
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Bibi Ingunn Klirpsvik Ofisini kwake Vuga, Zanzibar ambapo walipata wasaa wa kubadilishana mawazo juu ya uhusiano wa mataifa yao mawili
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshauriwa kujifunza kupitia Mataifa, Taasisi na Mashirika ya Kimataifa katika mpango wake wa kuelekea kwenye mradi mpya wa uzalishaji wa Mafuta.
Balozi wa Norway Nchini Tanzania Bibi Ingunn Klirpsvik alitoa ushauri huo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo ofisini kwake Vuga, Mjini Zanzibar.
Balozi Ingunn alisema hatua hiyo ya tahadhari inayofaa kuchukuliwa na Zanzibar inaweza kuwa mwanzo mzuri wa kuingia katika mradi huo mpya wa kiuchumi kwenye muelekeo wa mafanikio makubwa.
Balozi huyo wa Norway Nchini Tanzania alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Norway wakati wote ipo tayari kutumia ujuzi wake mkubwa katika masuala ya mafuta kuisaidia Zanzibar kitaalamu ili ifanikiwe katika malengo iliyojipangia katika kuendesha mradi huo.
Alifahamisha kwamba Nchi hiyo imekuwa mshirika mkubwa wa Tanzania na Zanzibar kwa ujumla katika kuunga mkono harakati za kiuchumi na ustawi wa jamii ya wananchi walio wengi nchini.
“ Tumekuwa na ushirikiano na uhusiano wa muda mrefu katika pande zetu hizi mbili unaolenga kustawisha harakati za kijamii na uchumi kwa wananchi walio wengi “. Alisisitiza Balozi huyo wa Norway Nchini Tanzania Bibi Ingunn Klirpsvik.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameishukuru Serikali ya Norway kwa juhudi zake za kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika maendeleo hasa uungaji mkono katika miradi ya miundo mbinu ya kiuchumi.
Akizungumzia suala la amani ambalo linaonekana kuiteteresha pembe ya Bara la Afrika Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Tanzania imelazimika kuchukuwa tahadhari ili kudhibiti wimbi hili linaloonekana kulikumba eneo hilo.
Balozi Seif alisema Serikali ya Tanzania iko makini katika kufuatilia wageni wasio na mfumo sahihi wa kuishi ndani ya ardhi ya Tanzania na jitihada zinachukuliwa katika kuratibu wageni walioamua kuishi nchini kupitia sheria na taratibu zilizopo za Kitaifa na Kimataifa.
“ Tanzania imelazimika kuwa na tahadhari katika masuala ya ulinzi wa amani ili kujaribu kuzuia au kudhibiti uasi ama ubabe unaoweza kufanywa na watu au vikundi vinavyopenda kuichezea amani “. Alisisitiza Balozi Seif.
Kuhusu suala la mchakato wa kuelea kwenye Katiba mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi huyo wa Norway Nchini Tanzania Bibi Ingunn kwamba mabaraza ya Katiba ya Wilaya yamekamilisha vyema mijadala yao.
Balozi Seif alisema hatua hiyo ndio iliyopelekea Bunge la Jamuhuri ya Muungano kujadili marekebisho ya sheria ya Katiba na kuipitisha ili kuundwa kwa Bunge la Katiba litakalojadili na kuidhinisha kupigwa kwa kura ya maoni hapo baadaye ili kukamilisha mchakato mzima wa kupata katiba mpya.
Balozi Seif aliendelea kusisitiza kwamba Zanzibar imeshirikishwa kikamilifu katika mchakato mzima wa kujadili Katiba hiyo kuanzia msingi licha ya malalamiko na shutuma zinazoendelea kutolewa na upande wa upinzani kwamba Zanzibar haikushirikishwa.
Chanzo: ZanzibariYetu
No comments :
Post a Comment