Ahmed Rajab Toleo la 328 4 Dec 2013
KUNA mengi ninayoweza kuyaandika kumhusu Ngũgĩ wa Thiong’o, mwandishi maarufu wa Kenya. Hata sijui nianzie wapi, nimguse wapi. Kuna wenye kufua dhahabu na wenye kufua shaba, Ngũgĩ hufua maneno. Ni maneno yenye thamani kubwa.
KUNA mengi ninayoweza kuyaandika kumhusu Ngũgĩ wa Thiong’o, mwandishi maarufu wa Kenya. Hata sijui nianzie wapi, nimguse wapi. Kuna wenye kufua dhahabu na wenye kufua shaba, Ngũgĩ hufua maneno. Ni maneno yenye thamani kubwa.
Huyu ni mhunzi wa maneno aliye mtunzi wa riwaya, wa hadithi fupi, wa tamthiliya, aliye mwandishi mahiri wa insha na gwiji wa fasihi. Zaidi ya hayo ni mwana nadharia wa fasihi.
Na Ngũgĩ si mwana nadharia wa fasihi tu bali pia ni mwana nadharia wa ukombozi na kwa vitendo ni mwanaharakati wa kisiasa. Yote hayo yalimchongea akatiwa korokoroni kwao Kenya. Binafsi ninatafahari kwa kuunda kamati London pamoja na wanaharakati wengine wa Kiafrika, akiwemo Chen Chimutengwendewa Zimbabwe, ya kumfanyia kampeni ya kimataifa ili aachiwe huru.
Uanaharakati wake ulijitokeza tena alipolazimika kuishi uhamishoni London ambapo pamoja na mshairi maarufu wa Kenya Abdilatif Abdalla, Yusuf Hassan, Wanyiri Kihoro na mkewe Marehemu Wanjiru Kihoro pamoja na wanaharakati wengine waliongoza vuguvugu la kuupinga utawala wa kimabavu wa Rais Daniel arap Moi.
Muda wote huo Ngũgĩ aliendelea kufua maneno. Hayo maneno ayafuayo huyachonga yakawa mishale ya ukombozi kwani Ngũgĩ ni mpiganiaji wa ukombozi wa Mwafrika na hasa ukombozi wa mawazo ya Mwafrika. Ukombozi wa akili, ukombozi wa fikra. Ndio maana akawa mtetezi wa umajumui wa Afrika. Na zaidi ya yote, yote hayo, Ngũgĩ ni muungwana.
Nimejuana naye Ngũgĩ wa Thiong’o kabla hajawa Ngũgĩ wa Thiong’o. Alikuwa James Ngugi.
Nilikutana naye mara ya kwanza 1965 alipokuwa akisomea shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza. Zilikuwa siku kabla hajajikomboa kwa kulikanya na kulitupa jina la James.
Mara kwa mara alipokuwa akija London kutoka Leeds alikuwa akituzuru BBC na hasa alikuwa akiwatembelea Wakenya wenzake, kina James Kangwana, Sal Davies, Dalail Mzee, Mohamed Bakhressa na Salim Juma.
Mkenya mwengine aliyekuwa akisoma Leeds na aliyekuwa na mazoea ya kututembelea London alikuwa Grant Kamenju ambaye baadaye alikuwa mhadhiri mwanzilishi wa idara ya fasihi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Grant juu ya mikasa yake mingi alikuwa na mengi ya kuufunza ulimwengu. Bahati mbaya ametutoka. Wasioijua siri ya kifo huenda wakasema kwamba alitutoka wakati si wake. Na iwe iwavyo, hatunaye. Alitutoka, kama alivyosema Ngũgĩ, kimya kimya bila ya kumtarajia.
Sidhani kama kuna vijana wengi wa Afrika ya Mashariki ya leo wenye kulijua jina la Grant Kamenju na mchango wake adhimu alioutoa katika mapinduzi ya fikra barani Afrika. Alikuwa safu ya mbele ya wasomi waliokuwa wakipigania lugha za Kiafrika na fasihi za Kiafrika zifundishwe kwenye vyuo vikuu vya Afrika na zitumiwe rasmi na serikali za Kiafrika.
Hayo hayakuwa mapambano ya lugha na fasihi tu; yalikuwa mapambano ya kijamii, ya kisiasa na ya kiitikadi. Ni hasara yao wasioujua mchango wake.
Juzi Jumatatu machozi yalinilenga lenga kwa furaha nilipokuwa nikiisoma hotuba aliyoitoa Ngũgĩ Novemba 23, mwaka huu, alipokuwa anaipokea shahada ya heshima ya udaktari wa falsafa aliyotunukiwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Ngũgĩ aliitoa hotuba hiyo kwa heshima ya Grant Kamenju, akilitukuza jina la Grant Kamenju. Jina ambalo liliyafufua mengi ya kumbukumbu zangu yaliyokuwa yamekwishazikika.
Kwa hakika, sherehe ya kumtunukia Ngũgĩ shahada hiyo ya heshima ya udaktari wa falsafa ilikuwa ni sherehe ya kihistoria. Kwanza, kwa sababu hiyo ilikuwa ni mara ya pili tu Ngũgĩ kutunukiwa shahada ya heshima na chuo kikuu cha Kiafrika (ya kwanza alitunukiwa na Chuo Kikuu cha Walter Sisulu cha Afrika ya Kusini). Ametunukiwa shahada nyingi za heshima lakini zote hizo nyingine ametunikiwa nje ya Bara la Afrika.
Sababu ya pili iliyolifanya tukio hilo liwe la kihistoria ni kwamba hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza Ngũgĩ kutoa hotuba nzima kwa Kiswahili. Hata mhadhara wake wa hadhara alioutoa baada ya kutunukiwa shahada ya heshima aliutoa pia kwa Kiswahili. Ameuita mhadhara huo “Wasomi, Lugha za Ulaya na za Afrika: Kati ya Kujiweza na Kuwezwa”.
Ulikuwa ni mhadhara wa kusisimua kwa aliyoyasema Ngũgĩ. Katika mhadhara huo tunamwona Ngũgĩ amejifunga kibwebwe silaha mkononi — au maneno mdomoni — ameingia tena vitani. Huku anawakebehi wasomi wa nje ya Afrika wanaopewa uprofesa wa mambo ya Kiafrika bila ya kujua hata lugha moja ya Kiafrika. Na huku anawakebehi pia Waafrika walio “mateka wa lugha za Ulaya” na wenye kuzidharau lugha zao.
Katika mhadhara huo amesema mengi Ngũgĩ yasiyo na ubishi na amempa sifa nyingi Mwalimu Julius Nyerere, sifa anazostahiki kupewa kwa jinsi alivyokifanya Kiswahili kuwa lugha ya taifa. Lakini lazima nibishane naye Ngũgĩ kwa kudai kwamba kwa Nyerere kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya taifa “Hatimaye, Kiswahili kikawa na kwao.”
Hapo kidogo Ngũgĩ ameteleza. Siku zote Kiswahili kimekuwa na kwao. Hakijatimliwa kikenda uhamishoni. Wakoloni walikuja wakakikuta kwao, wakaondoka, na wakakiacha huko huko kwao.
Na kwao ni kule ambako wenyeji wake wanasema “vita hivi” na “vita vya” nasi wasemao “vita hii” au “vita ya”. Ni wale wale wasemao “makala haya” na si wasemao “makala hii”. Na wasemao kwa inadi “makala hii” basi na waendelee na kusema “maradhi hii” badala ya “maradhi haya” kama kisemwavyo Kiswahili huko kwao.
Kwa vile neno “makala” liko katika ngeli ya JI/MA basi huwa “makala manana”. Na “kitabu chanana”/ “vitabu vyanana”; “nyumba nyanana”, “ndizi nyanana” na “tabia nyanana”.
Huko kuliko kwao Kiswahili humsikii mtu akisema “dhehebu”; wenye lugha yao wanajua kwamba madhehebu yanaweza kuwa mamoja kama makala yalivyo mamoja au mengi. Pia wanajua kwamba hakuna neno “dhumuni” bali ni “madhumuni”.
Huko ambako Kiswahili ni kwao wafuasi wa madhehebu ya Shi’a huitwa “Mashia” na humsikii mtu kuwaita “Washia”. Akiwa mmoja huitwa “Shia” nasi “Mshia”.
Vivyo hivyo kwa wafuasi wa madhehebu ya Suni. Waswahili wanawaita “Masuni” na si “Wasuni”. Kule ambako Kiswahili ni kwao mtu atauliza: “Yule ni Suni au ni Shia?” Humsikii mtu akiuliza: “Yule ni Msuni au ni Mshia?”
Mwalimu Nyerere kweli amefanya kazi kubwa ya kukinyanyua na kukisambaza Kiswahili katika taifa zima. Lakini si sahihi kamwe kusema kwamba kwa kufanya hivyo “Hatimaye, Kiswahili kikawa na kwao.” Kiswahili siku zote kimekuwa na kwao, ila katika huko kusambazwa kwake Kiswahili kimedakwa na wengine wanaokifanya kuwa ni chao. Hilo si jambo baya, la kujiweza kwa kujipa uwezo wa kuisarifu lugha nyingine ilimradi wasijaribu kutuweza. Wasikipotoshe Kiswahili chetu kwa kukisema tusivyokisema wenyewe Waswahili.
Chanzo: Raia Mwema

No comments :
Post a Comment