Sisikizi zenu hoja, nakwenda moja kwa moja
Naikidhi
yangu haja, siambiwe nimeroja.
Taanza pale Baghani, nimtafute mwandani
Si yule wa majiani, aletwe kutoka ndani
Anipendeze machoni, na
hata mwangu moyoni
Nakwenda owa
Unguja, nimpate wa faraja
Tasogea na
Shangani, nikachungulie ndani
Nimwage ya kifuani, bila
kujifanya duni
Wenyeji kuniamini,
niwekwe mwao vichwani
Nakwenda owa
Unguja, nimpate wa faraja
Tapita Vikokotoni, hodi
yangu mpaka ndani
Taomba kina fulani, yule
kiumbe wa shani
Niletewe ukumbini, irudi
nuru machoni
Nakwenda owa
Unguja, nimpate wa faraja
Nipelekwe Kinyasini,
nisisahau Chuwini
Nipite pia Bumbwini,
nitange na Mangapwani
Na uwanda wa Chaani,
khitamu Mkokotoni
Nakwenda owa
Unguja, nimpate wa faraja
Mnichukuwe na Mwera,
nituwe pale Uroa
Niwasalimu Makoba,
niwasilishe haiba
Yu wapi asio miba,
simtaki wa kuiba
Nakwenda owa
Unguja, nimpate wa faraja
Kimwana alie fana,
natafuta kumuona
Kwa tabia ilo njema,
ya urefu na mapana
Huyu wangu toka jana,
ndotoni nikimuona
Nakwenda owa
Unguja, nimpate wa faraja
By an Unknown author, Oct 2021 Muscat, Oman.
MAJIBU: Wa-Unguja wamejaa, hapo hapo unapokaa.
Wewe mtu wa viroja, kazi yako kuporoja,
Wa-Unguja wamejaa, hapo hapo napokaa,
Tafuta wako wasaa, siku inayokufaa
Sianze pale Baghani, wala siende Shanghani,
Wari wazuwiwa ndani, kuwaogopa wageni,
Huko kwenu wao duni, hata upo safarini?
Wa-Unguja wamejaa, hapo hapo napokaa.
Na wengine kama wewe, walifika Visiwani,
Tukiwapigia yowe, kote mwetu mitaani,
Mwenzangu ujielewe, si Unguja ya zamani,
Wa-Unguja wamejaa, hapo hapo napokaa.
Labda tafuta bubu, au asiesikia,
Atadhani wa Bububu, huyo atashangiria,
Msomi usijaribu, ajua ya Omania,
Wa-Unguja wamejaa, hapo hapo napokaa.
Usiende Kinyasini, wala kule Mangapwani,
Bora uende Bumbwini, upambane uchawini,
Kama wafuga majini, huko tapata mwandani,
Wa-Unguja wamejaa, hapo hapo napokaa.
Kimwana aliefana, tafuta utamuona,
Kama hujapata jana, endelea kutizama,
Ndotoni naemuona, huyo sie wa maana,
Wa-Unguja wamejaa, hapo hapo napokaa.
Kwani wataka ongeza, kutimiza yako sunna?
Kwa hilo nakupongeza, nenda hata kule China
Siwezi tena kubeza, Unguja tutaonana
Wa-Unguja wamejaa, hapo hapo napokaa.
Njoo ujichagulie, tupate changanya damu,
Mola akukubalie, umuache wa haramu,
Ili uje utulie, uwe kama mwanadamu,
Wa-Unguja wamejaa, hapo hapo napokaa.
/By An Unknown Author, Zanzibar!
TUNAKARIBISHA MASHAIRI, UTENZI, FEATURE ARTICLES, PHOTO EVENTS, NEWS, N.K KUTOKA KWA WASOMAJI WETU, LAKINI TUNAO UHURU WAKUBADILISHA INAPPROPRIATE WORDS ZILIZOTUMIKA BILA YA KUTAKA RIDHAA YA MTUNGAJI. KUWASILIANA NA SISI, TUMIA EMAIL: znzkwetu@gmail.com
ReplyDelete