NA MWANDISHI WETU
24th January 2013
Asema madaraka ya Rais ni makubwa, yapunguzwe.jpg)
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ametofautiana na Waziri Mkuu mwingine mstaafu ambaye aliwahi kushika madaraka hayo juu ya madaraka ya rais katika katiba mpya ijayo na ameweka wazi kuwa ni vyema ikampunguzia rais madaraka.
Waziri Pinda alitoa mapendekezo hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba, jijini Dar es Salaam jana, mara baada ya kuwasilisha maoni yake kwa tume hiyo kuhusu uundwaji wa katiba mpya.
“Nimejaribu kutazama majukumu ya Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu….Rais ana majukumu mengi ya kufanya, lakini kwa uzoefu wangu niliowahi kufanya kazi, maeneo mengine ni lazima tukasimu kwa wengine,” alisema Pinda na kuongeza:Waziri Pinda alitoa mapendekezo hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba, jijini Dar es Salaam jana, mara baada ya kuwasilisha maoni yake kwa tume hiyo kuhusu uundwaji wa katiba mpya.
“Rais huyo huyo ashughulikie mambo ya uteuzi, huyo huyo ashugulikie masuala ya nidhamu…ni lazima majukumu hayo pia vipewe vyombo vingine vishughulikie.”
Pinda anatofautina na John Malecela ambaye alikuwa waziri mkuu kati ya mwaka 1990 hadi 1994, ambaye wiki iliyopita baada ya kutoa maoni yake kwa Tume aliwaambia waandishi wa habari kuwa ni vyema madaraka ya Rais yakaachwa yalivyo na kuhoji kuwa ukipunguza madaraka hayo yatapelekwa wapi kwani ni muhimili unaojitegemea.
Malecela alisema nchi changa kama Tanzania bado kuna haja ya rais kuwa na madaraka makubwa ili kumwezesha kusimamia vizuri nchi anayoiongoza.
Pinda pia alizungumzia madaraka ya Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, na kutaka nao katiba mpya iwapunguzie madaraka kutokana na kukabiliwa na majukumu mengi, yakiwamo ya ubunge na serikali, huku akitaka suala hilo liangaliwe upya katika uundwaji wa katiba hiyo.
“Waziri Mkuu humsaidia Rais katika masuala yote ya utendaji wa serikali. Pia huyo huyo mbunge…nalo eneo hili lingetazamwa vizuri kwenye katiba mpya ijayo,” alisema Pinda.
ATAKA MAWAZIRI WASITOKANE na UBUNGE
Kuhusu kushika nafasi mbalimbali, Pinda alisema mawaziri wasitokane na wabunge ili wawe na muda mzuri wa kushughulikia majukumu ya kiserikali na wabunge washuhulikie majukumu ya majimbo yao.
MIHIMILI YA DOLA ISIINGILIANE
Kuhusu mihimili mitatu ya dola, ikiwamo Serikali, Mahakama na Bunge, Pinda alipendekeza kuwa katiba mpya iwe na kifungu kinachoeleza kutoingiliana kwao kwa madai ya kwamba kila chombo kifanye kazi kwa uhuru bila kuingiliwa na kingine.
MAHAKAMA
Kuhusu Mahakama, alipendekeza katiba mpya ieleze jinsi chombo hicho kinavyopaswa kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.
BUNGE
Alisema kuwa Bunge ni muhimili muhimu na kwamba lipewe nafasi ya kutosha kwa kujijengea uwezo ikiwa ni pamoja na kuwa na mifuko ambayo inapaswa kuelezwa ndani ya katiba mpya kwa ajili ya kujiendesha vyema.
SERIKALI ZA MITAA
Pinda alisema badala ya kuwa na ibara mbili tu zinazoelezea kuhusu serikali za mitaa kama ilivyo ndani ya katiba ya sasa, katiba mpya iongeze vifungu vingine kwa ajili ya kuzisaidia serikali hizo kujiendesha zenyewe, ikiwamo vile vinavyohusu mapato ndani ya vyombo hivyo.
MUUNGANO
Alipendekeza kuwa mfumo wa serikali mbili uliopo uendelee, huku akipendekeza kuundwa chombo maalumu kwa ajili ya kusimamia masuala yote yanayohusiana na Muungano.
“Muungano ulianzishwa mwaka 1964, miaka 49 ni mingi kujenga hisia. Mimi nilizaliwa mwaka 1948, hivyo ninao uzoefu wa kutosha kuhusu Muungano. Tangu kuanzishwa kwake, Muungano umeleta undugu kati ya pande hizi mbili,” alisema Pinda na kuongeza:
“Kuna changamoto, lakini dawa si kuuondoa bali kiundwe chombo maalumu. Chombo hicho hicho kiwe ni tume maalumu itakayokuwa inashughulikia masuala yote yahusuyo Muungano. Ndiyo maana hata Zanzibar walipoona vyema, waliamua kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Muungano ninaouafiki ni huu huu wa serikali mbili, uendelee.”
Mbali na kutoa maoni, Pinda pia alitumia muda huo kukagua kazi inayofanywa na tume hiyo tangu ianze kazi yake mwaka uliopita kwa kuzunguka takriban mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar kukusanya maoni kwa ajili ya uundwaji wa katiba mpya.
Alisema ameridhika na kazi ya Tume kwamba inafanya vizuri.
Mawaziri wakuu wengine wastaafu waliozungumzia madaraka ya Urais kwa tume ni Federick Sumaye, ambaye alitaka yapunguzwe.
Cleopa Msuya naye alitoa maoni yake lakini vyombo vya habari havikupata alichozungumza.
Mawaziri wakuu wastaafu wengine ni Jaji Mstaafu Joseph Warioba na Dk. Salm Ahmed Salim ambao ni wajumbe wa Tume. Warioba ni mwenyekiti na Salim ni makamu.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment