Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, December 27, 2013

Watatu mbaroni kwa tuhuma za kumteka, kumtesa Absalom Kibanda

NA SAMSON FRIDOLIN

27th December 2013


Absalom Kibanda, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Watu watatu wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kumteka, kumtesa na kumjeruhi Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda.
Katika tukio hilo, Kibanda aling'olewa meno pamoja na kutobolewa jicho na watu wasiojulikana.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Kamishna wa Polisi, Isaya Mngulu, alisema kuwa watu watatu wanashikiliwa mpaka sasa na wanahusishwa na tukio hilo.

Mngulu alisema kinachoendelea kwa sasa ni kwa Jeshi hilo kujiridhisha ikiwa ni pamoja na kukusanya ushahidi wa kutosha kuhusu watuhumiwa hao kuhusika kwenye tukio hilo ili wafikishwe mahakamani.

“Jeshi limefanikiwa kuwakamata watu watatu kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo, lakini kwa sasa upelelezi unaendelea kwani bado tunakusanya ushahidi wa kutosha ili tujiridhishe kwa watuhumiwa hao kuhusika na tukio hilo kabla hatujawafikisha mahakamani,” alisema Mngulu.

Kauli ya DCI inakuja baada ya kuwapo kwa kauli tofauti na tata zilizowahi kutolewa na jeshi hilo na serikali tangu kutokea kwa tukio hilo juu ya matukio ya Kibanda na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka.

Moja ya kauli iliyowahi kutolewa na Jeshi la Polisi ni ile ya kivihusisha vyombo vya habari kuwa vilichangia upelelezi wa matukio hayo kuzorota kutokana na kuandika sana ikiwamo wanaohusika na upelelezi (vyombo vya usalama) kushutumiwa.

Novemba, mwaka huu, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais hivi karibuni, Dk. Emmanuel Nchimbi na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, walilazimika kulizungumzia suala hilo baada ya waandishi wa habari kutaka ufafanuzi kutoka kwao.

Waandishi walihoji iweje upelelezi wa tukio la kuvamiwa, kujeruhiwa na kuporwa kwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, marehemu Dk. Sengondo Mvungi, ukamilike na watuhumiwa kukamatwa haraka huku matukio hayo mawili yakiwa kimya.

Wakati Dk. Nchimbi na Kova wakisema hayo, Oktoba 14, mwaka huu, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, (DCI) mstaafu Robert Manumba, aliliambia NIPASHE kuwa uchunguzi wa uhalifu nchini wa kuteka, kutesa na kujeruhi raia pamoja na matukio mengine ya kumwagiwa tindikali upo njia panda kutokana na kukosekana kwa vifaa vya kisasa kuwabaini wahusika.

Manumba alisema katika kupeleleza matukio hayo, polisi wanakabiliana na changamoto za kubaini wahusika kutokana na kutumia teknolojia duni pamoja na kukosa wataalam.

Alishauri kila taasisi ikiwamo misikiti, makanisa na sehemu nyingine zenye mikusanyiko ya watu wengi, kufunga kamera (CCTV) ili kusaidia kubaini namna uhalifu unavyotokea. Hata hivyo, ushauri wa Manumba wa kufunga kamera kwenye nyumba za ibada, hauwezi kubaini uhalifu ambao umeshatendwa siku zilizopita.

KAULI YA KOVA
Akijibu hoja hiyo, Kamanda Kova alisema kila tukio lina mazingira yake na hakuna linalofanana na lingine kwa asilimia 100, hivyo matukio hayo (ya Kibanda na Dk. Ulimboka) na la Dk. Mvungi, hayafanani kimazingira na kinyakati.

“Safari hii (katika tukio la marehemu Dk. Mvungi), media (vyombo vya habari) vimekuwa kimya hata tulivyowaomba wasiandike walikubaliana nasi, ndiyo maana upelelezi ukawa rahisi…matukio ya Kibanda na Ulimboka, yaliandikwa sana na wanaopeleleza walituhumiwa,” alisema.

Aidha, aliviomba vyombo vya habari kunyamaza kunapokuwa na tukio linalohitaji upelelezi ili kutoa nafasi kwa Idara ya Upelelezi kufanya kazi vizuri.

“Tukio la Dk. Mvungi liwe fundisho jema kwa vyombo vya habari kuwa kunapotokea tukio watuachie Polisi na vyombo vingine vya usalama tupeleleze ndipo tuwape taarifa,” alisisitiza Kova.

Hata hivyo, alipobanwa aeleze upelelezi umefikia wapi na iwapo kuna wanaoshikiliwa, Kova alisema: “Tusiyazungumzie ya Kibanda na Ulimboka jibu tulilotoa awali linatosha.”

KAULI YA NCHIMBI
Dk. Nchimbi aliwahi kusema kuwa upelelezi wa matukio hayo (la Kibanda na la Dk. Ulimboka), unaendelea na hata kama utachukua muda mrefu kiasi gani ni lazima waliohusika wakamatwe.

“Ninaandaa semina kwa waandishi wa habari niwaonyeshe mikanda ya matukio ya uhalifu nchi mbalimbali duniani na jinsi upelelezi ulivyofanyika …tunaweza kutumia miaka mitatu hadi minne na tukawakamata watuhumiwa,” alisema.

Dk. Nchimbi alisema kabla ya Desemba 31, mwaka huu, itaundwa Kurugenzi ya Intelijensia na itakuwa na Kamishna ikiwa ni pamoja na kuwa na mafunzo ili kuharakisha upelelezi.

Mara kadhaa, Jeshi la Polisi limekwepa kuzungumzia tukio la kutekwa, kupigwa na kuteswa kwa Kibanda huku kukiwa na kurushiana ‘mpira’ kati ya Kova, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), na Mkuu wa Jeshi hilo, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema.

Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited ambayo ni wachapishaji wa magazeti ya Rai, Dimba, Mtanzania, Bingwa na The African, alivamiwa na watu hao, wakati akirejea nyumbani kwake, Mbezi Juu, jijini Dar es Salaam Machi 5, mwaka huu.

Katika tukio hilo, watu hao walimng’oa meno, kumkata kidole, kumjeruhi kwa kitu kizito kichwani na kumharibu jicho la kushoto.

Mara baada ya tukio hilo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, alimkariri IGP Mwema, akisema kuwa ameunda timu ya wapelelezi wazoefu kufanya uchunguzi ili kuwabaini waliohusika katika uhalifu huo na kuwatia mbaroni. Timu hiyo ya makachero wanne kutoka makao makuu ya polisi iliunganisha nguvu na makachero wa Jeshi hilo Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ambayo hadi sasa haijatoa matokea ya uchunguzi huo, licha ya kuwapo kwa ahadi za kufanya hivyo mara kadhaa.
Jukwaa la Wahariri Tanzania kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania (MCT), waliunda timu kuchunguza tukio hilo na kutoa taarifa iliyohusisha tukio hilo na sababu mbalimbali ikiwamo kazi yake ya uandishi wa habari.

Dk. Ulimboka alikutwa na tukio hilo Juni 27, mwaka 2012 na baada ya muda mfupi polisi walimkamata raia wa Kenya, Joshua Gitu Mulundi (31), kwa madai ya kuhusika na tukio hilo na kufikishwa mahakamani.

Baada ya kitambo, Mwendesha Mashitaka wa Serikali aliamua kufuta kesi dhidi yake na aliachiwa huru kabla ya kukamatwa tena na polisi na kushtakiwa kwa kosa la kuwadanganya Polisi na kuhukumiwa kulipa faini ya Sh. 1,000 au kifungo cha miezi sita. Alilipa faini hiyo.

Aidha, Jeshi la Polisi mpaka sasa bado halijafanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa wa matukio mawili ya mabomu yaliyotokea jijini Arusha na kusababisha vifo vya watu kadhaa.

Matukio hayo ni yale ya bomu lililotokea kwenye mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata tano wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Juni 14, mwaka huu na kuua watu wawili. Lingine ni lililotokea katika Kanisa Katoliki Parokia ya Olasiti Mei 5, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu wanne pamoja na kujeruhi watu kadhaa.

Matukio ambayo hata hivyo, Mngulu aliiambia NIPASHE wiki iliyopita kuwa Jeshi lake bado linaendelea na upelelezi na kwamba mpaka sasa limefanikiwa kumtia nguvuni mtu mmoja kwa tuhuma za kuhusika kwenye tukio la Olasiti na kesi yake iko mahakamani. 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment