Written by Elbattawi // 08/10/2013
Na Mwandishi wetu
NAIBU Katibu Mkuu umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka amesema atawataja watendaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Idara ya nyaraka, vizazi na vifo wanaotoa vyeti vya kuzaliwa kwa mwelekeo wa kisiasa.
Kiongozi huyo umedai kwamba wafanyakazi wanaofanya hivyo wanalenga kuwapatia vitambulisho vya ‘Mzanzibari Mkaazi’, jamaa na ndugu zao wasio na sifa kwa lengo maalum.
Akihutubia mkutano wa hadhara juzi kwenye Uwanja wa Garagara, Jimbo la Mtoni Unguja, Shaka alisema baadhi ya wafanyakazi wa Idara hiyo wanakiuka utaratibu wa kazi.
Alisema kwamba kuwapa watu wasio na sifa vyeti vya kuzaliwa ni kinyume na utaratibu wa sheria na ni kosa. Kiongozi huyo wa UVCCM, Zanzibar alisema anao ushahidi wa madai yake hayo.
Alisema wafanyakazi hao wanashabiki siasa kwa kuwapa watu vyeti vya kuzaliwa, hatua itakayo wasaidia kupata vitambulisho vya ukaazi, na kuweza kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Shaka alisema Idara hiyo ipo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria, inayoongozwa na Waziri Abubakar Khamis Bakar kutoka Chama cha Wananchi (CUF).
Alisema Idaya hiyo imeajiri wafanyakazi wapya na kuwahamisha wa zamani ili kupata mwanya wa kufanya upendeleo kwa mtazamo wa kisiasa:
“Tunayo majina ya wafanayakazi wa Idara hiyo wanaofanya mchezo huo mchafu, wasipojirekebisha tangu sasa tutawataja majina yao,” alisema Shaka na kuongeza:
“Tunaitaka Wizara ya Katiba na Sheria ichukue hatua zinazostahili kuzuia mpango wa siri unaolenga kuleta vurugu na upendeleo,”.
Shaka, pia alimwambia Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kuacha kudhihaki Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Alisema Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif anaimba nyimbo kwenye majukwaa huku vitendo na matamshi yake hayaheshimu na kuyaenzi Mapinduzi hayo.
Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi wa CCM Zanzibar, Najma Murtaza Giga aliwaasa viongozi wa vyama vya upinzani kuachana na dhana kwamba CCM imechoka kiakili na wanaweza kuiburuza.
Chanzo: Mzalendo
No comments :
Post a Comment