Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, May 22, 2015

Serikali yapigwa kombora kura ya maoni ya Katiba.

Waziri wa Katiba na Sheria,Dk. Asha-Rose Migiro.
Kambi  Rasmi ya  Upinzani Bungeni imeshangilia kukwama  kwa Katiba mpya ikisema unabii  wao umetimia kwa kasi ambayo haikutegemewa.
 
Kambi hiyo imesema licha ya kuiandaa katiba hiyo kwa kutumia mafisadi, kuipitisha kwa kuipigia kura za wafu, kuipokea japo ilisusiwa na wadau wengi kilichojiri ni kwamba Rais Jakaya Kikwete, ataondoka madarakani bila kuacha Katiba mpya.
“Uhakika pekee tulio nao ni kuwa Rais Profesa Dokta Jakaya Kikwete, ataondoka madarakani bila Katiba mpya aliyowaahidi Watanzania,” alisema Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu.
 
Akiwasilisha taarifa ya kambi hiyo jana bungeni kuhusu hotuba ya makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2015/16 iliyosomwa bungeni jana na Waziri wake, Dk. Asha-Rose Migiro, Lissu alimnukuu Rais akiwahakikishia wananchi siku ya maadhimisho  ya miaka 50 ya Muungano mwaka jana, kuwa Katiba ingepatikana mwaka huu.
 
Aliiponda kuwa iliandaliwa na wajumbe wa Bunge Maalum lililojaa mafisadi watuhumiwa  wa kashfa za Escrow, Richmond/Dowans, Operesheni za Tokomeza na  Kimbunga dhidi ya Watanzania waishio mipakani.“Ilipitishwa na kura zilizopigwa na wafu, mahujaji waliokuwa wanafanya Hijja wakimpiga shetani mawe katika Mlima Arafa, Saudi Arabia, wagonjwa waliolazwa hospitalini,” alisema Lissu.
 
Alisisitiza kuwa hii ni serikali iliyoshindwa japo CCM inadai kuwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) uliweka mpira kwapani na kuondoka uwanjani, lakini CCM licha ya kubaki na washirika wao wameshindwa.
 
KURA YA MAONI LINI?
Lissu alihoji ni lini kura ya maoni itafanyika na kwa kutumia sheria ipi?
 
“Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani, kama Tume ya Uchaguzi  itasajili wapiga kura nchi nzima, hakuna  na hakutakuwa na  uhakika wa kufanyika kwa kura ya maoni kuhalalisha katiba inayopendekezwa,” alisema.
 
Anasema kitakachokwamisha ni matakwa ya Sheria ya Kura ya Maoni ambayo imeweka utaratibu mgumu wa uendeshaji wa kura ya maoni, ambapo kila hatua inayotakiwa kuchukuliwa haiwezekani kuahirishwa wala kuongezewa muda.
 
 “NEC ilishaeleza kuwa Sheria ya Kura ya Maoni ina maeneo ambayo hayawezi kutekelezeka na baadhi yake kuwa na tafsiri zaidi ya moja yakiwamo uhesabuji wa kura ya maoni na utangazaji wa matokeo,” alisema na kuongeza:
“Suluhisho la changamoto hii ni  sheria ya Kura ya Maoni ifanyiwe marekebisho kwenye maeneo ambayo hayatekelezeki au kuwa na tafsiri zaidi ya moja.” Alisema na kuongeza kuwa hadi sasa serikali haijaleta muswada  wa marekebisho ya sheria hiyo ili kuwezesha kufanyika kwa kura ya maoni siku za usoni.
 
“Kama ilivyokuwa ahadi hewa ya kura ya maoni mwezi uliopita serikali inadanganya Watanzania kuwa kutakuwa na kura ya maoni katika mazingira ya sasa ya kisheria. Kwa sababu hiyo, huyu ni Waziri aliyeshindwa.”
 
UKATA SEKTA YA SHERIA
Akizungumzia bajeti finyu ya mahakama, alisema tishio kubwa kwa uhuru wa mahakama za Tanzania, sio kuingiliwa na wanasiasa na watendaji wakuu wa serikali bali ni serikali kuinyima fedha.
 
 “Tishio ni serikali kutumia udhibiti wake wa hazina ya taifa kuinyima mahakama rasilimali za kuiwezesha kutimiza wajibu wake kikatiba,” alisema.
 
Alisema hali hiyo imeaiathiri na kushindwa kutoa haki, kutatua tatizo la mrundikano mkubwa wa kesi na mashauri katika ngazi zote.
 
Alimnukuu Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani, akisema  madeni ya majaji kuwa  ‘“Ni vigumu kwa Jaji anayeishi kwenye  nyumba inayodaiwa kodi  kusikiliza na kutoa hukumu katika kesi za mwenye nyumba  na mpangaji. Lazima atoe boriti kwenye jicho ili aone kibanzi kwenye jicho la mwingine.”
 
Alisema  Mahakama ya Rufani ya Tanzania haijawahi kumiliki  jengo tangu ilipoanzishwa 1979 na imekuwa mpangaji wa Hoteli ya Forodhani.
 
HAKI ZA BINADAMU
Alisema haki za binadamu katika miaka mitano ya awamu hii imezidi kuwa mbaya akitaja  mauaji na mashambulio dhidi ya viongozi wa kidini na waumini kama  mauaji ya Padri Mushi  aliuawa Zanzibar.
 
Wengine Mapadre wawili wa kanisa hilo waliomwagiwa  tindikali pamoja na  msaidizi wa Mufti wa Zanzibar.
 
“Hakuna aliyetiwa hatiani wala kuadhibiwa kwa bomu katika Kanisa Katoliki Olasiti Arusha lililoua watu watatu na kujeruhi wengi.”
 
DEMOKRASIA
Aliituhumu serikali kwa kuzuia mikutano  halali ya vyama vya siasa vya upinzani na kuwashambulia kwa mabomu na risasi za moto. Watu wengi wameuawa katika mashambulizi hayo. Wengine wengi wamejeruhiwa.
 
 “Viongozi, wanachama na wapita njia  wamepigwa, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya jinai kwa kushiriki mikutano halali ya vyama vya siasa vya upinzani, “ alisema
 
RIPOTI YA CHRAGG
Alisema  jana Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG)  imetoa taarifa rasmi kwamba Jeshi la Polisi lilikiuka haki za binadamu na sheria za nchi wakati wa kuwakamata viongozi waandamizi wa Chama cha Wananchi (CUF) mapema mwaka huu.
 
Lakini pia jeshi hilo limeripotiwa kuua raia  na kujeruhi mwingine baada ya kudaiwa kukutwa wakinywa pombe baada ya saa nne usiku Mjini Njombe.
“Matokeo ya mauaji hayo, siku nzima ya jana (juzi) Njombe imefuka kwa moshi wa mabomu ya machozi na kurindima kwa milio ya risasi baada ya wananchi wa Njombe kupinga mauaji hayo kwa maandamano,” alisema.
 
MKOSAMALI: WENGI WATAUAWA UCHAGUZI MKUU 
Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), alieleza wasiwasi wa kuuawa watu wengi katika uchaguzi mkuu ujao kutokana na Serikali kushindwa kuzingatia haki za binadamu.
 
Hata hivyo, alisema pamoja na serikali kufikiri watatumia nguvu kufanikisha malengo yao, hawataweza kitu.
 
Mkosamali alisema kwa mwelekeo uliopo sasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, watu wengi watauawa.
 
“Kwa trend (mwelekeo) mliyonao, katika uchaguzi mkuu mtaua watu wengi sana.
 
Alisema: “sisi wapinzani mnatu-treat (tendea) kama vile ambavyo serikali ya kikoloni ilivyokuwa ikiwa treat Mwalimu Julius Nyerere na wenzake waliokuwa wakipigania uhuru wa taifa hili.”
 
“Mnatulaza kwenye vyoo, mahabusu na kutuweka rumande,” alisema na kuongeza: “Serikali iliruhusu kuwepo kwa vyama vingi vya siasa nchini, na vimeruhusiwa kisheria.”
 
Lakini alisema serikali imekuwa ikifanya mambo yanayodhoofisha au kuua upinzani.
 
Alisema kama polisi nchini wataacha kuzingatia utaratibu kwa mujibu wa kazi zao, wananchi watatumia nguvu au watatumia sheria mkononi.
 
Akizungumzia Bunge la Katiba Mpya lililomalizika mwaka jana na kupatikana na Katiba Inayopendekezwa, alisema haikupatikana kwa maridhiano.
 
Alisema hapakuwa na maridhiano kufikia kupata Katiba Inayopendekezwa huku akiishutumu serikali kwa kugombana na viongozi wa dini ili kufanikisha azma hiyo.
 
“Waziri gani umepingana na masheikh, maskofu…wote wanasema Katiba Inayopendekezwa haikuwa ya maridhiano, sasa mkishaipata hiyo katiba mtaridhiana vipi na viongozi hao wa dini?” alihoji.
 
Alisema viongozi wa serikali wamekuwa wakiwahadaa wananchi kwamba Katiba Inayopendekezwa imezingatia haki zao kama vile haki za wafugaji, wakulima au wanafunzi, lakini akahoji ni kifungu gani kimewekwa kwenye katiba hiyo kinachosema iwapo watakosa haki hizo basi wanaweza kuishtaki serikali mahakamani.
 
“Hakuna kifungu kinachomruhusu mfugaji, mkulima au hata mwanafunzi kama amekosa haki yake kwenda mahakamani,” alisema.
 
“Katiba ya Afrika Kusini ina kifungu hicho, kwa mfano, mwanafunzi akikosa kwenda chuo kwa sababu ya kukosa mkopo basi anaweza kuishtaki serikali mahakamani ieleze kwanini imeshindwa kumpatia mkopo wa elimu,” alisema na kuhoji: “Serikali gani hii?”
 
Alitoa mfano mwingine kwamba katika za nchi nyingi zimewapunguzia marais wao madaraka, lakini Bunge Maalum la Katiba halikuweza kufanya hivyo.
 
Alisema zamani nchi kama Zimbabwe, Afrika Kusini, Zambia na zingine zilikuwa zikija kujifunza hapa lakini zimefanikiwa kwa kutunga katiba zao kwa maridhiano.
 
Akizungumzia matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa ambao CCM inadai kushinda kwa asilimia 80, alisema uchaguzi huo maeneo mengi vijijini wagombea kutoka upinzani walinyanyaswa na kuwekewa mapingamizi.
 
JOSEPH SELASINI
Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), alitoa angalizo dhidi ya mahakama kutumika kisiasa.
“Mahakama zinatumiwa kisiasa na tukifika hapo wanataidharau mahakama…mahakama zinafanya kazi kukiridhisha CCM,” alisema.
 
Alisema kwa mfano, katika jimbo lake wapo wagombea wa Chadema walioshinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa, lakini wameshindwa kufanya kazi baada ya CCM kuwapeleka mahakamani na kwamba kesi zao mpaka sasa zimechukua muda mrefu kutolewa hukumu.
 
NGELEJA: TUSIIHUKUMU SERIKALI RIPOTI YA CAG
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, (CCM), alisema Serikali haijapata nafasi ya kujibu kuhusu tuhuma za ubadhirifu na ufisadi serikalini kama zilivyotolewa na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, (CAG), hivyo wananchi wasiihukumu serikali kwa hilo.
 
Alisema kiutaratibu ripoti ya CAG, Profesa Mussa Juma Assad, aliyoitangaza Jumanne, inapaswa kupelekwa kwanza kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ili wapate nafasi ya kuitolea majibu.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment