Leo Novemba 27, 2021 Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania ofisi ya Zanzibar (THRDC- Zanzibar) kwa kushirikiana na Mahakama ya Zanzibar imeandaa warsha ya Siku mbili inayowakutanisha majaji na mahakimu kutoka Visiwa vya Unguja na Pemba kwa lengo kuu la kujadiliana, kukumbushana na kujengeana uwezo juu ya namna bora ya kuendesha mashauri ya haki za binadamu visiwani Zanzibar hasa katika kesi zihusuzo ukatili wa kijinsia (GBV).
Warsha hiyo imewakutanisha watendaji wa Mahakama takribani 50 kutoka Mahakama Kuu ya Zanzibar, akiwemo Kaimu Jaji Mkuu wa Mahakama ya Zanzibar, Mkurugenzi mkuu wa mashtaka kutoka visiwani Zanzibar, Kamishna Msaidizi wa Polisi- Zanzibar, Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na utawala bora Zanzibar, Mratibu THRDC - Zanzibar, Pamoja na Mwanasheria mkuu wa Serikali hii ni kwa lengo la kuongeza ari ya Mahakama katika kutatua kesi za haki za binadamu visiwani humo, huku watoa mada wakiwa ni
Jaji Mstaafu wa mahakama Kuu ya Tanzania, Mh. Jaji Joaquine De Mello, Jaji Mstaafu wa mahakama Kuu ya Tanzania, Mh. Jaji Awadh Bawazir, Dkt Clement Mashamba, Mhadhiri Shule ya sheria Tanzania ambaye ni Wakili mkuu wa Serikali mstaafu Pamoja na Prof. Chris Maina Peter, Mhadhiri wa chuo kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM).
Baada ya kubaini mapungufu katika mchakato wa utoaji haki katika kesi za haki za binadamu hasa kesi zinazohusu ukatili wa kijinsia (GBV), ambazo zimekuwa zikiripotiwa mara kwa mara visiwani Zanzibar, mahakama kwa kushirikiana na THRDC-Zanzibar iliamua kuandaa warsha hii ili kujadiliana namna bora ya kuisaidia jamii inayokumbana na maswaibu mbali mbali ikiwemo ukatili wa kijinsia ambao kwa kiasi kikubwa umekuwa ukiwaathiri wanawake na watoto.
Mahakama imebaini kuwa makundi haya (wanawake na watoto) yamekuwa yakishuhudia hukumu ndogo zinazotolewa kwa wahalifu pindi wanaporipotiwa katika vituo vya sheria, baadhi wamekuwa wakikumbana na vitendo vya rushwa huku wakati mwingine hukumu zikichukua muda mrefu kuhitimishwa jambo linaloipelekea jamii kuamua kukalia kimya vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyojitokeza katika jamii na hii ni kutokana na waathiriwa kukosa uwezo wa kifedha au kukosa uwakilishi mzuri wa kisheria katika kuendesha mashauri.
Hata hivyo ukatili wa kijinsia visiwani Zanzibar umekuwa ukitajwa kuongezeka siku hadi siku ambapo ripoti zinaonyesha kuwa kwa mwaka 2018 pekee, jumla ya kesi 942 za ukatili ziliripotiwa katika madawati ya kijinsia kwenye vituo vya polisi hii ni kwa mujibu wa ripoti ya (UNFPA, 2019), wakati Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGSZ) ikirekodi matukio 108 ya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto, Julai 2021, kesi 97 zilirekodiwa mwezi Juni. (Kwa mujibu wa Ripoti ya Afrika, 2021), hii inaonyesha ukubwa wa tatizo la ukatili wa kijinsia ambalo kwa kiasi kikubwa limekuwa likivunja haki za binadamu.
Kutokana na Takwimu hizi watetezi wa haki za binadamu bado wanaamini kuwa Kuna umuhimu kwa wawakilishi wa mahakama ambao pia ni watetezi wa haki za binadamu kuangalia mbinu huria, pindi linapokuja suala la hukumu katika mashahuri ya haki za binadamu ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Warsha hii ni muendelezo wa warsha mbali mbali zinazoendeshwa na mtandao zilizoanzia Tanzania Bara na sasa Visiwani ambazo zimekuwa zikiashiria mashirikiano endelevu ya Mtandao wa watetezi wa haki za Binadamu Tanzania (THRDC- Zanzibar) pamoja na mahakama katika kuhakikisha watendaji wa mahakama wanapata fursa ya kukutana kujadiliana na kukumbushana namna bora ya kuendesha mashauri haya, hii ni katika kuhakikisha kunakuwepo uzingatiwaji wa haki za Binadamu katika uendeshaji wa mashauri ya ukatili wa kijinsia ambayo yamekuwa yakiikumba jamii kwa kiasi kikubwa.
Imetolewa na Afisa Habari THDC
27 Novemba, 2021
No comments :
Post a Comment