Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, August 13, 2013

Risasi ya Ponda ni utata mtupu


13th August 2013

  Moi wajiweka kando kuthibitisha
  Polisi nao wasema hawajui kitu
  Familia yasisitiza ni risasi ya moto
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili huku katika bega lake la mkono wake wa kulia ukiwa na jeraha linalodaiwa lilitokana na kupigwa risasi.
Uongozi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu Muhimbili (Moi), umesema mpaka sasa umeshindwa kugundua kitu kilichomsababishia jeraha Sheikh Ponda kwenye bega lake la kulia baada ya kuhamishiwa kwenye taasisi hiyo akitokea katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Meneja wa Kitengo cha Ustawi wa Jamii na Mawasiliano cha Moi, Jumaa Almas, alisema kutokana na tiba ya awali aliyopewa Sheikh Ponda, ikiwa ni pamoja na kushonwa jeraha, imewawia vigumu kujua lilikuwa limesababishwa na kitu gani.

Almasi aliwaambia waandishi wa habari kuwa Sheikh Ponda alipokelewa Moi juzi saa 7:30 mchana akitokea MNH na kuwa baada ya kupokelewa alionekana akiwa na jeraha chini ya bega lake la mkono wa kulia lililokuwa tayari limeshonwa mbele na nyuma,
na madaktari walimfanyia uchunguzi na kushauri kuwa afanyiwe kipimo cha X– ray ili kubaini iwapo kuna mvunjiko kwenye sehemu ya jeraha hilo.

Almas alisema tathmini ya madaktari baada ya kupata majibu ya X– ray  ilionyesha kuwa alikuwa na mvunjiko wa mfupa mkubwa wa bega, ambao haukusababisha mifupa kupishana, na kwamba kidonda hakikuwa katika hali nzuri licha ya tiba ya mwanzo.

Kutokana na hilo, alisema madaktari waliamua afanyiwe upasuaji mpya ili kuzuia maambukizi endapo kidonda hicho kingeachwa hivyo hivyo.

Alisema mpaka sasa anaendelea na matibabu baada ya upasuaji huo.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kufahamu iwapo Sheikh huyo yupo chini ya ulinzi wa polisi baada ya kuonekana baadhi ya polisi na Kamanda wa Polisi Ilala, Marietha Minangi, wakiranda hospitalini hapo, alisema Ponda hana pingu mkononi na wao wanamchukulia kama vile wanavyowachukulia wagonjwa wengine wanaopelekwa Moi.

Hata hivyo, Almas alisema ingawa alimuna Kamanda Minangi hakujua sababu za kuwapo katika eneo hilo.

NIPASHE ilimshuhudia Kamanda Minangi akiingia Moi, saa 4:30 asubuhi, huku akiwa na mpambe wake na askari kanzu wanne. Baadhi ya askari hao walikuwa wakizungukazunguka na wengine wakiketi eneo la mapokezi wakipeana taarifa za kuwasili kwa kamanda wao katika eneo hilo kwa kupigiana simu.

BAKWATA YALAANI 


Wakati huo huo, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limelaani kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda na kuitaka serikali kuunda tume huru kuchunguza tukio hilo, pia wamemtaka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shigolile, ajiuzulu kupisha uchunguzi huo.

Tamko hilo la Bakwata lilitolewa jana na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaad Musa Salum, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, kwa niaba ya baraza hilo.

Hata hivyo, alisema Bakwata haina uhakika iwapo Sheikh Ponda alijeruhiwa kwa risasi kwa kuwa Jeshi la Polisi bado halijathibitisha hilo.

Lakini kasema kama Sheikh Ponda alijeruhiwa kwa risasi iliyofyatuliwa na askari polisi, basi kitendo hicho ni kibaya, kwani kinajenga uadui si kati ya waumini wa dini ya Kiislamu tu, bali na wananchi na Jeshi la Polisi.

“Tungeomba hatua zichukuliwe iwapo wahusika (wa tukio hilo) watajulikana. Tume huru na ya wazi itakayoshirikisha wadau wote iundwe ili ilete majibu ya kilichotokea. Kwa sababu hatujaridhishwa na kitendo alichofanyiwa Sheikh Ponda,” alisema Sheikh Alhaad na kuongeza:

“Kamanda Shilogile ajiuzulu ili kupisha uchunguzi wa tume huru kuchunguza jambo hili.”Alisema hata kama Sheikh Ponda alikuwa akitafutwa na polisi, utu na haki za binadamu vilipaswa kuzingatiwa, kwani Jeshi la Polisi lina mbinu nyingi, hivyo wangetumia weledi tu katika kumkamata.“Lakini siyo kumdhuru, hilo hatukubaliani nalo,” alisema Sheikh Alhaad.

Alisema Bakwata imelazimika kutoa tamko hilo bila kujali tofauti za mawazo zilizopo kati yake na Sheikh Ponda, kwa kuwa kutofautiana mawazo siyo uadui, bali ni jambo la kawaida katika uongozi.

“Sisi kama Bakwata hatukuridhishwa na mambo yaliyotokea, kwani yanahatarisha usalama wa nchi,” alisema Sheikh Alhaad na kulitaka Jeshi la Polisi lijipange vizuri kutumia weledi katika kazi zake.

Aliitaka tume itakayoundwa ifanye kazi yake kwa haki na kwamba, iwapo itathibitika kwamba, ilitumika risasi kumjeruhi Sheikh Ponda, hatua zichukuliwe, ikiwa ni pamoja na kumwajibisha Kamanda Shilogile.

WATETEZI HAKI ZA BINADAMU WALAANI


Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu umesema umepokea masikitiko makubwa taarifa rasmi ya Jeshi la Polisi nchini kuhusu tukio la kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda.

Mtandao huo unaundwa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ya Tanzania Human Rights Defender Coalition (THRDC), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Sikika, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Citizen Politics Rights Watch (CPW) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa).

Mratibu wa Mtandao huo, Onesmo Ole Ngurumwa, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa hawafungamani na taasisi yoyote ya dini wala chama chochote cha siasa, lakini wajibu wao mkuu ni kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinaheshimiwa na kulindwa kikamilifu bila upendeleo au ubaguzi kwa misingi yoyote ile.

“Tunasikitishwa sana na hali ya uvunjaji wa haki za binadamu inayotokana na tabia iliyokithiri ya vyombo vya dola kutumia nguvu inayokiuka haki za msingi za wananchi. Tunapenda kuwafahamisha kuwa tunalaani matumizi ya nguvu yanayofanywa na vyombo hivyo,” alisema Ole Ngurumwa.

Alisema mbali na kulaani, pia wanahuzunishwa na uhalifu, vurugu na tabia ya wananchi kujichukulia sheria mikononi na pia hawakubaliani na vitendo vyovyote vya kuvunja amani.
Baadhi ya vitendo hivyo, alivitaja kuwa ni vya wananchi kutumia tindikali kama silaha dhidi ya wenzao.

Alisema wanafahamu wajibu wa Jeshi la Polisi ni kulinda raia na mali zao na kuwa wanayo haki ya kuwakamata washukiwa wa uhalifu kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, alisema wanalaani kitendo alichofanyiwa Sheikh Ponda na kwamba, kutokana na uzoefu walionao wa matukio yanayofanana na hayo, hawana imani na timu iliyoteuliwa na Jeshi la Polisi kuchunguza tukio hilo.

Alisema hofu yao inatokana na ukweli kuwa jeshi hilo ndilo linalotuhumiwa kumjeruhi Sheikh Ponda na kutokana na misingi ya haki za asili, haikubaliki mhusika kuwa hakimu kwenye shauri linalomhusu.

Ole Ngurumwa alisema wanalaani utaratibu, ambao Jeshi la Polisi liliutumiwa ili kumkamata Sheikh Ponda, kwa kuwa utaratibu wa kumkamata mtuhumiwa mbele ya halaiki ya wafuasi wake ulikuwa ni hatarishi kwa maisha ya askari wenyewe pamoja na maisha ya raia na pia ilikuwa inaibua hamasa na hamaki ya umma.

FAMILIA YASISITIZA NI JERAHA LA RISASI

Msemaji wa Familia ya Sheikh Ponda, Ishaka Rashid, alisema familia imeshitushwa na kitendo cha Jeshi la Polisi kupindisha ukweli kuhusu aliyempiga risasi Sheikh Ponda, kwani madaktari wamesema kwamba, Sheikh huyo amepigwa risasi.

Alisema hata walioshuhudia tukio, walisema wazi kwamba, risasi ilifyatuliwa kutoka kwenye gari la polisi.

Kwa mujibu wa Rashid, waliomfikisha Sheikh Ponda MNH ni familia na siyo polisi, hivyo ukweli wanaojua ni wao.

Alikanusha polisi kumtafuta Sheikh Ponda, kwani familia haijapokea taarifa yoyote wala karatasi yoyote inayoonyesha kwamba, Sheikh huyo anatafutwa na polisi.


KAMANDA KOVA: TUNAMSHIKILIA PONDA

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limethibitisha kumuweka chini ya ulinzi Sheikh Ponda kwa tuhuma za kukiuka amri ya mahakama na kufanya mkutano mkoani Morogoro na Zanzibar.

Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa walifanikiwa kumkamata Sheikh Ponda baada ya kupata taarifa kuwa anapata matibabu MNH kutokana na majeraha aliyoyapata akiwa kwenye mkutano wa hadhara mkoani Morogoro.

Alisema Jeshi la Polisi lilikuwa linamtafuta Sheikh huyo baada ya kuvunja masharti ya mahakama ya “kutokusema chochote kuhusiana na serikali” alipohukumiwa kutumikia kifungo cha nje.

Kamanda Kova alisema mbali Ponda kuendelea na matibabu chini ya ulinzi, wanawasiliana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro kujua makosa mengine yanayomkabili.

Kuhusiana na taarifa za Sheikh Ponda kupigwa riasasi, Kamishna Kova alisema hajui isipokuwa madaktari ndiyo wanaweza kutoa taarifa kamili.
Imeandaliwa na Chevawe Mandari (Tumadarco), Muhibu Said, Samson Fridolin, Elizabeth Zaya na Christina Mwakangale.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment