
Kukamatwa na kushitakiwa kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kumeibua mjadala, ambapo nchi ya Marekani imeshauri kuwepo na majadiliano kati ya Rais Samia Suluhu Hassan na vyama vya upinzani.
Dar es Salaam. Kukamatwa na kushitakiwa kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kumeibua mjadala, ambapo nchi ya Marekani imeshauri kuwepo na majadiliano kati ya Rais Samia Suluhu Hassan na vyama vya upinzani.
Hayo yameelezwa jana na Naibu Waziri wa Nchi wa Masuala ya Siasa wa Marekani, Victoria Nuland alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kufuatia mkutano wake na Rais Samia na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa hapo jana.
Waziri huyo alisema miongoni mwa mambo aliyozungumza na Rais Samia ni hofu ya Marekani kwenye utaratibu uliotumika kumkamata na kumshitaki Mbowe, huku akiomba Serikali ifuate misingi ya haki na sheria katika kesi hiyo.

Nuland alisema ana matumaini kuwa suala hilo litapatiwa ufumbuzi kwa majadiliano baina ya pande zote mbili, baada ya wote kuonyesha utayari wa kukutana na kulizungumza.
“Kwa mtazamo wangu pande zote mbili ni wazalendo na wana malengo mema, kwa hiyo ni vyema wakatumia nafasi hii ya utayari walionao kupata ufumbuzi wa kidemokrasia,” aliongeza.

Pia alimsihi Rais Samia, kuhakikisha ulinzi wa haki za binadamu na raia wote watendewe haki chini ya sheria, bila kujali ushirika wao kisiasa.
“Wakati anaanza na matamanio makubwa kidemokrasia na wapinzani pia walionyesha utayari kumuunga mkono, hatua nzuri sana zilishachukuliwa mwanzoni,” alisema.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Balozi, Liberata Mulamula alisema Rais Samia alipanga kukutana na wapinzani lakini ratiba zikaingiliana.
No comments :
Post a Comment