NILIPOWASIKIA baadhi ya wabunge kutoka Zanzibar, walioko ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano ambalo hukutana mjini Dodoma, wakijadili muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni, nililikumbuka neno adhimu la Kiingereza – delete. Hili neno maana yake halisi ni “kutoa” au “kufuta.” Ni maana sawasawa na ya neno jengine omit au remove.
Kwa mnasaba wa makala hii, na kwa kuwa hapa ninalenga kuchambua mwenendo wa baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutokana na wanayoyasema kutoendana na ukweli ulivyo, nataka ieleweke mapema kuwa wapo wabunge vimeo.
Maana pana ya maneno hayo ya Kiingereza ni kutaka watupwe, au watolewe, au wanyimwe nafasi, au wadharauliwe, au wasiaminike.
Kwa tafsiri yoyote ile amayo mtu ataitumia, lengo ni kusema kuwa wabunge hawa hawafai na wasitegemewe kwa lolote jema katika kuuangalia mustakbali wa nchi yetu Zanzibar.
Mohammed (Eddy) Riyami ambaye ni kada maarufu wa CCM Zanzibar, alitumia neno hilo alipokuwa akihutubia halaiki ya wananchi kwenye ukumbi wa Salama wa Hoteli ya Bwawani, Agosti mwaka huu.
Huku akioneshwa kukerwa na namna alivyosulubiwa rafiki yake na mtetezi mwenziwe kindakindaki anayepigania maslahi ya Zanzibar katika kipindi hichi cha kutafutwa kwa katiba mpya ya Muungano, Eddy alisema mwanasiasa yeyote katika ngazi yoyote ya uongozi, ambaye mwenendo wake hautakuwa wa kuzingatia maslahi ya Zanzibar, lazima awe deleted – afutwe.
Eddy anayefahamika sana kwa ujasiri wake katika kutekeleza mipango ya kuinua chama chake tangu enzi, lakini siku hizi akijitokeza kama mtu makini katika kuitetea Zanzibar ya Mamlaka Kamili, anasema Wazanzibari hawapaswi kwanamna yoyote ile kuvumilia mtu anayeichimbia kaburi Zanzibar.
Alieleza haya mbele ya umma uliokuwa kwenye kongamano la wazi lililoandaliwa kwa ajili ya kusikiliza mapendekezo ya Kamati ya Maridhiano ya Zanzibar ya kuzingatiwa kama msingi wa mahitaji ya Wazanzibari katika mustakbali wa nchi yao.
Eddy alisema iwapo kuna watu wanadhani wana haki zaidi katika Zanzibar hata kuwafukuza watu wanaoitetea nchi basi hao wanastahili kudharauliwa, wasipewe nafasi ya kurudi kwenye nafasi za uongozi zinazowapatia umaarufu na maisha mazuri.
Kauli yake ilikuwa inalenga kumtetea Mansour Yussuf Himid ambaye alikuwa amefukuzwa CCM kwa sababu tu amekuwa mstari wa mbele katika kuitetea Zanzibar akitaka iachiwe ipumue. Kwamba kuna haja ya Zanzibar kupatiwa mamlaka yake kamili ya kujiongoza ili ijenge uchumi wake na isaidie watu wake kupata maisha yaliyo bora.
Lakini, huo ni mtizamo usiofurahisha baadhi ya makada wa CCM wakiwemo wabunge ambao huthubutu kujitokeza hadharani wanapokuwa Tanganyika na kutoa maeneo ambayo hata wenyewe wanajua ni ya kudanganya au kuupotosha ukweli wa mambo.
Sasa katika kujadili muswada wa sheria itakayotumika kufanya uamuzi wa kuidhinisha au kuikataa katiba mpya inayoandaliwa, baadhi ya wabunge wa Zanzibar walitamka waziwazi kuwa masheha hawana ubaguzi, hawambagui mtu yeyote katika utoaji wa haki za kikatiba.
Haki iliyokuwa inazungumzwa hasa katika muswada ni ya kupiga kura ya maoni ya kuamua mustakbali wa rasimu ya katiba. Baada ya rasimu ya awali iliyokuja na mapendekezo ya kuwepo kwa serikali tatu katika mfumo wa Muungano, badala ya serikali mbili zilizopo kwa miaka yote 49 ya Muungano huo, rasimu ya pili inatarajiwa kutolewa wakati wowote ndani ya wiki ijayo.
Rasimu hiyo itawasilishwa mbele ya Bunge Maalum la Katiba, ambalo, baada ya kuijadili, litaipitisha na kusubiri kupelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kupiga kura ya maoni.
Kumekuwa na wasiwasi kwamba kwa kuwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ndiye itakayosimamia kura hii upande wa Zanzibar (Unguja na Pemba) na kwa vile ni jambo lisilokuwa na ubishi kwamba wapo Wapiga Kura (DKWK) la Zanzibar, linalodhibitiwa na tume hii, maelfu ya watu watakosa haki ya kupiga kura ya kuamua hatima ya katiba mpya.
Lakini katika kujadili muswada wa kura ya maoni, wabunge kadhaa wa CCM walipinga ukweli huu, wengine wakijitia hamnazo kamwe, kama vile wananchi wenyewe walionyimwa haki ya kupiga kura hata katika uchaguzi mkuu wa kuchagua viongozi wa kitaifa, ni waongo wakubwa.
Yahya Kassim Issa wa jimbo la Chwaka, Wilaya ya Kati, Abdalla Sharia Ame wa jimbo la Dimani, Jadi Simai Jadi wa jimbo la Mkwajuni, walinishangaza sana. Walikataa ukweli huu na kusema hakuna tatizo lolote isipokuwa watu hawafuati sheria.
Kama vile wabunge hawa hawajui kuwa wananchi wanajua CCM inaingiza wapiga kura mamluki kwenye uchaguzi, wanatetea uovu huu. Kama vile hawajui kuwa wananchi wanajua kuwa kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi kinatumika kwa maslahi ya kisiasa yanayonufaisha CCM kwa gharama ya haki za wananchi. Kama vile hawajui kuwa wananchi wanajua wamekuwa wakidhulumiwa haki zao kwa sababu tu wanaaminika watakipigia kura Chama cha Wananchi (CUF). Wabunge wa CCM hawa wanasema hakuna tatizo lolote.
Mbunge Yahya ambaye anajua jimbo la Chwaka ni moja ya majimbo maarufu kwa Zanzibar yanayotumika kuingiza wapiga kura mamluki, Abdalla Sharia anayejua jimbo la Dimani linajulikana linavyotumika kupitisha wapiga kura feki, na Jadi asiyekosa kujua kwamba Mkwajuni wanapelekwa wapiga kura wageni kusaidia CCM, wanakataa kwamba masheha ni tatizo.
Wakambwatukia msemaji wa upinzani kuhusu wizara ya sheria na katiba, Tundu Lissu, mbunge wa Singida Mashariki anayetokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwamba anasema asiyoyajua.
Wakataka Wazanzibari wasisemewe na mbunge asiyewajua. Kwamba kwao, mbunge anayeweza kuwakilisha maoni ya wananchi wa Unguja na Pemba awe tu mbunge aliyechaguliwa na wananchi hao.
Wabunge hawa walimchupia Mussa Haji Kombo, mbunge wa Chake Chake, mbunge mpya wa Chambani, Yussuf Salim Hussein waliosema kwamba kila Mzanzibari aliye mkweli wa nafsi yake, anajua matatizo makubwa ya uchaguzi yanaanzia kwa masheha kukataa uhalali wa wananchi majimboni mwao.
Yahya alisema masheha wameteuliwa viongozi wa serikali, hawambagui mtu yeyote kwa sababu wao ni wawakilishi wa rais katika ngazi hiyo ya chini ya uongozi. Hakuna ubaguzi wowote kwa masheha, akasisitiza.
Jadi alisema tatizo kubwa kwa wananchi wengi ni kwamba hawaifuati sheria inayotaka kila mtu kutoa taarifa kwa sheha anapohamia eneo jingine.Akishadharau sheria hii, alisema, anajikuta ndani ya tatizo pale anapotaka kuandikishwa kule alikohamia.
Wakati Mbunge wa Chambani aliwakumbusha wabunge kuupenda ukweli na kumkumbuka muumba wao, ambaye atawaadhibu kwa kuutanguliza uongo panapostahili kuusema ukweli, na kuwatendea mema wananchi, mbunge Kombo alisema ni vema daftari la Zanzibar lisitumike kuendesha kura ya maoni ya katiba.
Kombo, mwanasiasa wa miaka mingi, alisema anasikitika kusikia wabunge wenzake kutoka ficha yaliyosomwa CCM wakifinyanga ukweli na kudai kama vile hakuna tatizo lolote kuhusu kero ya masheha. Alisema daftari lisitumike na badala yake tume iandikishe upya wananchi wa Zanzibar ili kuhakikisha kila mmoja anapata haki ya kupiga kura ya maoni.
Alisema daftari litaendelea kutumika kwa uchaguzi wa Zanzibar ambao ”sisi wenyewe tunajuana natushaamua kuendesha mambo kimazonge.”
Wabunge wa CCM hawana khabari kamwe kuwa achilia mbali wananchi wa Zanzibar wanaoishi Tanganyika, kwamba wananyimwa haki ya kupiga kura nyumbani kwao Zanzibar, mamia ya watu ambao wengine hawajawahi kutoka vijiji wanavyoishi ndani ya Zanzibar wananyima haki hiyo.
Sheria ya kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi imeongeza tatizo hilo. kwamba yule asiyekuwa nacho hapati fursa ya kuandikishwa kupiga kura. Sharti la kupata kitambulisho hichi ni mtu kuwa na cheti cha kuzaliwa, hati iliyo ngumu kwa mtu wa umri mkubwa ambaye hakuwahi kupata huko nyuma na ni vigumu kuipata leo kutokana na usumbufu wake ikiwemo gharama kubwa.
Wabunge hawa wa CCM wanavutia kamba kwenye maslahi ya kisiasa. Wanaukataa ukweli, hawajali madhila yanayowapata wananchi kwa sababu tu si wafuasi wa chama chao wao.
Wabunge hao wala hawakujisikia vibaya kusomewa majina bungeni ya wananchi walionyimwa haki ya kuandikishwa wakati wanazo sifa. Wala hawakupata hisia kusikia majina ya watoto walioandikishwa ilhali hawajafikia umri wa miaka 18 wa kisheria ndipo wapige kura.
Bila shaka wabunge hawa hawajali maslahi ya maendeleo. Hawajali kwamba Zanzibar sasa siasa za ubaguzi hazina nafasi tena.
Hawapati hisia kwamba siasa chafu zimefutwa kupitia maridhiano yaliyofikiwa mwaka 2009 na Amani Abeid Karume na Maalim Seif Shariff Hamad. Hawana khabari kabisa kuwa wananchi wameidhinisha serikali ya umoja wa kitaifa ili wajenge nchi badala ya kuendeleza chuki na fitna.
Hawapati hisia kwamba siasa chafu zimefutwa kupitia maridhiano yaliyofikiwa mwaka 2009 na Amani Abeid Karume na Maalim Seif Shariff Hamad. Hawana khabari kabisa kuwa wananchi wameidhinisha serikali ya umoja wa kitaifa ili wajenge nchi badala ya kuendeleza chuki na fitna.
Kama alivyosema Eddy, hawa ni ku delete. Wafutwe kabisa katika viongozi wanaoifaa nchi.
Kwao, lililo jema ni maslahi ya chama chao siyo nchi yao. Wakati maridhiano yanahimiza wananchi kupenda nchi yao, na kuamini katika maendeleo, wao wanataka kurudisha nchi nyuma.
Hawajali uzalendo wala hawaoneshi uadilifu. Mtu asiyekuwa muaminifu anapokuwa ni mwanasiasa, anapaswa kuogopwa. Haoni aibu kuikashifu nchi yake, wala kudhalilisha watu wake. Ataitia fitna na ataihujumu. Hatajali athari za yote haya.
Wanasiasa hawa wanafaa pasina shaka yoyote kuwekwa kundi lile ambalo kada mwenzao wa CCM, Eddy Riyami anahimiza wasulubiwe.
Chanzo: Fahamu
No comments :
Post a Comment