NA MWANDISHI WETU
13th December 2013
Timu hiyo inayoundwa na wataalamu kutoka serikalini, vyuo vikuu na sekta binafsi, ilizinduliwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, chini ya uratibu wa Taasisi ya Uongozi nchini.
Balozi Sefue, alitaja jopo la wataalamu hao na eneo analotoka kwenye mabano kuwa ni Mwenyekiti, Profesa Florens Luoga (UDSM), Julieth Kairuki (TIC), Mhandisi Nobert Kahyoza (Wizara ya Nishati na Madini), Charles Mwapinga (TRA) na Gabriel Bujulu (TPDC).
Wengine ni, Dk. Fidea Mgina (Wizara ya Viwanda na Biashara), Athman Kwariko (TEITI), Ignace Mchallo (Ofisi ya Rais), Siraji Majura (Wizara ya Fedha), Godwin Nyelo (Baraza la Madini na Nishati), John Ulanga (Taasisi ya Asasi za Kiraia), Deo Mwanyika (TPSF), Profesa Yonika Ngaga (Sua), Profesa Hamudi Majamba (UDSM) na wawili ambao watateuliwa muda wowote kuanzia sasa kutoka Benki Kuu (BoT) na Tume ya Mipango.
Alisema Mwenyezi Mungu amelijalia taifa hili wingi wa rasilimali zikiwamo gesi asilia, mafuta na madini, na kwamba jopo hilo sambamba na serikali litahakikisha linafanya maamuzi sahihi ya kuhakikisha utajiri huo unawanufaisha Watanzania.
Alisema jopo hilo mbali na majukumu mengine ndani ya kanuni 12 zitakazokuwa zinawaongoza, linaundwa na Watanzania wenyewe na kusimamiwa na serikali ili kuhakikisha makosa ambayo yalijitokeza kwa nchi nyingine kwenye eneo hilo la rasilimali, hayatokei na kujifunza mazuri kutoka kwa waliofanya vizuri.
“Ukweli ni kwamba, huu ni ubunifu wetu wenyewe na unaendeshwa na serikali yenyewe lakini tukisaidiana kwa masuala ya kiufundi na Taasisi ya Natural Resource Charter-Revenue Watch na wataalamu wengine kutoka maeneo mbalimbali,” alisema Sefue na kuongeza:
“Tumejipanga kuhakikisha kwamba, makosa ambayo wengine walishawahi kufanya katika sekta hii ya madini, hayatokei tena.”
Kwa upande wake, Profesa Paul Collier, ambaye pia ni Murugenzi katika Kituo cha Masomo ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Oxford, alisema iwapo serikali itasimamia vyema masuala ya uwekezaji, rasilimali zikiwamo gesi asilia, mafuta na madini zitaweza kuinua uchumi wa nchi kwa kiwango kikubwa.
Profesa Collier pia aliishauri serikali kuhakikisha uwazi na sheria zinazosimamia eneo hilo vinafuatwa huku Watanzania wakipewa elimu ya kutosha juu ya rasilimali hizo, vinginevyo itakuwa ni hatari kwa siku za usoni.
Aliongeza kuwa, wanasiasa pia wanayo nafasi ya kuwapa elimu wananchi juu ya rasilimali hizo huku uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali hizo vichukuliwe kwa umakini mkubwa.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Uongozi Profesa Joseph Semboja, alisema jopo hilo linapaswa kuhakikisha kuwa masuala yote yanayohusiana na kazi hizo kwa mujibu wa kanuni hizo 12, zinatekelezwa ipasavyo.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment