KUFAHAMU ukubwa wa kampuni ya mafuta ya Royal Dutch Shell ambayo inaonekana itapewa mkataba wa kutafuta na kuchimba mafuta visiwani Zanzibar, ni vema kufahamu kwamba mwaka jana ilipata mapato ambayo ni takribani mara 30 ya mapato iliyopata kampuni kubwa zaidi ya dhahabu duniani, Barrick Gold.
Barrick ndiyo ambao wanamiliki migodi yote mikubwa ya madini ya dhahabu Tanzania na barani Afrika kwa ujumla. Popote ambapo kuna dhahabu nyingi, kampuni hii ya Canada ipo.
Hii ndiyo kampuni ambayo iliwahi kutaka kumzuia aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamis Kagasheki, asiingie katika mojawapo ya migodi yao mkoani Mara.
Barrick ndiyo kampuni ambayo iliwahi kumwaga maji yenye madini ya zebaki katika mto Tigithe wilayani Tarime na kusababisha vifo na matatizo ya kiafya kwa viumbe hai, wakiwamo binadamu na wanyama, vilivyotumia maji hayo na hakuna aliyewafanya kitu.
Lakini, kwa jeuri yote ambayo Barrick wanayo, hawafui dafu kwa Shell.
Kama ilikuwa vigumu kupambana na Barrick kwa namna yoyote ile, itakuwa vigumu mara 30 kupambana na Shell kutokana na nguvu ya kiuchumi na historia ambayo tayari imejijengea.
Ukubwa wa Shell
Januari mwaka huu, jarida maarufu la masuala ya kiuchumi la Marekani la Forbes, lilitoa orodha ya makampuni 500 makubwa zaidi duniani na kampuni hii inayotarajiwa kuja kuwekeza hapa nchini (kama Tanzania na Zanzibar zitabaki kuwa nchi moja), iliibuka namba moja.
Fikiria kampuni yoyote kubwa unayoifahamu hapa duniani lakini bado itakuwa iko chini ya Shell.
Kueleza namna mapato ya Shell yalivyokuwa ya kushangaza, kiasi ilichoingiza kwa hesabu za Januari mwaka huu kilikuwa sawa na asilimia 84 ya kile kinachokusanywa na serikali ya Uholanzi (nchi iliyoendelea).
Kampuni hii inafanya shughuli zote zinazohusiana na biashara ya mafuta na gesi. Inatafuta mafuta na gesi, inachimba, inasafisha mafuta, inauza, inasambaza na kufanya mambo yote yaliyo katika mnyororo wa shughuli za bidhaa hiyo iliyopachikwa jina la dhahabu nyeusi.
Ina matawi katika nchi 90 tofauti duniani kote na ina vituo zaidi ya 44,000 katika nchi hizo –Ikiwa imeajiri wafanyakazi zaidi ya 87,000.
Bila shaka, hii ndiyo kampuni kubwa zaidi kuwahi kufanya biashara yoyote hapa Tanzania.
Ubabe
Mwanzoni mwa mwaka 1996, wanaharakati walianza kutoa ripoti na taarifa mbalimbali zilizoihusisha kampuni hii na vitendo vya mauaji, utesaji, ukiukwaji wa haki za binadamu na maovu mengine nchini Nigeria.
Shell ambayo ilikuwa inafanya biashara zake katika eneo nyeti la Delta ya Nigeria lenye utajiri mkubwa wa mafuta, ilidaiwa kushiriki katika mipango ya kuua wana harakati wote waliokuwa wakipinga shughuli zake.
Miongoni mwa wahanga wa vitendo hivi alikuwa ni Ken Saro-Wiwa ambaye aliuawa na utawala wa kijeshi wa hayati Jenerali Sani Abacha, kutokana na kupinga kwake shughuli za Shell.
Shell ilishutumiwa kwa kushirikiana na serikali katika mauaji hayo ya Saro Wiwa na viongozi wengine wanane wa kabila la Ogoni na ingawa imekuwa ikikana kuhusika kwa namna yoyote ile, ililipa dola milioni 15 ili suala hilo limalizwe nje ya mahakama mwaka 2009.
Kampuni hii inatajwa sana kuhusika na uchafuzi mkubwa wa mazingira katika maeneo inakofanya shughuli zake. Mifano inatolewa kuhusu hali mbaya ya kimazingira iliyopo katika eneo la Delta ya Nigeria na tukio moja la kusikitisha mwaka 1999.
Katika mji mmoja uitwao Magdalena nchini Argentina, matenki ya mafuta ya Shell yalidaiwa kumwaga mafuta machafu katika mojawapo ya maziwa yaliyopo nchini humo na kusababisha uchafuzi mkubwa zaidi wa maji masafi kuwahi kufanywa tangu dunia ilipoumbwa.
Utata
Utata umekuwa ukiigubika kampuni hii katika ufanyaji wake wa kazi. Kuna tuhuma kwamba mara zote Shell hujiingiza katika mahusiano yasiyo mazuri na serikali zilizo madarakani ili ijihakikishie kuendelea na shughuli zake.
Kwa mfano, Shell inadaiwa kupenyeza vibaraka wake katika ofisi zote nyeti za serikali ya Serikali pamoja na jeshi la nchi hiyo ili kuhakikisha inafahamu kila kinachoendelea serikalini kila siku.
Kuna madai yasiyothibitishwa kwamba kampuni hiyo imekuwa miongoni mwa wafadhili wa Tume ya Uchaguzi ya Nigeria inayosimamia chaguzi zote za nchi hiyo.
Kuna wanaotania kwamba Shell ndiyo huwa inaamua nani atakuwa Rais wa Nigeria na nchi zote nyingine ambako inafanya biashara vizuri.
Miaka michache, Shell iliingia katika kashfa baada ya kubainika kwamba ilimpa aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Ugavana wa Jimbo la Pennslyvania nchini Marekani, Tom Corbett, kiasi cha dola za Marekani 300,000 ili akipata fursa hiyo awapunguzie kodi.
Kwa vyovyote vile, Tanzania (Zanzibar?) imeingia katika hatua nzito kwa kukubali kuingia kwenye makubaliano na Shell.
Kuna kila sababu ya wanaharakati, waandishi wa habari, wafanyabiashara na wadau wengine wa gesi na mafuta kujiandaa na ujio huu wa Shell.
Historia huwa na kawaida ya kujirudia.
Chanzo: Raia Mwema

No comments :
Post a Comment