NA MWINYI SADALLAH
28th June 2013
.jpg)
Makadirio ya matumizi ya ofisi hiyo yalikwama kupitishwa juzi jioni baada ya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu kuzuia shilingi katika fungu la uratibu na utawala lililopangiwa kupata Sh. 768,000,000.
Kati ya fedha hizo, mwakilishi huyo alitaka Sh. milioni 270 zikatwe na kupelekwa kwenye shughuli za kudhibiti uharibifu wa mazingira, kupambana na dawa za kulevya na kusaidia watu wenye ulemavu.
Jussa alitoa hoja hiyo wakati Baraza lilipokaa kama kamati ya matumizi kupitisha vifungu vya makadirio ya bajeti ya ofisi hiyo, ambapo alisema eneo hilo linapatiwa fedha nyingi lakini tija inayopatikana hailingani na thamani ya fedha hizo.
Alisema mwaka ujao wa fedha Tume ya Ukimwi imepanga kutumia Sh. bilioni 3.5 zikiwemo fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo wakati kiwango cha maambukizi ya virusi vya ukimwi kimeongezeka pamoja na tume hiyo kupatiwa fedha nyingi katika mwaka wa fedha unaomalizika.
Jussa alisema kama serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kampeni ya kuzuia maambukizi lakini tija inayopatikana hailingani na thamani halisi ya fedha hizo, ni vizuri zikapelekwa kwenye maeneo ambayo ofisi yenyewe imekiri inakwama kutekeleza.
Mwakilishi wa Kiwani, Hija Hassan Hija naye alitaka maelezo kuhusu mgao mdogo wa bajeti unaopewa shughuli za hifadhi ya mazingira eneo ambalo alisema linapigiwa kelele dunia nzima.
Alisema bajeti ya Idara ya Mazingira imekuwa ikikosa fedha kulingana na mahitaji yake halisi na hivyo kusababisha kukwama kwa miradi mingi ya vikundi vinavyoshughulikia hifadhi ya mazingira kwenye maeneo yanayoathirika kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment