Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, March 19, 2021

Historia ya Maisha Rais Magufuli, Kuzaliwa, Shule, Uongozi Mpaka Kifo!

Kwa kawaida, katika jamii yoyote ya wanadamu, kuzaliwa kwa mtoto ni suala la shangwe. Hicho ndicho kilichotokea Alhamisi ya Oktoba 29, 1959 katika Kitongoji cha Katoma, Kata ya Bugando, Tarafa ya Nzela, Wilaya ya Geita, alipozaliwa John ‘Walwa’ Joseph Magufuli.

Miongoni mwa walioshuhudia kuzaliwa kwake, hakuna hata mmoja alijua kwamba miaka 56 baadaye mtoto huyo angekuja kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na mmoja wa viongozi mashuhuri zaidi duniani.
Wazazi wake ni Magufuli, Marco Nyahinga na Suzana Musa ambao kati ya mwaka 1960 na 1961 waliamua kuvuka ziwa Victoria kutoka Katoma Nkome, Wilaya ya Geita, Mkoa wa Mwanza wakati huo, kwenda Kijiji cha Lubambangwe, Chato, Wilaya ya Biharamulo, Mkoa wa Kagera wakati huo, kutafuta fursa za kiuchumi.

Mabadiliko yaliyotokea mwaka 2012, yaliiondoa Chato Mkoa wa Kagera na kuileta Mkoa mpya wa Geita baada ya Serikali kuanzisha mikoa minne mipya na wilaya 19. Tangazo la kuanzishwa kwa mikoa na wilaya hizo lilitiwa saini na Rais Jakaya Kikwete Machi 1, 2012.

Gazeti la Serikali ‘Daily News’ liliandika kuwa mikoa hiyo ni Geita, Katavi, Njombe na Simiyu. Mkoa wa Geita ulianzishwa rasmi kwa Tangazo la Serikali namba 72 la Machi 2, 2012 na kuzinduliwa Novemba 8, 2013 na Rais Kikwete.

Mkoa huo una wilaya tano ambazo ni Bukombe, Chato, Geita, Mbongwe na Nyang’hwale na majimbo saba ambayo ni Geita Mjini, Geita Vijijini, Busanda, Mbogwe, Bukombe, Nyang’wale na Chato.

Mwandishi Mathias Kabadi anaielezea familia ya John Magufuli kama: “…familia ya kawaida kabisa ya wakulima na wafugaji, yenye malezi na maadili mema na msimamo wa hali ya juu. Ni familia yenye ari na utashi katika kujituma kuchapa kazi kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla. Ni familia iliyopata mafanikio na mageuzi makubwa ya maendeleo kwa kuchapa kazi kwa bidii na maarifa.”

“Kama zilivyo koo nyingi za kabila la Wasukuma tangu enzi za kale, anaandika Kabadi, “familia hii wanachukia sana mambo ya ubabaishaji na uvivu katika kuchapa kazi za maendeleo, ulaghai, wizi, au ubadhirifu na udanganyifu wa aina yeyote ile. Ni familia ya watu wakarimu yenye desturi ya kupenda kusaidia watu kwa mahitaji mbalimbali.”

Kuhusu jina la ‘Pombe’, mwandishi huyo anafafanua kuwa siku aliyozaliwa John Magufuli, bibi mzaa baba yake alimwita “Walwa” kwa sababu siku hiyo nyumbani kwa bibi huyo kulikuwa na shughuli ya kuchuja pombe iliyotengenezwa kwa ulezi ambayo kwa lugha ya Kisukuma huitwa mapuya au ‘shidugugu’.

John Pombe Magufuli alianza elimu ya msingi katika Shule ya Chato mwaka 1967 na kuhitimu mwaka 1974. Alifaulu na kuchaguliwa kujiunga na Shule ya Seminari Katoke, Biharamulo, aliposoma kidato cha kwanza na cha pili mwaka (1975 – 1976), na baadaye kuhamia Sekondari ya Lake, iliyopo Mwanza, aliposoma kidato cha tatu na cha nne (1977 – 1978). Hii ni kwa mujibu wa Tovuti rasmi ya Serikali.

Baada ya kufaulu elimu ya Sekondari, John Magufuli alijiunga na Kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Mkwawa, mkoani Iringa, kati ya mwaka 1979 na 1981. Kuanzia mwaka 1981 na 1982, alijiunga na Chuo cha Ualimu Mkwawa, mkoani Iringa, kusomea Stashahada ya Elimu ya Sayansi, akibobea kwenye masomo ya Kemia, Hisabati na Elimu.

Mara baada ya kuhitimu masomo yake Chuo cha Mkwawa, alianza kazi ya ualimu katika Shule ya Sekondari Sengerema, akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati.

Alifanya kazi hiyo kuanzia mwaka 1982 hadi 1983 ambapo alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa Sheria katika Kambi ya Makutupora, Dodoma, kuanzia Julai hadi Desemba 1983. Baadaye kuanzia Januari 1984, alijiunga na Kambi ya Makuyuni mkoani Arusha ambapo alitumikia hadi mwisho wa mafunzo.

Kwa mujibu wa baadhi ya walioshiriki naye mafunzo ya JKT ndugu Magufuli alikuwa mtu wa kujituma na kufanya kazi wakati wote.

“Hakuwa selule kabisa, siku zote alikuwa mchapa kazi na mtu makini sana,” anasema Hassani (Siyo jina lake halisi) na kuongeza: “Ila kwenye masuala ya kujongo, kama kawaida, jeshini karibu kila mtu alipata kujongo, japo kwenda mjini mara moja kupata mahitaji mbalimbali.”

Mwaka 1985, alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea Shahada ya Sayansi ya Elimu akibobea katika Kemia na Hisabati. Kipindi akiwa Chuo Kikuu, Magufuli alijituma sana katika masomo yake na alihitimu chuoni hapo mwaka 1988.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mwaka 1989 hadi 1995 alifanya kazi katika kiwanda cha Nyanza Cooperative Union Ltd akiwa mkemia. Wakati huo alianza masomo ya Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Salford, Uingereza, (kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) kati ya mwaka 1991 na 1994.

Baadaye aliendelea na elimu ya juu zaidi ya Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Kemia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambayo aliisomea huku akiendelea na majukumu mengine serikalini na kuhitimu mwaka 2009.

Wapigakura wengi jimboni kwake waliamini Dk Magufuli hakuwa na ndoto ya kuwa mwanasiasa hadi aliposhawishiwa na wazee kugombea ubunge baada ya wao kubaki wanyonge kwa muda mrefu.

Mzee Emmanuel Francis anayakumbuka maisha ya ujana ya Magufuli, ‘Wazee tulikaa na kumuona huyu ndiye msomi wa kiwango cha juu anayeweza kutukomboa. Tulikuwa tunamfuatilia tangu akiwa mwalimu Shule ya Sekondari Sengerema na hata alipokuwa Mkemia kwenye Shirika la Pamba.”

Anasema Magufuli hakuwakatisha tamaa. Alikubali kujitosa kugombea ubunge akipambana na Phares Kabuye (sasa marehemu). Ingawa matokeo hayakukidhi kiu yao, mgombea mwenyewe, ndugu Magufuli, aliyakubali.” Huo ulikuwa ni Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 1990. “Tukio la Magufuli kumshika mkono na kumpongeza mshindani wake liliwashangaza wananchi wengi na walimuona kama kijana asiye na kinyongo.”

Mzee Francis alieleza kuwa kilichomponza Magufuli katika uchaguzi wa 1990, hata kama hakina maana ni kuwa uvaaji wake wa miwani ulimpunguzia kiasi fulani cha kura kutokana na baadhi ya wapigakura kuamini kuwa miwani ilikuwa kielelezo cha wale wasomi waliokuwa na tabia ya kujikweza enzi hizo.

“Wasukuma tuna kasumba ya kupigiwa magoti, baadhi ya wananchi walipomuona ni kijana anayependa kuvaa miwani walisema huyu ndiye atatusahau kabisa’,” alisema Mzee Emmanuel Francis katika makala iliyorejewa hapo juu.

Baada ya kushindwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1990, Magufuli hakukata tamaa. Mwaka 1995 alijitosa tena katika Jimbo la Chato (wakati huo Biharamulo Mashariki), kuwania ubunge kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na safari hii alishinda.

Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa alimteua John Pombe Magufuli kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi katika kipindi chake cha kwanza cha ubunge. Kutokana na kazi kubwa aliyokuwa ameifanya kwenye Serikali ya Awamu ya Tatu, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Magufuli alikuwa mmoja wa wabunge waliopita bila kupingwa jimboni kwake.

Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Dk John Pombe Joseph Magufuli alianza mbio za kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhamisi ya Juni 4, 2015, alipochukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Baada ya mchakato uliojaa msisimko wa ushindani mkubwa, Dk Magufuli aliingia tano bora katika mchujo uliowaondoa wagombea wengine 33 na hatimaye aliingia tatu bora kabla hajaibuka kidedea kama mgombea wa Urais kwa tiketi ya CCM na hatimaye kuchaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Chanzo GPL

No comments :

Post a Comment