NA RAPHAEL KIBIRITI
28th June 2013
.jpg)
Hivi karibuni, Rais Museveni alimwalika Rais Kenyatta kwenye mkutano uliomshirikisha Rais Kagame, ambao pamoja na mambo mengine, walikubaliana kuendesha miradi ya reli na bomba la mafuta kutoka Kigali, Uganda kwenda bandari ya Lamu, Kenya.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kitendo hicho kinaonyesha muelekeo usio mzuri kwa mustakabali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
“Kunapojadiliwa mradi mwingine kama wa reli, wakati tayari kuna mradi wa reli uliokwishapitishwa kujengwa na EAC unaotokea Burundi, Rwanda na kuja kuunganishwa na reli ya kati, katika eneo la Kahama unaleta utata,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema kitendo cha kutojumuishwa kwa Rais Kikwete kwenye masuala yanayohusiana na jumuiya, kunaweza kutafasiriwa kama ishara ya kutofurahishwa kwa baadhi ya viongozi wa eneo hilo, kutokana na kitendo cha Rais Barack Obama kufanya ziara nchini.
Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, utata huo unaweza kuunganishwa na kitendo cha Rwanda kufanya kampeni maalum na mashambulizi dhidi ya Rais Kikwete.
Alimkumbusha Rais Museveni kutoisahau Tanzania jinsi ilivyotoa mchango mkubwa wa ushirikiano kwa Uganda.
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Profesa MwesiguBaregu, alisemakuna haja ya kuratibu mipango na miradi katika eneo la Afrika Mashariki kwa pamoja.
“Ni kweli kwamba, kuna mikakati mingine ya kimaendeleo, kama ule mradi wa Maziwa Makuu unaohusiana na ujenzi wa miundo mbinu na miradi ya mawasiliano.
Lakini sasa unapozungumzia miradi ya aina moja na ile iliyo ndani ya jumuiya bila ya kuwashirikisha wenzenu, kunakuwa na wasiwasi kidogo,” alisema.
Alisema inawezekana hali hiyo inajitokeza kutokana na ukaribu wa Tanzania na Marekani na kuwa sasa kuna ugeni wa Rais Obama nchini hali, ambayo huenda haiwafurahishi majirani.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema haoni tatizo kwa Rais Museveni kumwalika Rais Kenyatta katika mkutano uliomshirikisha Rais Kagame kwa kuwa ni mwaliko wa nchi na nchi.
Hata hivyo, alisema umuhimu wa kumshirikisha Rais Kikwete unatokana na miradi inayotekelezwa kuwa katika mkataba.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alipotafutwa jana, ili kuzungumzia suala hilo, hakupatikana na hata alipopigiwa simu yake ya mkononi ilikuwa imezimwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment