Kiongozi wa jaribio la kumpindua na wenzake wakamatwa

Msemaji wa Ofisi ya Rais, Gervais Abayeho, alisema Rais Nkurunziza alirudi Bujumbura jana akitokea kijijini jimbo la nyumbani kwake. Maofisa walisema rais huyo alirudi nchini Alhamisi, akitokea kwenye mkutano Tanzania.
Taarifa zinasema kuwa Rais Nkurunzuza ameingia jijini Bujumbura akiwa katika msafara wa magari wenye ulinzi mkali akitokea kijijini kwake Ngozi.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) Kabla ya kuingia Ikulu, kiongozi huyo aliweka ujumbe kupitia akaunti yake ya Twitter, akiwashukuru wananchi wa nchi hiyo kumpokea baada ya jaribio la kumpindua kushindikana.
“Nilikuwa na furaha niliporejea na kuona wananchi wa Bujumbura na maeneo mengine wakinipokea kwa furaha,” alisema kupitia mtandao huo.
“Nilikuwa na furaha niliporejea na kuona wananchi wa Bujumbura na maeneo mengine wakinipokea kwa furaha,” alisema kupitia mtandao huo.
Akielezea hali ilivyo kwenye mji huo Ruth Nesoba, alisema watu wanamuunga mkono walitanda barabarani katika mitaa ya mji wa Bujumbura wakishangilia.
Alisema watu hao wengi kutoka kundi la vijana la Imbonerakure ambao ni wanachama wa chama chake walikuwa wakiimba na kubeba picha za Rais Nkurunziza.
Abayeho alisema kiongozi wa mapinduzi, Meja Jenerali Godefroid Niyombare alikamatwa siku mbili baada ya kutangaza kwamba Rais Nkurunziza alikuwa amepinduliwa.
"Ameshakamatwa. Hakujisalimisha," Abayeho alilieleza shirika la habari la Reuters. Awali, Abayeho alisema majenerali wengine watatu walikuwa wamekamatwa lakini Niyombare alikuwa bado hajapatikana.
Alipoulizwa nini kitatokea kwa waliopanga mapinduzi hayo, Abayeho alisema hiyo itakuwa juu ya mfumo wa sheria: "Watawajibika."
Taarifa zingine ziliema; “Rais Nkurunziza tayari ameingia nchini Burundi na kwamba, leo (jana) anatarajiwa kulihutubia taifa. Jeshi tiifu kwa serikali limefanikiwa kudhibiti maeneo muhimu kama redio na televisheni pamoja na uwanja wa ndege na kwamba, mapinduzi dhidi ya Nkurunziza yamefeli,” ilisema taarifa kutoka Ikulu ya nchi hiyo kupitia shirika la utangazaji la Ujerumani (DW).
Katika kile kinachoelezwa kama kweli Rais huyo amerejea nchini kwake ni ishara kuwa jaribio la kumpindua limeshindikana.
Wakati huo huo, Mkuu wa majeshi wa nchi hiyo Niyongabo, alisema vikosi vya serikali ya Burundi vimedhibiti Ikulu, kituo cha radio cha Taifa pamoja na uwanja wa ndege
Taarifa kutoka nchini humo zinaeleza viongozi watatu waliokuwa wakiongoza mpango huo chini ya Meja Jenerali Godfrey Niyombare, wamekamatwa na kupelekwa sehemu isiyojulikana.
Wanajeshi hao waliokamatwa, wote wana vyeo vya Jenerali, ambapo walitajwa kuwa ni msemaji wa Niyombare, Ndabaneze, Naibu kiongozi wa mapinduzi hayo, Cyrille Ndayirukiye na askari mwingine ambaye jina lake halijatambulika.
Wanajeshi watiifu kwa Nkurunziza walionekana kufanikiwa kuzima jaribio hilo la mapinduzi la Alhamisi, wakati kulipokuwepo na milio ya risasi kwenye mitaa ya mji huu mkuu.
Jaribio hilo la kumpindua rais, lilifuatia zaidi ya wiki mbili za maandamano ya wapinzani wanaosema Nkurunziza amekiuka katiba na makubaliano ya amani ya mwaka 2005 kwa kuwania awamu ya tatu.
"Maandamano kupinga nia ya kugombea kwa awamu ya tatu ya Nkurunziza yataendelea," alisema Gordien Niyungeko, Naibu Mkuu wa Focode, moja kati ya makundi 300 ya kijamii ambayo yanaunga mkono maandamano hayo. "Kundi letu halina uhusiano wowote na jaribio hilo la mapinduzi."
Mtu mmoja mwenye jeraha kubwa kichwani alikuwa amelala amekufa kwenye mtaa mmoja mjini Butarere, wilaya moja ya Bujumbura ambayo imekuwa ikikumbwa sana na maandamano. Wakazi walisema polisi walimpiga risasi mtu huyo na kujeruhi wengine wawili. Hakukuwepo na taarifa yoyote kutoka polisi.
Kundi moja la vijana kwenye kiunga cha Cibitoke cha Bujumbura lilisema lilikuwa limeonywa na polisi kwamba litashughulikiwa kama waasi kama wataandamana.
Polisi walikuja kwenye eneo hilo mapema asubuhi, wakawaeleza: "Sasa hatuwatafuti tena waandamanaji, tunawatafuta waasi," mmoja kwenye kundi hilo alisema.
Hata kabla ya jaribio hilo la mapinduzi, maofisa walikuwa waliyaita maandamano hayo "uasi".
Jaribio hilo la mapinduzi lilifuatia wiki mbili za maandamano mjini Bujumbura, ambapo mara nyingi waandamanaji walipambana na polisi, ambao walionekana wakifyatua risasi za moto kwa waandamanaji.
Watu zaidi ya 20 walikuwa wameuawa, kwa mujibu wa idadi isiyo rasmi ya wanaharakati. Wengine wengi pia walikuwa wamejeruhiwa.
Hatua ya polisi kujibu mapigo vikali iliibua shutuma kutoka wahisani wa Magharibi, ambao walishamuasa rais huyo kutogombea tena. Marekani, ambayo inatoa mafunzo na vifaa kwa jeshi hilo, ilitaka kusitishwa "nguvu kubwa" zinazotumiwa na polisi.
Katiba na makubaliano ya amani ambayo yalimaliza vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe viliweka ukomo wa awamu mbili za urais, lakini mahakama moja ilitoa uamuzi kwamba Nkurunziza anaweza kugombea tena kwa sababu aliteuliwa na bunge, na sio kuchaguliwa, kuongoza awamu ya kwanza.
Wapinzani wake na baadhi ya nchi wahisani wamekuwa wakihoji uamuzi wa mahakama hiyo.
Baadhi ya viongozi wa Afrika walishutumu nia ya Nkurunziza ya kugombea tena kwenye uchaguzi wa rais Juni 26, mwaka huu.
Umoja wa Afrika pia ulilaani jaribio lolote la kuchukuwa "madaraka kwa njia ya vurugu".
Makubaliano hayo ya amani yaliyodumu kwa muongo mmoja sasa, yalimaliza mgogoro ambao ulipapambanisha makundi ya waasi ya Wahutu walio wengi, likiwamo lililokuwa likiongozwa na Nkurunziza, dhidi ya jeshi ambalo wakati huo liliongozwa na Watutsi walio wachache.
Jeshi hilo hivi sasa lina mchanganyiko wa makabila yote na liliingiza ndani yake vikundi vya waasi.
Jumuia ya Ulaya, Ubelgiji na Uholanzi zote zimeshasimamisha baadhi ya misaada kutokana na hali ya ukosefu wa usalama, hususani misaada inayohusiana na chaguzi, ambazo pamoja na ule wa rais unahusisha pia kinyang’anyiro cha ubunge kilichopangiwa kufanyika Mei 26.
Wapinzani wa rais huyo na wengine walishatoa wito wa kucheleweshwa kwa chaguzi hizo, japokuwa walisema upigaji kura unapaswa kufanyika kabla ya Agosti 26, wakati awamu ya hivi sasa ya Nkurunziza itakapomalizika.
Hata hivyo, Rais Jakaya Kikwete mara baada ya mkutano wa Dar es Salaam kujadili mgogoro wa Burundi, alisema viongozi wa nchi za Maziwa Makuu wamelaani mapinduzi hayo na kutaka nchi hiyo kurejeshwa katika utawala wa kisheria.
Juhudi za kumtafuta Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe, kwa ajili ya kuelezea suala hilo zilishindikana baada ya kila alipopigiwa simu yake ya mkononi kuita bila kupokelewa.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment