2 July 2020|Habari, Makala, Siasa
Siku chache zijazo wajumbe wa CCM wataamua nani anafaa kubeba bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Rais Zanzibar 2020. Wamejitokeza makada wengi kuchukua fomu kuomba ridhaa hiyo, wengi wao ikiwa ama wana dhamira ya dhati ama wanatumika kimkakati. Kati ya walochukua fomu ni Mhandisi Hamad Yussuf Masauni. Huyu alitarajiwa kufanya hivyo na kwa miaka mingi sasa anaonekana kama mtu mwenye nafasi kubwa ya kuiongoza Zanzibar. Katika makala hii nitaeleza japo kwa ufupi kwa nini naamini Masauni ana nafasi kubwa na anafaa kuwa Rais ajaye Zanzibar ukimlinganisha na makada wengine walochukua fomu kuomba nafasi hiyo.
Kihistoria Masauni alizaliwa Oktoba 3 mwaka 1973, maana yake sasa ana umri wa miaka 46. Nafasi zake za kiuongozi kwa sasa ni Ubunge wa Kwikwajuni aliyemaliza muda wake na Unaibu Waziri wa Mambo ya Ndani katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Zanzibar ya leo inahitaji uongozi ambao utaiponya na siasa ambazo kwa hakika tunaweza kuziita za kale. Inahitaji mtu mwenye dira na wa kizazi hiki, anayeifahamu vyema Zanzibar ilipotoka, ilipo na inapohitaji kwenda. Katika hili tuchambue sifa za Masauni huku tukilandanisha na mahitaji ya sasa katika siasa za Zanzibar.
Moja, Masauni amekulia na kupikwa kwa muda mrefu ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), hii inamaanisha anazijua vyema siasa za CCM, ni mtu wa watu ndani na nje ya chama na anaujua vyema mfumo wa serikali. Mbali na hilo, hii pia ina maana kwamba ana nafasi ya kuleta kizazi kipya na makini chenye fikra mpya ndani ya SMZ kitakachoweza kupambana na changamoto za nyakati hizi ili kusogeza mbele gurudumu la maendeleo katika visiwa vyetu hivi, kuendelea pale anapoachia Dk Shein. Sifa hii wanakosa washindani wake kama Dk Hussein Mwinyi na Profesa Mbarawa. Miaka 15 iliyopita kwa mfano, hakuna alomjua Mbarawa ni nani ndani ya CCM, wakati huo akiwa mwalimu katika moja ya vyuo vikuu nchini Afrika Kusini.
Sifa ya pili na muhimu katika uchaguzi huu alo nayo Masauni ni kuwa anakubalika na pande zote, CCM na upinzani. Sifa hii ni muhimu kwa jamii ilogawanyika kisiasa kama Zanzibar. Upo ukweli usopingika kwamba Zanzibar ni ya makundi yenye uhasimu wa kisiasa na wakati mwingine hili linakwamisha maendeleo. Katika uchaguzi wa mwaka huu lazima CCM ipate mgombea anayeelewa hili na anayekubalika na pande zote mbili. Mgombea atakayeweza kuponesha majeraha ya kisiasa na kuipa Zanzibar mwanzo mpya. Wachambuzi wengi wa siasa Zanzibar na hata wanachama wa CCM wanamtaja Masauni kama mtu mwenye nafasi kubwa ya kuweza kufanya hilo ukimlinganisha na wapinzani wake katika mbio hizo.
Tatu, Masauni ameeleza wazi na mara nyingi pasi kificho kuwa yeye ni muumini wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU). Msimamo huu una mawili, kwanza unaonesha ana mkakati sahihi kuwezesha CCM kubaki imara ndani ya mfumo huo wa serikali lakini pili inampa uhakika wa kuungwa mkono na waliberali wa Unguja na wale wa Pemba ambao siku za karibuni wamekuwa wakiongezeka kwa kumomonyoka toka pande zote yani CCM na Upinzani. Hawa ni Wazanzibari walochoshwa na siasa za jino kwa jino na za kibabe, wanaoamini uongozi wa Zanzibar unahitaji kushirikisha makundi yote husika (inclusive). Sifa hii wanaikosa wapinzani wake kina Mwinyi na Mbarawa. Mwinyi anatajwa kutokuwa sana mtu wa watu huku Mbarawa tukijua wazi kuwa mbali ya kutokuwa mtu wa watu na kukataliwa katika Ubunge kwao Pemba mara mbili pia ni mgeni katika siasa za Zanzibar, na mtu hatari kiusalama hata kumsogeza karibu na Ikulu ya nchi achilia mbali Urais.
Nne, umri wa Masauni ni umri sahihi kuongoza nchi ambayo asilimia kubwa ni vijana, nguvu kazi ya taifa. Aina ya uongozi unaotakiwa kwa sasa Zanzibar ni ule wenye kujua mahitaji ya kizazi kilichopo na Masauni anaonekana kama mtia nia pekee mwenye umri unaoendana na hitaji hilo.
Tano, ni mtu mwenye busara ya kiuongozi na asiyekurupuka. Hili tumelishuhudia kwa namna alivyopambana na tuhumu na kashfa mbalimbali zilizomkabili kama sakata la uzushi la vyeti. Kiongozi mstaarabu, asiyeamini katika kubebwa na mtu kama ilivyokuwa kwa Magufuli mwaka 2015 ambaye alipita kwa vigezo. Urais Zanzibar 2020 wako wagombea wengi wanaojinadi kubebwa na Mwenyekiti Rais Magufuli ama makundi mbalimbali. Mfano ni Profesa Makame Mbarawa ambaye yeye na timu yake wameweka wazi katika vikao mbalimbali vya ndani na siri kuwa wanaungwa mkono na Mwenyekiti wa CCM Rais Dk Magufuli, jambo ambalo si kweli hata kidogo.
Sita, katika umri na madaraka yake Masauni amebaki kuwa msafi kwa maana ya uadilifu katika sekta ya utumishi wa umma. Tumeona makandokando lukuki ya watia nia wengi na namna ambavyo ni hatari kwa Zanzibar iwapo watapewa nafasi ya kutuongoza.
Saba, matendo yake yanaonesha wazi kuwa Masauni kaiweka Zanzibar moyoni mwake kwa mahaba na uzalendo wa dhati. Amesoma Tanzania, amefanya kazi Tanzania, amepata nafasi ya kusoma Uingereza na alipohitimu amerudi Tanzania, ameoa Zanzibar na familia na ndugu zake tunao hapa, mtu wa ibada na safi. Mtu wa namna hii tunaweza kumuamini na madaraka ya nchi. Sasa tumlinganishe na mtia nia kama Mbarawa, yeye kapewa nafasi kwenda kusoma Urusi akazamia kuanzia miaka ya 1980 hadi 2010 ndipo kaibuka baada ya kuahidiwa cheo na Dk Bilal na JK. Kazaa watoto Urusi na wanawake wawili wa huko na taarifa hizi anavificha vyombo vyetu vya usalama, kaoa mke Mganda, ana nyumba mbili Afrika Kusini (Pretoria na Cape Town). Tunaweza kabisa kabisa kuwaamini wagombea wa namna hii na kuwakabidhi funguo za Ikulu ya nchi? Hawa tunaweza kuwapa Wizara ama Mkoa, lakini nchi nzima? Hapana.
Tuko katika wakati tete sana na njia panda kuamua hatma ya Zanzibar. Mimi na Wazanzibari wengi tunayo imani ya dhati kabisa kwamba wajumbe wa CCM ambao ni sehemu muhimu sana ya mchakato huu watakuwa makini na jukumu hili kama ilivyo kawaida yao na kutupatia mgombea sahihi. Katika hili bila kupepesa macho ndoto yangu ni kuona Mhandisi Hamad Yussuf Masauni anapewa nafasi ili kuweza kuipa si tu Zanzibar pumzi mpya bali hata CCM yenyewe, hasa hapa visiwani.
Allahumma Barik!
Mohamed Ahmed Faki (Kada wa CCM, Chokocho Pemba)
No comments :
Post a Comment