NA MWANDISHI WETU
16th January 2013
(3).jpg)
Alisema kuwa ni jambo la hatari na lisilo na tija kwa wanasiasa kujaribu kuigawa nchi vipande vipande kwa sababu ya kujitafutia umaarufu kwa kutumia rasilimali za taifa.
Rais Kikwete aliyasema hayo jana alipokutana na Balozi wa Uingereza nchini ambaye anamaliza muda wake, Dianne Corner.
Kuhusu ugunduzi wa gesi asilia uliofanywa na Kampuni BG ya Uingereza katika eneo la Msimbati kwenye Bahari ya Hindi, walikubaliana kuwa hilo ni jambo jema na lenye kuleta matumaini kwa Tanzania.
Rais Kikwete alisema kuwa ni tabia ya hatari kwa wanasiasa kutumia gesi asilia hiyo ama rasilimali nyingine kujijengea umaarufu.
“Unawezaje kuwa na nchi moja na taifa moja wakati kila mmoja anadai rasilimali kutoka kwenye eneo moja ibakie na kunufaisha watu wa eneo hilo tu. Huwezi kuwa na nchi moja na yenye umoja wakati kuna nchi ya gesi asilia kule Mtwara, kuna nchi ya kahawa kule Kilimanjaro, kuna nchi ya chai na ndizi kule Bukoba,”
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilimkariri Rais Kikwete akisema.
“Kwa sababu kama gesi asilia inatakiwa kubakia na kunufaisha watu wa Mtwara tu, basi wenye haki zaidi ya kudai jambo hili siyo watu wa Mtwara bali ni watu wa Msimbati ambako ndiko ilipogunduliwa gesi ambako ni maili 60 kutoka Mtwara, kilomita 200 kutoka Newala,” aliongeza.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment