KATIKA siku chache hizi kuelekea uchaguzi, Zanzibar imegeuka eneo lililojaa vifaru, magari ya deraya, bunduki hasa AK 47 na zana zingine za kivita kila kona.
Hali ilianza kuchafuka zaidi siku mbili kabla ya kupiga kura za awali, Jumapili tarehe 25 Oktoba.
Ingawa watawala wanasema uwepo wa majeshi na zana hizo unalenga kuimarisha ulinzi, wananchi wanasema ni vitisho dhidi yao na ni mbinu ya kuiba kura ili kunufaisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika uchaguzi huu unaotarajiwa kufanyika Jumanne na Jumatano wiki hii, Dk. Hussein Mwinyi wa CCM anachuana na Seif Sharif Hamad wa ACT-Wazalendo.
Uwepo wa polisi na wanajeshi Zanzibar ni kero pia kwa wasafiri wa kawaida kwani kuna ulinzi, upekuzi na kuhojiwa bila mpangilio kwa watu wote wanaoingia Zanzibar katika bandari na uwanja wa ndege wa Zanzibar, na wanaotaka huduma katika ofisi zote za serikali.
Kura za awali zitapigwa keshokutwa, Oktoba 27, 2020 kwa watumishi wa Idara za Usalama, Majeshi na Watumishi wa Tume ya Uchaguzi. Hii ni ili kutoa nafasi kwa watendaji hao kushiriki kikamilifu kutekeleza majukumu yao katika Uchaguzi siku inayofuata.
Kazi ya kuhoji na kupekua kila anayekanyaga ardhi ya Zanzibar inafanywa na askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Uhamiaji na Kikosi Maalum kutoka Idara ya Usalama.
SAUTI KUBWA lina taarifa kuwa maofisa hao ni watumishi wa vyombo vya usalama vya Tanzania Bara. Miongoni mwao wapo wanaoficha sura zao kwa soksi-uso (face masks) ili wasitambulike.
Aidha, wanausalama hao wote wanavaa nguo za kijeshi, wakiwa na silaha za kivita, huku wengine wanaovaa kiraia wakiwa na bastola.
Mbali na kuwepo maeneo hayo, wanajeshi wanaonekana wakirandaranda mitaani katika maeneo mengi ya Zanzibar, wakiwa na silaha za moto. Idadi kubwa ya askari hao ipo maeneo ya Kisonge, Mkwajuni, Mlandege na Mnazi Mmoja.
Katika eneo la Kisonge jana barabarani kulikuwa na kundi la wanajeshi ambalo lilikuwa likikamata na kuhoji vijana waliokuwa wakitembea kwa makundi. Liliwalazimisha kuruka kichura-chura kabla ya kuwaamuru kutawanyika, kila mmoja akiondoka kivyake bila kuambatana.
Hali ya Usalama katika visiwa hivi ni tete, na zipo taarifa kuwa kunaweza kutokea vurugu katika siku ya kupiga kura au baada ya uchaguzi.
No comments :
Post a Comment