AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, July 3, 2015

Bunge latibuka.

  Spika alazimika kulisitisha kwa muda, Ni baada ya wapinzani kugomea miswada ya petroli, gesi kusomwa kwa hati ya dharura.

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika.
Kwa mara nyingine tena Bunge lilichafuka jana na kulazimika kuahirishwa kwa muda baada ya wabunge wa upinzani kugomea nia ya kuruhusu miswada mitatu ya mafuta na gesi, kuingizwa bungeni na kujadiliwa kwa hati ya dharura.
 
Kikao hicho cha 41 kilishindwa kuendelea baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, pale Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alipoomba mwongozo baada ya kukabidhiwa orodha ya shughuli za jana, ambayo alisema imekiuka kanuni za Bunge kwa kuweka miswada mitatu kwa ajili ya majadiliano.
 
Miswada hiyo ni wa sheria ya Petroli, usimamizi wa mapato ya mafuta na gesi na wa sheria ya uwazi na uwajibikaji katika tasnia ya uchimbaji Tanzania; yote ya mwaka 2015.
 
HALI ILIVYOKUWA
Mnyika aliomba muongozo huo kwa kutumia kifungu cha 53(6), masharti ya uwasilishaji wa hoja kama hiyo bungeni, na kanuni ya 86 inayoeleza siku ambayo muswada uliokwisha kujadiliwa na kamati umepangwa kwenye orodha ya shughuli, Waziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwenyekiti wa Kamati au Mbunge mwenye muswada husika atawasilisha hoja kwamba muswada wa sheria kusomwa mara ya pili."Kipindi cha uhai wa Bunge hili na miswada iliyowahi kuja, hoja ikishatolewa ni lazima ijadiliwe iamuliwe ndiyo ije nyingine, hapa tumeletewa orodha yenye hoja juu ya hoja kwa vyovyote haipaswi kukubalika bali kuondolewa, "alisema na kuongeza:  
 
"Uamuzi wa kuileta miswada hii kwa hati ya dharura umekiuka kabisa msingi wa mwelekeo wa makubaliano kwenye semina iliyofanyika Juni 30, mwaka huu, wabunge kwa wingi walikataa miswada hiyo isiletwe kwa hati ya dharura na utaratibu huu." alifafanua na kuongeza:
 
"Naomba mwongozo wako na naomba usiseme utautoa wakati mwingine, ndiyo mana sikutaka kusema tangu mwanzo, kwa sababu ukisema wakati mwingine huku shughuli zikiendelea kuharibika ni jambo lisilokubalika, tunahitaji majibu sasa, kwanini tuendelee na 'order paper' iliyokiuka kanuni na makubaliano ya wabunge."
 
Aidha, Spika Anne Makinda, alihamaki na kumtaka Mnyika kufuta kauli zenye kumwamrisha ndipo aweze kutoa mwongozo juu ya jambo hilo.
 
Baada ya Mbunge huyo kuondoa kauli hiyo, Spika Makinda alisema hakuna mtu yeyote anayeweza kumwamrisha na kwamba kanuni zipo sahihi na zimefuatwa hivyo upinzani wanatumia kanuni kudanganya umma.
 
"Katika kamati ya uongozi iliyokutana juzi ambayo Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde, alikuwapo tulikubaliana sisi (kamati ya uongozi) siyo wataalamu, leo Waziri awasilishe muswada wa kwanza, kamati na upinzani wawasilishe maoni yao, usomwe muswada wa pili," alitoa ufafanuzi ambao ulizua kelele bungeni.
 
Baada ya maelezo hayo, zilizuka kelele na Makinda aliwataka waamue wenyewe huku akisisitiza kuwa hakuna kanuni iliyovunjwa.
 
 Palizuka kelele nyingine huku wengine wakirusha maneno kuwa tokeni nje, lakini wapinzani walisisitiza hakuna wa kutoka, hali iliyosababisha kutokusikikizana na Spika kutangaza kuhairisha Bunge huku wabunge wa upinzani wakiimba hatutaki kuibiwa na kutaka kukutana ukumbi wa Msekwa.
 
Hata hivyo, walishindwa kutumia ukumbi huo baada ya wabunge wa CCM kukubaliana kukutana ukumbi wa Msekwa na kuwalazimu upinzani kubaki ndani ya ukumbi wa Bunge.
 
HALI ILIVYOKUWA BAADA WABUNGE WA CCM KUTOKA
Baada ya wabunge wa CCM na Mawaziri kutoka nje, wabunge wa kambi rasmi ya upinzani kwa umoja wao walibaki ndani ya Bunge na kutoa msimamo wa pamoja baada ya majadiliano ya dakika 20.
 
Akizungumza na wabunge hao, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alisema ndani ya siku sita tangu Juni 27, mwaka huu serikali imeleta miswada 10 yote kwa hati ya dharura, akisema ni kwa ajili ya kuigonga muhuri kwa muundo wa funika kombe wanaharamu wapite.
 
"Hili ni Bunge la kwanza kuwa na miswada mingi iliyoletwa kwa hati ya dharura, haya masuala ya kukabidhi rasilimali zetu kwa wageni kwa miaka 100 ijayo haikubaliki, hatutakwenda kwenye kikao cha kamati ya uongozi, tuondoke hapa ikifika saa 9:45 alasiri turudi huku kabla hawajatufungia nje," alisema.
 
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge, Lissu ambaye ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani bungeni, alisema upinzani umechoka kuburuzwa, kupitisha sheria zinazohusu mambo makubwa ya nchi bila kufuata kanuni za Bunge, kulazimishwa kupitisha maamuzi ya ovyo na uongozi usiozingatia maslahi ya taifa.
 
"Hatutaweka mpira kwapani na kutoka, wao ndiyo waweke kwapani watoke, tutaendelea na msimamo wa kubaki ndani, watuletee vifaru na majeshi ndani ya ukumbi wa Bunge ndiyo watatuondoa, maana yake ukitoka wanapitisha, tumechoka kufunika makombe maharamia wapite, hatutafunika tena," alisisitiza.
 
"Leo tumeletewa kwenye orodha ya shughuli za Bunge miswada minne ikiwa katika hati ya dharura ikiwa na maana hakuna mjadala wa maana, hakuna muda wa kuichambua na kuielewa na kupitisha jambo linalofahamika, imeletwa kwa mpigo ili kusiwe na mtu anayeelewa anachopitisha," alisema.
 
Lissu ambaye ni Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, alisema: “Tanzania imegundua milimita za ujazo trilioni 55, ni nyingi sana ikitumiwa kwa uangalifu itatutoa zaidi, ili itusaidie lazima tuitungie sheria zenye maslahi na nchi.”
 
"Sheria ya mafuta ina vifungu 261, vifungu na vipengele vidogo zaidi ya 3,000, wabunge hawa wa siku zote wanaosinzia, nani atakayeielewa sheria kubwa kama hiyo, sheria ya mapato ya gesi ina vifungu 30, vipengele na vifungu vidogo 200, wabunge gani wenye uwezo gani wataielewa na kuipitisha," alisema.
 
Alisema: “Wameleta sheria ya uwazi na uwajibikaji na wana iharakisha, wakati ni hao hao walikataa kuweka wazi mikataba ya gesi, mafuta na madini, na kwamba mwaka 1997 walipitisha sheria iliyofanya marekebisho katika sheria mbili za kodi iliyofuta kodi za makampuni ya madini na uliletwa kwa dharura, na sheria ya uwekezaji Tanzania na hivyo hawalipi kodi.”
 
Alifafanua kuwa mwaka 1998 ilitungwa sheria ya madini kwa hati ya dharura, ambayo imeligharimu taifa. “Wanataka watuingize mjini kwenye mafuta na gesi, sisi wa upinzani tunasema imetosha hatutakubali," alisema.
 
Alisema pia Zanzibar imeingizwa kwenye sheria hiyo licha ya kwamba suala la mafuta na gesi siyo la Muungano, kwa mujibu wa Katiba inayopendekezwa.
 
Lissu alisema yeye ni mwanasheria mwerevu na mjuzi wa sheria na kwamba kwa muswada wa sheria ya mafuta atahitaji miezi mitatu ya kuuchambua, mazuri na mabaya yake.
 
Alisema akipewa siku mbili ataishia kuhesabu na hawezi kusema idadi ya vifungu, kwani kurasa za muswada ni 177 na kwamba hakuna anayeweza kusoma kwa siku hizo na kupitisha.
 
"Hakuna muda wa kutisha kuelewa yaliyomo kwenye miswada, iletwe kwa utaratibu wa kawaida isomwe mara ya kwanza, ipelekwe kwenye kamati wadau waitwe watoe maoni, ipitishwe kwenye Bunge lijalo, hili siyo Bunge la mwisho, niwepo au nisiwepo watakaopitisha wawe na muda wa kuelewa, hatuwezi kupitisha kwa shinikizo la nje," alisema.
 
Alisema Wizara ya Nishati na Madini, walieleza kamati kuwa wameambiwa watakapoenda kwenye mkutano mkutano MCC Septemba, mwaka huu, wawe wamepitisha na kwamba kuna shinikizo la Rais Jakaya Kikwete.
 
WABUNGE WA CCM WALIOPINGA 
Baadhi ya wabunge wa CCM waliokutana katika ukumbi wa Msekwa wale waliopinga miswada hiyo wakati wa semina ya wabunge, mwanzoni mwa wiki hii.
 
Mbunge wa Igunga, Dk. Peter Kafumu, alisema awali hakuwa ameelewa vizuri ila baada ya kukutana kwenye kikao wameelimishwa vizuri.
 
"Muswada utaingizwa Bungeni kama kawaida, tunachotaka na idadi ya wabunge itimie, kuna mambo wamerekebisha nimeridhika, serikali pia imetueleza umuhimu wa muswada huu kwa maslahi mapana ya nchi, tumeelewa serikali inataka kufanya nini, muswada lazima uingie bungeni ujadiliwe," alisema.
 
Mbunge wa Viti Maalum, Dk. Mary Mwanjelwa, alisema amebadili msimamo wake baada ya kueleweshwa kilichopo ndani ya miswada na kama wabunge wa chama hicho tawala waliokuwa wanapinga wameridhika.
 
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Nishati na Madini, Richard Ndassa, alisema muswada huo utaingia Bungeni kutokana na umuhimu ulioonekana baada ya serikali kuchambua na kueleza kwa kina zaidi.
 
KAULI YA SERIKALI
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, alisema wabunge walishirikishwa katika hatua zote, kuanzia sera na kwamba kuendelea kuchelewa nchi nyingine zitatangulia sokoni.
 
"Kwa umuhimu wa miswada hii tungekubaliana kutunga sheria hizi, kutakuwa na uwazi kwenye mikataba ambayo itapelekwa bungeni na kwa wananchi miezi mitatu kabla ya kusainiwa, kwa sheria hizi tutatengeneza dili nzuri sana kwa manufaa ya Watanzania, tutakuwa na hisa kwa kila kampuni," alisema.
 
Alisema ni vema ikafahamika kuwa kampuni zinazotegemea kazi hiyo hazizidi 10 ambazo zinajulikana hivyo Tanzania kuchelewa kuwa na sheria inajichelewesha kiuchumi.
 
"Sisi ni wengi ndani ya Bunge na tumechanguliwa na wananchi, hivyo kanuni za Bunge zitafanya kazi yake ambayo inasema wengi ndiyo watakaopitisha hoja, hivyo wabunge wa CCM tupo wengi na sheria hazikutungiwa chumbani zilikuwa wazi na shirikishi, hivyo tutatunga sheria hizi," alisema.
 
KAULI YA AG
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, alisema gesi na mafuta viko katika orodha ya masuala ya Muungano na kwamba serikali kwa umakini wake haiwezi kutunga sheria inayogusa maslahi ya pande zote bila kushirikisha kwa kuwa unyeti wa jambo lenyewe unafahamika.
 
"Mawasiliano yetu ya serikali tofauti na Bunge siyo ya wazi, mhimili wa utawala una mambo ya wazi na yapo mawasiliano ambayo siyo kama Bungeni au Mahakamani, mawasiliano ndani ya serikali hayawezi kutangazwa baadaye mtayaona bungeni au kwenye mikutano ya hadhara...mawaziri walikwenda Zanzibar na miswada wakazungumza," alisema.
 
SIKU YA SEMINA 
Jumanne wiki hii wakati wa semina hiyo, wabunge waliungana kwa pamoja na kati ya 11 waliochangia ni mmoja pekee aliyeunga mkono huku wengine wakitaka iachiwe serikali ijayo.
 
Akichangia mjadala, Dk. Kafumu alisema kuna vifungu vilivyonakiliwa kutoka sheria ya mafuta ya Uganda, na kwamba kilichokumbukwa kuondolewa ni neno Uganda, kauli hiyo ilimwinua Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Charles Mwijage na kuanza kumrushia maneno mbunge huyo.
 
Mwenyekiti Ndassa aliingilia kati na kumtaka Naibu Waziri huyo kutulia kwa kuwa Waziri yupo na baadaye hali ilitulia na mbunge huyo aliomba radhi.
 
Aidha, alisema kazi za Shirika la Maendeleo ya Mafuta Tanzania (TPDC), zinaingiliana na Mamlaka ya usimamizi wa petroli (Pura) licha ya TPDC kujiendesha kibiashara lakini ina majukumu ya usimamizi.
 
Wabunge wengine wa CCM waliotaka miswada hiyo kusubiri serikali ijayo ni Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangwalla na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
 
Akizungumza baada ya msimamo wa wabunge, Simbachawene alisema serikali ilifanya kazi yake inavyotakiwa, wadau walihusishwa na maoni yao yalizingatiwa.
 
Alisema kuchelewa kwa miswada kutachelewesha matarajio ya uzalishaji gesi yaliyotakiwa kuanza mwaka 2018/19.
Hadi semina hiyo inamalizika wabunge walikuwa na msimamo mmoja, na Mwenyekiti wa Kamati, Ndassa aliahidi kupeleka mapendekezo kwa Spika Makinda.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment