Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, October 4, 2013

Jinamizi linalomwandama Kikwete usiku na mchana

Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete
Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete
Ahmed Rajab
Toleo la 3182
Oct 2013
NILIAMKA juzi Jumatatu alfajiri na nikajitosa katika maji ya Bahari ya Atlantiki nyuma na nilikolala jijini Accra nchini Ghana.  Nilipoibuka juu ya mawimbi yaliyokuwa yakiguna kwa madaha niliibuka na mawazo mawili kichwani mwangu.
La kwanza lilimhusu Kofi Awonoor, yule mshairi mzaliwa hapa Ghana niliyekuwa nikimjuwa na aliyeuliwa na magaidi wa Al Shabaab katika shambulio la Westgate huko Nairobi. Nilijiambia laiti Al Shabaab wangelimjuwa nani hasa waliyemuua.
Kofi kamwe hakuwaunga mkono magaidi wa sampuli yoyote ile lakini alikuwa akiwachukia baadhi ya wale wale wanaowachukiza Al Shabaab.
Baadhi ya maadui zao walikuwa wamoja. Kama ni Ukristo basi Kofi alikuwa na mengi dhidi ya Ukristo; na kama ni Marekani basi Kofi alikuwa mstari wa mbele wa wenye kuipinga Marekani.
Wakati mmoja alipokuwa Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa aliizuru Canada ambako alitoa hotuba akiziponda sera za Marekani. 
Aliikasirisha Serikali ya Marekani kiasi cha kuifanya ilalamike rasmi kwa Serikali ya Ghana kwa jinsi Balozi wake alivyokuwa akiikashifu na kuifedhehesha Marekani.
Al Shabaab waliyamaliza bure maisha yake, maisha ambayo jioni ya hiyo Jumatatu tuliyasherehekea kwa nyimbo, mashairi na hotuba katika jengo la Freedom Centre hapa Accra. Pamoja na marafiki zake Kofi walikuwako pia wanaharakati kutoka nchi kadhaa, Balozi wa Cuba nchini Ghana, Balozi mdogo wa Sahara ya Magharibi na mwakilishi wa Ubalozi wa Iran. Sikusita kujiambia mara kwa mara: lau kama Al Shabaab wangelijua nani hasa waliyemuua…
Wazo la pili nililoibuka nalo mapema Jumatatu lilimhusu Rais Jakaya Kikwete. Ghafla ilinijia picha ya Kikwete kila mkono wake ukiwa umeshikwa na vigogo vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliokuwa tayari kumrusha na kumtosa kwenye bahari ya nuksi na majanga ya kila aina.
Miongoni mwa vigogo hao ni maafriti, wengine ni mabazazi na wengine ni madalali wa Iblisi.  Wengine wanaamini kwamba wana nia njema lakini maskini hawajijui kuwa wamepitwa na wakati.  Wote wamemkalia vibaya Kikwete.
Kwa hakika, Kikwete anakabiliwa na mtihani mkubwa.  Ni mtihani wa kulijibu swali moja tu: asaini ama asisaini Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba 2013?
Hilo ni swali ambalo Kikwete lazima alijibu. Hana hila, hana hili wala lile; hana ujanja wa kuweza kuliepuka au njia ya kuweza kulipiga chenga.
Swali hilo ni mithili ya lile linalomkabili Hamlet, mwana wa kifalme wa Denmark, kwenye tamthiliya ya William Shakespeare iitwayo kwa jina hilo hilo la Hamlet.
Matamshi ya mwanzo katika tamthiliya hiyo ni yale ya Hamlet anapojiuliza mwenyewe kwa mwenyewe maswali kadhaa kuhusu faida ya uhai, manufaa ya maisha.  Anajisaili iwapo maisha yana thamani yoyote, iwapo kuna faida yoyote kuendelea kuishi wakati maisha yamejaa shida.
Anahitimisha kwa kujijibu kwamba sababu kuu inayowafanya watu waendelee kuishi ni hofu ya mauti. Wanayaogopa mauti kwa kuwa hawana uhakika watakumbana na nini watakapokufa.
“Kuishi au kutoishi, hilo ndilo swali,” alijiambia Hamlet mwanzoni mwa tamthiliya hiyo.
“Nisaini au nisisaini, hilo ndilo swali,” ndivyo anavyojiuliza mwana wa Mrisho Kikwete kila asubuhi anapojiangalia kwenye kioo.
Swali hilo linamfanya akune kichwa kutwa nzima na pengine linamwandama mpaka usiku anapofunga macho.  Pengine limekuwa jinamizi linalomzuru ndotoni mwake anapolala usiku na hata mchana akiwa macho.
Ni swali fupi laki ni zito. “Nisaini ama nisisaini?”
Ni zito kwa sababu haliyahusu maisha yake Kikwete pekee bali linahusu uzima wa taifa zima.  Hamna shaka yoyote kwamba jawabu lake litaliathiri taifa na ndilo litaloamua jinsi uongozi wake Kikwete utavyotathmiwa na kupimwa na historia.
Kuna swali jengine linalojitokeza na kumhangaisha akili: “Nimsikilize nani?”
Namna atavyolijibu swali hilo la pili kutaibua mengi kumhusu Kikwete: umahiri wake wa kisiasa na uzalendo wake. Jawabu lake litadhihirisha iwapo yeye ni kiongozi jina tu mwenye kubururwa na vigogo wa chama chake au ni kiongozi mwenye kuongoza na mwenye kuliweka mbele taifa badala ya chama chake.
Kwa ufupi, litadhihirisha iwapo yeye ni mzalendo wa kweli au mkereketwa tu wa chama kimoja cha siasa kinachojiona kuwa ndicho chenye uhalali wa pekee wa kulisukuma taifa kule chama hicho kinachotaka taifa lende.
Si jambo la ajabu ikiwa swali hilo limemfanya Kikwete achanganyikiwe kwani amejikuta katika hali mbaya.  Yuko katikati ya nguvu mbili, kila moja ikimvutia kwake. Nguvu moja ni yenye kujidai kuwa ina uhalali na nyingine inayoonekana bayana kwamba ndiyo ya uhalali.
Vigogo wachache wa CCM wanamvuta huku na wengi wa wananchi wa Tanzania wanamvuta kwingine.
Yote hayo yametokea kwa sababu hivi sasa hao viongozi wachache wa CCM wameazimia kuuteka nyara mchakato wa Katiba ili walitweke taifa Katiba waitakayo wao.
Takriban vyama vyote vya upinzani vinadai kwamba Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ulipitishwa kiubabe na Wabunge wa CCM licha ya kuwa unakasoro tele.
Kwa Zanzibar, kasoro kubwa ni kutoirejeshea mamlaka yake kamili pamoja na kiti chake katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na uwezo wa kujiamulia yenyewe mambo yake yote — ya ndani na ya nje, ikiwa pamoja na haki ya kujiunga na jumuiya yoyote ya kimataifa.
Kasoro nyingine ni ya kutowapa wadau wa Zanzibar fursa ya kutoa maoni yao kabla ya Mswada huo kurudishwa tena bungeni kujadiliwa.
Hili ni moja ya masharti yaliotolewa hivi karibuni na Kamati ya Maridhiano inayoongozwa na Hassan Nassor Moyo pamoja na Baraza la Katiba Zanzibar (Bakaza) lililo chini ya uenyekiti wa Profesa Abdul Shariff.
Pamoja na mengi mengine wote hao wawili wameukosoa muundo wa Bunge la Katiba.  Wamependekeza kwamba ili papatikane usawa katika Bunge hilo pawe na idadi sawa ya wajumbe kutoka Zanzibar na wale watokao Tanzania Bara kwa vile Katiba hiyo mpya inayotungwa ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa nchi mbili zilizokuwa na sifa sawa kabla ya kuundwa Muungano, Aprili 1964.
Abdul Shariff pia ametanabahisha kwamba litapoundwa Bunge hilo litakuwa na asilimia 72 ya uwakilishi wa chama kimoja cha siasa, hali ambayo inaweza ikawa ndio sababu ya kutopatikana Katiba inayozingatia maslahi ya wananchi.
Mswada huo umepingwa vikali huko Bara pia. Msimamo huo umeviunganisha vyama vikuu vya upinzani (CHADEMA, NCCR-Mageuzi na CUF) pamoja na wanasheria na wanaharakati vikimsihi Kikwete aukatae.
Hamna shaka yoyote kwamba wimbi la upinzani dhidi ya Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ni wimbi kubwa mno lililomlemea Kikwete.  Linaweza likamzamisha. Lakini anaweza kujinusuru kwani penye wimbi na milango ipapo. Na nusra yake ni kuukataa Mswada huo.
Chanzo: Raia Mwema

No comments :

Post a Comment