Ng'ombe wakiwa malishoni
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Posted Jumatatu,Julai14 2014.
Posted Jumatatu,Julai14 2014.
KWA UFUPI
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani alibainisha hayo alipotembelea ranchi hiyo akiwa na watendaji wa wizara kwa ajili ya kujiridhisha na mipaka ya ranchi sambamba na kujionea hali halisi kabla ya kupewa mwekezaji.
Mvomero. Wizara ya Mifugo na Uvuvi inakusudia kutoa kwa wawekezaji kutoka Marekani, eneo la Ranchi ya Taifa ya Mkata lililopo wilayani Kilosa.
Ranchi hiyo imekuwa haifanyi kazi tangu mwaka 2010 kutokana na ukame.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani alibainisha hayo alipotembelea ranchi hiyo akiwa na watendaji wa wizara kwa ajili ya kujiridhisha na mipaka ya ranchi sambamba na kujionea hali halisi kabla ya kupewa mwekezaji.
Dk Kamani alisema kuwapa wawekezaji ranchi hiyo kutoka Marekani, kutasaidia kuiendeleza na kuwa na ufugaji wa kisasa.
Alisema wawekezaji watakaoiendeleza ranchi hiyo wanakusudia kufuga kisasa, hali itakayowanufaisha pia wafugaji wa maeneo jirani kujifunza na kunufaika kibiashara kupitia sekta ya mifugo.
Alisema mwelekeo wa wizara kwa sasa kwa sekta hiyo ni kuvutia wawekezaji wakubwa wa kibiashara ili Serikali ipate mitaji.
Meneja wa ranchi hiyo, Keue Mbwambo alisema wakati akitoa taarifa kwa waziri kuwa walilazimika kuhamisha ng’ombe 1,842 kutokana na baadhi kufa kwa ukame.
Mbwambo alisema ranchi hiyo ina ukubwa wa hekta 19,446 ikiwa ni baada ya maeneo mengine, ikiwamo vitalu 11 kugawiwa kwa wafugaji wadogo.
Alisema viongozi wa vijiji vya Lubungo na Kimambila wamekuwa wakijichukulia hatua ya kuwagawia wafugaji wadogo na hata wakulima kwa kutoa hati ambazo hazitambuliki.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Walace Karia aliiomba wizara hiyo kuhakiki mipaka ya ranchi hiyo ili kuepusha migogoro.
Karia alisema migogoro mingi inatokana na mamlaka za vijiji kugawa maeneo kwa hati za kimila hata yale ambayo yana hati miliki za kisheria, bila kushirikisha wilaya
.
.

No comments :
Post a Comment