
Angalizo hilo lilitolewa na Mchungaji wa Kanisa la Renuel Healing Ministry, Alphonce Temba, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Alisema ijapokuwa serikali ya Tanzania haifungamani na dini yoyote, lakini si vema kusahau kuwa zipo hisia na tamaduni zimejengeka kwa Watanzania kuwa viongozi wanaoshika madaraka ya dola nchini hupokezana kutoka miongoni mwa dini hizo kuu mbili na kwamba, kwa sababu hiyo, anayepaswa kuteuliwa sasa kuwania nafasi hiyo anapaswa kuwa Mkristo.
Rais Jakaya Kikwete kutoka CCM anayemaliza vipindi viwili vya uongozi baada ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu ni Muislamu. Watangulizi wake, Rais Benjamin Mkapa wa awamu ya tatu ni Mkristo; Ali Hassan Mwinyi wa awamu ya pili ni Musilamu na rais wa awamu ya kwanza, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni Mkristo.Mchungaji Temba alisema kwa kuwa Watanzania wamezoea utaratibu huo wa kupeana zamu za kuongoza taifa (ijapokuwa haujaandikwa mahali popote), ni vizuri ukazingatiwa katika kipindi hiki ambacho Tanzania itapata rais wake wa awamu ya tano mwaka huu ili kuleta uwiano mzuri baina ya pande hizo mbili.
Aliongeza kuwa ni vizuri Rais Kikwete akasimamia jambo hilo na kuhakikisha kuwa utaratibu huo unazingatiwa hata kama hautambuliki kwa kuhakikisha kuwa rais anaiyemfuatia anakuwa Mkristo.
“Kama mnavyofahamu, taifa letu hivi sasa liko katika mhemko mkubwa wa kisiasa. Miongoni mwa vyama vilivyotia fora ni pamoja na CCM kutokana na wanachama wake kujitokeza kwa wingi kutafuta kuteuliwa kuwania nafasi ya urais kwa kuwa ni chama kikubwa, kinachoheshimika na chenye uzoefu wa kuongoza nchi kwa muda mrefu, (na) kinachoangaliwa na kupewa nafasi kubwa ya kushinda... ni vema kikazingatia utaratibu wa zamu za kuachiana madaraka katika dini hizo kubwa mbili,” alisema Mchungaji Temba.
Aliongeza:“ Pamoja na CCM kupewa nafasi hiyo kubwa, kuna mambo yameanza kujitokeza ndani ya chama hicho ambayo yanaibua maswali mengi kwamba huenda mambo yasiwe sawa. Hofu hiyo inaibuka kwa sababu katika siku za hivi karibuni, kuna watu ndani ya chama hicho wamejitokeza, na ambao wanaelekea kuvuruga uwezekano wa kutumika kwa utaratibu huo (wa kupeana zamu).”
Alisema ni vema suala la zamu likaheshimiwa kwa kuwa ndiko ndilo linaloimarisha amani, umoja na kuheshimiana miongoni mwa Watanzania bila kujali tofauti zao za kiimani.
“Yapo maneno ya chini chini ambayo yameanza kuzungumzwa juu ya hofu hii. Lakini mimi nimeona badala ya kuzungumza kwa chini chini, ni bora niwe wazi kulisema hili kwa sababu kwa sasa bado hakujapatikana uvumilivu ndani ya pande mbili za Waislamu na Wakristo, wa kuvumiliana kuona wanaongozwa na mtu wa dini moja vipindi vyote bila kubadilishana,” alisisitiza Mchungaji Temba.
Kamati Kuu (CC) ya CCM itakutana Julai 12, mwaka huu kuwachuja wagombea na kubaki na majina matano ya kupeleka mbele ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho ili mwishowe apatikane mgombea ataayechuana na vyama vya upinzani kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25.
WALIOJITOSA URAIS CCM
Miongoni mwa makada wa CCM 36 waliojitokeza kutaka wateuliwe kuwa wagombea wa nafasi ya urais ndani ya CCM hadi kufikia jana ni Makamu wa Rais, Dk. Muhamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta; Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira na Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk. Titus Kamani.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi Maalum, Prof. Mark Mwandosya; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha-Rose Migiro.
Pia wamo Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu; Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Wengine ni Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja; Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa Sospeter Muhongo; Maliki Marupu; Joseph Chagama; Makongoro Nyerere; Mwale Malecela; Monica Mbega; Balozi Ali Karume, Balozi Amina Salum Ali, Balozi Augustine Mahiga na Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani.
CHANZO: NIPASHE

No comments :
Post a Comment