Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, June 7, 2015

Ikiwa Muungano unavunjika, tutaingia vitani?

Julius Mtatiro 
Hoja yangu ya kwanza inajikita katika chimbuko la muungano. Baada ya kuwasoma watalaamu mbalimbali, binafsi nimefikia hitimisho kubwa kuwa chimbuko la Muungano ni Usalama wa Tanganyika na Zanzibar ambapo marais wa kwanza wa Jamhuri ya Zanzibar na ya Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume, kila mmoja kwa uzito wake aliona kuwa usalama wa nchi yake uko hatarini aidha kwa kutishwa na uwepo wa ukaribu wa kijiografia ama uwepo wa vitisho vya ndani ya nchi husika.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964, uliozaa Tanzania ya sasa uko shakani. Waandishi na wataalamu wa sheria na katiba na wataalamu wa tamaduni na masuala ya ushirikiano wa kimataifa, wamekuwa wakifanya uchambuzi juu ya muungano wetu kwa kuonyesha nadharia mbalimbali. Wameonyesha takwimu na ushahidi wa kila aina juu ya kuungana na athari za kutoungana. Wamekuwa wakitumia taaluma zao kuchanganua miundo mbalimbali ya muungano na kuonesha hali ya muungano wetu wa sasa.
Uchambuzi wangu utajikita katika kuonesha athari za muungano wa Tanganyika na Zanzibar, iwapo utavunjika.
Hoja yangu ya kwanza inajikita katika chimbuko la muungano. Baada ya kuwasoma watalaamu mbalimbali, binafsi nimefikia hitimisho kubwa kuwa chimbuko la Muungano ni Usalama wa Tanganyika na Zanzibar ambapo marais wa kwanza wa Jamhuri ya Zanzibar na ya Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume, kila mmoja kwa uzito wake aliona kuwa usalama wa nchi yake uko hatarini aidha kwa kutishwa na uwepo wa ukaribu wa kijiografia ama uwepo wa vitisho vya ndani ya nchi husika.
Kwa upande wake Mzee Karume alikuwa na kitisho kikubwa cha ndani. Pamoja na kuwa kiongozi wa juu wa Zanzibar, siyo kwamba alitosheleza matarajio ya Wazanzibari, la hasha! Palikuwa na malalamiko ya hapa na pale dhidi yake na hata baadhi ya watu waliofanya mapinduzi pamoja naye walianza kutofautiana naye baada ya muda si mrefu.
Karume aliona kuwa nguvu ya wanaompinga ikiwa kubwa zaidi bila shaka na yeye angepinduliwa na mapinduzi yangezaa mtoto ambaye bila shaka naye angekuwa mapinduzi. Karume aliona namna pekee ya kujikinga na kuulinda utawala wake ni kushikamana na Tanganyika kufa na kupona.
Baadhi ya taarifa zisizothibitika zinaeleza kuwa Rais Karume awali alitaka Tanganyika na Zanzibar ziwe nchi moja na Mwalimu Nyerere awe Rais huku Karume akiwa Makamu wa Rais, duru hizo zinaeleza kuwa Mwalimu Nyerere alikataa wazo hilo kwa kuona kuwa likifanyika, Zanzibar itamezwa na Tanganyika kutokana na udogo wake kijiografia na aliona kwamba njia ya pekee ni kuiachia Zanzibar mamlaka kadhaa ili ijiendeshe yenyewe ikiwa ndani ya muungano. Pamoja na duru hizo, ukweli unabakia kuwa mara tu baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar Mzee Karume alianza kumlalamikia Nyerere juu ya tabia ya Mwalimu kujilimbikizia baadhi ya madaraka ambayo hawakukubaliana.
Mzee Salim Hemed Hamis wa Zanzibar, ambaye amewahi kuajiriwa katika moja ya majeshi ya ulinzi na usalama na kufanya kazi Zanzibar na Tanganyika, ameniambia kuwa, wakati Nduli Iddi Amin (Dada) alipoleta chokochoko zake, Mwalimu Nyerere akiwa Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Ulinzi na Usalama wa Tanzania alitoa amri wanajeshi wapelekwe mpakani mwa Tanzania na Uganda. Upande wa Zanzibar wakuu wa majeshi walitekeleza agizo hilo. Mara Mzee Karume akajulishwa juu ya uamuzi wa Mwalimu. Mzee Karume akaona ya kwamba Mwalimu hakumshirikisha na hakumtendea haki, inasemekana Mzee Karume alitoa amri juu ya amri na akasitisha mpango wa Mwalimu wa kuwapeleka askari wa Zanzibar na vikosi vyake vitani. Huu ni uthibitisho mwingine kuwa Mzee Karume na Mwalimu Nyerere walikuwa na migogoro mingi mara baada ya kuwa katika muungano na kila mmoja wao kupata alichotaka.
Kwa upande wa Mwalimu Nyerere, wachambuzi wanaonesha kuwa yeye aliiona jamhuri ya Zanzibar kama kitisho kikubwa kwa usalama wa Tanganyika. Mwalimu aliona kuwa ikiwa mivutano yoyote itatokea Zanzibar lazima Tanzania itaathirika, alitambua vitisho vya usalama vinavyokabili Zanzibar kutoka ndani na nje ya nchi hiyo na aliona kuwa usalama wake upo mashakani. Kwa kuzingatia kuwa usalama wa Zanzibar ukiwa mashakani na Tanganyika itaathirika sana, Mwalimu aliona muungano ndiyo njia pekee ya kuondoa kitisho hicho.
Mwalimu alijua Zanzibar ikiwa karibu na Tanganyika kiuongozi itapelekea Tanganyika kuwa na uhakika na usalama wake. Kuna wakati Mwalimu Nyerere amewahi kusikika akisema “ningekuwa na uwezo ningevichukua visiwa vile na kuvipeleka mbali sana”. Mwalimu anaonesha kuwa visiwa vile si salama kwa utawala wake na hapa tusimdharau wala kumkebehi, Mwalimu hakuwa mtoto mdogo, alifikiri sawasawa na alijua hasa nini anamaanisha kiusalama.
Pamoja na maono hayo ya mwalimu wakati huo, lazima tukubali kuwa nyakati zinabadilika sana na kila nyakati zina namna ya kushughulikia changamoto zake, taifa la sasa (au mataifa yetu mawili) hayafungwi na mipango na maono ya Mwalimu Nyerere, kama wakati ulen hakuwa na teknolojia za kulinda mipaka hivi sasa zipo, hizi ni nyakati ambazo unaweza kuishi na jirani akafanya kirtendo kibaya ukawa unamuona kwenye vitunza kumbukumbu vya kisasa, ndiyo maana nataka kusisitiza kuwa pamoja na uzito wa Muungano na changamoto zake ni lazima sasa wataalam wa masuala haya waanze kutufanyia uchambuzi huru bila kututisha, lengo liwe ni mwisho wa siku waje watushauri namna bora ya kuuenzi muungano ambao utakubaliwa na wananchi wa pande zote mbili.
Uchambuzi wa leo utuweke katika tafakuri pana ya muungano wetu, na wiki ijayo ntaongelea juu ya ikiwa sababu zilizounganisha Tanganyika na Zanzibar bado zipo na katika andiko la tatu ntahitimisha hoja yangu kwa kuonesha hasa ni muungano wa aina ipi unapaswa kusisitizwa ili nchi yetu izidi kutamalaki kitaifa na kimataifa.
(Julius Mtatiro ni kiongozi mzoefu, ana shahada ya Uzamili (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (L LB): +255787536759, juliusmtatiro@yahoo.com).

No comments :

Post a Comment