
Kashfa ya Operesheni Tokomeza na ya ukwapuaji wa mabilioni ya fedha kutoka akaunti ya Tegeta Escrow, zimeibuliwa upya bungeni, baada ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhoji kitendo cha serikali kuwasafisha mawaziri waliowajibika kisiasa kutokana na kashfa hizo.
Kambi hiyo imesema hatua hiyo ya serikali ni mwendelezo wa tabia yake ya kukwepa kuwajibishwa na Bunge.
Kashfa ya Operesheni Tokomeza ilihusisha mauaji ya watu, wengine kudhalilishwa, kuharibiwa nyumba na mali, ikiwamo mifugo kupigwa risasi na kila aina ya uonevu wakati wa utekelezaji wake.
Kutokana na kashfa hiyo, waliokuwa mawaziri; Dk. Emanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa-JKT), Balozi Khamisi Kagasheki (Maliasili na Utalii) na Dk. Mathayo David (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi), walijiuzulu.
Pia kashfa ya Tegeta Escrow ilihusisha uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 200 uliofanywa kifisadi kutoka kwenye akaunti hiyo, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).Kutokana na kashfa hiyo, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, alijiuzulu, huku aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, akitimuliwa kazi na Rais.
Kashfa hizo ziliibuliwa na Msemaji wa Kambi hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Freeman Mbowe, wakati akiwasilisha maoni ya kambi kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016, bungeni jana.
Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi hiyo, alisema Taifa la Tanzania limekuwa majeruhi wa sakata juu ya sakata, ambazo serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kushindwa tu kusimama kama serikali na hivyo kusababisha madhara kwa wananchi na uchumi kwa jumla.
“Kwa mfano, wakati dunia inajua vilivyo kwamba, Bunge lilifanya kazi yake katika kuisimamia serikali juu ya kashfa ya Operesheni Tokomeza na mwishowe kuishia kwa mawaziri wanne kuachia madaraka kwa kuwajibika kisiasa, leo serikali inarudi kwa mlango wa nyuma na kudai eti hakukuwa na tatizo,” alisema Mbowe.
Alisema serikali imeshindwa kuwa makini katika suala hilo.
“Kwa mfano, wakati Tume iliyoundwa na Rais ya majaji watatu; Jaji Hamisi Msumi (Balozi) akiwa mwenyekiti; Jaji Stephen Ernest na Jaji Vincent Kitubio ikiwa imekabidhi ripoti yake serikalini na matokeo yake kutangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, kilichomo kimeacha maswali mengi sana juu ya utayari wa serikali hii kukubali kuwajibika,” alisema Mbowe.
Aliongeza: “Kwa mfano, Balozi Sefue anasema mawaziri wote wanne waliojiuzulu mwaka 2013 kwa sakata la Operesheni Tokomeza hawana hatia. Yaani serikali inataka hata kusema kwamba, hata kule viongozi hao kuchukua wajibu wa kisiasa kuwajibika ni kinyume cha utawala bora.”
Mbowe alisema wakati ikisema hivyo, serikali inakubali kwamba, kuna watu waliuawa kwa makosa.
Alisema idadi ya watu waliouawa ilikuwa inaonyesha ni 15, ingawa tume inathibitisha vifo tisa.
Mbowe alisema tume pia inakiri kwamba, kuna watu walidhalilishwa; kularibiwa nyumba na mali zao, kama mifugo kupigwa risasi na kila aina ya uonevu.
Alisema serikali imekubali kulipa fidia kwa wote waliokumbwa na madhila hayo na kuhoji katika mazingira hayo, uwajibikaji wa kisiasa unakuwaje kosa?
“Serikali inasafisha vipi waliowajibika kisiasa? Kwa nini hatujifunzi kwa Mzee wetu, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, alipowajibika miaka ya 1970 kwa sababu ya madhila waliyotendewa wananchi na askari ingawa yeye mwenyewe hakushiriki,” alisema Mbowe.
Aliongeza: “Serikali hii kwa nini inaogopa na kukwepa uwajibikaji? Kama serikali hii inaamini katika uwajibikaji na uwazi, iweke hadharani ripoti ya majaji watatu kuhusu kashfa ya Operesheni Tokomeza ili wananchi waisome na kujiridhisha, vinginevyo serikali hii inaendeleza tabia ile ile ya kukwepa kuwajibishwa na Bunge kama ilivyokuwa kwenye maazimio ya Operesheni Tomomeza.”
SAKATA LA ESCROW
Alisema juhudi za serikali kutaka kusafisha na kufunika kashfa zake pia zimethibitika wiki iliyopita, baada ya Balozi Sefue tena kujaribu kuwasafisha wahusika wa sakata la Tegeta Escrow.
“Watanzania wanajua na dunia inajua kwamba kama kuna wizi wa mchana kweupe umefanyiwa nchi hii ni kashfa ya Tegeta Escrow, watumishi wa umma wamehongwa mamilioni ya fedha, majina yametajwa; aliyekuwa Katibu Mkuu Nishati na Madini, Eliakim Maswi na Waziri wake, Profesa Sospeter Muhongo, walionyesha ni kwa jinsi gani walishindwa kuisaidia serikali na nchi isiibiwe kwenye kashfa hii,” alisema Mbowe.
Hata hivyo, alisema alisema pamoja na maazimio ya Bunge kuwataja Prof. Muhongo na Maswi kwa ushahidi jinsi walivyoshindwa kutekeleza majukumu yao, serikali imekuwa hailali ikitafuta njia ya kuwasafisha.
“Hii ni serikali pekee duniani inayokasirika Bunge likifanya kazi yake sawa sawa ya kuisimamia ndiyo maana mara nyingi imegeuka na kutafuta njia ya kufunika madudu ambayo siyo tu yameiaibisha sana, bali yamegharimu kodi nyingi za wananchi,” alisema Mbowe.
Aliongeza: “Serikali inajua kwamba, utekelezaji wa bajeti ya serikali inayomalizika ya mwaka 2014/15 umekwamishwa sana na kashfa ya Tegeta Escrow baada ya nchi wafadhili kuzuia kutoa fedha za kuchangia fungu la maendeleo kutokana na tabia ya serikali kufunika kombe mwanaharamu apite kwenye kashfa hii.”
Aliitaka serikali kusema inapofunika na kubeba wahusika wa kashfa hizo, wanataka kuwasaidia wananchi au viongozi kama wameamua kujiunga dhidi ya wananchi wao.
Alisema serikali inajua kuwa kashfa ya Escrow ina mizizi katika kashfa ya kampuni ya IPTL iliyoanza mwaka 1994 ndani ya Wizara ya Nishati na Madini wakati huo Rais Jakaya Kikwete akiwa waziri.
“Ikaidhinishwa mwaka 1995, Rais Jakaya Kikwete akiwa Waziri wa Fedha na sasa inafumuka katika sakata hili la Escrow na kuiparaganyisha serikali Rais Kikwete akiwa madarakani,” alisema Mbowe.
“Ni kwa nini mambo haya yanatokea na serikali inaendelea kuyabeba na kusafisha uoza huu? Ni kwa faida ya nani?” alihoji.
MINYUKANO YA RICHMOND NA MZIGO KWA TAIFA
Alisema katika mlolongo huu wa kushindwa kusimamia nchi, kuendekeza makundi na vita vya kisiasa ndani ya CCM na serikali yake kwa gharama ya Taifa, taifa hili sasa linadaiwa Sh. bilioni 120 baada ya kushindwa kwenye kesi ya Dowans/Richmond katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC) huko Paris. Serikali haijataka kuliweka jambo hili wazi na ni dhahiri kuna siri kubwa inayosababisha jambo hili kuwa la usiri mkubwa.
“Huko mbele ya safari jambo hili litaligharimu Taifa mabilioni haya ya fedha ambayo yangeweza kuepukika kama ukweli, uwazi na haki vingetawala mchakato mzima wa kashfa ya Richmond. Serikali isimame sasa na ilieleze Taifa ni nani anasema kweli, ni nani alilidanganya Bunge na ni nani analindwa na serikali katika kashfa hii?,” alisema Mbowe katika hotiba hiyo.
Kiongozi huyo wa upinzani alisema mapambano ya mitandao ndani ya serikali ya CCM na minyukano ya kupigania maslahi na ulaji ndani ya mikataba mbalimbali ya miradi ya umma ikiongozwa na walio karibu na watawala na familia zao imeota mizizi katika serikali ya awamu ya nne.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ingependa kujua kwamba serikali hii ya CCM ambayo imefikia mwisho wake ni kwa nini inawaachia Watanzania madeni makubwa hivi? Je, kashfa hizo zote za serikali kushindwa kuwajibika, kutafuta visingizio vya kufunika madhambi yake, ndiyo maisha bora kwa kila Mtanzania ambayo wananchi waliahidiwa miaka 10 iliyopita? Nini kauli ya serikali juu ya tabia hii ya kuwabebesha wananchi mizigo ya madeni huku serikali hiyo hiyo ikijitahidi kwa nguvu zake zote kuwasafisha viongozi walioitumbukiza nchi kwenye madhila haya?” alihoji.
Hata hivyo alisema ni jambo la kumshukuru Mungu kuwa sasa hatimaye utawala wa CCM unakaribia ukingoni na ni rai yake kwa Watanzania wote waonyeshe hasira yao ya kuibiwa, kudhalilishwa na hata kufanywa mafukara kwa kikinyima chama hiki cha zamani kilichogawana rasilimali za Taifa hili kwa misingi ya kifisadi kwa muda mrefu.
WANAHARAKATI WAPINGA MAWAZIRI KUSAFISHWA
Katika hatua nyingine, wanaharakati wamepinga hatua ya Ikulu kuwasafisha mawaziri watano waliojiuzulu kufuatia maazimio ya Bunge.
Mkurugenzi wa Sikika, Irenei Kiria, alisema hatua iliyochukuliwa na Ikulu ni ishara ya serikali iliyoshindwa kupambana na ufisadi na ambayo inashirikiana na mafisadi katika kudhulumu mali ya umma.
Alisema iwapo taarifa za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na katika mijadala ikabaini wanatakiwa kuwajibika, serikali ambayo ndiyo kimsingi ilikuwa inawajibishwa na Bunge ilichotakiwa ni kutekeleza maazimio ya Bunge na siyo kufanya uchunguzi upya au kusafisha watu.
“Sakata la akaunti ya Tegeta iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), lilishajadiliwa na wabunge wakaona watu wanatakiwa kuwajibika na kwamba kuanza kuwasafisha waliotajwa ni sawa na serikali, ambayo imeshindwa kusimamia uwajibikaji na inashirikiana na mafisadi na wahujumu mali za umma,” alisema.
Alisema uwajibikaji uliofanywa na mawaziri wanne kutokana na sakata la Operesheni Tokomeza siyo kwamba walishika bunduki au walitekeleza mateso kwa wananchi, bali vyombo vilivyofanya matukio vilikuwa chini ya himaya yao na mtu anaposema hawakuhusika anaonyesha uelewa wake wa dhana ya uwajibikaji ni mdogo au anafanya makusudi kwamba hajui.
“Kwa dhana hiyo ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, mawaziri hao wasingetajwa bungeni wajibu hoja, bali tuwaite waliotenda kazi husika ndiyo wajibu hoja, sakata la Tokomeza waziri hakupaswa kujibu lolote bali wale waliohusika moja kwa moja walipaswa kujitokeza kujibu,” alisema.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo-Bisimba, alisema hadi sasa hakuna kusafishwa kulikofanyika kwa kuwa uhusika wa viongozi hao haukwepeki.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment