dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, August 26, 2013

Mbowe, Lissu, Msigwa mbaroni

NA WAANDISHI WETU

26th August 2013


  Ni kutokana mikutano ya mabaraza ya katiba
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, akiwahutubia wakazi wa Kawe kwenye viwanja vya Tanganyika Parkers jijini Dar es Salaam jana, katika mkutano wa Baraza la Katiba wa kujadili na kuboresha rasimu ya Katiba mpya.
Kamatakamata ya Polisi dhidi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imeendelea baada ya  Mwenyekiti wa Chama hicho, Taifa, Freeman Mbowe na wabunge wawili kutiwa mbaroni na Jeshi hilo mkoani IIringa kwa madai ya kutaka kuvunja amani.

Viongozi hao wamekamatwa na kuhojiwa kwa zaidi ya saa tatu, wakidaiwa kutaka kuvunja amani, ingawa haikuelezwa ni jinsi gani walitaka kuvunja amani hiyo.

Mbali na Mbowe, wengine waliokamatwa ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Mashariki, Tundu Lissu; Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na Diwani wa Kata ya Mivinjeni katika Manispaa ya Iringa, Frank Nyalusi.

Mbowe na wenzake walikamatwa jana  asubuhi katika Hoteli ya Country Side iliyopo Kata ya Kihesa Manispaa ya Iringa wakati wakijiandaa kuondoka kuelekea mjini Dodoma kuhudhuria Mkutano wa 11 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano unaotarajiwa kuanza kesho.

Juzi viongozi hao walifanya mikutano kadhaa ya hadhara ya mabaraza ya katiba mkoani Iringa.
Kwa wiki kadhaa,viongozi waandamizi wa Chadema wakiongozwa na Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa wamekuwa katika ziara ya mikoa yote nchini kufanya mikutano ya hadhara ya mabaraza ya katiba kwa kutumia helkopta kwa lengo la kupata maoni ya wananchi kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi, alisema kuwa  Mbowe na wenzake, walikamatwa na kuhojiwa kutokana na Polisi kushindwa kuvumilia vitendo vyao vya ukiukwaji wa sheria kwa kuwa vilivyolenga kuvuruga amani katika mkoa huo.

“Ni kweli tumewakamata na tunawahoji ili watueleze sababu za kutaka kuvuruga amani katika mji wetu. Hawa viongozi waliomba kibali cha kufanya mikutano yao ya mabaraza ya katiba ya Chadema katika miji ya Mafinga (Mufindi), Ilula Wilaya ya Kilolo na Iringa mjini kwenye uwanja wa Mwembetogwa, lakini walivunja taratibu kwa kujiongezea muda tofauti na kibali kinavyoeleza,” alisema Kamanda Mungi.

Kwa mujibu wa Mungi, kibali cha mikutano hiyo ya Mbowe kilionyesha kwamba alitakiwa kuhutubia Mafinga kati ya saa 3:20 hadi saa 4:00 asubuhi, lakini alitua kwa helikopta na kuhutubia kati ya saa 4:00 na saa 6:00.

Katika Wilaya ya Kilolo,Mbowe, Lissu na Mchungaji Msigwa walitakiwa kuhutubia saa 6:00 hadi 9:00 alasiri, badala yake walianza mkutano kati ya saa 10:30-11:15 jioni na baadaye kutua katika uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa na kuanza mkutano saa 11:30 hadi 12:25 badala ya saa 8:00 hadi saa12:00 jioni.

“OCD (Kamanda wa Wilaya) wangu wa Iringa mjini (ASP Mjengi), alimfuata Mbowe jukwaani, lakini alifanikiwa kuongea na Tundu Lissu, tena kwa kilugha cha huko kwao Singida na kumwambia ndugu yangu utanifukuzisha kazi mwenzio.

Hawakumsikiliza na kujiongezea dakika kumi, kwa hiyo nikawaambia waacheni tutawakamata ili watueleze sababu za kutaka kuvunja amani kwa sababu kibali hakisemi hivyo,” aliongeza Kamanda Mungi.

Baada ya kushikiliwa kwa saa kadhaa kwa ajili ya mahojiano katika kituo kikuu cha Polisi Miyomboni, hatimaye waliachiwa saa 5.30 asubuhi kwa dhamana ya Shilingi  2,000,000 kila mmoja.

MSIGWA: NI MAAGIZO YA CCM

Akizungumza na NIPASHE baada ya kuachiwa kwa dhamana, Mchungaji Msigwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Iringa,

alidai kuwa Polisi waliwakamata kutokana na maelekezo yaliyotolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa.

“Sisi tumewaambia Polisi waache kufanya kazi kwa kufuata maelekezo ya CCM ambayo kimsingi hayana mashiko zaidi ya kutaka chokochoko za kisiasa. Mabaraza ya katiba ya chama chetu hayaepukiki kwa sasa kwa sababu tunataka kupata maoni ya wananchi wasiozidi milioni tano,” alisema Mchungaji  Msigwa.

Gavana wa Chadema  katika mikoa ya Nyanda za Kusini, Frank Mwaisumbe, alisema Polisi wameteleza katika kushughulikia migogoro ya kisiasa mkoani Iringa kwa kuwa mikutano ya wazi ya mabaraza ya katiba hiyo ya kisiasa na haiwezi kuathiri amani kana wanavyodai.

“Polisi wameteleza katika kudhibiti Chadema wakati wa kufunga mikutano yetu ya mabaraza ya katiba. Tumefanya mikutano 17 katika mikoa ya Mbeya, Njombe na Ruvuma na hakuna dosari zaidi ya hapa iringa ambako ushindani wa kisiasa umeota mizizi,” alisema Mwaisumbe.

Mikoa ambayo viongozi wa Chadema wameshafanya mikutano ya mabaraza ya katiba ni Kilimanjaro, Manyara, Arusha, Tanga, Singida, Dodoma, Morogoro, Dar na Pwani ambayo ilihutubiwa na Dk. Slaa.
Mingine ambayo ilihutubiwa na Mbowe katika mikoa ya Mwanza, Mara, Simiyu, Shinyanga, Geita, Kagera, Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Mbeya, Mjombe na Iringa.

‘SERIKALI TATU HAZINA GHARAMA’

Wakati huo huo, Chadema kimetetea mfumo wa Muungano wa serikali tatu kwa kusema kuwa hauna gharama.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema taifa, Edson Mbogoro, kwa kusema kuwa muundo wa serikali tatu kuwapo kwenye katiba, siyo gharama kama vyama vingine vya siasa vinavyodai.

Akizungumza na wakazi wa Kata ya Kawe katika Viwanja vya Tanganyika Packers, wakati wa mkutano wa mabaraza huru ya katiba ya chama hicho kujadili  Rasimu ya Katiba Mpya, Mbogoro ambaye pia ni wakili, alisema muundo wa serikali tatu utapunguza gharama kwani idadi ya wabunge itapungua kutoka ya sasa 360 na kufikia 314.

Kwa mujibu wa Mbogoro, pia idadi ya mawaziri itapungua kutoka ya sasa ambayo ni 48 hadi 15.

SLAA: MA-DC MZIGO
Naye Dk. Slaa alisema kuwa chama hicho kinapendekeza kuwa, wakuu wa mikoa na wilaya waondolewe kwenye rasimu hiyo ya katiba mpya kwa kuwa ni moja ya vikwazo vya maendeleo ya taifa.

“Jambo linalokwamisha maendeleo katika nchi hii ni kuwa na viongozi wengi kama utitiri, lakini hawana tija. Kwa mfano mshahara wa mkuu wa wilaya mmoja kwa mwezi ni takribani Sh. milioni 11 unaweza kumzidi ule wa mbunge.

Sasa zidisha kwa mwaka na kwa idadi ya wote nchi nzima, ni Shilingi ngapi?” alihoji na kuongeza Je, fedha hizo hazingeweza kutumika kujengea zahanati?”

Imeandikwa na Godfrey Mushi, Moshi;   George Tarimo, Iringa na Isaya Kisimbilu, Dar.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment