NA EDITOR
21st May 2013
.jpg)
Pamoja na kugundulika kwa utajiri, hofu ya kutokuwapo kwa sheria madhubuti ambazo zinaongoza sekta hiyo ambayo huenda kwa miaka mingi ijayo ikawa ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa taifa hili, imekuwa ni changamoto kubwa.
Rasimu ya sera hii inatazamwa kama moja ya msingi wa kuwa na sheria nzuri ambayo itajibu maswali mengi ambayo hayana majibu kwa sasa katika sekta hiyo.
Kwa bahati mbaya tayari rasimu hiyo imepokewa kwa hisia tofauti miongoni mwa wabunge, kuna baadhi wamekwisha kutoa maoni yao kwamba imeshindwa kutofautisha suala la mafuta na gesi kuwa ni suala la Muungano.
Hoja hii inajengwa kwa misingi kwamba wakati Zanzibar inajiandaa kuwa na sera na sheria yake ya mafuta ya gesi, rasimu hiyo inaeleza kwamba gesi asilia ni mali ya Jamhuri ya Muungano wakati upande mmoja wa Muungano utakuwa unafaidi utajiri wake peke yake.
Changamoto mpya inayoibuliwa hapa ni kwamba rasimu hiyo pia imeshindwa kutambua kuwa kuna vitalu vya mafuta na gesi ya (vitalu namba 9-12) vimesimamisha shughuli kwa sababu Serikali ya Zanzibar haitambui mafuta na gesi kuwa suala la Muungano.
Pia rasimu hii inaelezwa kutokuitambua shughuli za utafutaji gesi na hivyo inakuwa ya upande wa biashara na kuacha kazi yenyewe haswa ya utafutaji na uchimbaji bila kuratibiwa na kudhibitiwa na sera na baadaye sheria itakayozaliwa kutokana nayo.
Mfumo wa sera kama huu siyo tu unaacha makampuni makubwa ya nje kunufaika na sekta ya gesi kwa sababu ndiyo yanajishughulisha na kazi ya utafiti wa nishati hiyo, bali inaendeleza hofu kuwa sekta hii kama taifa halitakuwa macho litabakia kuwa watazamaji wakati gesi ikinufaisha wengine kama ambavyo hadi sasa sekta ya madini ilivyo.
Rasimu hii inatukumbusha tahariri tuliyoandika katika safu hii Oktoba 3, mwaka jana tukisema kuwa ‘Tunataka usimamizi madhubuti gesi asilia’ tukirejea hotuba ambayo alikuwa ametoa Rais mwisho wa Julai mwaka jana juu ya hazina ya gesi nchini.
Katika hotuba hiyo Rais alisema kuwa neema hiyo inatarajia kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa taifa hili kwa sasa na siku za usoni. Hata hivyo, alionya kwamba kuna changamoto kubwa kufikiwa kwa matamanio ya neema hiyo kwani bila kujipanga sawasawa kama taifa inaweza kuwa laana. Ni kweli imetokea hivyo kwa mataifa mengi ya Afrika.
Yapo mataifa mengi tu duniani yanaendesha uchumi wao kwa kutegemea gesi asilia pekee yake. Kwa Tanzania gesi inakuwa ni nyongeza juu ya madini mengi kama dhahabu, almasi na madini mengine mengi vito yanayopatikana nchini, mengine yakipatikana Tanzania tu; tuna ardhi yenye rutuba iliyotanda kote, maji ya mito na maziwa makubwa yenye maji safi ya yanayofaa kuendesha kilimo cha kibiashara na shughuli nyingine za kiuchumi. Ipo misitu mingi na minene.
Hata hivyo, ingawa tuna neema zote hizi, kumekuwa na mjadala wa nini hasa kiini cha umasikini wetu kama taifa pamoja na kuwa na rasilimali zote hizi. Wapo wanaojiuliza na kwa kweli kwa hoja kwamba inawezekana vipi kwa neema zote hizi bado tunakuwa taifa ombaomba na masikini linaloshindana na mataifa ambayo hayana rasilimali yoyote ya maana na yakiwa yamedumu kwenye vita kwa miaka na miaka?
Pengine ndiyo maana Rais Kikwete alisema changamoto zinazotukabili kama taifa ili kweli tunufaike na gesi hii ni nyingi; kama vile kuandaa watu wetu; kutengeneza sera na sheria, lakini la umuhimu zaidi kujenga rasilimali watu itakayosimamia rasilimali hii pamoja na mifumo inayoeleweka ili taifa linufaike kwanza na siyo mataifa ya nje.
Angalizo hilo la Rais linafanana kabisa la mengine mengi ambayo yametolewa na wataalama mbalimbali likiwamo Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambalo lilitaka Serikali ijipange na kuweka kipaumbele kwenye maandalizi ya mifumo ya udhibiti na kisera kwa ajili ya kuratibu mapato yatokanayo na gesi asilia na mafuta, ili rasilimali hiyo iwanufaishe wananchi pamoja na kukuza uchumi.
Ushauri huo ulitolewa mwkaa jana na ujumbe wa timu ya maofisa wa IMF waliokuwa nchini, kwa lengo la kufanya majadiliano ya Tathmini ya Mapitio ya Tano, chini ya Mpango wa Ushauri wa Sera za Uchumi na Tathmini ya Kwanza ya Mpango wa Msaada wa Dharura, ambao uligusa hisia za ndani kabisa za wananchi wa nchi hii juu ya faida ya kugundulika kwa gesi hiyo.
Hakuna ubishi kama ambavyo inaeleweka kote duniani kwamba gesi asilia ni neema kwa uchumi wa nchi yoyote endapo tu rasilimali hiyo itawekewa mifumo na kuratibiwa vizuri kwa ajili ya ustawi wa wananchi wake.
Ingawa hadhari hizi zinatolewa sasa, kuna hofu miongoni mwa wananchi kwamba huenda gesi asilia ikafuata mkondo wa uvunaji wa rasilimali nyingine nchini, ambazo hazijaonyesha tija kwa maana ya kuleta mabadiliko kwa taifa kwa ujumla wake; bado Watanzania wanajiona kuwa ni watanzamaji katika kushiriki na kunufaika na utajiri unaovunwa ndani ya nchi yao.
Rasimu hii mpya ya sera ya gesi inazidi kujenga hofu kwamba hunda rasilimali ikawa laana badala ya neema kwa taifa letu; tunachukua fursa hii kuchagiza wadau wote wa maendeleo ya nchi hii kujipanga kutoa maoni yao juu ya rasimu hii ili kuokoa gesi. Wakati ni sasa.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment