitozwe kodi hadi hapo Serikali itakapotangaza kuisha kwa ugonjwa huu. Lengo la mabadiliko haya ni kuhamasisha uchangiaji wa hiari katika Mfuko wa Ukimwi na kwa Serikali ili kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi na COVID 19;
  • Kumpa Mamlaka Waziri wa Fedha kutoa msamaha wa Kodi ya Mapato kwenye Miradi ya Kimkakati yenye jumla ya Kodi ya Mapato isiyozidi shilingi bilioni moja kwa kipindi chote cha mradi (1,000,000,000/=) bila kuwasilisha mapendekezo hayo kwenye Baraza la Mawaziri. Lengo la hatua hii ni kuwezesha miradi yenye kiwango kidogo cha kodi ya mapato kutekelezwa kwa haraka. Waziri mwenye dhamana ya fedha atafanya mashauriano na Mamlaka ya Mapato kabla ya kutoa msamaha wa kodi husika;
  • Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani ya Mtaji (Capital Gains) kwenye mapato yatokanayo na ubadilishaji wa leseni (concessional right) katika ardhi iliyohodhiwa (reserved land) na kupangishwa kwa mwekezaji mwingine. Lengo la hatua hii ni kupanua wigo wa kodi na kuongeza mapato ya Serikali;
  • Kutoza kodi ya zuio ya asilimia 10 kwenye malipo ya uwakala inayolipwa kwa mawakala wa Benki kama ilivyo kwa mawakala wa huduma za uhamishaji fedha za kieletroniki. Lengo la hatua hii ni kuweka usawa katika utozaji wa kodi ya mapato kwa watoa huduma za kibenki, kielektroniki na huduma za usafirishaji fedha kwa njia ya mitandao ya simu; na
  • Kufanya marekebisho kwenye vifungu vya 3, 4, 6 na 69 vya Sheria ya Kodi ya Mapato ili kuongeza tafsiri ya maneno “beneficial owner”; “representative assessee” na “business connection”. Lengo la maboresho haya ni kutekeleza matakwa ya nchi kujiunga kwenye Jukwaa la Kimataifa la kubadilishana taarifa za kikodi ili kukabiliana na ukwepaji kodi unaofanywa na kampuni za kimataifa. Aidha, maboresho haya yanalenga kuziba mianya ya ukwepaji kodi ya mapato unaofanywa na makampuni yenye mahusiano mbalimbali ya kibiashara kupitia matawi ya kampuni hizo kwenye nchi mbalimbali.
Hatua hizi za Kodi ya Mapato kwa ujumla wake zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni 514.0.
  • Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147
  1. Mheshimiwa SpikaKwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa bidhaa kifungu cha 124(2), marekebisho ya viwango maalum vya ushuru wa bidhaa (specific duty rates) kwa bidhaa zote zisizo za petroli yanaweza kufanyika kila mwaka ili kuviwianisha na mfumuko wa bei na viashiria vingine vya uchumi jumla. Hata hivyo, kutokana na biashara za bidhaa hizi kuzorota kutokana na athari za kiuchumi zilizosababishwa na COVID-19napendekeza kutofanya mabadiliko ya viwango maalum vya Ushuru wa Bidhaa kwa bidhaa zote. Aidha, hatua hii inazingatia kiwango kidogo cha mfumuko wa bei nchini na azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda, na hivyo kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta ya viwanda, kuvilinda na hatimaye kukuza ajira na mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa.
  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza pia kufanya marekebisho ya Ushuru wa Bidhaa kwenye bidhaa zifuatazo:
  • Kutoza Ushuru wa Bidhaa kwenye bia za unga (powdered beer) zinazotambulika kwa HS Code 2106.90.99 kwa kiwango cha shilingi 844 kwa kilo ya bia ya unga inayoagizwa kutoka nje ya nchi. Lengo la mabadiliko haya ni kupanua wigo wa kodi kwa kuwa bidhaa hizi kwa sasa zinaagizwa toka nje ya nchi; na
  • Kutoza Ushuru wa Bidhaa kwenye juisi za unga zinazotambulika kwa HS Code90.99 kwa kiwango cha shilingi 232/= kwa kilo ya juisi ya unga inayoagizwa kutoka nje ya nchi. Lengo la mabadiliko haya ni kupanua wigo wa kodi kwa kuwa bidhaa hizi kwa sasa zinaagizwa toka nje ya nchi.
Hatua za kutoza Ushuru wa Bidhaa kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni 45.8.
  • Sheria ya Usimamizi wa Kodi, SURA 438
  1. Mheshimiwa Spikanapendekeza kufanya maboresho kwenye Sheria ya Usimamizi wa Kodi Sura 438, ili kumwezesha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kutatua mapingamizi ya kodi kwa ufanisi na haraka. Marekebisho haya ni pamoja na kuweka ukomo wa muda wa siku 30 za kuwasilisha nyaraka zitakazotumika kwenye utatuzi wa pingamizi. Aidha marekebisho haya yataweka ukomo wa miezi 6 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania kufanya maamuzi ya mapingamizi ya kodi. Kwa sasa, sheria haitoi ukomo kwa walipakodi kuwasilisha nyaraka zitazoisaidia Mamlaka ya Mapato kufanya uamuzi kuhusu pingamizi. Vile vile, kwa sasa sheria haitoi muda wa ukomo kwa Kamishna Mkuu kwa Mamlaka ya Mapato kufanya uamuzi kuhusu pingamizi.
  • Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, SURA 290
  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290, ili kumpa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya masuala yanayohusu Serikali za Mitaa kukusanya tozo ya huduma (Service Levy) ya asilimia 0.3 ya mapato ghafi kwenye Sekta ya Mawasiliano kwa niaba ya Halmashauri, na kuyagawa mapato hayo kwa Halmashauri zote ndani ya siku 14 baada ya kukusanywa. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- TAMISEMI ataandaa kanuni ambazo zitaweka utaratibu wa ukusanyaji na ugawaji wa mapato hayo kwa kutumia kikokotoo maalum kwa kuzingatia kiasi cha Tozo ya Huduma kutoka Sekta ya Mawasiliano kwa kila Halmashauri. Hatua hii itasaidia kuziondolea kero baadhi ya Halmashauri ya kukosa mapato kutoka kwenye chanzo hiki na kupunguza usumbufu wa ufuatiliaji wa kila Halmashauri kwenye Makao Makuu ya Makampuni yanayotoa huduma za mawasiliano nchini.

  • Sheria ya Fedha za Umma, Sura 348
  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Fedha za Umma Sura 348 ili kuziongeza Taasisi za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC); Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA); Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA); na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwenye orodha ya taasisi zinazochangia gawio au asilimia 15 ya Mapato ghafi kwenye Mfuko wa Hazina.
Hatua hiyo ya marekebisho ya Sheria ya Fedha za Umma inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni 5.89.
  • Sheria ya Msajili wa Hazina, Sura 370
  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya Marekebisho ya Kifungu cha 10A (1) cha Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 kwa kuondoa maneno “not financed through Government Budget” ili kuruhusu Ofisi ya Msajili wa Hazina kukusanya asilimia 70 ya fedha za ziada kutoka kwenye Mashirika, Taasisi au Wakala yoyote itakayoonekana kuwa na ziada. Lengo la hatua hizi ni kuongeza udhibiti wa fedha za Serikali.
  • Sheria ya Usajili wa Magari, Sura 124
  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Usajili wa Magari Sura 124, ili kuanzisha usajili wa magari kwa kutumia namba maalum (mfano T. 777 DDD) kwa ada ya shilingi laki tano (500,000/=). Ili kuwezesha wateja kuchagua namba ya usajili wa gari katika namba zilizopo katika regista ya namba za magari katika muda husika.
Hatua hizi za marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Magari inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 200.
  • Sheria ya Madini, SURA 123
  1. Mheshimiwa Spikanapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Madini, Sura 123 ili kuweka vipengele vinavyomtaka mwombaji wa leseni au anayetaka kuhuisha leseni za uchimbaji madini kuwa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi na Cheti cha Kodi (Tax Clearance) kutoka Mamlaka ya Mapato. Lengo la hatua hii ni kuchochea uwajibikaji wa hiari.
  • Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA 82
  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza kupunguza kiwango cha tozo kwa ajili ya maendeleo ya ufundi stadi (Skills Development Levy) kutoka asilimia 4.5 hadi asilimia 4. Lengo la marekebeisho haya ni kuwapunguzia waajiri mzigo na gharama za uendeshaji wa shughuli zao na kutimiza azma ya kupunguza tozo hizi hatua kwa hatua bila kuathiri mapato kwa kiasi kikubwa.
Marekebisho haya yanategemea kupunguza Mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni 42.07.
  • Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kielektroniki, SURA 306
  1. Mheshimiwa Spikanapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kielektroniki Sura 306 ili kuziondoa kampuni zinazomilikiwa na Serikali na ambazo Serikali inamiliki hisa asilimia 25 na zaidi katika takwa la kuorodheshwa kwenye soko la hisa. Hatua hii inalenga kutokusababisha kupungua kwa hisa zinazomilikiwa na Serikali baada ya Kampuni kuorodheshwa kwenye soko la hisa. Aidha, napendekeza kuondoa kampuni zinazokodisha minara ya mawasiliano zisiwe sehemu ya makampuni ya mawasiliano zinazotakiwa kuorodheshwa kwenye soko la hisa.
  • Sheria ya Ardhi, Na. 4 ya Mwaka 1999
  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Ardhi, Na. 4 ya Mwaka 1999 ili kuweka ulazima wa mwananchi yeyote ambaye ardhi yake imefanyiwa upimaji (survey) na michoro yake kuidhinishwa na Wizara yenye dhamana ya masuala ya ardhi kupeleka maombi kwa Kamishna wa Ardhi kupatiwa hati ya kumiliki ardhi ndani ya siku tisini (90) kuanzia tarehe ya kuidhinishwa kwa michoro ya upimaji. Lengo la marekebisho haya ni kuwafanya wananchi wanaohodhi ardhi bila umiliki wafanye taratibu za kuomba umiliki.
  • Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004
  1. Mheshimiwa Spika, kikao cha Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki cha Maandalizi ya Bajeti kilichofanyika tarehe 13 Mei, 2020 kwa njia ya mtandao (Video Conference), kilipendekeza kufanya marekebisho ya Viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha (EAC – Common External Tariff “CET”) na Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act, 2004) kwa mwaka wa fedha 2020/21.
  1. Mheshimiwa Spikamapendekezo ya Mawaziri wa Fedha ya kufanya marekebisho kwenye Viwango vya Pamoja vya Ushuru wa Forodha yanahusisha hatua mpya na zinazoendelea ambazo zimekuwa zikitekelezwa katika mwaka 2019/20.
  • Mapendekezo ya hatua mpya za viwango vya Ushuru wa Forodha ni kama ifuatavyo: –
  • Kupunguza Ushuru wa Forodha hadi asilimia 0 kutoka viwango vya awali vya asilimia 10 na asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa vifaa maalum vinavyotumika katika kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID-19) vikiwemo Barakoa (Masks)kipukusi (sanitizer), mashine za kusaidia kupumua (ventilators), na mavazi maalum ya kujikinga yanayotumiwa na madaktari na wahudumu wa afya (PPE). Msamaha huu utatolewa kwa utaratibu wa “duty remission”. Hatua hii inalenga kutoa unafuu wa uzalishaji wa vifaa hivyo hapa nchini ili kuongeza kasi katika kupambana na ugonjwa huo;
  • Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye mashine za kielektroniki zinazotumika kukusanya mapato ya Serikali (Cash registers, Electronic Fiscal Device (EFD) Machines and Point of Sale (POS) machines zinazotambulika katika HS Code 8470.50.00 na 8470.90.00;
  • Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vinavyotumiwa na wazalishaji wa maziwa kwa joto la juu yanayodumu kwa muda mrefu (UHT Milk) vinavyotambulika kwa HS codes 4819.50.00. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji wa maziwa hapa nchini. Aidha utaratibu utakaotumika kutoa unafuu huo ni wa “Duty Remission”;
  • Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka kiwango cha asilimia 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifuniko vya chupa za mvinyo (corks) vinavyotambulika kwa HS Codes 4503.10.00 kwa kuzingatia kuwa hazizalishwi hapa nchini. Hatua hii inalenga kuwapunguzia gharama wazalishaji wa mvinyo ili kuhamasisha na kuendeleza kilimo cha zao la zabibu nchini pamoja na ajira. Aidha utaratibu utakaotumika kutoa unafuu huo ni wa “Duty Remission”;
  • Kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za marumaru zinazotambulika kwa HS Code 6907.21.00; 6907.22.00; na 6907.23.00 zinazoingizwa kutoka nje. Lengo la hatua hii ni kulinda na kukuza viwanda vya ndani vinavyozalisha marumaru pamoja na kuongeza ajira;
  • Kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye chai inayotambulika kwa HS Code 09.02 inayoagizwa kutoka nje. Lengo la pendekezo hili ni kulinda viwanda vya ndani na kuhamasisha kilimo cha chai hapa nchini pamoja na kuongeza ajira katika sekta ya kilimo.
  • Kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye magunia (sacks and bags of jute or other textile bast fibers of heading 03) yanayotambulika kwa HS Code 6305.10.00 yanayoagizwa kutoka nje. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani vinavyotengeneza magunia ya mkonge, kukuza na kuendeleza kilimo cha zao la mkonge hapa nchini pamoja na kuongeza ajira na mapato ya Serikali;
  • Kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 0 hadi asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye kakao inayoingizwa kutoka nje inayotambulika kwa HS Code 1805.00.00. Lengo ni kuchochea na kuhamasisha kilimo cha zao la kakao nchini pamoja na kuongeza mapato ya Serikali;
  • Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vya kuhifadhia kahawa vinavyotumiwa na viwanda vya kusaga kahawa Vifungashio vitakavyohusika ni vile vinavyotambulika katika HS codes 7310.21.00; 6305.10.00; 3923.50.10; 3923.50.90; 3920.30.90 na 48.19. Hatua hii inalenga kuongeza thamani kwenye zao la kahawa na kuvipa unafuu wa gharama viwanda vinavyosaga kahawa hapa nchini. Aidha utaratibu wa “Duty Remission” utatumika katika kuagiza vifungashio hivyo;
  • Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vya kuhifadhia korosho. Vifungashio vitakavyohusika ni vile vinavyotambulika katika HS codes 3923.21.00. Hatua hii inatarajiwa kuongeza thamani kwenye zao la korosho na kuzipa unafuu wa gharama taasisi zinazohusika na kuchakata korosho hapa nchini. Aidha utaratibu wa “Duty Remission” utatumika katika kuagiza vifungashio hivyo; na
  • Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifungashio vya kuhifadhia pamba. Vifungashio vitakavyohusika ni vile vinavyotambulika katika HS codes 3920.30.90; 6305.39.00 na 7217.90.00. Hatua hii inalenga kuvutia uwekezaji ili kuongeza thamani ya zao la pamba nchini.
  • Mapendekezo ya kuendelea na utekelezaji wa viwango vya Ushuru wa Forodha vya mwaka 2019/20 ni kama ifuatavyo; –
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 0 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 25 kwenye malighafi za kutengeneza taulo za watoto (Baby Diapers) zinazotumbulika kwa HS code 3506.91.00 Hot Melt AdhesivePE film HS Code 3920.10.90, Empty bag for Baby Diapers HS Code 6305.33.00, Plastic cask HS Code 3926.90.90; na kiwango cha awali cha asilimia 10 kwenye Super Absorbent Polymer HS Code 3906.90.00, Wet strength paper HS Code 4803.00.00, Non-woven HS Code 5603.11.00, Polyethylene laminated Nonwovens HS Code 5903.90.00, Spandex HS Code 5402.44.00 na Dust free paper HS Code 4803.00.00. Aidha, msamaha huu utatolewa kwa utaratibu wa “Duty Remission”. Hatua hii inatarajiwa kutoa unafuu wa gharama za uzalishaji, kuongeza ajira na mapato ya Serikali;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 0 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 25 kwenye vifaa vinavyotumika katika kukata, kung’arisha na kuongeza thamani ya madini ya vito vinavyotambulika kwa HS Codes 6804.10.00; 7018.90.00; 7020.00.99; na kiwango cha awali cha asilimia 10 kwenye HS Codes 3606.90.00; 6813.20.00; 8202.20.00; 8202.99.00; 8203.20.00; 8205.10.00; 8423.89.90; 8513.10.90; na 9002.19.00. Hatua hii itawanufaisha wanaofanya shughuli hizo na utaratibu wa “Duty Remission” ndio utatumika katika kuagiza vifaa hivyo;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 0 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 10 kwenye makaratasi (HS Code 4805.11.00 na 4805.19.00) pamoja na asilimia 25 hadi 10kwa mwaka mmoja kwenye makaratasi (HS Code 4805.24.00 na 4805.25.00) yanayotumika kama malighafi ya kutengeneza vifungashio vya mboga mboga kwa ajili ya kuuza nje ya nchi. Utaratibu wa “Duty Remission” utatumika ambapo viwanda vinavyotengeneza vifungashio hivyo tu ndivyo vitakavyonufaika. Aidha, karatasi hizi hazizalishwi na kiwanda chetu cha Mufindi hapa nchini. Lengo la hii ni kuwapa unafuu wazalishaji wa vifungashio vya mbogamboga hapa nchini pamoja na kuwawezesha wakulima kupata vifungashio hapa nchini ambapo kwa sasa vinaagizwa kutoka nje kwa gharama kubwa;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 0 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 25 kwenye vifungashio vya mbegu vinavyotambulika katika HS codes 3923.29.00; 6305.10.00; 4819.40.00; 7310.29.90; 6305.33.00; 6305.20.00; 6304.91.90; 7607.19.90. Utaratibu utakaotumika kutoa unafuu huo ni wa “duty remission”. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wazalishaji wa mbegu hapa nchini;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye kahawa inayotambulika kwa HS Code 09.01 inayoagizwa kutoka nje ya nchi za EAC. Lengo la pendekezo hili ni kulinda viwanda vya ndani na kuhamasisha kilimo cha kahawa hapa nchini pamoja na kuongeza ajira katika sekta ya kilimo;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 au dola za kimarekani 125 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kwenye bidhaa za chuma kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa. Bidhaa hizo ni “Flat -rolled products of iron or Non-alloy steel na Flat –rolled products of other alloy steel.” Bidhaa hizi hutambulika katika HS Codes 7209.16.00; 7209.17.00; 7209.18.00; 7209.26.00; 7209.27.00; 7209.28.00; 7209.90.00; 7211.23.00; 7211.90.00; 7225.50.0 na 7226.92.00. Lengo la kuendelea kutoza viwango hivyo ni kulinda viwanda vya hapa nchini, kukuza ajira pamoja na kudhibiti udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa hizo kutoka nje;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 250 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za mabati zinazotambulika kwa HS codes 7210.41.00; 7210.49.00; 7210.61.00; 7210.69.00; 7210.70.00 na 7210.90.00 kutegemea kiwango kipi ni kikubwa badala ya ushuru wa asilimia 25 au dola za kimarekani 200 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton), kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kuwalinda wazalishaji wa bidhaa hizo hapa nchini kutokana na ushindani wa nje;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 au dola za kimarekani 250 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye bidhaa za mabati zinazotambulika katika HS Code 7212.60.00 badala ya ushuru wa asilimia 10 pekee. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani kutokana na udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa hizo zinapoingizwa kutoka nje (under-invoicing and under valuation), na kulinda ajira na mapato ya Serikali;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 250 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kwenye bidhaa za mabati kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa. Ushuru huo unahusu bidhaa zinazotambulika katika HS Code 7212.30.00; 7212.40.00 na 7212.50,00. Hatua hii ina lengo la kulinda viwanda vya ndani kutokana na udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa hizo zinapoingizwa kutoka nje (under-invoicing and under valuation), na kulinda ajira na mapato ya Serikali;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 250 badala ya kiwango cha asilimia 25 au dola za kimarekani 200 kwa kila tani moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za chuma kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye nondo kwa mwaka mmoja. (Reinforment bars and hallow profile). Hatua hii inahusu bidhaa zinazotambulika katika Hs codes 7213.10.00; 7213.20.00; 7213.99.00; 7214.10.00; 7214.20.00; 7214.30.00; 7214.90.00; 7214.99.00; 7215.10.00; 7215.50.00; 7215.90.00; 7225.90.00; 7225.92.00; 7225.99.00; 7306.30.00; 7306.50.00; 7306.61.00; 7306.69.00; na 7306.90.00. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vinavyozalisha nondo hapa nchini na kuongeza ajira;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za mboga mboga (horticultural products) zinazotambulika kwa HS codes 0603.11.00; 0603.12.00; 0603.13.00; 0603.14.00; 0603.19.00; 0604.20.00; 0604.90.00; 0701.90.00; 0702.00.00; 0703.10.00; 0703.20.00; 0706.10.00; 0710.10.00; 0710.21.00; 0710.22.00; 0710.30.00; 0714.10.00; 0714.20.00; 0804.30.00; 0804.40.00; 0804.50.00; 0805.10.00; 0805.40.00; 0805.50.00; 0806.10.00; 0807.11.00; 0807.20.00; 0808.10.00; 0808.20.00. Hatua hii ni katika kulinda wakulima wa ndani ili kuendeleza kilimo cha mbogamboga na maua hapa nchini;
  • Kuendelea kutoza ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa za fito za plastiki zijulikanazo kama PVC Profiles HS Code 3916.10.00; 3916.20.00; 3916.90.00 ambazo hutumika kwa ajili ya kutengenezea fremu za milango, madirisha n.k. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye karatasi zinazozalishwa na kiwanda cha mufindi hapa nchini ambazo zinazotambulika kwa HS codes 4804.11.00; 4804.21.00; 4804.29.00; 4804.31.00 na 4804.41.00.
Lengo la hatua hii ni kuendelea kulinda kiwanda cha mufindi na kuongeza uzalishaji wa karatasi hapa nchini;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 10 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 35 kwenye ngano inayotambulika kwa HS Code 1001.99.10 na HS Code 1001.99.90 kwa utaratibu wa “Duty Remission” ambapo wanaonufaika na unafuu huu ni wenye viwanda vya kusaga ngano. Hatua hii imezingatia makubaliano na Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kutokana na kwamba uzalishaji wa ngano katika nchi hizi hautoshelezi mahitaji, na bidhaa hii ni muhimu katika kutengeneza vyakula mbalimbali. Lengo la Serikali ni kuwezesha Viwanda na walaji wa vyakula vilivyotengenezwa kwa ngano waweze kupata vyakula husika kwa bei nafuu na tulivu;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 0 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 25 kwa utaratibu wa duty remission kwenye bidhaa ijulikanayo kama “Printed Alluminium Barrier Laminates” (ABL) HS Code 3920.10.90 ambayo hutumika kama malighafi ya kutengeneza vifungashio vya dawa ya meno kwenye viwanda vya ndani, kwa mwaka mmoja;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 0 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 10 kwa utaratibu wa “Duty Remission” kwenye malighafi ya kutengeneza sabuni ijulikanayo kama RBD Palm Stearin (HS Code 1511.90.40) kwa viwanda vinavyotengeneza sabuni nchini. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa viwanda vya kuzalisha sabuni nchini;
  • Kuendelea kutoza kwa mwaka mmoja Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 1.35 kwa kilo moja ya viberiti (safety match boxes) vinavyotambuliwa kwenye HS code 3605.00.00 kutegemea kiwango kipi ni kikubwa badala ya asilimia 25 pekee;
  • Kuendelea kutoza kwa mwaka mmoja Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 350 kwa kila tani moja ya ujazo (Metric ton) kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye bidhaa za chuma za misumari zinazotambulika kwa HS code 7317.00.00 (nails, tacks, drawing pins, corrugated nails, and staples other than those of heading05) badala ya asilimia 25 pekee;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye soseji (sausages) na bidhaa za aina hiyo zinazotambulika kwa HS code 1601.00.00. Lengo ni kuendelea kulinda wajasiliamali wa ndani wanaozalisha bidhaa hizo;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye chingamu (chewing gum) zinazotambulika kwa HS code 1704.10.00 zinazoagizwa kutoka nje. Lengo ni kuendelea kulinda viwana vya ndani;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye peremende zinazotambulika kwa HS code 1704.90.00 zinazoagizwa kutoka nje. Lengo ni kuendelea kulinda viwanda vya ndani na kukuza ajira;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye chokoleti (chocolates) HS code 18.06 kwa mwaka mmoja. Lengo ni kulinda viwanda vya ndani na kukuza ajira;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye biskuti (HS code 1905) kwa mwaka mmoja;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye nyanya zilizosindikwa (tomato sauces) zinazotambulika katika HS code 2103.20.00;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 60 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye maji (mineral water) yanayotambulika katika HS code 2201.10.00;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye nyama zilizoainishwa katika sura ya 2 katika Viwango vya pamoja vya ushuru wa forodha (meat and edible meat offal in chapter 2) kwa mwaka mmoja. Lengo la hatua hii ni kuendelea kulinda na kuchochea sekta ya ufugaji nchini;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 25 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha awali cha asilimia 0 kwenye mafuta Ghafi ya kula (mfano alizeti, mawese, soya, mizeituni, nazi, karanga, mahindi n.k) yanayotambulika kwa HS code 1507.10.00; 1508.10.00; 1511.10.00; 1513.11.00; 1514.11.00; 1514.91.00; 1515.11.00; na kiwango cha awali cha asilimia 10 kwenye HS Codes 1512.11.00, 1515.21.00; na 1515.30.00. Hatua hii inalenga katika kuendelea kulinda na kuhamasisha uzalishaji wa mbegu za mafuta na mafuta ya kula hapa nchini pamoja na kuongeza ajira mashambani, viwandani na pia kulinda fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta hayo nje ya nchi;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye mafuta ya kula yaliyochakatwa kwa kiwango cha kati na mwisho (semi-refined, refined/double refined oil) mfano alizeti, mawese, soya, mizeituni, karanga, nazi, mahindi n.k zinazotambulika kwa HS codes 1507.90.00; 1508.90.00; 1509.90.00; 1510.00.00; 1511.90.10; 1511.90.30; 1511.90.90; 1512.19.00; 1512.29.00; 1513.19.00; 1513.29.00; 1514.19.00; 1514.99.00; 1515.19.00; 1515.29.00; 1515.50.00; 1515.90.00. Lengo ni kuhamasisha uchakataji wa mbegu za mafuta hapa nchini na kuongeza ajira viwandani na mashambani pamoja na kulinda fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta hayo nje ya nchi;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 badala ya asilimia 0 kwenye “Gypsum Powder” HS code 2520.20.00 kwa mwaka mmoja;
  • Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha kwa kiwango cha asilimia 35 kwa mwaka mmoja kutoka kiwango cha asilimia 100 kwenye sukari ya matumizi ya kawaida (consumption sugar) inayoagizwa kutoka nje ya nchi kwa vibali maalum kwa lengo la kuziba pengo (gap sugar) la uzalishaji hapa nchini;
  • Kuendelea kutoza kwa mwaka mmoja Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 kwenye mitumba inayoingia kutoka nje (badala ya asilimia 35 au dola za marekani 0.40 kwa kilo moja kutegemea kiwango kipi kikubwa); na
  • Kuendelea kusamehe Ushuru wa Forodha kwenye malighafi, vipuri na mashine vinavyotumika katika kutengeneza viatu vya ngozi na nguo. Aidha, sambamba na pendekezo hilo, Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaendelea kutoa unafuu wa ushuru wa forodha kwa pamoja kwenye orodha iliyooanishwa (harmonized list) ya malighafi na vipuri ili nchi hizo ziweze kufanya biashara kwa bidhaa za nguo na viatu vya ngozi vitakavyozalishwa ndani ya Jumuiya bila kutozana ushuru.
  1. Mheshimiwa SpikaMawaziri wa Fedha wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya pia marekebisho kwenye Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act, 2004) kama ifuatavyo:
  • Kufanya marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACCMA, 2004) ili kutoa msamaha kwenye madawa na vifaa muhimu vinavyotumika kupima, kukinga, kutibu na kupambana na mlipuko wa magonjwa (supplies for diagnosis, prevention, treatment, and management of epidemics, pandemics and health hazards) kama vile ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID- 19). Hatua hii inalenga kutoa unafuu wa bidhaa hizo ili kurahisisha mapambano na udhibiti wa magonjwa hayo pindi yanapojitokeza;
  • Kufanya marekebisho katika Jedwali la Tano la Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACCMA, 2004) ili kusamehe ushuru wa forodha kwenye zana (implements) zinazoingizwa nchini na watu au taasisi zinazohusika katika kilimo, kilimo cha mbogamboga, kilimo cha maua pamoja na ufugaji wa samaki. Lengo la kutoa msamaha huo ni kuchochea na kuhamasisha ukuaji wa sekta ya kilimo pamoja na kuvutia uwekezaji mpya katika sekta ndogo ya ufugaji wa samaki nchini; na
  • Kufanya marekebisho katika Jedwali la Tano la Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACCMA, 2004) ili kutoa msamaha wa ushuru wa forodha kwenye Mayai ya kutotolesha vifaranga vya kuku (fertilized eggs for incubation) yanayoingizwa na watu au taasisi zinazohusika na ufugaji wa kuku. Lengo ni kukuza na kuhamasisha ufugaji wa kuku nchini.
Hatua hizi za Ushuru wa Forodha kwa pamoja zinatarajiwa yatapunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni 208.04.
  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza kuongeza uthaminishaji wa vitenge vinavyoingizwa nchini kutoka uthaminishaji wa sasa wa dola za Marekani 0.40 kwa kila mita moja hadi dola za Marekani 1 kwa kila mita moja ya kitenge. Lengo la hatua hii ni kuzuia udanganyifu wa thamani unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kwenye ankara wanazowasilisha Mamlaka ya Mapato Tanzania.
  • Utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara (Blueprint) kwa kurekebisha Ada na Tozo mbalimbali.
  1. Mheshimiwa SpikaNapendekeza kufuta au kupunguza ada na tozo sitini (60) zinazotozwa na Wizara, Idara na Taasisi zinazojitegemea ili Kuondoa kero na urasimu kwa wafanyabiashara na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa janga la homa kali ya mapafu duniani. Hatua hizi ni sehemu ya mwendelezo wa utekelezaji wa Mpango wa kuboresha Mfumo wa udhibiti wa Biashara (Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment). Marekebisho hayo yatajumuisha:
  • Tume ya Ushindani
Napendekeza kufanya marekebisho ya kifungu cha 60 cha Sheria ya Ushindani kinachohusu adhabu ya makosa ya ushindani ili ihusishe tu pato ghafi lililopatikana ndani ya Tanzania Bara pekee na si duniani kote. Lengo la mabadiliko haya ni kuifanya Sheria hii itekelezeke kwa kuwa adhabu inayotokana na pato ghafi la Kampuni za nje ni kubwa mno na hivyo kutolipika.
  • Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA)
Napendekeza kufuta kipengele cha 16(2) cha Sheria ya makampuni ili kuondoa takwa la kugongewa muhuri na Kamishna wa Viapo ili kuonyesha umetimiza matakwa ya Sheria hiyo wakati unafungua kampuni au kuhuisha usajili. Aidha, Kifungu cha 14(4) kinatosheleza matakwa yote hayo na hivyo hatua hii itapunguza urasimu na gharama za kupata tamko la kutimiza matakwa ya kisheria (Declaration of Competence).
  • Bodi ya Sukari
Napendekeza kupunguza tozo inayotozwa na Bodi ya Sukari kutoka asilimia 2 ya thamani ya mzigo au asilimia 2 ya dola za Marekani mia nne na sitini (460) sawa na takriban dola za Marekani 9 kwa tani, chochote kitakachokuwa kikubwa hadi dola 7.5 kwa tani moja.
  • OSHA
    • Napendekeza kufuta tozo ya mafunzo ya elimu kwa umma iliyokuwa inatozwa kiasi cha shilingi laki mbili na nusu (250,000/=) kwa kila mshiriki kwa kuwa hili ni jukumu la msingi la OSHA kuelimisha umma;
  • Napendekeza kufuta ada ya ukaguzi iliyokuwa inatozwa kwa kiwango cha asilimia 80 ya ada ya usajili, ada hii inaleta mkanganyiko kwa kuwa tozo ya usajili ilishafutwa; na
  • Napendekeza kupunguza ada ya uchunguzi wa ajali iliyokuwa ikitozwa kiasi cha shilingi laki tano (500,000/=) kwa kila mtaalamu anayefanya uchunguzi hadi shilingi laki moja na elfu ishirini (120,000/=) kwa kila mtaalamu lakini si zaidi ya shilingi milioni moja (1,000,000/=).
  • Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
Napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Jeshi ya Zimamoto na Uokoaji Sura 427 kwa kupunguza ada na tozo zifuatazo:
  • Kupunguza tozo ya Cheti cha Umahiri (Certificate of Competence) inayotozwa kwa wauzaji wa vifaa vya zimamoto na uokoaji kutoka shilingi laki tano (500,000/=) hadi shilingi laki mbili (200,000/=);
  • Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye maeneo ya uchimbaji madini yenye ukubwa usiozidi mita za mraba 2,000 kutoka shilingi milioni sita (6,000,000/=) hadi shilingi laki moja (100,000/=);
  • Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye maeneo ya uchimbaji madini yenye ukubwa kati ya mita za mraba 2001 hadi 4000 kutoka shilingi milioni sita (6,000,000/=) hadi shilingi laki moja na elfu hamsini (150,000/=);
  • Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye maeneo ya uchimbaji madini yenye ukubwa kati ya mita za mraba 4001 hadi 9000 kutoka shilingi milioni sita (6,000,000/=) hadi shilingi laki mbili (200,000/=);
  • Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye mitungi ya gesi yenye ujazo wa gesi kati ya tani 1 hadi tani 10 kutoka shilingi milioni mbili (2,000,000/=) hadi shilingi milioni moja na laki tano (1,500,000=/);
  • Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye maduka yanayouza mitungi ya gesi yasiyozidi ukubwa wa mita za mraba 100 kutoka shilingi laki moja (100,000/=) hadi shilingi elfu arobaini (40,000/=);
  • Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye maduka ya rejareja na maduka ya jumla kutoka shilingi elfu arobaini (40,000) hadi shilingi elfu ishirini (20,000/=);
  • Kupunguza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kwenye vituo vidogo vya kuzalisha na kugawa umeme chini ya Megawatt 10 kutoka shilingi milioni sita (6,000,000/=) hadi shilingi laki mbili (200,000/=);
Aidha, napendekeza pia kufanya marekebisho ya Sheria ya Jeshi ya Zimamoto na Uokoaji Sura 427, ili kuanzisha viwango vipya vya tozo kama ifuatavyo:
  • Kutoza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto ya shilingi milioni mbili (2,000,000/=) kwenye mitungi ya gesi yenye ujazo wa gesi kati ya tani 11 hadi tani 20; na
  • Kutoza tozo ya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto kati ya shilingi elfu arobaini (40,000/=) hadi shilingi milioni tano (5,000,000/=) kwenye taasisi ndogo za mikopo kutegemea na ukubwa wa eneo.
Lengo la hatua hizi ni kuweka mazingira rafiki ya kibiashara na uwekezaji ili kuchochea uzingatiaji wa sheria kwa hiari na kuongeza wigo wa wadau wanautumia huduma za Jeshi la Zimamoto.
  • Wizara ya Mifugo na Uvuvi
  • Sekta ya Mifugo
  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye tozo mbalimbali kwenye Sekta ya Mifugo kama ifuatavyo:
  • kufuta tozo ya kibali cha kusafirisha ngozi ndani na nje ya wilaya iliyokuwa ikitozwa shilingi elfu tano (5000/=) kwa kibali; na
  • Kupunguza tozo mbalimbali kwenye sekta ya mifugo na mazao kama zilivyoanishwa kwenye Jedwali Na 2 na Na.3: –

Jedwali Na. 2: Tozo za Vibali vya Kusafirisha Mifugo na Mazao Yake kwenda Nje ya Nchi (shilingi)
Na.Aina ya Mfugo/ZaoKipimoTozo za ZamaniTozo Pendekezwa
1Ng’ombeKila mmoja30,00025,000
2Kondoo/MbuziKila mmoja7,5005,000
3Nyama ya ng’ombeKilo moja150100
4Chakula cha wanyamaTani20,00010,000
5Mayai ya kulaTrei 1 (mayai 30)1,000100
Jedwali Na. 3: Tozo za Vibali vya Kuingiza Mifugo na Mazao yake ndani ya Nchi (shilingi)
Na.Aina ya Mfugo/ZaoKipimoTozo za zamaniTozo mpya
1PundaKila mmoja10,0005,000
2NgamiaKila mmoja10,0005,000
3Nyama ya ng’ombeKilo moja5,0004,000
4Chakula cha wanyamaTani20,00010,000
  • Kuongeza tozo mbalimbali kwenye sekta ya mifugo kama zilivyoainishwa kwenye Jedwali Na 4 na 5 ili kuhuisha tozo hizo kulingana na hali ya sasa ya thamani ya fedha;
Jedwali Na. 4: Tozo za Vibali vya Kusafirisha Mifugo na Mazao yake kwenda Nje ya Nchi (shilingi)
Na.Aina ya Mfugo/ZaoKipimoTozo za ZamaniTozo Pendekezwa
1FarasiKila mmoja30,00050,000
2Mbwa/pakaKila mmoja20,00050,000
3NgamiaKila mmoja30,00050,000
4Wanyama poriKila mmoja30,00050,000
5MbeguKwa mrija1,0002,000

Jedwali Na. 5: Tozo za Vibali vya Kuingiza Mifugo na Mazao yake ndani ya Nchini (shilingi)
Na.Aina ya Mfugo/ZaoKipimoTozo za zamaniTozo Pendekezwa
1FarasiKila mmoja10,00050,000
2Mbwa/pakaKila mmoja30,00050,000
3Mayai ya kulaTrei (Mayai 30)2,5005,000
  • Kuongeza ada ya kutunza mbuzi au kondoo kwenye vituo vya karantini, kupumzishia mifugo na ukaguzi kwa kila mmoja kutoka shilingi mia mbili (200/) hadi shilingi mia tano (500);
  • Kutoza tozo mpya za vibali vya kusafirisha nje ya nchi na kuingiza ndani ya nchi mifugo na mazao yake kama ilivyoainishwa kwenye Kiambatisho Na. 5
  • Kutoza shilingi elfu ishirini (20,000/=) kwa kibali cha kusafirisha pembe za ng’ombe, mbuzi na kondoo pamoja na kwato na mifupa ndani na nje ya Wilaya;
  • Kutoza shilingi elfu tano 5,000/= kwa kila kibali cha kusafirisha chakula cha Wanyama ndani na nje ya Wilaya;
  • Kutoza kibali kwa ajili ya huduma kwa mifugo na mazao yake wanaopita nchini kwenda nchi nyingine kama zilivyoainishwa kwenye Kiambatisho Na. 6.
  • Sekta ya Uvuvi
  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufuta tozo mbalimbali kwenye Sekta ya Uvuvi kama ifuatavyo:
  • Kufuta tozo ya mrabaha wa dola za Marekani 0.4 kwa kilo ya samaki katika uvuvi wa bahari kuu;
  • Kupunguza ada za leseni ya kuuza samaki na mazao ya uvuvi yanayovuliwa kwenye maji baridi (maziwa, mabwawa na mito) nje ya nchi kama zilivyoainisha kwenye Jedwali Na. 6
  • Kupunguza ada za leseni ya kuuza samaki na mazao ya uvuvi yanayovuliwa kwenye maji chumvi (bahari) nje ya nchi kama zilivyoainisha kwenye Jedwali Na. 7.
  • Kupunguza tozo za mrabaha wa kusafirisha samaki nje ya nchi kama ilivyoainishwa kwenye Kiambatisho Na. 7.
  • Kuongeza ada ya leseni ya kuuza Mapezi /taya za papa nje ya nchi kutoka dola za kimarekani 2,700 hadi dola za kimarekani 5,000 kwa ajili ya kuendelea kuhifadhi papa na jamii zake ambao wako hatarini kutoweka;
  • Kutoza ada ya leseni ya kusafirisha aina nyingine ya mabondo na makome nje ya nchi kama ilivyoainishwa kwenye Jedwali Na. 8.
  • Kutoza ada ya cheti cha afya ya samaki na mazao yake yanayosafirishwa nje ya nchi (QA/APP/02) shilingi 30,000/= kwa ajili ya kukidhi matakwa ya soko la nje na afya ya mlaji;
  • Kutoza tozo za vibali vipya vya kusafirisha samaki na mazao yake kama ilivyoainishwa kwenye Jedwali Na. 9 kwa ajili ya kuendeleza uhifadhi wa mazao hayo.
Jedwali Na. 9: Mapendekezo ya Kutoza vibali vipya vya kusafirisha samaki na mazao yake
Na.Aina ya Samaki/ZaoIdadiTozo Pendekezwa (Shilingi)
1Kaa haiKilo moja100
2Kamba kochi haiKilo moja100
3Samaki hai wa mapambo waliokamatwa maji ya asiliKipande kimoja200
  • Wizara ya Maliasili na Utalii
  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya mabadiliko ya tozo za viingilio na huduma mbalimbali zinazotolewa na Makumbusho ya Taifa kama zilivyoainishwa kwenye Kiambatisho Na. 8. Lengo la mabadiliko haya ni kuongeza Mapato ya Serikali kwa kuwa viwango vinavyotumika sasa ni vya toka mwaka 2002.
  • Mabango na Matangazo
  1. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho kwenye Jedwali la viwango vya tozo chini ya Kanuni za Ada ya Mabango na Matangazo [Local Government Finance (fees for Billboards, Posters and Hoarding) Order 2019], ili kupunguza kiwango cha tozo ya matangazo kwenye magari ya wazalishaji wa bidhaa yanayotumika kusafirisha bidhaa hizo toka viwandani kwenda kwa wasambazaji kutoka kiwango cha sasa cha shilingi 10,000 hadi shilingi 4,000. Lengo la mabadiliko haya ni kukidhi maombi ya wazalishaji dhidi ya tozo hii iliyosababisha wazalishaji wa bidhaa kuondoa matangazo kwenye magari hayo hivyo kupunguza mapato ya Serikali kutoka kwenye chanzo hicho.
Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni 1.25
  • Mfumo wa ukusanyaji wa maduhuli yanayotokana na sekta ya utalii na mazao ya misitu
  1. Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa maduhuli yanayotokana na sekta ya utalii na mazao ya misitu, Serikali inapendekeza ukusanyaji wa maduhuli hayo ufanywe na Mamlaka ya Mapato Tanzania na mapato hayo yaingie katika Mfuko Mkuu wa Hazina. Utekelezaji wa hatua hii utahusisha marekebisho katika Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Sura 399, Sheria ya Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro, Sura 284, Hati ya Kuanzisha Mamlaka ya Hifadhi ya Wanyamapori ya mwaka 2014, na Sheria ya Hifadhi za Taifa, Sura 282 kupitia Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2020 (The Finance Bill, 2020) ili:
  • Kuipa TRA mamlaka kisheria ya kukusanya maduhuli yanayokusanywa hivi sasa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), na Mamlaka ya Hifadhi ya Wanyamapori (TAWA);
  • Kuweka sharti la kisheria ili kuwezesha maduhuli yatakayokusanywa na TRA yahifadhiwe Mfuko Mkuu wa Hazina badala ya utaratibu wa sasa unaoruhusu taasisi hizi kubaki na mapato yake;
  • Kuweka utaratibu wa kisheria kwa taasisi hizo kutumia utaratibu wa bajeti ya Serikali na kuondoa mfumo wa kibajeti unaotumiwa na taasisi hizo kwa sasa.

  • Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na   Sheria nyingine mbalimbali.
  1. Mheshimiwa Spikanapendekeza kufanya marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika sheria mbalimbali za kodi pamoja na sheria nyingine ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha utekelezaji wake.
  • Tarehe ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi.
  1. Mheshimiwa Spika, hatua hizi za kikodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2020, isipokuwa pale itakapoelezwa vinginevyo. Aidha, Marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2020 na Matangazo ya Serikali (Government Notices).

  1. SURA YA BAJETI KWA MWAKA 2020/21
  1. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia shabaha, malengo pamoja na sera za bajeti kwa mwaka 2020/21, Sura ya Bajeti inaonesha kuwa jumla ya shilingi trilioni 34.88 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho. Jumla ya mapato ya ndani (ikijumuisha mapato ya Halmashauri) yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 24.07, sawa na asilimia 69.0 ya bajeti yote. Kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya shilingi trilioni 20.33; mapato yasiyo ya kodi ya shilingi trilioni 2.92 na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri shilingi bilioni 815.0.
  1. Mheshimiwa Spika, Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 4.90 kutoka soko la ndani. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 3.32 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na kiasi cha Shilingi trilioni 1.59 sawa na asilimia 1.0 ya Pato la Taifa ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Aidha, shilingi trilioni 3.04 zinatarajiwa kukopwa kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara kwa lengo la kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu.
  2. Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wanatarajia kuchangia misaada na mikopo nafuu yenye jumla ya shilingi trilioni 2.87 ambayo ni asilimia 8.2 ya bajeti. Kati ya kiasi hicho, miradi ya maendeleo ni shilingi trilioni 2.46; Mifuko ya Pamoja ya Kisekta shilingi bilioni 138.3; na Misaada na Mikopo nafuu ya Kibajeti (General Budget Support-GBS) shilingi bilioni 275.5.
  1. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2020/21, Serikali inapanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 34.88 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 22.10 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 63 ya bajeti na shilingi trilioni 12.78 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida zinajumuisha shilingi trilioni 10.48 kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali, shilingi trilioni 7.76 kwa ajili ya mishahara na shilingi trilioni 3.74 kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (OC) ambayo yanajumuisha shilingi bilioni 481.9 kwa ajili ya matumizi yatokanayo na vyanzo vya ndani vya Halmashauri.
  1. Mheshimiwa Spika, matumizi ya maendeleo ni shilingi trilioni 12.78, ambayo ni sawa na asilimia 37 ya bajeti yote na yanajumuisha fedha za ndani shilingi trilioni 10.04 na fedha za nje shilingi trilioni 2.74. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 2.10 ni kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa reli kwa kiwango cha Standard Gauge; shilingi trilioni 1.60 ni kwa ajili ya mradi wa kufua umeme Mto Rufiji; shilingi bilioni 823.7 ni kwa ajili ya mifuko ya Reli, Maji na REA; shilingi bilioni 490 ni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; na shilingi bilioni 298.1 kwa ajili ya elimumsingi bila ada. Aidha, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 600.0 kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya watumishi, watoa huduma na makandarasi wa barabara, maji na umeme.
  1. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa bajeti kama nilivyoeleza, sura ya bajeti kwa mwaka 2020/21 ni kama inavyooneshwa katika Jedwali A.
  • SHUKRANI
  1. Mheshimiwa Spika, tofauti na ilivyozoeleka naomba nianze salamu za shukrani kwa kutoa pole kwa Watanzania waliopatwa na majanga mbalimbali na misiba, nikianza na Bunge ambalo liliwapoteza wenzetu, Mheshimiwa Rashid Ajali Akbar, aliyekuwa Mbunge wa Newala vijijini (CCM), Mheshimiwa Mchungaji Dkt. Getrude Pangalile Rwakatare, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mheshimiwa Richard Mganga Ndasa aliyekuwa Mbunge wa Sumve (CCM) na Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga, aliyekuwa Mbunge wa kuteuliwa (CCM) na Waziri wa Katiba na Sheria. Ninawashukuru wote hawa kwa mchango wao mkubwa kwa Taifa na tunamwomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema peponi. Amina! Aidha, natoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao kutokana na majanga mbalimbali ikiwemo homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Natumia nafasi hii kuwashukuru watu wote walio katika mstari wa mbele kupambana na ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na: Madaktari na wahudumu wa afya; timu ya Serikali ya uratibu; na wadau mbalimbali ambao kwa namna moja au nyingine wamechangia fedha na vifaa kusaidia katika mapambano haya. Aidha, napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru viongozi wote wa dini zetu zote kwa kuendelea kuiombea nchi yetu amani, umoja na mshikamano wa Kitaifa.
  1. Mheshimiwa Spika, niwashukuru pia wananchi wenzangu wa Wilaya za Buhigwe na Kasulu na mkoa wetu wa Kigoma kwa ujumla ambao walinilea na kunifunda kufanya kazi kwa bidii. Pia naendelea kuwashukuru wananchi wa vijiji vya Nzinje (Zuzu) na Mayamaya hapa Dodoma kwa kunipokea mimi na familia vizuri sana. Aidha, naishukuru familia yangu, hususan mke wangu Mbonimpaye kwa kuniombea na kunipa raha na utulivu nyumbani na hivyo kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu ipasavyo. Shukrani zangu pia, kwa wanangu, wajukuu, ndugu zangu, majirani na marafiki wote wa familia kwa kunivumilia, kunibariki na kunitia moyo.
  1. Mheshimiwa Spika, ninawashukuru viongozi na watumishi wenzangu wa Wizara ya Fedha na Mipango, kwa ushirikiano mkubwa walionipa na kwa kujituma katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara na maandalizi ya bajeti hii ya Watanzania. Kipekee ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Ashatu K. Kijaji, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Jimbo la Kondoa. Nawasihi wananchi wa Kondoa wamrudishe mama huyu kwa kura za kishindo katika Bunge lijalo; Ninamshukuru sana Katibu Mkuu HAZINA na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Doto M. James, pamoja na Naibu Makatibu Wakuu, Amina Kh. Shaaban, Adolf H. Ndunguru na Mary N. Maganga pamoja na watumishi wa kada zote wa Wizara ya Fedha na Mipango. Nawakumbusha mwendelee kuchapa kazi. Ninawapenda na Mungu awabariki. Aidha, ninamshukuru Profesa Florens D. Luoga, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania kwa kusimamia sekta ya fedha kwa ustadi pamoja na Naibu Gavana wote watatu (Dkt. Yamungu Kayandabila, Dkt. Bernard Kibesse na Bw. Julian R. Banzi). Pia namshukuru Dkt. Edwin Mhede Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Naibu wake Bw. Msafiri Mbibo kwa kuvunja rekodi ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Vile vile, namshukuru CPA Charles E. Kichere, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kazi nzuri ikiwa ni pamoja na kukagua mashirika yetu makubwa kwa kutumia wataalam wa ndani kwa mara ya kwanza na CPA Athumani S. Mbuttuka, Msajili wa Hazina kwa kuvunja rekodi ya ukusanyaji wa gawio na michango ya mashirika kwenye Mfuko Mkuu. Ninamshukuru pia Dkt. Albina A. Chuwa, Mtakwimu Mkuu wa Serikali kwa kusimamia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) vizuri.
  1. Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru Washirika wetu wa Maendeleo kwa misaada na mikopo nafuu wanayoendelea kutupatia katika kutekeleza miradi na programu mbalimbali za maendeleo nchini. Katika bajeti ya mwaka 2020/21, Washirika wa Maendeleo kwa pamoja wanatarajia kuchangia jumla ya shilingi trilioni 2.87. Washirika wanaotarajiwa kuchangia bajeti ya Serikali ni pamoja na: nchi wahisani ikijumuisha Canada, China, Denmark, Finland, India, Ireland, Italia, Japan, Korea ya Kusini, Marekani, Norway, Poland, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Ujerumani, Uingereza, na Uswisi. Aidha, yapo mashirika ya fedha ya kimataifa yakiwemo: Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Benki ya Dunia, Arab Bank for Economic Development in Afrika (BADEA), Global Fund, Kuwait Fund, Abu Dhabi Fund, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU), Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), OPEC Fund, Global Environmental Facility (GEF), Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA), Mfuko wa kukinga Hatari ya Kimazingira (GRMF), Climate Development Special Fund, African Legal Support Facility (ALSF), Dignity, Global Agriculture and Food Security Program (GAFSP),na Mashirika ya Umoja wa Mataifa yakiwemo UNICEF, IFAD, UNDP, UNFPA, Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), na United Nations Environment Programme (UNEP). Napenda pia kutambua ushirikiano mzuri tulionao na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Ni matarajio yetu kuwa misaada ya kiufundi na fedha zilizoahidiwa na marafiki zetu hawa zitatolewa kwa wakati na kwa kiasi kilichoahidiwa. Nasi, kwa upande wa Serikali tunaahidi kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha hizo kama ilivyokusudiwa.
  1. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kutoa shukrani za dhati kwa Katibu Mkuu Kiongozi Mheshimiwa Balozi Mhandisi John William Kijazi, Waheshimiwa Mawaziri wa SMT na SMZ, Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Prof. Adelardus Kilangi, Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Wakuu, Katibu wa Bunge Bw. Stephen Kagaigai, Mtendaji Mkuu wa Mahakama Bw. Mathias Kabunduguru, Naibu Makatibu Wakuu pamoja na watumishi wote wa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma kwa kazi zao nzuri za kuwatumikia wananchi katika maeneo yao na kwa ushirikiano mkubwa sana walionipa mimi na watumishi wenzangu wa Wizara ya Fedha na Mipango katika kutekeleza majukumu ya msingi ya Wizara hii.
  1. Mheshimiwa Spika, Napenda pia nitumie fursa hii kumpongeza na kumshukuru kwa dhati Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, kwa kuongoza shughuli za Kamati hii muhimu kwa umahiri mkubwa. Ninawashukuru wajumbe wote wa Kamati ya Bajeti. Ninakiri kuwa wakati wote wametupatia maoni na ushauri makini ambao umeisadia Serikali katika kuimarisha utekelezaji wa bajeti na mpango wa maendeleo wa Taifa na katika kuboresha mapendekezo ya bajeti hii. Kati yao ninawaombea wale wenye sare za kijani wapate ushindi usio na shaka katika majimbo yao ili warejee katika Bunge lijalo.
  1. Mheshimiwa Spika, napenda niwapongeze na kuwashukuru kwa dhati wakuu wote wa vyombo vya ulinzi na usalama, makamanda na askari wote kwa uzalendo na nidhamu ya hali ya juu. Naomba niwataje Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo; Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Nyakoro Sirro; Kamishna Jenerali wa Magereza, Suleiman Mungiya Mzee; Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala; Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji, John William Hasunga; Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Diwani Athuman Msuya; Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Brigedia John Julius Mbungo; na Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, James Wilbert Kaji. Hakika, Watanzania tunatembea kifua mbele na kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi bila wasiwasi kutokana na umahiri wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.
  1. Mheshimiwa Spika, nampongeza Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa utendaji wake makini hususan katika kusimamia misingi ya Chama Cha Mapinduzi, kuimarisha umoja, mshikamano na kutetea haki za wanyonge. Aidha, naipongeza Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kuendelea kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 uliozaa matokeo ya kishindo niliyoeleza hapo awali.
  1. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza waheshimiwa Marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa mzee Ally Hassan Mwinyi, Mheshimiwa mzee Benjamin William Mkapa na Mheshimiwa mzee Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na wenzi wao kwa mchango mkubwa waliotoa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Taifa letu na tunaendelea kunufaika na busara na hekima za wazee hawa katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
  1. Mheshimiwa Spika, nakushukuru pia wewe binafsi Mhe. Job Yustino Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Kongwa bila kumsahau Naibu Spika Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson kwa kuendesha Bunge kwa umahiri mkubwa wakati wote na kwa ubunifu wako hadi kulifikisha Bunge kuwa la kidigitali. Kadhalika, ninampongeza sana Mheshimiwa Profesa Ibrahim Hamisi Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania pamoja na Mheshimiwa Dkt. Eliezer Feleshi, Jaji Kiongozi kwa uongozi makini na mahiri wa mhimili wa Mahakama.
  1. Mheshimiwa Spika, kwa umuhimu wa kipekee nawapongeza na kuwashukuru waheshimiwa wenzi wa viongozi wakuu wa kitaifa, Mwalimu Janet Magufuli, Bwana Ameir Hafidh Ameir, Mama Mwanamwema Shein, Mwalimu Mary Majaliwa, Dkt. Fatuma Ramadhani Mganga, na Mama Marina Papadopoulos Juma kwa kuwawezesha viongozi wetu wakuu wa kitaifa kutekeleza vizuri majukumu yao kwa utulivu.
  1. Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa kwa kusimamia bila kuchoka shughuli za Serikali. Ni mchapa kazi, muungwana na mnyenyekevu ambaye kwenye vikao anavyoviongoza vya Baraza la Kazi anajishusha kwa kutuita sisi “Mawaziri wenzangu’’. Kwa heshima na taadhima rai yangu kwa wananchi wa Ruangwa ni kuwa wampitishe Mheshimiwa Kassim Majaliwa bila kupingwa katika Uchaguzi Mkuu ujao. Aidha, napenda kumshukuru Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kazi nzuri na ushauri wake kwa Rais wa Zanzibar. Naomba pia nimpongeze kipekee Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuendelea kuiongoza Zanzibar kwa hekima na uadilifu, hali ambayo imewaletea wananchi wa Zanzibar umoja, utulivu na maendeleo ya kijamii na uchumi katika kipindi chote cha uongozi wake. Tunamwombea maisha ya amani baada ya kukabidhi kijiti kwa Rais wa Zanzibar atakayefuata. Vile vile, natoa shukrani za kipekee kwa Mheshimiwa mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hekima na mfano maridhawa wa uwezo mkubwa wa wanawake katika uongozi ambao umechangia mafanikio tuliyoyapata katika kujenga nchi yetu na kuimarisha Muungano wetu.
  1. Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha hotuba hii, naomba kutoa ushuhuda wangu juu ya Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Natanguliza kuomba msamaha wake kama baadhi ya haya nitakayosema asingependa niyaseme hapa. Nimeamua niyaseme kwa ajili ya kumbukumbu lakini zaidi ili watanzania wajue waziwazi mkuu wa nchi tuliyenaye hivi sasa ni kiongozi wa namna gani ili itusaidie wote kutambua na kutimiza wajibu wetu kwa Taifa letu la Tanzania.
  2. Mheshimiwa Spika, Baba huyu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ni kiongozi mwenye maono na uwezo mkubwa. Aidha, ana kipaji cha hali ya juu cha kufanya yasiyowezekana (ability to make the impossible happen)! Ni kiongozi ambaye anafahamu vema kuwa ili nchi ifanikiwe kuleta mabadiliko chanya ni lazima kuvunja kabisa utaratibu wa kufanya kila kitu kwa mazoea (break the status quo in order to break through). Ni jemadari anayetambua vema kwamba bila jasho hakuna tuzo (no pain, no gain) na huu ndiyo msingi wa kauli mbiu ya HAPA KAZI TU! Ni kiongozi jasiri ambaye anajiamini na ana ndoto kubwa kwa maendeleo ya nchi (has no room for small dreams), tena hana woga wa kushindwa (has guts to conquer the fear of failure). Kwa sababu hizo amekuwa akituasa watanzania tubadilike na kujiamini. Kwa maneno yake mwenyewe amekuwa akituambia “watanzania tunaweza, Tanzania siyo masikini”.
  1. Mheshimiwa Spika, tangu mwanzo wa utawala wake Rais Magufuli amepambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi. Amevunjavunja mazoea ya udanganyifu uliokuwa umekithiri kila kona kama vile watumishi hewa, mishahara na posho kwa watumishi vizuka, mikopo kwa wanafunzi ambao hawapo, madai ya kugushi ya pembejeo na marejesho ya kodi ya ongezeko la thamani. Rais huyu ni mfuatiliaji makini, tena kwa takwimu, wa kila kinachoendelea katika kila eneo la utawala. Rais Magufuli alijipa kazi ya kutumbua majipu na ameifanya kazi hiyo bila kupepesa macho ndani ya Serikali na hata ndani ya CCM. Ni dhahiri kwangu kuwa Rais Magufuli ni muumini wa mafundisho ya uongozi ya Peter Ferdinand Drucker (ingawa sina hakika kama Rais wetu alisoma maandishi ya mtaalam huyo mashuhuri) kwamba, naomba kunukuu kwa Kiingereza “It is the duty of the executive to remove ruthlessly anyone – and especially any manager – who consistently fails to perform with high distinction. To let such a man stay on corrupts others“. Tafsiri yake ni kuwa ni wajibu wa mtendaji mkuu kumuondoa bila huruma mtumishi yeyote – na hasa meneja yeyote – ambaye daima anashindwa kutekeleza kazi zake kwa kiwango cha kupata nishani. Kuacha mtu kama huyo aendelee kazini inashawishi wengine kufanya vibaya!
  1. Mheshimiwa Spika, kiongozi wetu mkuu amesimamia kwa karibu nidhamu ya matumizi katika wizara, idara na taasisi za Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa ikiwa ni pamoja na kudhibiti safari za watumishi wa umma nje ya nchi, hata yeye mwenyewe hajasafiri nje ya Bara la Afrika tangu alipochukua hatamu za uongozi wa nchi hadi sasa; amefuta baadhi ya sherehe za kitaifa na kuelekeza fedha zilizokuwa zimepangwa zitumike kwenye maeneo mengine yenye uhitaji mkubwa; na alipiga marufuku “MKUKUBI”. Kwa wasiofahamu MKUKUBI ni kifupi cha kilichokuwa kinaitwa kininja kama ‘Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Binafsi’ kupitia posho za kwenye makongamano, semina na warsha zilizokuwa zinafanyika kwenye kumbi za kukodi na hoteli. Aidha, alipunguza misafara mirefu ya kusindikiza viongozi kwenda kwenye matibabu au kupima afya zao nje ya nchi huku wakiacha hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali za rufaa nchini zikiwa zinadidimia. Mtakumbuka pia alichukua hatua isiyotarajiwa ambayo iliduwaza watu wengi na hata kupelekea wengine kumlaumu pale alipoamua kumpeleka mke wake (First Lady) hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu ambapo alilazwa kwa siku kadhaa badala ya kumpeleka nje!
  1. Mheshimiwa Spika, Rais Magufuli ni Jemadari mwenye msimamo usiotetereka hata kwenye kilele cha hatari (crisis) kama wakati wa malalamiko kuwa “vyuma vimebana”, pia katika kipindi cha uhaba wa mafuta ya kula na hivi karibuni wakati watawala wengine wakilazimisha wananchi wao kubakia majumbani (Lock down) ili kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID – 19), kwa mshangao wa wengi Rais Magufuli aliagiza watanzania waendelee kuchapa kazi, na wazingatie maelekezo ya wataalam wa afya kujikinga na CORONA huku wakiendelea kumwomba Mungu! Aidha, katika nafasi yake ya Amiri Jeshi Mkuu, ameendelea kiliamini Jeshi, kulijengea uwezo na kulishirikisha katika miradi mbalimbali ya kimkakati ya ujenzi wa uchumi wa nchi yetu.
  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha utawala wake Rais Magufuli ameendelea kumtanguliza Mungu katika kazi zake na kuwaelekeza viongozi anaowateua na wananchi kwa ujumla nao wafanye hivyo hivyo. Ameonesha unyenyekevu na ukarimu sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuenzi mchango wa awamu za uongozi zilizotangulia, kuchangia ujenzi wa nyumba za ibada (misikiti na makanisa), kukusanya sadaka kanisani yeye mwenyewe, kushiriki misiba ikiwa pamoja na ile inayogusa viongozi wa vyama vya upinzani, kutembeza sinia lenye vitafunio vya chai pale ikulu Dar es Salaam na Chamwino kwa ajili ya wageni wake, na kunywa kahawa au kununua bidhaa na matunda kutoka kwa wajasiriamali wadogo. Rais Magufuli ana huruma na anaumizwa na kilio na machozi ya wanyonge au waliodhulumiwa na hasiti kuwafuta machozi hapo hapo. Ni kwa mantiki hiyo kiongozi wetu huyu amewatembelea wafungwa magerezani kujionea hali halisi na kuongea nao na kufanya uamuzi wa kusamehe idadi kubwa sana ya wafungwa na mahabusu. Kama hiyo haitoshi, baba huyu ameendeleza moyo wake wa msamaha hata kwa waliombeza na kumtusi!
  1. Mheshimiwa Spika, Kiongozi wetu mkuu ni mzalendo namba moja ambaye amevaa koti la Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius K. Nyerere na kufufua ndoto zake za maendeleo ya Taifa letu. Alianza kwa kupiga vita rushwa na ukwepaji kodi vilivyokuwa vimekithiri bandarini na TRA na kufanikiwa kuongeza ukusanyaji wa mapato ya kodi kutoka wastani wa shilingi bilioni 825 kwa mwezi kabla ya utawala wake hadi wastani wa shilingi trilioni 1.5 kwa mwezi katika mwaka 2019/20; Aidha alielekeza mikataba ya madini na huduma muhimu kama mawasiliano ipitiwe upya na kutunga Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusiana na Umiliki wa Maliasili ya mwaka 2017 ili kulinda rasilimali za Taifa na kuhakikisha watanzania wananufaika, na kujenga uzio wenye urefu wa kilometa 24.5 kuzunguka mgodi wa madini ya tanzanite Mirerani na kuanzisha masoko ya madini; Aidha, aliamua kutekeleza maamuzi ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama cha TANU kilichofanyika tarehe 30 Agosti hadi tarehe 1 Septemba mwaka 1973 kuhamisha makao makuu ya Serikali kutoka Dar es Salaam kuja hapa Dodoma.
  1. Mheshimiwa Spika, Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli amethubutu kutekeleza miradi mikubwa ya kielelezo iliyobuniwa na Baba wa Taifa ikiwa ni pamoja na bwawa la Nyerere la kuzalisha umeme wa MW 2,115 katika mto Rufiji; kujenga uchumi wa viwanda; kujenga reli ya kati ya kisasa (Standard Gauge Railway); kufufua Shirika la Ndege la Tanzania kwa kununua ndege mpya 11 na kujenga viwanja vya ndege; kuendeleza ujenzi wa barabara kuu na za mikoa kwa kiwango cha lami na madaraja makubwa; kununua meli mpya za abiria na mizigo na kukarabati zile za zamani na vivuko pamoja na kupanua au kuboresha bandari katika ukanda wa bahari na maziwa makuu; kutoa elimumsingi (shule ya msingi hadi kidato cha nne) bila ada na kuongeza mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu; mradi kabambe wa kupeleka umeme vijijini (REA) ambapo hadi sasa vijiji 9,112 kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara (asilimia 74.3) vimeunganishiwa umeme; ameendelea kupiga vita adui maradhi kwa kuimarisha huduma za afya nchini kama ilivyoelezwa kwa kirefu katika taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa niliyosoma leo asubuhi.
  1. Mheshimiwa Spika, Rais wetu huyu ana akili ya kisayansi ya kudadisi na kuhoji kila jambo ikiwa ni pamoja na usahihi wa vipimo vya mafuta ghafi ya kula na hata ugonjwa wa CORONA. Rais Magufuli amekuwa mfano bora wa kutumia na kuenzi lugha ya kiswahili hata kufikia kuwa moja ya lugha zilizokubalika kutumika katika Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC.
  1. Mheshimiwa Spika, Rais Magufuli ni kiongozi anayetuhimiza watanzania kuwa wamoja na kusisitiza kuwa maendeleo hayana chama. Mheshimiwa Rais Magufuli ana nidhamu kubwa ya kufanya kazi (relentless work ethic). Waheshimiwa mawaziri wenzangu wanafahamu vizuri simu zake za usiku wa manane kuanzia saa 8 hadi saa 11 alfajiri! Kwa sababu hiyo baadhi yetu ilitubidi kubadilisha hata muda wa kulala usingizi! Hii ilinikumbusha maneno ya Shimon Peres aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israel kwa mawaziri wake kwamba wakati wa vita, waziri wa Israel hana budi kutosinzia… Ni wajibu wake kubaki macho! (An Israel Minister shouldn’t sleep … It is a minister’s duty to stay awake).
  1. Mheshimiwa Spika, mwisho, japo si kwa umuhimu Rais wetu ni mkakamavu na mpenzi wa maendeleo ya michezo nchini. Mnafahamu katika ubora wake, mazoezi ya push-ups anazopiga usiige! Mtakumbuka pia jinsi alivyowaalika ikulu Dar es Salaam vijana wetu wa timu ya Taifa wenye umri chini ya miaka 17 na makocha wao ili kuwajengea ari ya utaifa na kushinda. Aidha, naamini hamjasahau siku Mhe. Magufuli alipokwenda uwanja wa Taifa kujionea mpambano wa watani wa jadi Yanga na Simba na kushuhudia mnyama akipigwa mkuki mmoja wa sumu kali na Benard Morrison! Inaonekana Mheshimiwa Waziri Mkuu, na wewe Mheshimiwa Spika na hata Mheshimiwa Naibu Spika machale yaliwacheza mapema siku hiyo hamkuonekana uwanjani!!
  1. Mheshimiwa Spika, huo ndio ushuhuda wangu juu ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa, na ushuhuda wangu ni wa kweli. Swali ambalo napenda kila Mtanzania ajiulize ni: Je, mimi na wewe tunatimiza kikamilifu wajibu wetu kwa nchi yetu? Kisha achukue hatua. Mojawapo ya suala ambalo nataka kuwaomba kwa unyenyekevu mkubwa, ni kwamba watanzania wote tuliojiandikisha kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba 2020 tumpe zawadi ya kura ya NDIYO Rais huyu ambaye amekuwa mfano wa kuigwa na wa kipekee katika bara la Afrika kama shukrani yetu kwake kwa kazi yake iliyotukuka ili aendelee kuipaisha nchi yetu ya Tanzania kwa kipindi cha pili cha miaka mitano. Watanzania msisahau pia kumpatia Rais wetu wabunge na madiwani wanaomudu maadili na mwendo wa HAPA KAZI TU, na kama itawapendeza wananchi wenzangu wa Buhigwe na Chama chetu, basi iwe pamoja na mimi mtumishi wenu! Nawaambia kweli watanzania wenzangu, Rais huyu ni tunu ya thamani kubwa kwa Tanzania na utawala wake ni fursa kubwa ambayo kama hatutaitumia vizuri, basi mjue itachukua miaka mingi ijayo kuifikia Tanzania mpya tunayoitamani. Na kwa mheshimiwa Rais, najua unafuatilia hotuba hii, sina maneno mazuri ya kukushukuru kwa kuniinua, kunipa heshima kubwa ya kulitumikia Taifa katika Serikali yako na kwa kuniongoza vizuri katika utumishi huu. Mwenyezi Mungu akubariki, akulinde, akufadhili na kukupa amani wewe na familia yako.

  • HITIMISHO
  1. Mheshimiwa Spika, hii ni hotuba yangu ya mwisho katika Bunge hili ambayo imeeleza mwenendo wa utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20, mafanikio ya kishindo yaliyopatikana na hatua muhimu ambazo Serikali inakusudia kutekeleza katika mwaka 2020/21.
  1. Mheshimiwa Spika, kwa kipindi hiki cha miaka 4 na miezi 5 ambacho nimepewa heshima na dhamana kubwa wa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango wa nchi yetu, nina jambo moja tu la kusema kwa watanzania: ASANTENI SANA!
Ninasema asanteni sana kwa sababu watanzania wengi nje na ndani ya Serikali wamekuwa wakinitia moyo na kuniongezea ujasiri wa kufanya kazi hii kwa manufaa ya Tanzania. Hata hivyo, mimi ni binadamu na kwa hakika siyo mkamilifu. Ninawashukuru kwa dhati wote walionikosoa kuhusu sera za uchumi na utekelezaji wa bajeti kwa nia ya kujenga na ninawaomba radhi pale ambapo niliwakwaza katika kutekeleza majukumu yangu lakini kwa wale wenye maslahi binafsi walioniona mimi ni kikwazo kwao, natumaini sasa wamenielewa na Mungu awasamehe! Na kwa yale niliyoweza kufanya vizuri sistahili kupewa sifa peke yangu kwa sababu tuliyafanya pamoja. Napenda niseme mambo mawili tu ya kuwaaga:
  • Kwa yeyote atakayeteuliwa katika nafasi hii baada yangu ajitahidi kujinyenyekeza kwa kuwa na hofu ya Mungu, asimamie maslahi ya Taifa na haki za wananchi wanyonge, ashinde vishawishi vya rushwa, azingatie sheria, kanuni na taratibu zinazo ongoza ukusanyaji wa mapato, ukopaji wa mikopo, upokeaji wa misaada, ugawaji wa rasilimali fedha na kusimamia matumizi ya Serikali ili yawe yenye tija na afanye hivyo bila kuyumba. Aidha, ajitahidi kuwa makini kufuatilia mwenendo wa uchumi wa Taifa na Dunia ili kushauri ipasavyo juu ya sera na mipango ya kiuchumi na hatua za kuipeleka Tanzania mbele. Katika hili, atumie ujuzi na uzoefu alio nao lakini pia ashirikiane na kuthamini ushauri wa wataalam ndani ya Serikali na taasisi zake. Aidha, ni muhimu sana afungue masikio yake kwa mahitaji ya sekta binafsi na ushauri wa Bunge.
  • Tanzania tuko katika vita ya kiuchumi ambayo ni lazima tushinde. Hakuna mbadala wa ushindi! Jambo la muhimu ni kwamba hatuna budi kujitambua, tuwajue vema maadui zetu wa ndani na nje na mbinu wanazotumia na tujipange kimkakati ikiwa ni pamoja na kuwahi kutumia vema fursa zinazoibuka na vile vile kuingia ubia na marafiki zetu ambao unanufaisha pande zote. Uwezo wa kupambana na kushinda vita hivyo tunao, sababu tunazo na nia tunayo. Hata hivyo, ili tushinde sharti la kwanza: lazima tuendelee kuwa wamoja na kuwa na uaminifu wa hali ya juu kwa Taifa hususan kulinda maslahi ya Taifa. Sharti la pili: Kuanzia muhula unaofuata wa Serikali ya Awamu ya Tano na kuendelea ni lazima pawepo ujasiri na kufanya maamuzi ya kuwekeza kwa kiasi kikubwa kibajeti kwenye sayansi na teknolojia mpya na ya kisasa kabisa kwa kuibua, kujenga, kulea na kuthamini vipaji na utaalamu na kwa kipekee kabisa ndani ya majeshi yetu na vile vile kwenye taasisi za utafiti na ufundi stadi na vyuo vikuu. Wakati umefika sasa Taifa letu liweke msukumo mahsusi kuamsha fikra bunifu za watanzania hasa vijana ambazo hazijatumika ipasavyo. Aidha, ni muhimu sekta binafsi ishiriki kuwekeza katika maendeleo ya sayansi na teknolojia na ichangamkie fursa zinazoambatana na uwekezaji huo katika sekta zote za uzalishaji na huduma. Nina hakika pia kuwa Mungu yuko upande wetu kama tutaendelea kumtegemea. Kwa upande wangu nawahakikishia kwamba nitaona fahari kuendelea kulitumikia Taifa letu katika Sekta ya umma au Sekta binafsi kadri Mungu atakavyonituma.
  1. Mheshimiwa Spika, napenda kumalizia kusoma hotuba yangu ya mwisho ya bajeti kuu ya Serikali kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa moyo wangu wote kwa ajili ya fadhili zake na uaminifu wake. Siku niliyomuita aliniitikia, akanifariji kwa kunitia nguvu. Nitaendelea kumhimidi kila wakati. Mtukuzeni Mungu pamoja nami.
MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Kiambatisho Na.5
Mapendekezo ya Tozo Mpya za Vibali vya Kusafirisha Nje ya Nchi na Kuingiza Ndani ya Nchi Mifugo na Mazao (shilingi)
Na.Aina ya Mfugo/ZaoKipimoKuingiza ndani ya NchiKusafirisha nje ya Nchi
1SunguraKila mmoja5005,000
2Mbegu zilizochambuliwa kijinsiaMrija2,0002,000
3Sampuli za kibailojiaKwa kibali5,000100,000
4Nyama ya kondoo/mbuziKilo moja4,00050
5Nyama ya nguruweKilo moja4,00020
6Nyama ya Wanyama poriKilo moja4,000500
7Nyama ya pundaKilo moja5,0001,000
8SosejiKilo moja4,00050
9mjeledi/misuliKilo moja150150
10Bidhaa zingine za nyamaKilo moja1,000150
11Vifungashio vya sosejiKibali50,0000
12Maziwa condensedLita moja2000100
13Maziwa yaliyotolewa mafutaLita moja2,000100
14Maziwa mtindiLita moja2,00050
15Maziwa ya ungaKilo moja2,000100
16Jibini / siagiKilo moja2,00020
17NyongoKibali100,000300,000
18Mbolea ya asiliTani moja5,0005,000
19Kemikali na vifaa vya maabaraKibali100,000100,000
20KitotoleshiKibali50,00010,000
21Vitamini/mawe ya madini/amino acids/ vyakula vilivyoongezewa virutubishoTani moja10,00010,000
22Vifaa vya utambuzi hereni za sikoni)Kibali50,000NIL
23Mawe ya kwenye nyongoKibali10,0000300,000
24Kuongeza muda ya leseni ambayo imepita mudaKibali50,00050,000
25Mikojo ya wanyamaKibali5,0005,000
26AsaliKibali200,000100,000
27Mbwa na paka kwa ajili ya vinasaba kwa ajili ya utafitiKila mmoja5,0003,000
28Kuku au ndege wafugwao kwa ajili ya vinasaba na utafitiKila mmoja2001,000
29Wanyama kwa ajili ya mapamboKibali20,00020,000

Kiambatisho Na.6
Mapendekezo ya Kutoza Kibali kwa Ajili ya Huduma kwa Mifugo na Mazao Yake Wanaopita Nchini Kwenda Nje ya Nchi (shilingi)
S/NAina ya Mfugo/zaoKipimoTozo (Tshs)
1Ng’ombeKila mmoja2,500
2Kondoo/mbuziKila mmoja1,500
3NguruweKila mmoja1,500
4Farasi / Mule / PundaKila mmoja2,500
5Mbwa/pakaKila mmoja1,000
6NgamiaKila mmoja2,500
7Kuku / KangaKila mmoja200
8Vifaranga1001,000
9Zaidi ya trei 100 za mayai ya kulaTrei la mayai 30500
10Zaidi ya trei 10 za mayai ya kutotoleaKila mmoja1,000
11Bata mzingaKila mmoja1000
12Kasuku/falcon/MbuniKila mmoja15,000
13Ndege wa poriniKila mmoja500
14SunguraKila mmoja500
15Vyura/ mijusi / waduduKibali20,000
16Wanyama wa maabaraKibali30,000
17Wanyama wa poriniKila mmoja1,000
18Nyara za SerikaliKibali30,000
19Nyama na mazao yake zaidi ya kilo 50Kilo50
20Soseji / nyama ya kusaga/ bidhaa zingine za nyamaKilo50
21NyongoKibali50,000
22Korodani/tendonsKibali200,000
23MaziwaLita500
24MtindiLita2,000
25Maziwa ya ungaKilo4,000
26Jibini / siagiKilo2,000
27Ngozi ya ng’ombeKipande500
28Ngozi ya mbuzi/kondooKipande100
29Pembe za ng’ombe, Mbuzi, kondoo, kwato na mifupaTani10,000
30Manyoya / sufuKibali20,000
31Chakula cha wanyamaTone10,000
32Mbolea ya kiboniTon5,000
33EmbryosEach500
34SemenStraws50
35SpecimenPermit20,000
36Maunzi / vifaa vya maabaraPermit300,000
37Vifaa vya utambuzi (mfano hereni za sikioni)Permit200,000

Kiambatisho Na. 7
Mapendekezo ya Kupunguza Tozo za Mrabaha wa kusafirisha samaki nje
No.Aina ya Samaki/ZaoTozo ya Sasa (US$)Tozo Pendekezwa (US$)
1Minofu ya samaki0.240.2
2Sangara aliyetolewa kichwa na matumbo0.250.21
3Sangara nzima aliyetolewa matumbo0.25
4Ngozi ya samaki0.15
5Dagaa-Victoria0.20.16
6Dagaa-Tanganyika10.5
7Dagaa-Nyasa0.30.16
8Furu waliokaushwa0.160.16
9Samaki wakavu0.30.3
10Kayabo, Ng’onda0.3
11Migebuka wabichi0.50.3
12Migebuka wakavu0.40.2
13Vipande vya minofu ya sangara0.240.2
14Sangara Wakavu0.30.2
15Makome ya Baharini0.075
16Kamba miti wasiokuwa na vichwa0.9
17Kamba miti wenye vichwa1.2
18Aina ya samaki wengine10.2
19Makome ya Maji baridi0.01
20Makome (Nyumba za Konokono)0.3
21Mabondo mabichi5% ya bei ya soko4% ya bei ya soko
22Mabondo makavu5% ya bei ya soko4% ya bei ya soko
23Mabondo mengineyo mabichi/makavu0.5

Kiambatisho Na 8
Tozo za Viingilio na huduma mbalimbali za makumbusho.
Na.HudumaKiingilio/Tozo zaa Sasa (Shilingi)Kiingilio /Tozo Pendekezwa (Shilingi)
Kwa Watanzania na Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
1.Kiingilio katika makumbusho
i)    Mtu mzima1,5002,500
ii)  Mwanafunzi5001,000
2.Kiingilio kwa makundi (Group)
i)            1-155,00010,000
ii)          15-307,00015,000
iii)        30-5010,00020,000
3.Kazi Miradi (school project)2,0002,500
4.Tozo za Tafiti (Research fee)9,00015,000
5.Maktaba /kusoma (studying)1,0002,000
6.Picha Mnato (still picture /Video shooting – educational)130,000300,000
7.Picha Mnato (commercial still picture /Video shooting)260,000500,000
8.Huduma za Maktaba (Library services / Archival pictures)2,0005,000
9.Majengo ya maonesho ya muda (Temporary Exhibition Halls)500,000600,000
10.Mifumo ya matangazo kwa umma (Public Adressing System – PA)250,000300,000
11.Jopo la maonesho (Exhibition Panel)10,00020,000
12.Maeneo tengefu ya kuona viumbe vya kale(Special reservation to see original hominids)20,000
13.Vyumba vya mikutano (Conference Room)700,000750,000
kwa wageni wa kutoka Nje ya Nchi za EAC
1.Kiingilio katika makumbusho
i)    Mtu mzima6,50012,000
ii)  Mwanafunzi (student)2,6006,300
2.Kiingilio kwa makundi (Group)
i)    1 – 1519,50030,000
ii)  15 – 3020,00035,000
iii)30-5030,00055,000
3.Tozo za tafiti (Research fee)$200$300 per month
4.Huduma za Maktaba (Library services / Archival pictures)20,000
5.Mfumo wa muziki (Music system)250,000300,000
6.Kutembelea viumbe wa kale (Visit Original Homide (zinj)$15$30 per head

No comments :

Post a Comment