AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, July 3, 2015

Haraka hii ni ya nini kupitisha kwa dharura miswada gesi na mafuta?

NA EDITOR

3rd July 2015

Katuni.
Ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana ulikumbwa na hali isiyokuwa ya kawaida wakati wabunge wa upinzani walipocharuka kupinga kuwasilishwa bungeni kwa miswada mitatu inayohusiana na mafuta na gesi kwa hati ya dharura. 
 
Wabunge walipinga kuwasilishwa kwa miswada hiyo kutokana na kile walichoeleza kuwa ni kuwapo kwa muda mfupi wa kujadili na pia kukumbushia makubaliano yao katika semina kuhusu miswada hiyo ambapo kwa kauli moja walipinga uwasilishwaji wake sasa na kutaka ishughulikiwe na bunge lijalo.
 
Siyo nia yetu kutaka kujadili kiundani juu ya kile kilichojiri bungeni. Hata hivyo, tunadhani kwamba ni kweli, ipo haja ya kufikiria mara mbili juu ya uamuzi huu wa kuingiza miswada hiyo kwa ‘hati ya dharura’.
 
Kadri tunavyofahamu, na ilivyoelezwa pia na baadhi ya wabunge katika kujenga hoja za kupinga miswada hiyo ya mafuta na gesi kusomwa bungeni kwa hati ya dharura, ni kwamba Sheria ya Mafuta ina vifungu 261 na vifungu na vipengele vidogo zaidi ya 3,000. Sheria ya mapato ya gesi ina vifungu 30, vipengele na vifungu vidogo 200. Idadi kubwa ya nyaraka hizi inadhihirisha wazi kuwa mjadala wowote kuhusiana na kile kilichomo unahitaji muda wa kutosha na siyo kwa njia inayotaka kutumia. 
 
Ni kwa sababu kitendo chochote kile cha kuruhusu 'rundo' la vifungu vya muswada wa sheria kuhusiana na mafuta na gesi, na ambavyo kwa ujumla vinatajwa kuwa na kurasa 177, ni sawa na kuiingiza nchi katika uwezekano mkubwa wa kuwa na sheria zisizokuwa na maslahi kwa taifa. Hii ni kutokana na ukweli kuwa wabunge hawatakuwa na fursa ya kutosha ya kupitia kila kifungu kwa kina na kushiriki mjadala kwa hoja zenye tija kwa taifa.
 
Ikumbukwe kuwa tunakoelekea, taifa letu litakuwa likitegemea uchumi wake kukua kwa kasi kubwa zaidi kupitia sekta ya gesi na mafuta. Tafiti katika maeneo mbalimbali nchini zimethibitisha kuwa hadi kufikia sasa, taifa lina rasilimali ya gesi asilia ya futi za ujazo zaidi ya trilioni 50.    
 
Zipo pia tafiti nyingine nyingi zinazotoa matumaini ya kupatikana kwa kiwango kingine kikubwa zaidi cha rasilimali ya gesi na mafuta. Kwa sababu hiyo, sekta hii inatarajiwa kuwa mhimili mkuu wa kiuchumi. Itaingiza mapato ya moja kwa moja kupitia kodi, mauzo ya gesi na mafuta ughaibuni, kutoa ajira, kuwezesha ustawi wa viwanda nchini na pia kufanikisha uzalishaji wa mbolea utakaoongeza uzalishaji wa chakula. Hakika, zipo faida nyingi zitokanazo na gesi na mafuta na hivyo, hakuna ubishi kuwa hii ni sekta muhimu na nyeti kwa maslahi ya taifa ambalo kufikia mwaka 2025 linatarajiwa kuwa la uchumi wa kati.
 
Kwa kuzingatia yote hayo, sisi tunaona kwamba ni kweli, kuna kila sababu ya kujipa muda wa kutosha katika kujadili masuala ya gesi na mafuta na siyo kwa ‘hati ya dharura’. 
 
Aidha, kuna ukweli kuwa wabunge wengi hivi sasa hawana utulivu wa kutosha kiasi cha kuweza kujadili kwa kina miswada hii. Na hili liko wazi. Kwamba huu ni mkutano wa mwisho kwao na hivyo kifikra, wengi wao hawako bungeni hata kama wanaonekana kimwili. Wengi wanawazia hatma yao katika uchaguzi. Na wengi wao hawaonekani bungeni Dodoma kwa sababu wangali wakiweka mambo yao sawa kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba. 
 
Ushahidi ni kuwapo kwa mahudhurio ya chini mno katika baadhi ya vikao, kimojawapo kikiwa ni kile kilichokuwa na wabunge 68 tu kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2015/2016, badala ya zaidi ya 300.
 
Katika mazingira kama hayo, hatuoni uwezekano wowote wa kuwa na wabunge wenye kujadili mambo kwa kina kama tuliowazoea. Ni kwa sababu hawana utulivu.
 
Mathalan, inaelezwa kuwa kipengele kimojawapo cha miswada hiyo kinatoa nafasi kwa mikataba yote iliyosainiwa kabla ya kuwapo kwa sheria hiyo itabaki kama ilivyo. Kama hivyo ndivyo, sisi tunadhani kwamba hii ni hatari kwani kwa muda mrefu sasa kumekuwa na kilio kuhusu usiri wa mikataba mingi yenye utata na isiyokuwa na tija kwa taifa, hasa kuhusiana na madini na pia ya mafuta na gesi. Tunadhani kwamba siyo busara kufikisha miswada hii kwa hati ya dharura, tena kwa wakati huu wa siku chache kabla Bunge halijavunjwa Julai 9.
 
Yafaa pia tukajiuiliza kwamba je, haraka hiiya sasa ni kwa maslahi ya nani? Ikiwa ni kwa maslahi ya taifa na siyo ya watu wachache, kwa nini miswada hiyo isifuate utaratibu wa kawaida? Na kwa nini miswada nyeti na yenye maslahi makubwa kwa taifa iharakishwe wakati huu kwa mgongo wa hati za dharura wakati wabunge wakiwazia hatma yao katika uchaguzi? 
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment