dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, August 8, 2013

JUSSA-TAASWIRA YA ZANZIBAR INACHAFULIWA

POSTED BY   //  08/08/2013  

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mwakilishi wa Jimbo la Mji mkongwe,Mh,Ismail Jussa Ladhu.
Mwakilishi wa Jimbo la Mji mkongwe,Mh,Ismail Jussa Ladhu.

Taswira ya Zanzibar kama kisiwa cha amani imechafuliwa tena jana usiku
pale watu wasiojulikana walipofanya kitendo cha kinyama na kishenzi
cha kuwamwagia tindikali (acid) wananchi wawili wa Uingereza katika
maeneo ya Shangani, jimbo la Mji Mkongwe. Taarifa za awali
nilizozipata ni kwamba vijana hao wawili wapo Zanzibar wakiwa ni
sehemu ya vijana wanaojitolea (volunteers) katika shughuli za sanaa
(Arts).
Nikiwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe,
mwananchi wa Zanzibar ninayeipenda nchi yangu na pia nikiwa kama
binadamu ninayethamini utu wa kila mtu nalaani vikali na kwa nguvu
zote uovu na uhalifu huo ambao umekiuka misingi ya ubinadamu na utu.
Polisi na mamlaka nyengine za nchi zinapaswa kufanya uchunguzi wa kina
na wa haraka wa kuwajua ni nani waliohusika na tukio hili na
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Hili la kuchukua hatua za haraka na za dharura na kuongeza kasi ya
uchunguzi ni la muhimu sana maana sasa matukio ya hujuma kwa kutumia
tindikali (acid) yamekuwa ni jambo la kawaida na yanaendelea
kuongezeka.
Tukio hili la jana linakwenda moja kwa moja na kupiga moyo
wa uchumi wa Zanzibar kwa maana ya sekta ya utalii. Tusipochukua hatua
za haraka na za dharura na kuonekana tunajali, uchumi wa Zanzibar
unaweza kuathirika kwa kiasi kikubwa na kuyumbisha utoaji wa huduma
kwa wananchi, huduma ambazo zinategemea mapato yanayotokana na utalii.

Nilipata nafasi ya kufika haraka pale walipokuwepo waathirika wa tukio
hilo mara baada ya kupata taarifa na pia kuwasindikiza hadi Uwanja wa
Ndege wa Zanzibar nikiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na
Michezo, viongozi wa Jumuiya ya Wawekezaji katika Sekta ya Utalii
(ZATI) na Balozi wa Heshima wa Uingereza aliyepo Zanzibar. Nawapa pole
wasichana hao wawili na nawaombea wapone kwa haraka. Fikra, hisia na
dua zetu ziko pamoja nao.
Sifa ya Zanzibar kwa karne nyingi imekuwa ni kisiwa cha amani ambacho
watu wake ni wastaarabu, wakarimu na wanaopenda wageni. Mjengeko wa
jamii ya yetu ya Kizanzibari wenyewe umetokana na mchanganyiko wa watu
kutoka sehemu mbali mbali duniani ambao walihamia Zanzibar na
kupafanya ndiyo maskani yao. Kitendo kama hichi kilichotokea jana
kinakwenda kinyume na misingi ya historia yetu hiyo.
Ni mapema kusema ni nani aliyepo nyuma ya kitendo hichi lakini jambo
moja la wazi ni kuwa yeyote anayehusika amekusudia kuiumiza Zanzibar
na Wazanzibari. Kuuhujumu utalii ni kuuhujumu uchumi wa Zanzibar na
kuyahujumu maisha ya Wazanzibari.
Wakati mamlaka zinazohusika zikiendelea na uchunguzi wa tukio hili,
kuwasaka waliohusika na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, natoa
wito kwa Serikali kuchukua hatua zifuatazo:
1. Kuongeza doria za polisi ndani ya Mji Mkongwe ambao bado unabakia
kuwa ndiyo mji mkuu wa Zanzibar na pia kituo kikuu cha harakati zote
za kiuchumi ikiwemo biashara na utalii. Kuwepo kwa Polisi Jamii chini
ya dhana ya Ulinzi Shirikishi kusiwe ndiyo mbadala wa Jeshi la Polisi
kutekeleza wajibu wake hasa kufanya doria za kawaida.
2. Kuuwekea Mji Mkongwe kamera za mitaani za kufuatilia nyenendo za
watu (surveillance cameras) hasa ikizingatiwa kuwa Mji Mkongwe ndiko
kwenye harakati nyingi zinazopelekea mkusanyiko wa watu wengi wakiwemo
watalii na wageni wengine wanaotembelea Zanzibar.
3. Mji Mkongwe kurejeshewa huduma ya taa za njiani na za mitaa (street
lights) ili kuongeza usalama wa watu wakiwemo wageni wanaotembelea
eneo hili ambako kuna idadi kubwa ya hoteli za kitalii.
4. Jeshi la Polisi Zanzibar limekuwa likilalamika kwa kuwa na bajeti
ndogo isiyokidhi mahitaji ya kutekeleza wajibu wao ipasavyo ikiwa ni
pamoja na kutokuwa na usafiri wa uhakika, mafuta na vifaa vya kazi.
Mamlaka zinazohusika zinapaswa kukaa pamoja na kutatua matatizo haya.
5. Serikali, Jeshi la Polisi, na mamlaka nyengine zinazohusika pia
wanapaswa kuwa na vikao vya mashauriano vya mara kwa mara na Jumuiya
ya Wawekezaji katika Sekta ya Utalii (ZATI) na Jumuiya ya Watoa Huduma
za Usafirishaji na Utembezaji Watalii (ZATO) ili kushughulikia
matatizo mbali mbali yanayojitokeza hususan yale yanayohusu masuala ya
usalama wa wageni wanaotembelea Zanzibar.
Mwisho, natoa wito kwa wananchi na wakaazi wote wa Mji Mkongwe na
Zanzibar kwa ujumla kuwa makini na kufuatilia nyenendo zinazotia
mashaka au zinazoashiria mwelekeo wa kufanya vitendo vya uhalifu ndani
ya Mji wetu na ndani ya Zanzibar au hata nje ya Zanzibar na pale
wanapobaini mwelekeo kama huo kutoa taarifa haraka kwa mamlaka
zinazohusika.
ISMAIL JUSSA
MJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI
JIMBO LA MJI MKONGWE

CHANZO: MZALENDO

No comments :

Post a Comment