dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, November 22, 2021

SHAIRI: GOOD NEWS!!!... - FATUMA APOSWA NA KAKAE BIDADA NA AUFUNGA MJADALA!


Subira Bidada nnayo, naogopa kula mbovu,
Ya leo yetu mioyo, imekosa utulivu,
Najihisi ovyo ovyo, peke yangu sina nguvu,
Kila anaesubiri, kweli yupo nae Mola.

Wawili ndio wawili, moja si sawa na mbili,
Mmoja bila wapili, maisha sio kamili,
Hata uwe na akili, pekee hufungi dili,
Kila anaesubiri, kweli yupo nae Mola.

Tabu shida kuhimili, ni bora muwe wawili,
Hata ile baskeli, inamaringi mawili,
Uwe kweli mkatili, umkatae wapili,
Kila anaesubiri, kweli yupo nae Mola.

Wala sifati mkumbo, kua nani kaolewa,
Lakini huku si ng'ambo, nani anae elewa?
Utapigiwa mafumbo, kama bado kuolewa,
Kila anaesubiri, kweli yupo nae Mola.

Hutoweza fanya jambo, utabaki kuzomewa,
Huku kwetu kuna mambo, sijui wayaelewa?
Utaulizwa hujambo, kama vile mezowewa,
Kila anaesubiri, kweli yupo nae Mola.

Ukipita mitaani, gari honi zitalizwa,
Utadhani we shetani, au ulotelekezwa,
Kila mtu hamkani, kama vile unauzwa,
Kila anaesubiri, kweli yupo nae Mola.

Utakuwa bado mwari, hata sitini miaka,
Au ni kichinchiri, mpaka watakuzika,
Kitaka kujistiri, chukuwa hata kibaka,
Kila anaesubiri, kweli yupo nae Mola.

Nimefurahi Bidada, kakayo keshaniposa,
Sasa takuja Canada, siendi tena Mombasa,
Nashukuru kwa msada, ningekufa kiofisa,
Kila anaesubiri, kweli yupo nae Mola.

Umefanya jitihada, kumbe ni mwana-siasa? 
Kama sio wewe dada, na pwani ningejitosa,
Nilishatoa shahada, na maisha kuyasusa,
Kila anaesubiri, kweli yupo nae Mola.

Harusi huko Toronto, anza kubuku hoteli,
Umekwisha mchakato, nitalipa zote bili,
Naona kama ni ndoto, wewe kwangu ni asali,
Kila anaesubiri, kweli yupo nae Mola.

Tamati napumzika, naenda zangu kulala,
Wiki sasa inafika, mbioni kama Impala,
Nishapata nachotaka, NAUFUNGA MJADALA!
Kila anaesubiri, kweli yupo nae Mola.

Fatuma binti Faki / Zanzibar, November 21, 2021.

https://zanzibarnikwetu.blogspot.com/2021/11/shairi-bidada-hits-back-fatuma-hebu_20.html

Support us by considering joining our Patreon scheme at: 

No comments :

Post a Comment