13th January 2013
Ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 50, aina ya Bombardier - Dash 8 ambayo ilitoka kwenye matengenezo na kuanza safari yake ya kwanza mkoani humo ilikuwa inaelekea jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili jana, Meneja wa Uwanja wa Ndege Mkoa wa Kigoma, Elipidi Tesha, alisema tukio hilo lilitokea Ijumaa majira ya saa 9.30, mchana eneo la uwanja wa ndege huo.
Tesha alisema, “ndege hii imefika tarehe 11 hapa Kigoma ikitokea Dar es Salaam, ikashusha abiria kisha ikapakia abiria 43 na wafanyakazi wanne ikaruka kuelekea Dar, baada ya dakika 20 ndege hiyo ilipasuka kioo cha mbele ikiwa angani ikabidi irudi tena katika uwanja wa ndege Kigoma hadi hapo watakapo leta kioo kingine ndipo ndege hiyo itaanza tena safari zake,” alisema Meneja huyo.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari gharama za kununua kioo kingine cha kuweka kwenye ndege hiyo ni kati ya Dola za Kimarekani 10,000 hadi 15,000. (Sh milioni 15.8 hadi Sh. milioni 23.7)
Meneja huyo alisema abiria waliokuwa kwenye ndege hiyo baadhi yao walirudishiwa nauli zao na wengine waliondoka kwa ndege ya kukodi kuelekea Mwanza kwa ajili ya kuunganisha usafiri wa kuelekea Dar es Salaam.
Alisema chanzo cha kupasuka kioo hicho hakijajulikana hadi hapo wataalamu watakapofika kutoka Dar es Salaam na kutoa ripoti kamili.
Alisema kuwa kioo hicho kinatarajiwa kupelekwa mkoani humo Jumatano ijayo ili ndege hiyo iweze kuendelea na safari zake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Hili ni tukio la pili la ajali ya ndege ya ATCL kutokea mkoani Kigoma, tukio la kwanza lilitokea Aprili 9, mwaka 2012 ambapo ilipata ajali ya kukatika bawa na tairi kuzama.
Hili ni pigo nyingine kwa ATCL ambayo katika kipindi kifupi imekuwa ikiyumba kujiimarisha lakini ikikumbana na mikiki. Itakumbukwa kuwa mwaka 2010 ndege ya kampuni hiyo Boeing 737 ikiwa na abiria wakati inakaribia kutua kwenye uwanja wa ndege ya Mwanza iliserereka na kuanguka kisha injini yake moja kuharibika.
Ajali hiyo isiyokuwa na madhara kwa binadamu ilisababisha ndege hiyo kuachwa juu ya mawe kwenye uwanja huo wa Mwanza na taarifa zilizopo ni kwamba gharama ya kuikarabati ni kubwa na ATCL haina uwezo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment