3 July 2020|Habari, Makala, Siasa
Zimebaki siku chache Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanya uteuzi wa Mgombea wake wa nafasi ya Urais Zanzibar 2020. Duru za kisiasa zinaonesha mgombea huyo ambaye atakuwa na kazi ngumu atakutana ulingoni na Maalim Seif Sharif Hamad mwishoni mwa mwezi Oktoba.
Kati ya majina mengi ambayo awali yalitajwa na baadaye kuchukua fomu liko jina la Waziri Kiongozi wa zamani SMZ Shamsi Vuai Nahodha. Nahodha mzaliwa wa Makunduchi Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja anatimiza umri wa miaka 58 baadaye mwaka huu. Miaka 20 iliyopita akiwa na umri wa miaka 38 (kinda kabisa kwenye siasa za Zanzibar) Rais Amani Karume alimteua kuwa Waziri Kiongozi SMZ nafasi ambayo alidumu kwa miaka 10 (2000 hadi 2010).
Nafasi yake ni ipi?
Amechukua fomu kuomba ridhaa ya CCM lakini je ana nafasi gani kushinda kinyang’anyiro hicho ukimlinganisha na wagombea wengine? Wachambuzi wa kisiasa Zanzibar wanataja mambo matano yanayompa Shamsi Vuai Nahodha wakati mgumu katika mbio za Urais Zanzibar 2020.
Jambo la kwanza ni lile la Kufeli kwa Operesheni Tokomeza Ujangili wakati Nahodha akiwa Waziri wa Ulinzi. Jambo hili lilimfanya akatimuliwa kazi.
Nyaraka zinaonesha kuwa Wizara ya Ulinzi Tanzania chini ya Nahodha ilikuwa na jukumu kubwa la kujenga nidhamu na kusimamia utekelezaji wa Operesheni hii ya maliasili na ulinzi mwaka 2013 baada ya maelfu ya tembo kupotea katika kipindi cha muda mfupi na ujangili kukua kwa kiwango cha kutisha. Hata hivyo inaelezwa kuwa dharau za Nahodha na kutopatana kwake na baadhi ya majenerali jeshini pamoja na kukosa umakini vilifanya operesheni iende mrama. Ripoti ya Operesheni hii inaonesha namna wanawake walivyobakwa, nyumba kuchomwa moto, watu kupata vilema vya maisha, mauaji na mateso kwa raia pamoja na wizi mkubwa wa mali. Yako madai ya fidia toka kwa wahanga wa dhahma hiyo ambayo serikali bado inayalipa mpaka leo.
Jambo la pili ni zile tuhuma za ugomvi, dharau na lugha isiyo na staha kwa baadhi ya majenerali wa jeshini. Inaelezwa kuwa tatizo hilo lilikuwa kubwa zaidi baada ya Nahodha akiwa Waziri wa Ulinzi kutaka kulazimisha kuuzwa kwa mojawapo ya maeneo ya Jeshi. Eneo alilokuwa akilazimisha kuuzwa ni moja ya maeneo ya ardhi nyeti yenye maslahi mapana kwa Jeshi kuliko mwekezaji ambaye aliletwa na Nahodha na watu wake wa karibu.
Tatu, ipo kashfa ya kuhusika kwake kupokea fedha za maharamia wa Kisomali akiwa Waziri wa Ulinzi. Vyombo vya ujasusi vya Uingereza na Marekani vimeonesha kuwa sehemu ya fedha ambazo maharamia wa Somalia walilipwa kuachia meli walizoteka ziliingizwa katika matumizi na kutakatishwa kupitia eneo la ujenzi wa majumba kwenye majiji ya Nairobi (Eastleigh) na Dar es Salaam (Kariakoo). Nahodha anatajwa kama mmoja ya watu walionufaika na fedha hizo wakati akiwa Waziri wa Ulinzi Tanzania. Kutokana na hili hadi sasa amekuwa na wakati mgumu kutumia moja ya apartment ambayo alipewa na washirika wake hao eneo la Kariakoo. Wanasheria wanaeleza kuwa kosa kama hilo ni la utakatishaji fedha na halifi hivyo basi tusishangae siku moja akashtakiwa, hata miaka ijayo. Vyombo vya kijasusi nchini vikishiriana na vile vya nje vilipata taarifa hizi na kuzihakiki na inatajwa kuwa sababu mojawapo ya Nahodha kuondolewa katika nafasi ya Uwaziri wa Ulinzi. Akihojiwa na Jarida la Uingereza la Financial Times tarehe 7 Mei 2012, Nahodha alieleza kwa kina suala la Watanzania kukamatwa Somalia lakini vyanzo vinasema aligoma kuzungumzia suala la uharamia wa meli akijua waandishi wachokonozi wanajua nini walikuwa wakiuliza na namna anavyohusika.
Nne, inaelezwa kuwa Nahodha si mtu kupima madhara ya kauli zake kama kiongozi, kitu ambacho kinatajwa kuwa hatari kwa nchi. Tukio mojawapo ni lile alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani (pia hakudumu) alipotoa kauli za kuitishia Rwanda akiwa ziarani Ngara mkoani Kagera bila kujua madhara yake kidiplomasia. Tukio hilo lilileta mvutano wa muda kati ya Tanzania na Rwanda mpaka Wizara ya Mambo ya Nje kulitolea maelezo.
Tano, kukosa uungwana. Hii inaweza isionekane jambo muhimu kwa baadhi ya watu hasa kwenye siasa lakini kwa eneo la pwani ni jambo muhimu sana. Duru za kisiasa visiwani Zanzibar zinaonesha kuwa mwaka 2010 alipojitosa kuingia katika kinyan’ganyiro cha urais, Dk Ali Mohamed Shein alimuomba Nahodha ajitoe ili yeye aweze kusonga mbele bila mushkeli lakini Nahodha alimkatalia na kumwambia “tukutane tatu ya mwisho”. Maneno haya yanatajwa kuwa dharau na ukosefu wa maono ya mwelekeo wa siasa na kuwa yalitolewa katika namna ambayo haikuwa sahihi/ya kiungwana.
Jambo la sita na pengine kubwa zaidi ni kina nani hasa wanamuunga mkono Shamsi Vuai Nahodha katika mbio hizi za Urais.
Taarifa za kiuchunguzi zinaonesha kuwa Nahodha anaungwa mkono na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Bernard Kamillius Membe. Nahodha na watu wake wamerekodiwa pia wakijinadi kuwa na baraka za Rais mstaafu Jakaya Kikwete, taarifa ambazo huenda ni kweli ama ni za kujimbwafai tu. Membe ni moja ya makada wa CCM waliochukua fomu za kugombea Urais kupitia CCM mwaka 2015 na kuingia tano bora kabla ya kushindwa na Magufuli.
Inaelezwa kuwa Membe ambaye ni mbobezi wa mikakati ya kijasusi anajipanga kurudi katika siasa Bara akipitia Zanzibar. Imani ya Membe kuwa iwapo yeye na washirika wake watafanikiwa kutimiza azma ya Nahodha kuwa Rais Zanzibar basi wataweza kumtumia kwa namna nyingi ikiwemo ushawishi kwa wajumbe wa CCM Zanzibar kwenye kufanya maamuzi ndani ya CCM ikiwemo kumuondoa Magufuli madarakani hata akipita kwa awamu ya pili (kama ANC kilivyofanya kwa Thabo Mbeki ambaye alikuwa amebakiza miezi 9 tu kumaliza muhula wake wa pili wa uongozi). Uchambuzi unaonesha pia kwamba Membe hapendezwi na namna Mwenyekiti wa CCM Rais Dk Magufuli anavyoendesha chama na nchi na hata matatizo yake kisiasa na kibishara anaamini ni chuki na maamuzi binafsi ya Magufuli dhidi yake.
Tayari Membe ametangaza nia ya kugombea Urais iwapo vyama vya upinzani vitaungana na kumpa nafasi hiyo. Zinatajwa namna nyingi ambazo Membe amekuwa akifanya kujaribu kulipa kisasi kwa Magufuli wakati mwingine bila kujali athari kwa nchi kwa ujumla ikiwemo kujaribu kushinikiza Magufuli kutengwa na Marais wa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara (strategic lockout)kama ambavyo tumeona katika baadhi ya mambo. Membe kumtumia Nahodha Zanzibar inaelezwa kuwa kete yake kuu na muhimu wakati huu.
Rekodi zinaonesha kuwa Shamsi Vuai Nahodha ndiye alikuwa kiongozi wa kampeni za harakati za Urais za Membe mwaka 2015 kwa upande wa Zanzibar.
Uchunguzi unaonyesha Nahodha anafahamu nia hiyo ya Membe kumtumia yeye na CCM Zanzibar kurejea kwa kishindo CCM na kwenye siasa za Tanzania. Fedha kuhonga baadhi ya wajumbe wa NEC kwa azma hiyo zimeanza kutolewa tangu Novemba mwaka jana kutoka kwa Membe na washirika wake na baadhi ya ushahidi umenaswa na vyombo vya kiuchunguzi. Kama ilivyoelezwa, lengo hasa la Membe linatajwa kuwa ni kutaka kurejea CCM na kulipiza kisasi kwa Magufuli kwa namna ambavyo amemtendea mpaka kutimuliwa chamani na biashara zake na washirika wake kuharibiwa kwa kiasi kikubwa. Membe anaamini Nahodha akipata Urais Zanzibar basi Nahodha naye ataisaidia timu ya Membe kumuweka mgombea wanayemtaka Bara 2025 au hata kabla ya hapo iwapo watatumia wajumbe wa Zanzibar na baadhi ya wale wa Bara kumvua uanachama Magufuli kama ANC walivyomfanyia Thabo Mbeki kupitia mkakati wa Zuma, Mbeki akiwa amebakiza miezi michache tu kumaliza muhula wake wa pili. Kwa Membe, Nahodha ni fimbo ya kujaribu kumchapia Magufuli bila kujali athari zake kwa nchi nzima.
Mbali na Membe, Nahodha pia kifedha anafadhiliwa na wafanyabiashara Mohamed Raza, Naushad Mohamed Suleiman, Haroon Zakaria, Hassan Raza na Salim Turky (ana makando kando mengi ikiwemo lile la kumpa Balozi wa Comoros passport ya Tanzania kinyume cha sheria, kitu ambacho ni kosa la jinai).
Wanachofanya wafanyabiashara hao ni kama kamari na Ikulu ya Zanzibar na Wazanzibari. Wanalo kundi la wagombea kote CCM na upinzani, wanagawa fedha viwango tofauti tofauti na atayepitishwa na chama chake na kushinda watamtumia kuendelea kuibaka Zanzibar kwa kila aina ya uchafu kuanzia dawa za kulevya, ukwepaji kodi, tenda za serikali na magendo. Moja ya kazi kubwa ya CCM na serikali ijayo Zanzibar ni kusambaratisha genge hili.
Wachambuzi wa siasa za Zanzibr wanasema ukitaka kuamua kuhusu kufaa au kutofaa kwa Shamsi Vuai Nahodha kwenye Urais Zanzibar 2020 kwa muhtasari tizama haya: Moja, ushahidi namna Membe na washirika wake wanavyomfadhili na kupanga kumtumia kurudi Bara na kusafisha waliomsulubu akiwemo Mwenyekiti wa CCM Rais Dk Magufuli. Hii inaamanisha nia yake si kuwatumikia Wazanzibari bali kuwa nyenzo ya mtu kujipatia madaraka na kulipa visasi. Sasa kulipa visasi inawezekana kwenye ugomvi wa familia au baa lakini huwezi kumpa mtu nchi akaitumia kulipa kisasi.
Mbili, anavyoungwa mkono na wafanyabiashara wanne vinara wa magendo, dawa za kulevya, ulanguzi wa sukari na ukwepaji kodi Zanzibar (Raza, Naushad, Turky na Zakaria). Hii inaamanisha kuna watu anakwenda Ikulu kuwatumikia, si Wazanzibari. Sote twafahamu hawampi fedha zao kuhonga wajumbe bure bure.
Tatu, historia ya utumishi wake Wizara na ofisi nyeti kama ambavyo tumeona katika makala hii. Nne, afya yake ambayo imekuwa na usiri mkubwa siku za karibuni akisumbuliwa na maradhi ya kupoteza kumbukumbuku (Dementia) na kisukari.
Wazanzibari wengi wanahoji uthubutu wake hata wa kuchukua fomu katika mazingira ya namna hiyo. Baadhi ya watu katika vijiwe mbalimbali visiwani Zanzibzar wanampa nafasi kubwa Mhandishi Hamad Yussuf Masauni, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Tanzania na Mbunge wa Kikwajuni. Masauni anaonekana kama pumzi mpya itakayoleta zama mpya ndani ya CCM na Zanzibar na kiongozi sahihi wa zama hizi.
Mbio za Urais Zanzibar zinaelekea ukingoni na mjadala umekuwa mkali kuhusu mgombea wa CCM kutokana na umuhimu wa chama hicho katika mustakabali wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Ni muda wa kusubiri kuona nani toka CCM atavaana na Maalim Seif toka ACT Wazalendo hapo Oktoba.
Rajab Ibrahim (Kada wa CCM, Vuga Unguja)
No comments :
Post a Comment