Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Khamis Mussa Omar amejitosa kwenye mbio za Urais Zanzibar 2020 na kuchukua fomu kuomba ridhaa ya CCM. Khamis Mussa ndiye mshika funguo za hazina ya visiwa hivi, sehemu nyeti ambayo ili ukae lazima ama kuaminiwa ama kuwa sehemu ya ulaji. Amedumu muda mrefu katika nafasi hiyo. Mjadala mkubwa ulioibuka visiwani hapa baada ya yeye kuchukua fomu ni ule wa yeye ni nani hasa, ipi nafasi yake kwenye mbio hizi na nani wanamuunga mkono.
Khamis Mussa Omar
Khamis Mussa amekuwa ndani ya SMZ kwa muda mrefu na aliingia katika nafasi za juu toka enzi za awamu ya sita chini ya Amani Karume.
Kwa upande wa nguvu yake kwenye mbio hizi, Khamis Mussa anaungwa mkono na baadhi ya viongozi wa upinzani akiwemo Mansoor Himid wa ACT Wazalendo. Hata hivyo uswahiba wake na Mansoor ni wa kimaslahi kwani wawili hao walishirikiana kutoa Jumba la Msiige na kulikodisha kwa dola 1 kwa mwaka huku binafsi wakitia mamilioni ya dola mifukoni.
Kukaa kwake ndani ya SMZ kwa muda mrefu kunawezekana pia kuwa nguvu yake kwani imemsaidia kujenga marafiki na kufahamu maadui zake kwa muda wa kutosha.
Hata hivyo Khamis Mussa ana mnazi mrefu kukwea ili kuweza kupata nazi ya ugombea wa Urais Zanzibar kupitia CCM.
Mapungufu yake
Taarifa ziaonesha kuwa anaungwa mkono na watu mbalimbali mashuhuri kwenye siasa na biashara na mfanyabiashara Salim Hassan Abdullah Turky (Mr. White) ni mmoja ya watu hao. Turky anafahamika kama mcheza kamari za siasa Zanzibar akifadhili wanasiasa wengi ili kupata fadhila na ahueni mbalimbali kwenye kodi na sheria. Kama kuna jambo moja kubwa serikali ijayo Zanzibar inapaswa kulivunja vunja ni mahusiano kati ya Rais na wafanyabiashara wajanja wajanja wa namna hii. Mbali na madudu mengi, Turky amewahi kusema anayo SMZ mkononi pale alipompa Balozi wa Comoros passport ya Tanzania kinyume na sheria jambo ambalo ni kosa la jinai.
Mbali na mahusiano hayo na wafanyabiashara ambayo kwa namna ya uongozi wa sasa chini ya Magufuli anaweza kupigwa nyundo mapema, Khamis Mussa ni mfanyabiashara muri, akiwa mmoja ya wamiliki wa kampuni Exotic Tours & Safaris. Nyaraka zinaonesha kampuni hiyo imekuwa ikitumika kama wakala wa tiketi zote za ndege za wasafiri walio waajiriwa SMZ huku ikivuna mamilioni ya shilingi kwa mwaka kinyume na utaratibu wa manunuzi serikalini.
Jambo jengine linalompa doa katika mbio hizi ni hatua yake ya kulazimisha mkewe (Bi Nasra) kukaa kitengo cha kupokea marejesho kwenye Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRB). Mbali na hilo, yeye na mkewe huyo wanamiliki vitega uchumi vingi maeneno ya Forodhani tofauti na kipato chao jambo ambalo baadhi ya makachero wamekuwa wakilifanyia utafiti tangu Januari 2020 na sasa tayari wamekabidhi taarifa yao Kamati Kuu ya CCM.
Khamis Mussa pia anatajwa kuwa mmoja ya wanufaika wa ufisadi kwenye miradi ya ZSFF kama ule wa Mnara wa Kisonge. Mradi huo uliandikiwa bajeti mara mbili zaidi ya bajeti yake ya kawaida.
Katika sakata ka ufisadi wa Jumba la Mambo Msiige ambalo sasa ni Hoteli ya Park Hyatt, mwekezaji ASB Holding alilipa dola za Kimarekani milioni 3 (karibu shilingi bilioni saba), katika akaunti iliyofunguliwa PBZ kwa jina la serikali. Baadaye akaunti hiyo ilifungwa na fedha haikuingizwa kwenye hazina ya serikali na inaelezwa zilichotwa na Khamis Mussa akisaidiana na washirika wake.
Madudu yake wakati wa utawala wa Amani Karume
Kati ya mwaka 2005 hadi 2010, Khamis Mussa aliteuliwa na Amani Karume kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha. Inaelezwa kuwa Karume alimchukua kwa kazi maalumu ya kumuandalia mazingira mazuri ya kuchota fedha SMZ ili astaafu vizuri. Ikumbukwe kuwa hiki kilikuwa kipindi chake cha mwisho kama Rais wa Zanzibar.
Akiwa katika nafasi hii kwa kazi maalumu ya kuchota kwa tumbo lake na la Karume, Khamis Mussa aliunda timu kufanikisha hilo. Katika timu hii walikwepo aliyekuwa Mhasibu Mkuu Omar King (sasa msaidizi wa Ali Karume) na mwenye utajiri mkubwa Zanzibar na Tanzania Bara. Omar King pia ndiye mshika fedha za Khamis Mussa katika mbio za Urais. Katika timu hii pia yuko Katibu Mkuu Kiongozi Dk Abulahmid Yahya Mzee (Dudu Baya). Hawa wameapa kutumia kila nguvu kuulinda mfumo wa ulaji ambao waliuasisi mwaka 2005 huku Zanzibar ikiendelea kusinzia.
Khamis Mussa pia ana rekodi katika sakata la tenda za barabara wakati wa utawala wa Karume. Yeye ndiye aliyeamua kampuni aliyokuwa na maslahi nayo ipewe tenda na matokeo yake barabara zikajengwa bila kiwango Zanzibar. Kampuni hiyo ina ushirikiano wa kibiashara na familia ya Karume.
Ziko pia taarifa kuwa Khamis Mussa anatumia jina la Rais Dk Shein kuwa ndiye kamtuma na ndiye anamuunga mkono. Zanzibar Daily bado inafanyia kazi taarifa hizi kwani inawezekana analitumia vibaya jina la kiongozi wa nchi.
Sakata la Ufisadi mkubwa ZSSF
Akiwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Khamis Mussa amehusika kuidhinisha miradi mikubwa zaidi ya kifisadi kuwahi kutokea katika historia ya Zanzibar kwa kutumia fedha za walipo kodi masikini za Shirika la Maendeleo ya Hifadhi ya Jamii (ZSFF).
ZSSF Apartments Mbweni
Mradi wa kwanza ni ule wa apartments za ZSSF Mbweni. Ujenzi wa nyumba hizi ulipitishwa wakati Khamis Mussa akiwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na kupewa baraka zake. Ujenzi huo umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 20 fedha za walipa kodi wa Zanzibar. Wataalamu wa miradi ya namna hii wanasema kiasi hicho cha fedha ni karibu 35% zaidi ya gharama halisi, huku sehemu ya fedha hiyo ya chajuu (35%) ikiingia katika mifuko binafsi ya Khamis Mussa, Waziri aliyekuja kutimuliwa Dk Khalid Salum Mohamed, Waziri Issa Usi Gavu (aliyeshinikiza ZSSF kutoa fedha hizo) na washirika wao wengine ambao Zanzibar Daily ina orodha yao na namna wanavyotumia sehemu ya fedha hizo kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu.
Waziri Issa Usi Gavu (aliyeshinikiza ZSSF kutoa fedha hizo)
Wachambuzi wa siasa za Zanzibar wanasema Khamis Mussa ana wakati mgumu kupita katika kinyang’anyiro hicho hasa kutokana na ufisadi mkubwa ambao umepita katika mikono yake akiwa SMZ. Wengi wanasema waliomshauri kuchukua fomu wanataka kumuondoa katika utumishi wa umma kwa aibu. Nadharia yao inafafanuliwa kuwa, Khamis Mussa ni mtumishi wa umma mwandamizi, fisadi aliyedumu katika mfumo kwa muda. Mtumishi wa namna hii huwezi tu kumfukuza kazi, lazima kwanza kumuaminisha kwamba anaweza kuwa Rais. Imani hiyo huwa ni feki, akishaamini anaachwa kuendelea na mchakato ambao ataanguka kutokana na kupungukiwa sifa. Akianguka anakuwa pia ameanza rasmi anguko lake katika utumishi wa umma, na hapa anakuwa hana mchawi wa kutafuta wala mtu wa kumlaumu au kumtisha kuvujisha taarifa zake hasa kwa watawala waliomtumia kuchota SMZ. Inaelezwa kuwa kumsukuma kuchukua fomu ni mkakati wa kummaliza kistaarabu.
No comments :
Post a Comment