Chama cha Wananchi (CUF) kimesema
hakiikubali Katiba inayopendekezwa kwa kuwa haina maslahi ya wananchi wa
Zanzibar.Badala yake chama hicho kimewataka Wazanzibari waikatae Katiba
iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba (BMK).
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu
wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif
Sharif Hamad, wakati akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika viwanja
vya Demokrasia vya Kibanda Maiti, mjini Zanzibar.
Maalim Seif
“Wananchi, Katiba haikubaliki kwa
Wazanzibari, mimi mwenzenu siikubali, sijui nyinyi wenzangu?” alihoji
Maalim Seif na wananchi kuitikia kuwa nao hawaikubali.
Alisema kuwa miongoni mwa mambo
yanayoipokonya Zanzibar hadhi yake ni Katiba inayopendekezwa kumpokonya
Rais wa Zanzibar mamlaka ya kugawa mikoa, tofauti na Katiba ya Zanzibar
ya sasa.
Alisema kwa maana hiyo Rais wa Muungano
anachukua mamlaka ya Rais wa Zanzibar na anaweza kuteuliwa wakuu wa
mikoa, wakuu wa wilaya wa Zanzibar.
“Kwa mabadiliko hayo ya rasimu ya Chenge,
Rais wa Muungano anaweza kututeulia Sheha wa Shehia ya Mtoni Zanzibar
kutoka Bukoba,” alisema Maalim Seif huku akishangiliwa na wanachama na
wafuasi wa CUF.
Maalim Seif alisema Katiba ya Zanzibar na
marekebisho yake ya mwaka 2010 iko sahihi kabisa na inazingatia matakwa
ya Makubaliano ya Muungano.
Alisema hayuko tayari kuona rasimu hiyo inakubalika na kwamba Wazanzibari hawataki kuiona.
Alisema hakubaliani na kauli za baadhi ya
watu waliosema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)
inaridhishwa na mchakato wa Katiba mpya.
“Nataka kuwambia hakuna kikao chochote
cha SMZ kilichokaa na kusema tunaijadili rasimu, kama kuna mtu anataka
kusema eti Smz imeridhishwa aseme mwenyewe binafsi na siyo Serikali ya
Umoja wa Kitaifa,” alisema Maalim Seif.
Maalim Seif aliisifu Rasimu ya Jaji
Joseph Warioba ambayo ndiyo ilizingatia matakwa ya Watanzania walio
wengi na kwamba pamoja na awali Wazanzibari kupendekeza muundo wa
Muungano wa mkataba, lakini kwa busara ya tume hiyo waliikubali muundo
wa serikali tatu.
Maalim Seif alisema anahutubia mkutano
huo akiwa na furaha kubwa kutokana na umma ulioteremka katika viwanja
vya Kibandamaiti, na hiyo ni sababu tosha na ujumbe kuwa hawaitaki
Katiba inayopendekezwa.
“Ndugu yangu, rafiki yangu Rais Jakaya
Kikwete ufahamu kuwa umma huu uliohudhuria Kibandamaiti ni ujumbe tosha
kuwa Katiba hiyo hawaitaki, na mwambia Rais Kikwete kuwa Katiba hii
hatuikubali,” alisema Maalim Seif.
Maalim Seif alisema Katiba bora ni ile
inayozingatia maoni ya wananchi. “Lakini Rais (Rais Jakaya Kikwete),
Katiba yenu mmeweka upande maoni ya wananchi, mmejifungia wenyewe,
mmeipitisha wenyewe na mmeichezea ngoma wenyewe”, alisema.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed
Mazrui, alisema wajumbe saba wa Bunge Maalum la Katiba waliopiga kura ya
Hapana hadharani kukataa rasimu hiyo ni mashujaa wa Zanzibar na
Wazanzibari wote wanapaswa kuwapa heshima kubwa.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF,
Salum Bimani, alisema wananchi wa Zanzibar wameshaamua na hawatarejea
nyuma zaidi ya kuiondoa CCM mwaka 2015 na kuipa Zanzibar mamlaka kamili.
Bimani alisema msiwape kura viongozi wa CCM ambao wanauza nchi ya Zanzibar huku wakicheza ngoma.
“Kwa Shilingi 300,000 watu hawa
wanadiriki kuuza nchi, hawa waliopiga kura za ndiyo ni madalali wa
Zanzibar, hata wale waliopiga kura za siri pia ni madalali,” alisema
Bimani.
Alisema wanasheria wawili wameitetea Zanzibar na wakafikwa na masahiba mazito.
Aliwataka wanasheria hao kuwa Jaji Walfgong Dourado na Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyefutwa kazi, Masoud Othman Masoud.
Bimani alisema Wazanzibari wapo pamoja
nao katika kuhakikisha Zanzibar inabaki na wale wenye nia mbaya wajue
kwamba Zanzibar wataitapika watake wasitake.
Mansour alisema naendelea kuwa muumini wa Maridhiano ya Zanzibar. Katiba hii ni yao wenyewe si ya Wazanzibari.
Mansour alisema naendelea kuwa muumini wa Maridhiano ya Zanzibar. Katiba hii ni yao wenyewe si ya Wazanzibari.
“Baada ya kuona umma huu uliohudhuria katika mkutano huu tunapaswa kumhofia Mwenyezi Mungu,” alisema.
“Naendelea kumuunga mkono Maalim Seif
Sharif Hamad, ni kiongozi asiyekuwa mnafiki anajitambua na hatawaliwi na
utawala wa Dodoma, anatawaliwa na Wazanzibari wenyewe na matakwa na
matumaini yao,” alisema na kuwataka Wazanzibari wasiwe na hofu kwani
hawawezi kufungwa wote wako wengi sana, wakati umefika.
“Tumeungana kwa hiari yetu, tukakubali
kwa hiari yetu, sisi si watumwa wa mtu yoyote, tumefungwa tumefukuzwa
makazini kwa sababu ya nchi hii, hatuwezi kurudi nyuma,” alisema.
Alieleza kuwa watu wasishangae kumuona
Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano, Mzee Nassoro Moyo, amesimama kwenye
jukwa anatetea nchi yake.
Mzee Moyo alisema Wazanzibari hawakubalini kuona watu wanataka kuichukua nchi yao ovyo ovyo.
Mkutano huo ambao ni wa kwanza kuhutubia
na Maalim Seif tangu BMK limalize kazi yake na kuwasilisha rasimu kwa
Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein,
ulihudhuriwa na maelefu ya wananchi huku baadhi yao wakibeba mabango.
Baadhi ya mabango hayo yalibeba ujumbe
usemao “Wapige mabomu rasimu yao hatuitaki, Hongera Othman Masoud,
Katiba ya vijisenti (Chenge) hatuitaki”.
Katika hatua nyingine, Maalim Seif
alikanusha taarifa kwenye mitandao kuwa hatajiuzulu wadhifa huo na
ataendelea kukiongoza CUF kushika madaraka na kushika Serikali ya Umoja
wa Kitaifa katika uchaguzi mkuu wa mwakani, akiwa kwenye nafasi hiyo.
Maalim alisema taarifa zilizoenezwa
kwenye mitandao ya kijamii kuwa baada ya kufukuzwa Mwanasheria Mkuu wa
Zanzibar, Masoud Othman Masoud, naye amejiuzulu Umakamu wa Kwanza ni
uzushi mtupu.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment