- Walikuwa wakishutumiana kuhusu kuhusu mkuu wa wilaya
Blandes alitoa shutuma hizo jana wakati akichangia mjadala wa makadirio ya matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Bajeti ya mwaka 2015/16.
Tukio hilo lilitokea jana saa nane mchana mara baada ya kuahirishwa kwa mjadala huo na wabunge hao kukutana nje, huku Kirigini akienda mbali zaidi na ‘kumpiga mkwara’ Blandes kuwa licha ya kuwa ni mwanaume, atakiona cha moto.
Wabunge hao waliokuwa wameongozana walionekana wakizungumza kwa sauti ya chini, lakini kadri walivyozidi kupiga hatua, Kirigini alianza kuzungumza kwa sauti kali na kumtuhumu Blandes kuwa hakufanya jambo sahihi kuzungumza suala hilo bungeni.
Wakati akichangia mjadala huo, Blandes alimlipua Rwegasira kuwa anafanya kazi kwa manufaa ya wahamiaji haramu kutoka Rwanda, kuitaka Serikali kumhamisha mkuu huyo wa wilaya vinginevyo yeye na wapiga kuwa wake, ‘watamfanyika kitu kibaya.
Kauli hiyo ilionekana kumkera Kirigini ambaye ni mkuu wa wilaya ya Meatu, ambapo kabla ya kuahirishwa kwa kikao hicho aliomba muongozo wa Spika, akisema kuwa kauli za Blandes zimejaa uchochezi, kutaka suala hilo litolewe ufafanuzi wa Serikali.
Ilivyokuwa ndani ya Bunge
Akichangia mjadala huo, Blandes alisema Rwegasira amekuwa mstari wa mbele kunyanyasa wananchi kwa kuwanyang’anya ardhi katika vijiji vilivyo mpakani na nchi ya Rwanda, huku akiwapendelea wahamiaji haramu.
“Mkuu huyu wa wilaya ni bomu ni mzigo. Anafanya kazi lakini mwili wake uko Tanzania na roho yake ipo Rwanda. Ninaiomba serikali msiwe mnatuletea watu waliochoka kiasi hiki,” alisema Blandes.
Aliongeza, “Kwanza huyu mama amechoka na anakaribia kustaafu. Siku zote anadhani mbunge anafanyakazi chini yake na hajui kabisa kuwa mimi ndiye ninayepaswa kumsimamia. Yaani kama hamtamwondoa mtaona tutakachokifanya.”
Mara baada ya kauli hiyo, ndipo Kirigini alipoibuka mchana na kuomba muongozo kuhusu kauli hiyo ya Blandes.
Huku akitumia kanuni ya 68 (7) kuomba muongozo huo Kirigini alisema, “Naomba mwongozo huu kwa kutambua kuwa mkuu wa wilaya ni msimamizi mkuu wa amani, kwa kutambua nafasi yake kuwa ndiye mkuu na mwakilishi wa ulinzi na usalama na ndiye mwakilishi wa rais kule wilayani."
Alisema kauli iliyotolewa na Blandes ni ya uchochezi, huku akikiri wazi kuwa ana masilahi kwa sababu naye ni mkuu wa wilaya.
Waziri aingilia kati
Muongozo huo ulimnyanyua Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama kusema ameyasikia malalamiko ya pande zote mbili na yatafanyiwa kazi.
“Tumesikia malalamiko ya Kirigini na kwa kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo inaratibu shughuli zote za serikali ndani na nje ya Bunge. Tuachiwe jambo hili tutalifanyia taratibu ambazo zitakwenda kupima pande zote mbili na hatua zitachukuliwa,” alisema Mhagama.
Ilivyokuwa nje ya Bunge
Baada ya kikao hicho kuahirishwa na wabunge kuanza kutoka nje, huku Blandes akiwa anaongozana mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali na Mbunge wa Kibaha Mjini (CCM), Abuu Hamoud Jumaa, alikutana na Kirigini.
Wakati Blandes akiendelea kuongozana na mbunge huyo aliyekuwa mbele yake kama hatua nne, aligeuka nyuma na kuanza kumrushia maneno, “Wewe si mwanaume unavaa suruali sasa tutaona.”
Wakati Kirigini akitoa kauli hizo, Blandes alikuwa akizungumza kwa upole na kusisitiza kuwa na ushahidi wa mambo yote yanayofanywa na mkuu huyo wa wilaya, huku akisisitiza, “Tutakutana tu mbele ya safari”. Hata hivyo wabunge waliokuwa karibu nao waliwasihi kuacha malumbano hayo na kila mmoja kuendelea na shughuli zake.
Kauli ya Blandes nje ya Bunge
Akizungumza nje ya Bunge Blandes alisema, “Kazi ya mbunge ni kuisimamia Serikali na katika hilo siwezi kuogopa. Jambo hili tayari limeshalifikisha serikali. Si jambo la kificho linagusa jimbo langu na mimi ni mwakilishi wa wananchi.”
Alisema Kirigini ni nani mpaka asimame na kupinga yeye (Blandes) kusisitiza, “Hizi sijui ni kanuni ya wapi kwamba mbunge unapangiwa maneno ya kuzungumza.”
Alisema wapo watu wanaoamini kuwa mbunge na mkuu wa wilaya wako sawa jambo ambalo si sawa.
“Siwezi kushindana na mkuu wa wilaya anachotakiwa ni kufanya kazi kwa mujibu wa sheria. Ndiyo maana nchi haiendi mtu anavuruga harafu unalindwa na kutetewa,” alisema.
Aliongeza, “Hawezi kunipiga mkwara ila namheshimu kama mbunge. Kitu alichokosea ni kuingilia uhuru wangu wa kuzungumza. Angesimama kumtetea ili watu wa Karagwe wamsikie. Mimi nina ushahidi na ni mwanasheria hivyo nimeanza kulisema hili jambo ili watu wakitoa shutuma nitoe ushahidi.”

No comments :
Post a Comment