Tunataka Mambo matano yaondolewe
katika muungano’
Micheweni. Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, wametoa mapendekezo ya pamoja wakitaka mambo matano yaondolewe kwenye Muungano, yabaki kwenye Serikali washirika.
Waliyopendekeza yaondolewe ni Mambo ya Nje, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki kuu, usajili wa vyama vya siasa pamoja na ushuru wa bidhaa wakisema kwamba kama yataendelea kuwepo kwenye Muungano kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba yatasababisha Serikali shirikishi kuwa dhaifu.Wakizungumza baada ya kuwasilishwa kwa kazi za makundi yaliyopewa jukumu la kujadili suala la mihimili, wajumbe hao walisema mambo hayo matano ndiyo yanayoweza kuzipa nguvu Serikali shirikishi ambazo zitakuwa Tanganyika na Zanzibar.
Walitolea mfano wa mambo ya nje na kusema kuwa ikiwa Rais wa Serikali ya Tanganyika au Zanzibar ataondolewa jukumu la kuteua mabalozi na hata kuiwakilisha nchi nje ya nchi atakuwa ameondolewa meno. “Nchi washirika ziachiwe masuala ya mambo ya nje,”alisema Kassim Mohamed Kassi, mkazi wa Chimba akiwakilisha vijana.
Kuhusu Sarafu na Benki Kuu, walisema sababu za kupendekeza iondolewe katika muungano ni kuwa itadhoofisha uchumi wa nchi washirika.
Aidha kwa upande wa uraia na uhamiaji, walisisitiza kuwa kila nchi watu wake wana utamaduni usioingiliana na nchi nyingine washirika, hivyo kila upande uwe huru.
Ushuru wa bidhaa, wajumbe hao walipendekeza ubaki kwenye nchi washirika na siyo Muungano kama inavyopendekezwa kwa sababu ikiwa itaachwa hivyo sehemu kubwa ya kodi na ushuru kutoka nchi washirika zitashindwa kuwanufaisha watu wake.
Kuhusu usajili wa vyama vya kisiasa, wajumbe hao walisema hiyo ni moja ya kero za muungano iliyojitokeza baada ya kuingia kwa mfumo wa vyama vingi. Sheria ya chama ili kisajiliwe sharti kipate wanachama wa mikoa ya Tanzania bara na Zanzibar. Walitaka mambo ya muungano yabaki mawili tu ambayo ni Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano.
Mwananchi
No comments :
Post a Comment