dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, October 6, 2020

Uchaguzi Tanzania 2020: Watu hususiana hadi usafiri na mazishi Zanzibar kisa siasa!


Rashid Abdallah
Mchambuzi (bbc)


Zanzibar ni mkusanyiko wa visiwa vinavyoelea katika Bahari ya Hindi. Miongoni mwa visiwa hivyo ni vile vya Unguja na Pemba ambavyo ndiyo mashuhuri zaidi.

Kijiografia na kiuchumi, Zanzibar ni nchi ndogo kulinganisha na jirani zake.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2002, Zanzibar ilikuwa na takribani wakazi milioni 1.3.

Uchumi wa Zanzibar unategemea zaidi sekta za utalii, kilimo na uvuvi. Visiwa hivi huundwa na watu wenye asili mbalimbali za Waafrika; wakiwemo Wabantu wa Kiafrika na wale wenye asili ya Asia.
Karibu Wazanzibari wote ni waumini wa dini ya Kiislamu, wanazungumza walau lugha moja ya Kiswahili, wana mila na desturi zinazofanana kuanzia vyakula hadi mavazi. Kwa kifupi, Wazanzibari kwa ujumla wao ni jamii yenye kufanana kwa mambo mengi.

Kipi huharibu mtangamano wa Wazanzibari?

Tarehe 22 ya mwezi huu, Jeshi la Polisi Tanzania lilithibitisha tukio la kushambuliwa kwa mapanga kwa wakereketwa watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakitoka msikitini kwa swala ya Alfajiri huko kijiji cha Kangagani, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Baadhi ya wadadisi wa mambo wanalihusisha tukio hilo na joto la kisiasa lililopo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu uliopangwa kufanyika mwishoni wa mwezi Oktoba.

Sura ya tukio lenyewe ina harufu ya chuki za kisiasa. Kwa wafuatiliaji wa siasa za Pemba, moja kwa moja wamejielekeza kwenye dhana kwamba tukio halikuwa la uhalifu wa kawaida bali siasa.

Seif Sharrif Hamadi alijiunga na chama cha ACT wazalendo ili kuwania urais Zanzibar

Dhana hii inachagizwa na ukweli kwamba walioshambuliwa ni wafuasi wa chama kimoja cha CCM na mhalifu ametokomea bila kujulikana alipo.

Nje ya siasa jamii ya Wazanzibari haina uhasama wala chuki kati yao. Mara nyingi mparaganyiko na sintofahamu katika jamii hiyo chanzo chake ni siasa.

Siasa za Zanzibar nyakati za uchaguzi zinasisimua kutokana na matukio yasiyo ya kawaida yanayotokea. Lakini upande mwengine wa sarafu nchi hiyo ina siasa za kuogopesha kwa sababu ya historia yake.

Mauaji yaliyochochewa na siasa

Zanzibar ina historia ya umwagaji damu katika siasa zake. Mapinduzi ya Januari 12, 1964 lilikuwa ni tukio la kuiondoa kwa nguvu serikali ya Kisultani iliyokuwepo madarakani wakati huo.

Hadi leo, jamii ya Wazanzibari imegawanyika kuhusu uhalali wa mapinduzi yenyewe na kilichotokea wakati na baada ya mapinduzi.

Mambo hayakuishia hapo. Kuuawa kwa Rais wa kwanza wa visiwa hivyo Sheikh Abeid Amani Karume, Aprili 1972, lilikuwa doa jengine la damu katika kapu la siasa za Zanzibar. Ukubwa wa doa hilo ukazidi kukua kufuatia kamata kamata na mateso kwa waliotuhumiwa kuhusika na mauaji hayo.

Januari 2001, Zanzibar iliandika historia nyengine ya umwagaji damu katika siasa zake. Haya yalikuwa ni maandamano yaliyofanywa na chama kikuu cha upinzani cha CUF kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2000.

Makumi ya watu waliuwawa kwa risasi, mamia walijeruhiwa na wengine wakakimbia nchi.

Mkusanyiko wa historia hiyo unaifanya siasa ya Zanzibar kutisha, daima inakuwa ya moto na ya kuogofya. Ukikaribia uchaguzi mkuu hali huzidi kuwa tete. Mbali ya mauaji ya namna hiyo, yapo mengine yanayoifanya siasa yake kuogopesha.

Makundi ya wahalifu

Kwa miaka mingi makundi ya wahalifu yamekuwa yakizuka kila ufikapo wakati wa uchaguzi mkuu. Ingawa yamekuwa yakibadilishwa majina na wakaazi. Huendesha uhalifu wao kwa kutumia silaha za moto na jadi.

Yanatuhumiwa kuhusika na uvamizi katika majumba ya watu, kupiga raia, kuharibu mali na kutia hofu wananchi.

Katika uchaguzi wa 1995 na 2000 makundi hayo yalipewa jina la Melody.

Ulipofika uchaguzi wa mwaka 2005 jina likabadilika na kuitwa Janjaweed. Jina hilo lilizuka kwa kunasibishwa na wale Janjaweed waliokuwa wakiendeleza unyama katika mgogoro wa Darfur nchini Sudan.

Katika uchaguzi wa mwaka 2010 makundi hayo hayakuonekana. Hilo lilitokana na maridhiano yaliyopelekea kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa. Huo ndio uliokuwa uchaguzi wenye utulivu zaidi katika historia ya chaguzi za visiwa vya Zanzibar. Lakini uchaguzi wa mwaka 2015 yalirudi tena na wananchi waliyapachika jina la Mazombi.

Vyama vya upinzani vinayahusisha makundi hayo na serikali, japo serikali zote mbili za Jamhuri ya Muungano na ile ya Zanzibar daima zimekuwa zikikanusha kuhusika nayo.

Maswali ambayo mamlaka zimesuasua kutoa majibu ni; makundi hayo yanaendeshwa na nani? Yanatokea wapi? Na kwanini huzuka nyakati za uchaguzi?

Swali jengine lisilo na jawabu ni hili: Je, yatazuka tena kuendeleza uhalifu katika uchaguzi wa 2020?

Chuki na Visasi

Umewahi kusikia mtu anasusia harusi ya jirani yake kwa sababu yeye ni wa chama chengine?

Umewahi kuona mtu anasusia duka kwa sababu mmiliki si mfuasi wa chama anachokipenda yeye?

Watu hususiana hadi usafiri na mazishi. Yote hayo hutokea Zanzibar.

Rais Magufuli na Mohamed Shein wa Zanzibar

Mashamba pia huharibiwa kwa chuki za kisiasa. Unaweza kuamka asubuhi ukakuta shamba lako lote la migomba au mihogo limelala chini kwa mapanga ya watu wasiojuliakana.

Matukio hayo sio ya kila siku katika maisha ya kawaida ya Wazanzibari bali huzuka baada ya uchaguzi mkuu kuisha.

Wale ambao wanaamini hawakutendewa haki katika uchaguzi, huzihamishia hasira zao kwa wafuasi wa kawaida wa chama kilichokuwa mshindani katika uchaguzi.

Maelezo ya video,

Dua maalum Zanzibar kumuenzi Sultani wa Omani

Hapa bila kutafuna maneno, wafuasi wa CCM ndio wahanga wakubwa wa kutengwa katika shughuli hizo za kijamii.

Inapofika hatua hiyo serikali hulazimika kutumia viongozi wakidini na vyombo vya habari kuhimiza umoja na upendo.

Baada ya miezi michache uhasama huondoka na watu hurudi katika maisha ya kawaida. Bahati mbaya uchaguzi ukifika na matokeo yakitangazwa uhasama wa namna hiyo huzuka tena kama awali.

Maisha na siasa za ushindani

Shauku kubwa ya kisiasa ya wakaazi wa visiwa vya Zanzibar ipo tangu kipindi cha ukoloni. Hata ule ushindani ulioanza baada ya kuasisiwa mfumo wa vyama vingi umeendelea katika hali ile ile.

CUF ambacho kilikuwa na ngome yake kuu visiwani kabla ya mgogoro na kufukuzwa kwa aliyekuwa Katibu mkuu Maalim Seif Sharif Hamad, wakati wote kilibaki kuwa tishio kwa chama tawala.

Kitisho hicho kingalipo hata sasa wakati Maalim na wafuasi wake wamehamia chama chengine cha upinzani cha ACT Wazalendo.

Siasa ina nafasi kubwa katika maisha ya kila siku ya wananchi wa Zanzibar. Siasa pia inatazamwa kama chanzo cha changamoto zilizopo za muungano wa visiwa hivyo na bara na siasa pia inatazamwa kama tumaini la ufumbuzi wa changamoto hizo.

Ni muda wa kusubiri kuona, ikiwa matukio ya kihistoria yatajirudia au kipi kitatokea katika uchaguzi wa mwaka huu.

https://www.bbc.com/swahili/habari-54430348


No comments :

Post a Comment