dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, May 28, 2015

Wabunge 42 kulamba Sh3.3 bilioni kwa mwaka

 Katika Bunge Maalumu la Katiba, wajumbe wengi hasa kutoka CCM, walipinga pendekezo hilo kwa maelezo kwamba ni gharama kuendesha serikali tatu katika nchi maskini kama Tanzania na kwamba pendekezo hilo lililenga kugawana vyeo tu na si kuimarisha utendaji.
Dar es Salaam. Kipindi kama hiki, mwaka jana kulikuwa na mnyukano mkubwa wa maoni kuhusiana na pendekezo la Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwamba muundo wa Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar uwe wa Serikali tatu.
Katika Bunge Maalumu la Katiba, wajumbe wengi hasa kutoka CCM, walipinga pendekezo hilo kwa maelezo kwamba ni gharama kuendesha serikali tatu katika nchi maskini kama Tanzania na kwamba pendekezo hilo lililenga kugawana vyeo tu na si kuimarisha utendaji.
Lakini safari hii, madiwani na wabunge wengi wa CCM wako mstari wa mbele kuridhia pendekezo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), la kuongeza gharama za uendeshaji wa Bunge kwa kuongeza majimbo 42.
Nyongeza hiyo ina maana kwamba wabunge wataongezeka pamoja na mishahara yao, posho, fedha za mfuko wa jimbo na hata kiinua mgongo. Kiasi cha jumla ya Sh3.382 bilioni kitaongezeka kila mwaka kwa ajili ya kugharamia wabunge hiyo ikiwa ni mbali ya mafao yao baada ya ubunge.
Mshahara wa mbunge mmoja pamoja na matumizi mengine madogomadogo ni jumla ya Sh11 milioni. Hivyo, kwa miezi 12 mbunge mmoja atalipwa Sh132 milioni na kwa wabunge 42 itakuwa Sh554 milioni.
Kila mbunge atakuwa akilipwa Sh80,000 ikiwa ni posho ya kujikimu anapokuwa nje jimbo lake, posho ya kikao Sh200,000 na posho ya mafuta ya gari Sh50,000 jumla ni Sh330,000 kwa siku.
Posho hizo akilipwa akiwa kwenye vikao vya Bunge; siku 56 za Bunge la Bajeti mjini Dodoma; siku 14 kikao cha Februari; siku 14 za vikao vya Kamati za Bunge jijini Dar es Salaam; siku 14 kikao cha Oktoba jumla ya siku 98, atalipwa Sh32,340,000. Malipo kwa wabunge 42 yatakuwa Sh1.35 bilioni.
Aidha, kila mbunge ana mfuko wa jimbo wa kati ya Sh35milioni na Sh45milioni kulingana na ukubwa wa jimbo, kwa ajili ya maendeleo ya jimbo lake. Hivyo, ikiwa kila mmoja atapewa wastani wa Sh35milioni katika jimbo, kwa wabunge hao 42 itakuwa Sh1.47 bilioni.
Kwa hiyo, bila kuingiza posho za safari za ndani au nje akiwa na kamati ya Bunge, misamaha ya kodi, mafao na posho za semina, kwa mwaka wabunge hao wapya watatumia Sh3.38 bilioni.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema tume imezingatia vigezo vya idadi ya watu, upatikanaji wa mawasiliano, hali ya kijiografia na vigezo vingine kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa rais na wabunge ya mwaka 2010.
Maoni ya wadau
Katibu Mkuu wa NCCR - Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema ongezeko la majimbo hayo halitakuwa na tija yoyote na badala yake yataongeza mzigo kupitia uchangiaji wa bajeti ambazo ni kodi za Watanzania.
Kada mwingine wa chama hicho, Samwel Ruhuza alisema hali hiyo itafanya nchi ishindwe kujiendesha... “Mpaka sasa tunao wabunge 357 lakini angalia ni wangapi wanaochangia mada na kujenga hoja bungeni hata robo ya hao hawafiki.”
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Alexander Makulilo alionya kwamba wakati NEC inafikiria kuongeza majimbo, ni vyema ikazingatia uchumi wa nchi na manufaa ya majimbo haya kwa mwananchi mmojammoja.
Mhadhiri wa chuo hicho, Bashiru Ally alisema NEC imefanya uamuzi sahihi kwani imepewa mamlaka ya kupitisha majimbo mapya kulingana na vigezo vilivyopo.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Zarina Madabida alisema takwimu za idadi ya watu zinapaswa kuangaliwa kabla ya kuipelekea NEC kugawanya majimbo.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alieleza kushangazwa na watu waliokuwa wanapinga serikali tatu katika Bunge la Katiba kwa kigezo cha gharama, kuwa leo ndiyo wanaotaka majimbo yaongezeke bila kujali gharama.
Mfanyabiashara Masoud Ally wa Dar es Salaam alisema: “Ugawaji wa majimbo utagharimu fedha nyingi za Taifa wakati kuna mahitaji makubwa.
Kauli ya NEC
Mkurugenzi wa NEC, Julius Malaba alisema madai hayo hayana tija kwani siyo kila aliyeomba jimbo atapata.
Malaba alisema si sahihi kulalamikia mchakato huo wakati Tume haijapokea hata mapendekezo ya majimbo.
“Watanzania wanatakiwa kusubiri kwanza tupokee mapendekezo ya kuongeza majimbo, tugawanye kwa vigezo vilivyopo halafu ndipo wapime hoja zao lakini siyo sahihi kuibua umuhimu wa kuongeza majimbo kiuchumi au kuhofia upendeleo,” alisema Malaba.
Mgawanyo wa Dar
Mkoa wa Dar es Salaam umependekeza majimbo mapya matano ya Mbagala, Kijichi, Kibamba, Bunju na Chanika yaliyopitishwa juzi katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na kufanya jumla ya majimbo 13 kutoka manane ya sasa.
Mbeya wagoma
RCC ya Mbeya imetupilia mbali maombi matano ya mapendekezo ya kugawa majimbo yaliyowasilishwa na halmashauri saba kutokana na kutokidhi kigezo cha idadi ya watu. Majimbo ya uchaguzi yaliyopendekezwa katika kikao cha dharura cha RCC kilichofanyika jana ni Halmashauri ya Mbeya, Momba, Mbozi, Kyela, Jiji la Mbeya, Rungwe na Mbarali na yaliyokataliwa ni Rungwe, Mbarali, Kyela na Jiji la Mbeya.
Rukwa waridhia
Wadau wa Maendeleo mkoani Rukwa, wameridhia kugawanywa majimbo ya mawili ya Kwela na Kalambo.
Tanga bado
Mapendekezo ya kuongezwa majimbo ya Mkoa wa Tanga kutoka 11 hadi kufikia 17 yaliyowasilishwa RCC yamepitishwa kwa shaka baada ya baadhi ya wajumbe kudai ni mengi mno. Maombi yaliyowasilishwa ni ya Handeni Mjini, Handeni Vijijini, Tanga Kaskazini, Tanga Kusini Korogwe Mashariki na Korogwe Magharibi, Muheza Mjini na Muheza Vijijini huku Mlalo ikitakiwa igawanywe kuwa Mtae na Umba.
Imeandikwa na Burhani Yakub, Brandy Nelson na Justa Mussa, Mussa Mwangoka na Harieth Makwetta.

No comments :

Post a Comment