NA MUHIBU SAID
28th June 2013

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, aliwaambia waandishi wa habari, Ikulu, jijini Dar es Salaam jana kuwa majadiliano hayo yatajikita katika kubadilishana uzoefu kuhusu matumizi ya teknolojia katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii barani Afrika.
“Tulifanya majadiliano hayo kwenye kanda zaidi ya 11. Washiriki zaidi ya 500 walishiriki. Vikundi mbalimbali vilishiriki katika ngazi ya nchi na kanda,” alisema Balozi Sefue.
Alisema mbali na marais, majadiliano yanayoanza leo, pia yatahudhuriwa na makamu wa rais wawili, mawaziri wakuu na mawaziri kutoka baadhi ya nchi duniani.
Marais, ambao walitarajiwa kuwasili nchini kushiriki majadiliano hayo, aliwataja kuwa ni pamoja na Uhuru Kenyatta (Kenya) na Yoweri Museveni (Uganda).
Wengine ni Thomas Boni Yayi (Benin), Mahinda Rajapaksa (Sri Lanka), Ali Bongo (Gabon), Dhoinine Ikililou (Visiwa vya Comoro), Mfalme Mswati wa II (Swaziland), Blaise Compaore (Burkina Faso) na Faure Gnassingbé (Togo).
Balozi Sefue alisema majadiliano hayo yatahudhuriwa pia na Makamu wa Rais wa Botswana, Luteni Jenerali Mompati Merafhe; mawaziri wakuu; Najib Razak (Malaysia) na Abdelmalek Sellal (Algeria).
Alisema majadiliano hayo yanalenga kubadilishana uzoefu wa namna nchi hizo zitakavyoweza kuimarisha ushirikiano.
Balozi Sefue alisema mbali na kupata uzoefu kutoka nchi nyingine, Tanzania itafaidika pia na teknolojia kuharakisha maendeleo katika maeneo mbalimbali, ikiwamo nishati, elimu na namna ya kuongeza mapato.
Alisema mbali na viongozi hao wakuu wa nchi, wengine wanaotaraji kuipa heshima Tanzania, ni pamoja na Rais wa Marekani, Barack Obama, Rais mstaafu wa nchi hiyo, George W. Bush na mkewe pamoja na wake wa baadhi ya marais, ambao wanatarajiwa kuwasili nchini kwa shughuli maalum.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment