Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, May 12, 2015

Siku Rais Nyerere aliponyukana na IMF, Edwin Mtei akatoswa!


MWEZI Novemba mwaka 1979, Rais wa Awamu ya Kwanza wa Tanzania, Julius Kambarage Nyerere, alivua shati na kuvaa glovu [kiswahili kizuri, glavu] na kuingia ulingoni kuzichapa na Shirika la Fedha la Kimataifa [IMF] kwa kuipa nchi yetu masharti magumu ya mkopo wa dola za Kimarekani milioni 2000; kwa kutaka kuangamiza nchi.
Na kufuatia mnyukano huo, uliomwacha Nyerere akitweta kwa jasho na majeraha kiasi lakini mzima wa afya; ujumbe wa IMF uliondoka nchini hima bila kutazama nyuma.
Waziri wa Mipango na Fedha wa wakati huo na Gavana wa kwanza mzalendo wa Benki Kuu [BOT], Edwin Mtei, na ambaye ni miaka miwili tu alikuwa ameshika wadhifa huo, akitokea Jumuiya ya Afrika Mashariki [EAC] iliyovunjika, ambako alikuwa Katibu Mkuu wake; ilibidi aachie ngazi kwa mkuku kwa kushangilia upande wa IMF.
Kukataliwa kwa masharti ya IMF kulitanguliwa na majadiliano makali kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri chini ya Uenyekiti wa Rais, ambapo masharti hayo ya mkopo ya IMF yaliyowasilishwa na Mtei ili yajadiliwe na kama sehemu ya juhudi za “kuokoa” uchumi wa nchi ulioparanganyika.
Mtei alikuwa ameridhiana na IMF juu ya mkopo huo na masharti yake, ambayo yalitaka mambo matano kutekelezwa: sharti la kwanza lilitaka nchi ipunguze thamani ya fedha yake; Pili, kuongeza viwango vya riba ya Benki kwa mikopo na wakopaji ili kuzuia ukopaji usio wa lazima.
Tatu, kupunguza Matumizi ya Serikali; Nne kudhibiti au kuondoa kabisa ruzuku kwa bidhaa na mahitaji ya msingi kwa umma, kama vile matibabu, bidhaa za msingi kwa mlaji, elimu, pembejeo na zana za kilimo, na mengine.
Tano, IMF lilitaka kufutwa kwa Tume ya Kudhibiti bei [Price Control Commission] ili kuruhusu nguvu ya soko itawale na kuweka bei
Rais Nyerere, kwa kuudhika na shinikizo hilo, hakuwa tayari kumeza vidonge hivyo vyenye sumu kwa taifa na watu wake.
Na siku ujumbe wa IMF ulipoondoka nchini bila kutazama nyuma, Mwalimu alihutubia Wafanyakazi wa Kiwanda kilichojengwa na Wachina cha Zana za Kilimo, Ubungo [Ubungo Farm Implements] – UFI, akasema: “Wale wanaodhani Tanzania itabadili sera yake ya Ujamaa na Kujitegemea kwa sababu ya matatizo yetu ya sasa ya kiuchumi wanapoteza muda wao, hatutabadili sera hiyo”.
Katika kikao cha Baraza la Mawaziri, Mtei alikuwa amejenga hoja kwamba, kupunguza thamani ya fedha ya Tanzania [shilingi] kulikuwa na manufaa mengi, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa uagizaji bidhaa kutoka nje na kuhamasisha uuzaji nje.
Kwamba, kwa kawaida, hatua kama hiyo husababisha gharama za kuagiza bidhaa kutoka nje kupanda na hivyo uagizaji huo na waagizaji kujidhibiti wenyewe; na kwa kufanya hivyo bidhaa zinazouzwa nje huwa rahisi na kuongeza kuhitajika kwake katika Soko la Dunia na kuuzika haraka.
Hata hivyo, dhana hii inapata upinzani mara nyingi kutoka kwa wachumi na uzoefu wa nchi nyingi kwamba, ongezeko la bei ya bidhaa kutoka nje na kushusha thamani ya fedha pekee haihakikishii nchi kwamba bidhaa kutoka nje zitadhibitiwa.
Ukatolewa mfano kwa Tanzania yenye viwanda tegemezi kwa malighafi kutoka nje, kwamba ilikuwa bado ni lazima tu kuagiza malighafi hizo; na kwamba, kilichotakiwa ni kubaini na kuweka kipaumbele kwa kile muhimu tu kwa matumizi ya Watanzania na kwa uchumi wa nchi ili kulinda akiba ndogo ya fedha za Kigeni iliyokuwepo.
Wakati huo, viwanda vya nchini, ambavyo karibu vyote vilimilikiwa na serikali, vilikuwa vimeomba jumla ya shilingi bilioni 5.092 ili viweze kujiendesha; lakini serikali ilikuwa na uwezo wa shilingi bilioni 1.294 pekee.
Na ile hoja ya Mtei ya kushusha thamani ya fedha [shilingi] ili bidhaa za Tanzania ziweze kushindana katika soko la dunia; swali lilikuwa: je, tulikuwa na kingi cha kuuza nje?.Kingetoka wapi? Nini madhara ya kuingia kichwa kichwa kwa jambo hilo kwa umma masikini wa Kitanzania?.
Na kuhusu riba kubwa, Mwalimu Nyerere alishikilia kuwa, kwa kuwa viwanda vingi vilikuwa mali ya serikali, ongezeko la riba lingeongeza gharama kwa serikali ambazo ingebidi zilipwe na walaji kwa njia ya ongezeko la bei za bidhaa.
Wakati huo, bei za bidhaa nchini zilidhibitiwa na Tume ya Bei ambayo haikufurahia pendekezo la Waziri Mtei na watetezi wengine wa sera za IMF na Benki ya Dunia [WB].
Msimamo wa mwisho wa Nyerere, mtu mwenye hekima na aliyeipenda nchi na watu wake kuliko kitu kingine; ulikuwa kwamba, kuongeza riba kwa mikopo na kushusha thamani ya fedha kungeongeza ugumu wa maisha kwa Watanzania.
Kwamba kupunguza matumizi ya serikali kwa kuondoa ruzuku kwa vitu muhimu kwa wananchi na kwa uchumi wa nchi, kungesababisha mgando wa mishahara kwa wafanyakazi na hivyo kulazimisha zoezi la kupunguza watumishi; kupanda kwa bei za pembejeo na zana za kilimo na hivyo gharama za uzalishaji kwa mkulima mdogo; zaidi kwamba, kile ambacho angezalisha kisingeweza kupenya Soko la Dunia kwa sababu ya bei yake kubwa hivi kwamba mkulima huyo angelazimika kukubali bei duni ili mradi tu auze kile alichozalisha kwa bei kubwa.
Kwa haya yote, Mwalimu alihofia machafuko ya kijamii kama yangetekelezwa. Alikumbuka na kuingiwa hofu zaidi juu ya machafuko na maandamano kama hayo ya Januari 1978 nchini Misri, pale Rais Anwar Sadat wa nchi hiyo alipokubali mkopo kutoka IMF wenye masharti kama hayo, na hatimaye kuuawa kutokana na ghadhabu ya umma kwa kupigwa risasi wakati akiangalia gwaride la jeshi lake.
Kilichomponza Sadat ni pale alipokubali masharti ya IMF na kuipiga teke sera ya Ujamaa na Kujitegemea, iliyoanzishwa na mtangulizi wake, Rais Gamal Abdul Nasser, kwa ubinafsishaji usiojali na kwa kasi ya kutisha chini ya Mpango aliouita “Economic Crossing Plan” [ECP] na kuweka uchumi mikononi mwa sekta binafsi na ubepari wa kimataifa, kwa kushirikiana na “Wazalendo” wasaliti wa umma kuhodhi uchumi huo na maamuzi ya nchi.
Nyerere akakosa usingizi; kwa wiki nzima kufuatia kujiuzulu kwa Mtei, aliweza kubuni na kuweka mkakati mpya wenye njia mbili: Kwanza, Serikali kudhibiti uagizaji wa bidhaa kutoka nje; akaiagiza Benki kutoa Leseni za Uagizaji malighafi muhimu tu kwa ajili ya viwanda vya ndani vilivyohusu kilimo, uzalishaji wa bidhaa muhimu na za msingi kwa mlaji, bidhaa kwa ajili ya kuuza nje na kwa ajili ya Sekta ya Uchukuzi.
Pili alielekeza serikali kupitia upya malengo yake kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara kwa ajili ya soko la nje na chakula, katika kipindi ambacho nchi ndiyo tu ilikuwa imetoka kwenye vita kwa gharama kubwa, ya kumng’oa “Nduli” Idi Amini wa Uganda aliyevamia nchi yetu mwaka 1978.
Chini ya Mpango wa “Kilimo cha Kufa na Kupona”, tuliweza kuzalisha chakula cha kutosha kwa matumizi ya ndani na ziada kuweza kuuza nje. Kwa upande wa mazao ya biashara hata hivyo, mapato yaliendelea kuathiriwa na bei duni katika Soko la Dunia.
Nyerere aipigia magoti IMF
Kwa nchi masikini kama Tanzania, kushindana na IMF ilikuwa ni sawa na kijana Daudi wa Biblia, kutangaza vita isiyoisha na mpiganaji pandikizi lenye nguvu na silaha kali, Goliath wa Wafilisti; au kwa ngano za Wasukuma na Wanyamwezi, kwa kijana Masalakulangwa kupambana na mnyama pandikizi, “Shing’weng’we”, lililoweza kumeza watu wa kijiji kizima lisioneshe kumeza kitu.
Kwa hiyo, miezi minane baadaye, hapo Juni 1980, Nyerere alijikuta uso kwa uso tena na IMF; safari hii akiomba msaada kwa unyenyekevu, baada ya nchi tisa za Magharibi – Marekani, Uingereza, Shirikisho la Ujerumani, Netherland, Sweden, Denmark, Norway, Canada na Japan,kususia kufadhili dola za Kimarekani milioni 375 za Maendeleo kwa njia ya mkopo, kwa sababu tu ya Mwalimu Nyerere kukataa masharti ya IMF, Novemba 1979.
Vita vya kumng’oa Nduli Idi Amin viliiacha nchi hoi kiuchumi na hivyo kulazimisha kuahirisha baadhi ya miradi ya maendeleo, kuathirika kwa nyenzo za usafiri na zaidi, na kudhoofisha kwa uwezo wa nchi wa kuuza bidhaa nje.
Nyerere alibainisha kuwa, hata bila vita, bado nchi ingepungukiwa zaidi ya Shs. 582m na pamoja na vita, shimo katika uchumi wa Taifa lilifikia dola za Kimarekani milioni 4,283.
Wakati huohuo, Marekani na Uingereza, ambazo hapo mwanzo ziliahidi kugawana gharama za vita ya kumng’oa Nduli Idi Amin, zilikataa ghafla kufanya hivyo bila matarajio.
Zaidi ya hayo, hali ya Usalama nchini Uganda kufuatia vita, ilikuwa haijawa ya kuridhisha hivi kwamba Nyerere alilazimika kuelekeza sehemu ya Jeshi la Tanzania kuendelea kubakia huko kwa gharama kubwa.
Na kana kwamba hilo halikutosha, Uganda ilikuwa haijapata mikopo na ufadhili iliotarajia kutoka mataifa makubwa ya Magharibi na kuzua hali tete kiuchumi na kijamii.
Nyerere awa IMF mwema
Kwa hiyo, Nyerere, pamoja na umasikini wa nchi yake, alilazimika kuipa kwa kuikopesha Uganda shilingi milioni 100 kwa mwezi ili iweze kununua bidhaa kutoka Tanzania, kama vile sukari, unga, mafuta na majembe na kuifanya nchi na Nyerere kuwa IMF nyingine kwa Uganda.
Mgogoro kati ya Mwalimu Nyerere kwa upande mmoja na IMF na Edwin Mtei kwa upande wa pili, ulijengeka wakati huo kwenye mawazo kinzani, kati ya kambi ya ubepari wa Magharibi, na kambi ya Usoshalisti wa Mashariki ulioelekea kufikia kilele cha mnyukano wa kumalizana ili moja kati ya kambi hizo iweze kutawala mfumo wa uchumi wa dunia.
Wakati Mtei na IMF wakitenda kwa ushawishi wa mawazo ya wachumi wahafidhina wa ubepari wa Magharibi kama P. T. Bauer, kwamba kwa serikali kupanga uchumi na kusimamia utekelezaji wake pamoja na soko ni kuua ufanisi na tija; Nyerere kwa upande wake, kwa kuongozwa na kufanyia kazi mawazo ya wachumi wa Kimataifa wa sera za Maendeleo vijijini kama Rene Dumont, aliona kuwa uchumi uliopangika na kusimamiwa na serikali kwa niaba ya wananchi ambao ndio walengwa wa uchumi huo, ilikuwa ndio njia pekee ya kufikia maendeleo ya kweli.
Ukweli, Nyerere aliagiza kila waziri asome kwa rejea, kitabu cha Rene Dumont, “False Start in Africa [Afrika Inakwenda Kombo] kuelewa nini kilichotakiwa kwa maendeleo kwa nchi za Dunia ya Tatu kama Tanzania.
Aliona, bila kupanga na kusimamia uchumi wa nchi, kungeruhusu mamlaka ya serikali kunyakuliwa, kutumikia, kunufaisha na kulinda matakwa ya kikundi kidogo kwa “maangamizi” ya mwananchi wa kawaida.
Awamu hii ya pili ya Nyerere uso kwa uso na IMF, ilikuja wakati Benki ya Dunia [WB] ilikuwa imeungana na IMF kuweka msimamo kuisigina Afrika kiuchumi kupitia Ripoti ya Tume ya Benki hiyo, iliyoongozwa na Mchumi Dk. Elliot Berg, iitwayo “Accelerated Development in Sub-Saharan Africa: AN Agenda for Action”.
Kwa ripoti hiyo, mashirika hayo ya Brettonwoods, yaliweka wazi kuwa, uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi masikini za Dunia ya Tatu na nchi za Dunia ya Kwanza, utategemea nchi hizo masikini kukubali kikamilifu masharti ya IMF.
Mwaka mmoja baada ya Mwalimu kung’atuka madarakani hapo mwaka 1985, Tanzania chini ya Uongozi wa Awamu ya Pili ya Ali Hassan Mwinyi, iliingia makubaliano [1986] na IMF juu ya “kufufua uchumi” wa Tanzania.
Mwaka 1992, Azimio la Arusha lilipinduliwa na Azimio la Zanzibar; ubinafsishaji ukaanza na kukua kwa kasi ya kutisha kiasi kwamba, Mwalimu, akiwa ameumia moyoni, alilazimika kutahadharisha akisema, “Msipojihadhari, mtabinafsisha hata Magereza”.
Je, ubinafsishaji huo umeleta manufaa gani kwa mwananchi wa kawaida leo?.Je, kama Nyerere angetawala hadi sasa, angeruhusu hali hii? Je, angeshinda vita ya uchumi kama Korea Kaskazini, tuliyoanza nayo mwaka mmoja [1967], safari kuelekea Ujamaa?.


No comments :

Post a Comment