NA MWANDISHI WETU
18th May 2013
.jpg)
Mkakati huo unadaiwa kutekelezwa kupitia kamati kadhaa za Bunge, mojawapo ikiwa ni Kamati ya Kudumu ya Miundombinu inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba.
Serukamba anadaiwa kuandika ripoti ya kamati hiyo, akitumia `maneno makali’ kupitia maoni ya kamati kuhusu bajeti ya wizara ya uchukuzi kwa mwaka 2013/2014.
Taarifa za ndani kutoka kwenye kikao cha kamati hiyo, zinaeleza kuwa ripoti ya Serukamba ilijumuisha maswali ya moja kwa moja kwa Dk mwakyembe, tofauti na inavyotakiwa, kuihoji na kuishauri serikali.
Lakini ilikataliwa na wajumbe wenzake wakiwamo wanaotokana na CCM. Hatua hiyo inadaiwa kutokea siku tatu kabla ya kuwasilishwa kwa ripoti ya kamati hiyo bungeni.
“Lugha iliyotumika katika ripoti iliyoandikwa na Serukamba ililenga kumshambulia Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, tukaikataa,” kilieleza chanzo chetu.
“Haya yote ni sababu ya makundi yanayowania urais ndani ya chama chetu, hakuna hotuba ya kamati inayoweza kuandikwa kwa namna ile kwa sababu madhumuni ya kuwapo kwa kamati ni kuishauri serikali na si kuihoji tu,”alisema mtoa taarifa.
“Yaani hata kama wabunge ni wasimamizi wa wizara, lakini `staili’ ya namna hii haifai, haimtendei haki Dk Mwakyembe,” alieleza.
Kutokana na kukataliwa kwa maoni ya Serukamba, iliundwa kamati ndogo ya wabunge watatu, kusahihisha lugha iliyotumika katika kuandaa maoni ya kamati hiyo ya Bunge.
Wajumbe wa kamati hiyo iliyoundwa Jumatatu wiki hii walikuwa Ramo Makani (Tunduru Kaskazini) na wabunge wa Viti Maalum (CCM), Rita Kabati na Zarina Madabida.
Hotuba za bajeti za kamati za kisekta, zinaandikwa na Mwenyekiti akisaidiana na katibu wa kamati husika.
“Unajua sisi kazi yetu kubwa ni kuishauri serikali na si kuhoji maswali, maswali unaweza kuhoji wakati wa kuchangia mbunge mwenyewe, lakini si kwa kuandika katika maoni ya kamati,” kilisema chanzo kingine.
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge toleo la 2007 ya 114(18), Kamati ya Kudumu ya Bunge inaweza kuunda kamati ndogo kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli zake, kadri itakavyoona inafaa.
Inapotokea hivyo, kila kamati ndogo itapangiwa kazi zake na kamati husika ya kudumu ya Bunge.
Aidha, baadhi ya wajumbe walieleza kutoridhishwa na uongozi wa Serukamba hasa inapotokea kamati hiyo kuwaita Dk Mwakyembe, Naibu wake, Gerson Lwenge na Katibu Mkuu, Omar Chambo.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Juma Kapuya, alithibitisha kuundwa kwa kamati ndogo ndani ya kamati hiyo, lakini alikana si kwa ajili ya kurekebisha lugha iliyotumika kwenye hotuba hiyo.
Habari zilisema Serukamba ambaye alirejea bungeni Alhamisi akitokea China, alikuta marekebisho hayo, hivyo kususia kutoisoma bungeni.
Lakini, inaelezwa kwamba alishauriwa na mmoja wa wajumbe ‘rafiki zake’ kuwa aisome vinginevyo, ingeleta taswira hasi kwake ndani na nje ya Bunge.
Hata hivyo, Serukamba alikana kuhusika na tuhuma hizo na kusema hotuba za maoni zinaandikwa na makatibu, kisha kuwasilishwa kwa wajumbe wa kamati wanaoteua kamati ndogo inayoongeza majadiliano ya wajumbe katika maoni hayo.
“Mimi kwanza sikuwepo, nilikuwa China….huu ni ndio utaratibu tuliouzoa nashangaa mambo haya yamekuzwa bure,”alisema Serukamba.
Kwa upande wake, Dk. Mwakyembe alishangaa waandishi kuzipata hotuba za maoni ya kamati hiyo na kusema kuwa alikuwa akiisubiri kwa hamu asome maoni hayo ili amjibu.
“Bahati mbaya hakuisoma , nilikuwa namsubiri aisome ningemchanachana,”alisema Dk. Mwakyembe alipoulizwa kuhusiana na habari za kuwapo kwa maoni yaliyolenga kumshambulia.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment