Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, December 27, 2013

Dk. Slaa: Tutaanika mateso ya Tokomeza

NA THOBIAS MWANAKATWE

24th December 2013


Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa.
Wakati mawaziri wanne wakiwa wamejiuzulu kutokana na kashfa iliyotokana na Operesheni Tokomeza Ujangili, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kitachapisha kitabu chenye picha zinazoonyesha mateso waliyofanyiwa wananchi na mifugo wakati wa operesheni hiyo na kukisambaza nchi nzima.

Mawaziri  waliojiuzulu Ijumaa iliyopita kufuatia shinikizo la wabunge kuwataka wawajibike kutokana na kushindwa kusimamia operesheni hiyo na kusababisha wananchi wauawe, kuteswa, kubakwa na kufanyiwa vitendo vingine vinavyokiuka haki za binadamu ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi; Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mathayo David Mathayo.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, akizungumza na mamia ya wananchi wa Jimbo la Igunga mkoani Tabora katika mkutano wa hadhara, alisema baada ya kukichapisha kitabu hicho, kitasambazwa nchi nzima ili wananchi waone unyama waliofanyiwa watu wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo.

Dk. Slaa alisema kuwa unyama waliofanyiwa wananchi pamoja na mifugo yao ni ukatili ambao hauwezi kuvumiliwa na hata hatua iliyochukuliwa dhidi ya mawaziri ambao wizara zao zilihusika katika operesheni hiyo, hazitoshi kutuliza machungu waliyopata Watanzania.

Alisema maeneo ambayo unyanyasaji na mateso kwa wananchi na mifugo ulipita kipimo ni pamoja na Tarime, Babati na katika wilaya za mikoa ya Shinyanga, Singida na Kigoma ambazo watu waliokamatwa na waliokuwa wakiendesha operesheni hiyo waliingizwa spoko na chupa za baiskeli katika sehemu zao za siri.

“Tarime (Mara), Kakonko (Kigoma) na Bukoba (Kagera), kuna vijana walikamatwa wakaingizwa spoko ya baiskeli sehemu za siri, sijui kama hao vijana wataweza tena hata kuzaa, unyama gani huu,” alisema Dk. Slaa na kuongeza:

“Chadema tutahakikisha kuwa tuna picha za matukio yote hayo, tutayachapisha na kuyasambaza kwa wananchi waone unyama uliofanywa na serikali yao.”

Aliongeza kuwa vijana wengine waliokamatwa na kulazimishwa wataje kuwa wanamiliki silaha za uwindaji walipewa mateso ya kutakiwa kuandika neno tembo katika miguu yao kwa kutumia wembe.

Dk. Slaa alisema wananchi ambao wanaendelea kunyanyaswa wasisite kutoa taarifa kwa viongozi wa Chadema ili chama hicho kipate ushahidi na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu waliohusika na unyanyasaji huo.

Alisema viongozi wamekuwa wakiimba kuwa Tanzania ni nchi ya amani, lakini katika matukio haya yaliyotokea wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili yameondoa kabisa dhana hiyo na kuonekana nchi ya kikatili kwa wananchi wake.

Katibu Mkuu huyo alisema kutokana na hali hiyo, mbali na mawaziri wanne waliowajibishwa, wengine wanaotakiwa kuwajibishwa ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange na maofisa wa wizara zote zilizohusika katika utekelezaji wa operesheni hiyo.

Dk. Slaa alisisitiza kuwa Rais Jakaya Kikwete, atakaporejea nchini kutoka nje, Watanzania watataka kuona Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, naye anang’olewa badala ya kuwatoa kafara mawaziri hao wanne peke yao.

“Mawaziri waliolazimishwa wajiuzulu ni dagaa tu na walifanya hivyo ili kumnusuru Waziri Mkuu Pinda, tunamuomba Rais Kikwete akirejea nchini amwajibishe na Pinda ili kutenda haki kwa wote,” alisema Dk. Slaa huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment