Mshirika mkuu wa serikali ya rais Felix Tshisekedi nchini DR Congo Vital Kamerhe amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela
Wakati Vital Kamerhe akifunga ndoa na Hamida Shatur mwezi Februari mwaka jana -miezi michache tu baada ya kufanyika kwa uchaguzi uliomuweka madarakani Rais Felix Tshisekedi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ilionekana kama dunia nzima iko miguuni mwake.
Lakini, leo hii, takribani miezi 16 tangu tukio hilo, Kamerhe yuko gerezani baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 kwa tuhuma za ufisadi na wizi wa dola milioni 50 za Marekani.
Yeye ndiye hasa aliyesababisha Rais Tshisekedi leo hii awe Rais wa DRC. Kupitia Muungano walioufanya wa CACH, wawili hao walifanikiwa kumshinda Martin Fayulu aliyekuwa akipewa nafasi kubwa ya kuwa mbadala wa Rais Joseph Kabila, aliyemaliza muda wake wa kikatiba kuongoza DRC.
Kesi hiyo imetikisa DRC na kuzua maswali mengi na mshangao. Taifa hilo linajulikana kwa viongozi wake kuhusika na rushwa lakini hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa serikali iliyo madarakani kufikishwa mahakamani na kufungwa kwa sababu ya rushwa tangu nchi hiyo ijipatie Uhuru.
Kamerhe hakuwa kiongozi wa kada ya chini wa serikali ya Tshisekedi. Ingawa cheo chake rasmi serikalini kilikuwa ni Katibu Mkuu Kiongozi au Mkuu wa Watumishi wa Umma wa DRC, wapo waliokuwa wakimwona kama Makamu wa Rais.
Nini hasa kimetokea kufikia hapa?
Fahali wawili hawakai zizi moja
Katika siasa za bara la Afrika, msemo wa mafahari wawili hawakai zizi moja umekuwa na ukweli mwingi na unaotimia kwa zaidi ya miaka 60 tangu nchi nyingi zipate Uhuru.
Mara nyingi, imekuwa vigumu kuwa na watu wawili wenye nguvu katika utawala mmoja. Ingawa mwanzo huwa mzuri, mara zote mwisho huwa si mzuri.
Kenya ya miaka ya 1960, ilishuhudia maswahiba wawili wa kisiasa; Jaramogi Oginga Odinga na Jomo Kenyatta wakiwa pamoja hadi wakati wakoloni walipoondoka lakini waligombana na kuwa maadui walipobaki wenyewe kuongoza serikali.
Ilikuwa hivyohivyo kwa Thomas Sankara na Blaise Compaore wa Burkina Faso kwenye miaka ya 1980. Ikawa hivyo kwa Jakaya Kikwete na Edward Lowassa mwanzoni mwa karne hii na tunashuhudia tatizo hilohilo kwa Uhuru Kenyatta na William Ruto nchini Kenya.
Kuna mtazamo miongoni mwa taasisi za kishushushu kwamba "Urais hauna Ubia" na kwamba Rais atabaki kuwa Rais na hana wa kufanana naye.
Kamerhe, pamoja na uzoefu na umahiri wake wa siasa za DRC, haonekani kwamba alilisoma somo hili mapema. Wakati bosi wake akizunguka Afrika na nje ya bara hili kutafuta kuungwa mkono, Kamerhe alitumia nafasi hiyo kujijenga na kujitengeneza kama mbadala wake ndani ya DRC.
Lilikuwa ni suala la muda tu kabla taasisi za kidola za DRC hazijachukua hatua kuhakikisha kwamba Kamerhe anawekwa katika nafasi yake ili sasa Tshisekedi abaki mwenyewe na aiongoze nchi kama anavyotaka yeye.
Kesi hii ya rushwa ambayo - pamoja na mambo mengine, inamzuia pia Kamerhe kutowania nafasi yoyote ya uongozi katika kipindi cha miaka 10 ijayo, imempa Tshisekedi nafasi kubwa ya kupumua na kumuondoa mshindani katika madaraka yake.
Mkataba usiotekelezeka
Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa DRC mwaka juzi, Kamerhe na chama chake cha CNC na Tshisekedi walikutana katika Hoteli ya Serena, Nairobi, Kenya kwa ajili ya kutengeneza mkataba wa ushirikiano. Ni makubaliano hayo ambayo yalimweka Fayulu pembeni na kufanikisha ushindi kwao.
Inafahamika kwamba sehemu ya makubaliano hayo ilikuwa kwamba Kamerhe atamuunga mkono Tshisekedi mwaka 2018 na mtoto huyo wa Waziri Mkuu wa zamani wa Zaire, Etienne Tshisekedi, ataongoza kwa muhula mmoja na kisha kumuachia mwenzake katika uchaguzi ujao wa mwaka 2023.
Ilielezwa pia kwamba kwa kumtengenezea njia, ilitakiwa Tshisekedi amteua Kamerhe awe Waziri Mkuu wake mara atapoingia madarakani. Hata hivyo, makubaliano ya mkataba huo yalikuwa hayatetekezeki kwa sababu moja.
Katiba ya DRC inataka Waziri Mkuu atoke katika chama chenye wabunge wengi. Kwa bahati mbaya, chama cha Kamerhe cha CNC kina wafuasi wengi katika eneo moja tu la Kusini mwa Jimbo la Kivu Kusini anakotoka yeye na kwa sababu ya kushindwa kupata wabunge wa kutosha, haikuwezekana kwa Tshisekedi kumpa nafasi hiyo kama walivyokubaliana.
Matokeo yake akaamua kumpa nafasi ya Mkuu wa Watumishi (Chief of Staff), nafasi yenye mamlaka makubwa lakini ikihusika zaidi na utumishi wa umma kuliko ya kisiasa ya Waziri Mkuu.
Jambo hili pekee, lilianza kuleta utata tangu katika siku za kwanza za ushirikiano wa maswahiba hawa wawili wa kisiasa.
Kamerhe na mali
Ingawa hili si tatizo la peke yake, kwa muda mrefu inajulikana kwamba Kamerhe ni mwanasiasa anayependa fedha. Muda mfupi baada ya kuingia na kufanya kazi katika Ikulu ya Tshisekedi, kulikuwa na tuhuma katika duru za kisiasa za DRC kwamba Kamerhe alianza kuonekana kujilimbikizia mali.
Ifahamike kwamba mara baada ya kuingia madarakani, Tshisekedi alitangaza mpango kabambe wa kutumia takribani dola za marekani milioni 350 katika siku zake 100 za kwanza madarakani kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya taifa hilo.
Jukumu hilo liliwekwa mikononi mwa Kamerhe. Wachunguzi wa siasa za DRC wanaamini kwamba kitendo cha kumpa Kamerhe mabilioni hayo ya faranga kusimamia mambo makubwa ilikuwa sawa na kumpa kamba ajinyonge mwenyewe.
Miezi michache tu baada ya kuingia madarakani, kukawa na maneno kwamba Kamerhe alijenga jumba la kifahari nyumbani kwake Kivu na kuhusishwa katika ujenzi wa vitu ambavyo thamani yake ilizidi makadirio ya awali ya serikali kwa mbali kupitia mpango huo wa siku 100.
Kama lengo la Tshisekedi lilikuwa kumpa Kamerhe kamba ya kujinyongea mwenyewe, inaonekana mpango huo ulifanikiwa.
Tishio la madaraka na biashara
Jambo moja ambalo wadadisi wa siasa za DRC wanakubaliana ni kwamba kuna mambo mawili ambayo Kamerhe alikuwa akionekana tishio kwa wenzake; kisiasa na kibiashara.
Wafuasi wa Tshisekedi walimwona kama tishio kisiasa kwa sababu ya tabia yake ya kuonesha waziwazi kwamba yeye ndiye atakuwa mrithi wa Tshisekedi ndani ya miaka mitatu kutoka sasa. Lakini wapo pia waliomwona kama tishio katika biashara zao kutokana na tabia yake ya kupenda 'kupiga dili'.
Barani Afrika, tishio lolote dhidi ya mamlaka ya kisiasa au kibiashara huchukuliwa pia kama ni tishio dhidi ya uhai wa watu; hasa katika nchi zilizo katika eneo la maziwa makuu.
Mara nyingi, njia zinazotumika kuondoa tishio la namna hiyo ni mbili tu; kuua au kufunga jela wahusika. Ni bahati kwamba Kamerhe kaangukiwa na njia ya pili ambayo ina nafuu kuliko ile ya kwanza.
Kivuli cha Joseph Kabila
Ingawa Kabila ameachia madaraka, wengi wa wafuatiliaji wa siasa za DRC wanaamini kuwa anajipanga kurejea madarakani. Minong'ono ya kumhusisha na kurejea madarakani inazidi kumea kwa sababu yeye mwenyewe hajawahi kukataa na mara ya mwisho alinukuliwa akisema; "Kwenye siasa lolote linaweza kutokea". Katiba haimkatazi kugombea katika uchaguzi ujao.
Inaaminika kwamba Kabila alitaka Kamerhe na Tshisekedi washinde uchaguzi huu kwa sababu alijua kuhusu udhaifu wa wawili; kwenye mambo ya fedha na kukosa uzoefu.
Kulikuwa na maneno kwamba kitendo cha kwanza kwa Fayulu na wenzake akina Moise Katumbi endapo wangeingia madarakani ilikuwa kuhakikisha wanamkamata na kufungua uchunguzi kuhusu familia ya Rais Kabila.
Kwa kutengana huku kwa Kamerhe na Tshisekedi baada ya kesi hii, imekuwa rahisi zaidi kushindana na Tshisekedi katika uchaguzi ujao kuliko kama wangebaki kama walivyokuwa kabla ya kesi hii.
Katika viunga vya Kinshasa leo, wakati Tshisekedi akijulikana kama President, Kabila anajulikana kwa jina la utani kama Rais; ambalo ni neno la lugha ya Kiswahili lenye maana sawa na President.
Kama nia ya Kabila ni kurejea ulingoni mwaka 2023, yeye ni mfaidikaji wa hukumu hii ya Kamerhe.
Huu ni mwisho wa Kamerhe?
Siasa za DRC hazijawahi kuwa rahisi au zenye kutabirika. Kama kifungo na adhabu hizi kwa Kamerhe zitabaki kama zilivyo, itakuwa vigumu sana kwa Kamerhe kurejea tena katika kilele cha kisiasa.
Hata hivyo, kama ataweza kutengeneza dili nyingine kutokea gerezani kati yake na Rais Tshisekedi, Kamerhe anaweza kujikuta akiwa uraiani ndani ya muda mfupi ujao.
Mpira uko mikononi mwa Rais Tshisekedi.
No comments :
Post a Comment