dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, May 17, 2015

Hatma kina Lowassa, CCM bado kigugumizi

  NAPE: Uchunguzi wao haujakamilika... Wamo Sumaye, Membe, Wassira, Makamba na Ngeleja

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
Hatma ya makada sita wa Chama cha Mapinduzi (CCM), waliokuwa kwenye adhabu ya kuchunguzwa kwa kukiuka taratibu za chama, bado haijajulikana baada ya chama hicho kusema kuwa uchunguzi wao haujakamilika.

Makada waliokuwa kwenye adhabu hiyo ni Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Wengine ni Waziri wa Kilimo na Chakula,  Steven Wassira, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia January Makamba na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja.

Makanda hao walifungiwa kwa zaidi ya miezi 12 kutokana na kujihusisha na kutangaza nia ya kugombea urais kinyume na taratibu za chama.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, kuhusu mabadiliko ya ratiba ya vikao vya chama hicho, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema vikao hivyo vitajadili ratiba ya mchakato wa uteuzi wa wagombea katika nafasi mbalimbali ndani ya chama.

Akifafanua kuhusu makada hao waliokuwa kwenye adhabu, Nape alisema haelewi kama watagombea ama la kwa kuwa bado wapo chini ya uangalizi mpaka hapo uchunguzi wao utakapokamilika.

“Hatma ya makada hao sita sijui mimi, kwa sababu ni lazima ule mchakato wa kuwachunguza ufike mwisho na nilisema unaweza kuchukua wiki moja, wiki mbili, miezi miwili  na hata mwaka, mimi sijui mchakato ukimalizika taarifa italetwa na kama mchakato haujamalizika basi wanaendelea nayo,” alisema.

Alisema kuna baadhi ya watu wanampigia simu wakimuuliza mbona anazuia watu kuchukua fomu. “Kanuni ipo pale pale inasema kuwa mtu ukiwa kwenye kifungo hauruhusiwi kugombea chochote, nadhani mambo yao yanaweza kuzungumzwa au hayatazungumzwa mimi sijui,” alisema.

Akizungumzia ratiba ya vikao vya chama, Nnauye alisema awali walitangaza kuwa Mei 20, kutakuwa na Kamati Kuu ya Taifa (CC) na Mei 21 na 22 Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Alisema katika ratiba hiyo kuna mabadiliko na kwamba kikao cha CC kinatarajiwa kufanyika Mei 22, mkoani Dodoma na kitaongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Dk. Jakaya Kikwete.

Alieleza kuwa Mei 23 na 24 kitafanyika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na kitafanyikia mjini Dodoma na kuongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama.

Nnauye alisema vikao vya maandalizi kwa ajili ya vikao hivyo vinaendelea na vitaanza kesho (Jumatatu) mpaka Mei 21 ambavyo vitafanyika jijini Dar es Salaam na vingine Dodoma ikiwamo vikao vya sekretarieti.

Alisema vikao vyote vya awali vinafanyakazi ya kuandaa kikao cha CC na NEC  na kwamba mabadiliko ya  tarehe yametokana na  kuingiliana kwa ratiba ya Baraza la Wawakilishi,  hali ambayo imesababisha kufanya mabadiliko ya vikao.

Nnauye alisema vikao vya awali vya kuanzia Mei 18 hadi 21,  vinaanda na kuthibitisha ajenda ambazo zitajadiliwa ambapo moja ya ajenda za kudumu ambazo zitajadiliwa ni hali ya kisiasa nchini.

“Kwa kuwa tunakwenda kwenye uchaguzi, mchakato wa namna ya kuwapata wagombea wa CCM, ikiwamo ratiba, lini watachukua fomu, lini watajadiliwa, majina yatarudishwa lini na kikao hicho,  watajulishwa maandalizi ya ilani ya uchaguzi walipofikia na wajumbe watapata fursa ya kutoa maoni yao,” alisema.

Aidha, alisema kutakuwa na kanuni za namna ya kuwapata wagombea hao kwani yapo mapendekezo ya kuangalia namna ya kuboresha kura za maoni yote hayo yatawekwa katika kikao hicho na kupanga namna ya mchakato huo utakavyokwenda.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments :

Post a Comment