NA JOHN NGUNGE
13th December 2013
Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Rukia Kassim Ahmed (CUF), katika muda wa Maswali na Majibu kwa Waziri Mkuu jana asubuhi.
Rukia alitaka kujua kauli iliyotolewa bungeni humo wiki iliyopita na baadhi ya wabunge kwa kumtaja kuwa ni mzigo namba moja na hivyo atimuliwe kazi.
Katika swali lake la nyongeza Rukia alianza: "Juzi, Mbunge wa CCM alinukuu kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu Mwenezi wake, Nape Nnauye, na kusema kama wapo mawaziri mizigo basi wewe ni mzigo namba moja, unasemaje kuhusu kauli hiyo?.”
Jumamosi iliyopita, wabunge wawili, mmoja wa CCM, Kangi Lugola, (Mwibara) na David Kafulila, (NCCR-Mageuzi- Kigoma Kusini), walimlipua bungeni Waziri Mkuu Pinda, wakimweleza kuwa ni mzigo namba moja na wamemtaka Rais Jakaya Kikwete, amtimue kazi.
Pamoja na Waziri Mkuu Pinda, mwingine anayepaswa kutimuliwa kazi ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Hawa Ghasia, ambaye walimweleza kuwa ameshindwa kufanya kazi kwa kulea mafisadi, kuwahamisha wabadhirifu wa fedha za umma kutoka sehemu moja kwenda nyingine hali ambayo inasababisha upotevu wa fedha nyingi za serikali.
Akianza kujibu Pinda alisema, hili ndilo swali ulilotaka kuuliza, mwanzo ulikuwa unazunguka tu.
Alisema hakuomba kuwa waziri mkuu isipokuwa aliteuliwa na Rais kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu.
“Wala hili lisikusumbue, unajua vizuri kabisa kwamba nafasi hii ya uwaziri mkuu huombi, Msheshimiwa Rais anateua kwa mapenzi yake akiongozwa na Mwenyezi Mungu mmojna ashike jukumu hilo. Unaweza kuteuliwa hata wewe.
Lakini alisema kuna njia mbili za kumwondoa Waziri Mkuu, moja, “isipompendeza ni rahisi sana kumwambia tu Pinda nilikupa jukumu hili lakini umeshindwa kuwajibika, basi unatoka, wala hunung’uniki, unacheka tu na kusema asante.
“Bunge hili linaweza kumwondoa Waziri Mkuu kwa uwezo ilionao. Kwa hiyo dada Rukia kama unafikiri na wabunge wote wakaona sawa, nipo tayari, mkiniweka kitimoto, utaona la, tena mtashangaa, nitafurahi kweli kweli angalau nimeutua msalaba huu, maana yake hii kazi ni ngumu,” alisema.
Akizungumzia majukumu yake alisema anasimamia wizara kama 20 na zote zinafanya kazi vizuri, lakini kama kuna wizara moja au mbili hazijafanya vizuri sana, hiyo haitoshi kudai atimuliwe kazi.
“Ninasimamia wizara 20, kama utanihukumu kwa wizara moja au mbili, hamnitendei haki,” alisema.
Mapema katika swali lake la kwanza, Rukia alitaka kujua anasemaje kuhusu kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Mwenezi wake, Nape Nnauye na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Mambo ya nje, Dk. Asha-Rose Migiro, wakiwa katika ziara mkoani Mbeya walinukuliwa wakiwataja baadhi ya mawaziri kuwa ni mizigo.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema: " Hata mimi niliyasikia kwenye vyombo vya habari na hasa magazeti, lakini kiutu uzima huwezi kutolea kauli taarifa za kwenye magazeti…tunamsubiri arudi, aandike taarifa yake, tukae nae tuone alifikiri nini kusema hayo kichwani mwake.”
Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa (CUF), alitaka kujua kwa nini fedha za chenji ya rada zimetumika Tanzania Bara pekee na Zanzibar haijapata kitu.
Waziri Mkuu Pinda alisema: “Yaani mheshimiwa umekaa nalo muda wote huo hadi leo. Ungenitip na jambo hili lingeisha, lakini hata hivyo tutafuatilia kujua hatua iliyofikia.”
Mnyaa pia alitaka kujua kuhusu ujenzi wa nyumba za walimu, madawati na kadhalika na kwamba utekelezaji wake umefikia hatua gani.
Waziri Mkuu Pinda, alisema atawasiliana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kujua hatua iliyofikiwa kwa miradi hiyo na taarifa itatolewa.
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alihoji mpango wa serikali kuanzisha zoezi la kuhakiki watu wanaomiliki silaha ndogo ndogo kwa kuwa imejitokeza kuwa baadhi ya watu wanaomiliki silaha hizo wamebainika kuwa na matatizo ya akili.
“Kuna ushahidi hata vichaa wanamiliki silaha, ni vizuri serikali ikafanya uhakiki wa watu waliomilikishwa silaha hizo kama wana uhalali wa kuendelea kuzimiliki,” alisema.
Waziri Mkuu Pinda alikubaliana na mbunge huyo kwa kusema serikali hufanya operesheni na akawataka wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha polisi.
Alisema serikali itafanya zoezi hilo la uhakiki na kwa kuanzisha wataanza na Mkoa wa Arusha.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment